Tuesday, November 24, 2009

Lishe duni inadumaza ukuaji wa watoto

NA MWANDISHI WETU


24th November 2009















Watoto wakisubiri mgao wa chakula.

Utapiamlo kwa watoto bado ni tatizo kwa nchi zinazoendelea duniani ingawa wataalam wanasema nchi nyingi zimeweza kupiga hatua .

Moja ya tatu ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwenye nchi hizo zinahusishwa na ulaji duni , ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (Unicef) inasema.

UNICEF wanasema pia kuwa katika watoto wapatao milioni 195 mmoja kati ya watatu amedumaa kutokana na kukosa lishe bora , ingawa kiwango chao kimekuwa kikipungua kuanzia mwaka 1990.

Ripoti hiyo inaeleza pia kuwa idadi ya watoto ambao wana uzito mdogo ukilinganisha na umri wao imebakia kubwa huku nchi nyingi zikifanya jitihada ili kuweza kufikia malengo yanayotakiwa walao kupunguza idadi hiyo ifikie nusu yake.

Kiwango cha watoto wanaodumaa kukua kinaweza kuwa kikubwa kwa sababu wakati watoto wengine wana uzito wa kawaida wako pia watoto ambao wana uzito mkubwa zaidi- hii ni kutokana na kuwa chakula wanachokula ni duni na hivyo kuathiri ukuaji wao.

Wataalam wanaonya kuwa mara nyingi hali kama hiyo ikitokea ni kitu kisichoweza kurekebishwa na mara nyingi inamfanya mtu kama huyo abakie na afya mbaya maisha yake yote.

Kiongozi wa Unicef, Ann Veneman anasema kuwa : " Lishe duni inawanyima watoto nguvu kiasi kwamba baadhi ya magonjwa ambayo mwili ungeweza kupambana nayo unaweza ukashindwa na hiyo ni hatari kwao”.

"Kama hatua za lazima hazitachukuliwa ili kuhakikisha kuwa mama na mtoto wanapata chakula bora tujue kuwa gharama yake itakuwa kubwa siku za baadaye.."

Tunawezaje kumaliza tatizo hilo

Moja ya maeneo ambayo yamefanyiwa kazi ni huko Peru, Amerika ya Kusini ambako tatizo la lishe duni lilikuwa kubwa.

Mwaka 1999, serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na Unicef walianzisha kwa pamoja na shirika la Maendeleola Marekani mradi wa kuwahudumia watoto katika umri mdogo.

Mradi huo uliweza kuwatumia wafanyakazi wa afya kutoa huduma kwa akina mama baada ya kujifungua kwa kuwahimiza kunyonyesha watoto na kutoa chakula cha kulikiza katika majimbo matano ya vijiini.

Ilipofika mwaka 2004, zaidi ya watoto 75,000 waliokuwa chini ya miaka mitatu ambao walikuwa wananufaika na mpango huo kiwango cha watoto wengi kudumaa kilipungua kutoka asilimia 54 hadi kufikia 37.

Mpango huo kwa sasa unaendeshwa kwa nchi nzima ambapo wataalam wanaeleza kuwa siku za kwanza 1,000 za mtoto ambazo ni sawa na miaka mitatu ya mwanzo ni muhimu ili kuweza kutatua tatizo hilo.

Wataalam hao wanasema kuwa suala la kuhimiza unyonyeshaji katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ni muhimu.

Hata hivyo Unicef wanasema kuwapatia watoto pia vyakula vya ziada ni suala litakalosaidia tatizo la lishe duni

Mipango mingi inayohusiana na lishe imekuwa ikiongeza madini ya joto kwenye chumvi ili kuwasaidia watoto kupata madini hayo yanayochangia katika ukuaji wa ubongo pia kuwapatia vitamini Ambayo inasaidia katika ukuaji wa mifupa na kuuwezesha mwili kupambana na maambukizo.Hatua kama hiyo repoti hiyo ya Unicef inasema itasaidia kupunguza moja ya tano ya vifo vya watoto.

Unicef inasema kuwa kwa kushirikiana na wadau wengine zikiwemo na serikali husika na mashirika ya misaada imekuwa ikipiga hatua katika kuboresha lishe kwa watoto kwenye nchi 150 zinazoendelea.

Kuanzia mwaka 1990 uwiano wa watoto ambao wanakuwa na uzito mdogo imepungua kwa kiwango cha moja ya sita ,kulingana na mipango na takwimu ambazo Unicef na mashrika menginge wanayofuatilia suala hilo kama Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia.

Hata hivyo pamoja na hatua hizo zote kuchukuliwa kwenye baadhi ya nchi hali ni mbaya kwani takwimu zinaonyesha kuwa kati ya nchi 117 ambazo zina tatizo hilo ni nchi 63 tu ndizo zitaweza kufikia Malengo ya Milenia katika kipengere hicho ambapo lengo ni kupunguza nusu ya idadi ya watoto wanaokuwa na uzito mdogo ifikapo 2015.

Kwa upande wa Afrika hali ya mafanikio bado siyo makubwa wakati nchi za Asia zina afadhali kidogo na wakati Amerika ya Kusini imekuwa ikipiga hatua zaidi.

Kitty Arie, mtaalam wa masuala ya sera kwenye shirika la Save the Children, anasema kuwa lishe duni ina madhara ya muda mrefu ikiwemo mtoto kushindwa kufanya vizuri shuleni.

"Hili ni suala muhimu sana na linawezakana na ni lazima litafutiwe dawa.."

Monday, November 23, 2009

Mwakyembe akataa kuzungumzia hoja za Rostam Aziz

Fidelis Butahe na Mussa Mkama


MBUNGE wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe jana aliamua kutozungumzia sakata la Richmond, na hasa hoja za hivi karibuni za mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ya kutaka uchunguzi mpya wa kashfa hiyo kwa kuwa ripoti ya kamati teule ya Bunge ni ya uongo na haikuwa na baadhi ya nyaraka muhimu.


Katika siku za karibuni, Rostam amenukuliwa akitaka uchunguzi mpya wa kashfa hiyo ufanyike, akipendekeza kazi hiyo ifanywe na jopo la majaji na kwamba endapo jopo hilo litamkuta na hatia, atakuwa tayari kujiuzulu nyadhifa zake zote, hoja ambayo imepingwa kwa maelezo kuwa maamuzi ya Bunge hayawezi kuchunguzwa upya na muhimili mwingine wa dola.


Dk Mwakyembe, mmoja wa wabunge wanaojilikana kama makamanda wa vita ya ufisadi, ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo teule ya Bunge ambayo ripoti yake ilisababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu na mawaziri wengine wawili.


Lakini jana, mbunge huyo wa Kyela alikataa kata kata kuzungumzia suala hilo pamoja na hoja za Rostam.


Dk Mwakyembe aliombwa kuzungumzia suala hilo wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa Mfuko wa Maendeleo wa Watu wa Kyela (KDF), uliofanyika Chuo Cha Ufundi (Veta) jijini Dar es Salaam.


"Hapana siwezi kuzungumza lolote leo hapa ni masuala ya KDF tu... nisingependa kuzungumza mambo ambayo sikupanga kuyasema na wala hayahusiani na mkutano huu,"alifafanua na Dk Mwakyembe.


"Nimetoka Mbeya leo na kule kuna ugeni wa Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa, lakini watu wa Kyela wameniambia nije kwa sababu ya umuhimu wa mkutano huu. Kwa hiyo siwezi kuzungumza mada iliyo nje ya mkutano huu, samahani sana."


Mwenyekiti wa KDF, Gray Mwakalukwa alisema katika ufunguzi wa mkutano huo kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuchangia juhudi za serikali katika maendeleo hasa katika elimu.


"Tangu kuanza kwa mfuko huu mwaka 2006 hivi sasa Kyela kuna maendeleo makubwa, hasa katika sekta ya elimu... sasa kuna shule nyingi za sekondari tofauti na kipindi cha nyuma," alisema Mwakalukwa ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na ambaye alikuwa kamishna wa madini.


"KDF imefanya mengi Kyela, ilinunua vitanda 60 kwa ajili wa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Kiwira Coal Mines, lakini pamoja na hayo tumefanya mengi sana ambayo kuyasema yote inahitaji muda wa kutosha."

Friday, November 20, 2009

Umasikini wa Tanzania ni wa Kujitakia

Africar T Kagema

UNDP inatoa taarifa juu ya "The concentrated poverty". Yaani umaskini wa kutisha, kwa bahati mbaya Tanzania ni moja ya nchi zilizo chini ya mstari mwekundu wa umaskini ambao wao wanaita "below poverty level" au absolutely poverty". Huu ni umaskini unaozidi kawaida ya umaskini, waweza kuita umaskini sana, au umaskini zaidi, ama umaskini mno, lakini yote hayo yanaashiria neno moja tu nalo ni kwamba umaskini unaoikabili nchi yetu ni sawa kabisa na ugonjwa wa ukimwi kwa maana ya kwamba umaskini wetu sasa hautibiki.

KATIKA kuufafanua umaskini, mtu aweza kuuweka ama kuugawanya katika mafungu mawili, umaskini wa nchi (au taifa) na umaskini wa watu au "mass poverty" yaani walio wengi katika ujumla wao. Enzi za mkoloni nchi yetu ilikuwa na umaskini wa watu tu yaani "individuals" lakini haikuwa na umaskini wa dola kama uliopo sasa ambapo takribani asilimia 50 ya bajeti ya serikali inatoka kwa wahisani.

Katika uhalisi wa mambo nchi yetu ni ombaomba, hata wanaodai Mkapa amerudisha heshima ya Tanzania kimataifa sijui wanatumia vigezo gani kwani katika ukweli wa maisha hakuna omba omba yeyote aliyepata kuheshimika. Heshima ya Tanzania italetwa kwa kujitegemea na kujitosheleza, kwanza kwa chakula na baadaye kwa mahitaji mengine, yaliyo muhimu kwa taifa. Enzi za mkoloni Tanganyika ilikuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa mkonge ambapo ilitoa asilimia 28 ya mahitaji ya dunia ukiacha mazao mengine kama nyonyo, karanga, pamba na ngozi, na kahawa.

Kwa mapato hayo serikali ya mkoloni haikuwa lofa iliweza kujenga mabarabara, njia za mawasiliano, na kutoa elimu bora kwa hao waliobahatika kusoma. Kwa maneno mengine walau serikali iliweza kujitegemea, lakini sasa kila kitu kiko nyang'anyang'a na hoi bin taabani. Hakuna mradi wowote wa kitaifa ambao ungeweza kutoa ajira ya maelfu kama ukoloni, hakuna watu wabunifu ndani ya hiyo kada ya watawala badala yake umahili wao uko kwenye kudhibiti wapinzani na kuendesha mizengwe ya kuwawezesha kubaki madarakani. Wao watawala, ushindi wanaouona muhimu ni ule tu wa uchaguzi mkuu. Ule ukweli kwamba wao baada ya kuwashinda wapinzani, nao wameshindwa na umaskini hawaujali wala hawaoni aibu.

Inapotokea kwamba dola imekuwa maskini hadi kuendeshwa kwa misaada toka nje ya nchi na watu (wananchi) nao wakawa maskini hadi kufikia kiwango cha kushindwa kufanya lolote na kubaki kama walemavu kungojea kudra za Mungu basi hapo kuna tatizo mara mbili yaani tatizo la umaskini na tatizo la watu wenyewe. Lakini papo hapo viongozi wakuu wa serikali wanapokuwa ni matajiri kuliko serikali yao, basi hapo ndipo kinapoinuka kitendawili cha uongozi bora.

Mawaziri walio matajiri, wakuu wa mikoa walio tajiri, makatibu wakuu walio tajiri, na wabunge walio tajiri, je, wamefanya biashara gani madarakani hadi wakaupata utajiri walio nao? Kisha je wameulipia kodi ya mapato? Maana inaonyesha kwa utajiri wao basi wanavyo vyanzo vya uhakika vya mapato na kwa kuwa katika nchi yetu kuna sera ya kutoza kodi ya mapato (wakati mwingine hata kabla ya mtu hajapata) basi na wao watoe mchanganuo wao kuthibitisha kwamba nao ni raia wema wanaoilipa serikali mapato sawa na sheria za nchi zinavyoagiza!!

Kitendawili hiki ni kigumu kuteguliwa ingawa jibu lake liko wazi, kitendawili chenyewe ni kwamba hapa kuna nchi yenye rasilimali za kila namna lakini bado nchi hiyo ni maskini ya kupindukia duniani, nchi hiyo ilipotawaliwa na Wakoloni haikuwa maskini kama ilivyotawaliwa na watawala waliopo sasa, wakati nchi ni maskini, na watu ni maskini mno. Viongozi ni matajiri wa kupindukia. Je kuna mchezo gani umechezwa kuyaleta haya? Jibu wanalo wenyewe watawala, wanajua jinsi walivyofanya hata kuupata utajiri walio nao sasa isipokuwa wanajifanya hawajui wafanye nini ili kuondoa umaskini kwa nchi yao na watu wao, kwa kuwa akili yao imeishia kujitajirisha wao na siyo nchi. Vijana wapatao laki nne wanamaliza elimu ya msingi kila mwaka lakini uongozi uliopo madarakani haujui ufanye nini au uwapeleke wapi,hivyo baada ya kutoka darasani wanaishia "vijiweni".

Viwanda vingi vimekufa, na mashirika ya umma mengi yameanguka waliokuwa wafanyakazi nao inabidi waungane kwenye vijiwe na vijana wao wanaotoka darasani hadi vijiweni. Kutokana kukosekana sera ya uhakika ya kilimo, kilimo kimebaki duni toka enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa na kwa uduni huo.Kilimo kimejiunga kwenye siasa na kutengenezewa majina mazuri ya kisiasa kama ‘’KILIMO KWANZA’’ wakati uhalisia sio huo. Tumebaki kudanganyana tu ili mradi siku iende. Hakuna elimu ya kuwaelimisha wananchi hasa vijana wajue umuhimu wa kilimo. Mikopo ya Kikwete inatolewa kwa wafanyabiashara badala ya wakulima, na wafanyabiashara wenyewe sio wahitaji halisi wa mikopo hiyo kwania tayari walishakuwa na mitaji ya kutosha. Wakulima wanaachwa kama walivyo, vijana wanaona kilimo kama hakiwezekani kwani hakiwaondoi katika dimbwi la umasikini wa kutupwa. Wakulima hawapendelewi wala hawajengewi mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao kama wanavyofanyiwa wafanyabiashara, hivyo vijana wanaona ni bora kufanya biashara ili wajiingize kwenye mazingira mazuri kuliko kiliko kulimo. Kizazi kipya cha vijana wanakimbia kilimo vijijini na kuja mjini kubahatisha maisha mapya. Wale vijana wanaozaliwa mijini, wao wanakimbilia majuu (wanazamia meli), kizazi cha kale cha wakulima kinazeeka na kudhoofu na hakuna wa kuziba pengo, hivyo usemi wa kwamba Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi umebaki kauli za maandishi tu, lakini katika uhalisi wa mambo Tanzania haina wakulima ndiyo maana ni nchi inayoumwa njaa kila mwaka. Pia Tanzania si nchi ya wafanyakazi maana hakuna kazi nyingi za kufanya kwa sababu hakuna viwanda wala makampuni au mashirika ya kutoa ajira.

Yale yaliyokuwepo yameuawa na watawala waliopo madarakani. Sasa inabidi wote wenye kutazama mambo katika umakini wajiulize nchi ambayo imepukutisha maelfu ya askari wake toka jeshini baada ya kulazimishwa na sera za IMF za kuwa na jeshi dogo, na hivyo kuwalazimisha askari hao kujiunga na walalahoi wengine vijiweni, nchi ambayo imeua mfumo wake wa elimu na kuwafanya vijana wake wasipate elimu ya kuwasaidia kuishi badala yake vijana wake wakawa na elimu ya nadharia ambayo baada ya mtu kumaliza shule (kutoka darasani) anashindwa kuitumia (to apply) aidha hapo kijijini au mjini, mwisho anaishia kijiweni kuvuta bangi au kulamba unga. Ndio vijana hawa wanalaghaiwa na wafanyabiashara wakubwa kujiingiza katika biashara haramu.

Nchi ambayo inashindwa kuzalisha kizazi kipya cha wakulima na waliopo inawaacha wawe wachovu zaidi kwa kuvuruga mfumo wa masoko ya mazao yao na kuwasababishia umaskini usiomithilika, nchi ambayo haina mpango wowote wa kuongeza ajira kwa maelfu ya wananchi wake, nchi ambayo imeua mfumo wa utoaji haki na kusababisha magereza kufurika wafungwa na mahabusu, nchi ambayo haina mikakati yoyote ya kuwatumia wafungwa kuzalisha mali ili kujikimu wawapo magerezani badala ya kutegemea pesa kutoka serikalini, na mahakama zake kuwa na mafuriko ya kesi za jinai. Je nchi ya namna hiyo ina uhakika gani wa kudumisha amani yake wakati inayaacha mabomu yanayongojea wakati wake ufike yalipuke?

Kwa hakika nchi yetu ni mfano wa mtu anayetembea sambamba na gema ambaye kuna uwezekano wa kutumbukia wakati wowote. Hata hivyo ieleweke wazi kwamba tatizo la umaskini ni matokeo tu ya uzembe wa watawala, endapo nchi itapata utawala ulio makini na ulio dhamiria kuondoa tatizo hili, umaskini wa Tanzania unaweza kufutika baada ya muda mfupi na Tanzania ikawa miongoni mwa nchi tajiri na zenye uchumi imara au "economic giant" katika dunia hii.

Mtu hawezi kuamini akielezwa kwamba umaskini wa Tanzania ni sera ya makusudi kabisa ambayo lengo lake kuu ni kudhibiti wananchi na kuwawezesha watawala kuendelea kudumu madarakani hadi siku ya kufa. Watawala wa nchi hii wanajua wazi kwamba wakiwaondoa watu wao katika dimbwi la umasikini hawawezi kutawalika na pia hawawezi kuburuzwa, kwa hiyo umaskini ni silaha yao nzuri ya kuendelea kutawala.

Fikiria kama Watanzania wangekuwa na elimu, shibe, na utajiri, ni wazi kwamba asingekuweko mgombea yeyote wa ubunge, urais, au udiwani wa kuhonga watu soda, pilau, khanga au pombe za kienyeji. Pasingekuweko na mtu wa kuuza shahada yake ya kupigia kura kwa Tshs: 2,000. Hapo ndipo yangekuweko mashindano ya sera na programu za kuendeleza nchi, majimbo, maeneo, au mitaa.

Kwa ajili hiyo umaskini kama ulivyo katika nchi hii ni kikwazo cha mengi, ni kikwazo dhidi ya demokrasia, ni kikwazo dhidi ya utawala bora kutokana na ukweli kwamba wezi wa mali za umma na walaji rushwa na mafisadi ndio wenye tabia za kuwanunua wapiga kura walio hoi kwa njaa na umaskini wa kupindukia. Pia umaskini ni kikwazo dhidi ya mabadiliko yoyote.

Sasa kwa bahati mbaya tatizo la umaskini haliwezi kuondoshwa na utawala unaoona kwamba kuwatawala watu masikini ni raha zaidi kuliko kuwatawala watu walioridhika kimaisha, wakoloni walijitahidi kuwagawa wananchi ili wabaki hawaelewani kati ya walionacho na wasionacho, waliosoma na wasiosoma ili wapate kinga ya kuwafanya waendelee kutawala bila shida. Wao walihakikisha wananchi wanaowatawala wanabaki wajinga. Wagonjwa, na maskini ili wasiwe na ubavu wa kuwaondoa madarakani. Cha kushangaza ni kwamba takribani miaka 48 (2009-1961) tangu tupate uhuru wetu kutoka kwa Mwingereza watawala wetu bado wanaendeleza mbinu za wakoloni za kutawala za kutufanya tuwe wajinga, masikini na tunaosumbuliwa na magonjwa kila wakati.

Kwa mfano Maasi ya Maji Maji 1905-1907 yalifanya Mjerumani kuyaelewa makabila ya kusini kwamba ni ya watu jeuri na wagumu kutawalika endapo wataachiwa kutulia pasipo kuvurugwa na njaa, umaskini au magonjwa alichokifanya ni kutokupeleka maendeleo makubwa kama vile reli, shule, na mahospitali makubwa. Serikali ya TANU pia ilifuata nyayo za Mjerumani, ilijua wazi kwamba watu wa kusini, Wangoni, Wapangwa, wamatengo, Wamakua, Wamwera, Wanyasa, Wamakonde, Wayao, na Warufiji kwa asili yao ni watu jeuri na wagumu kuburuzwa endapo wataachiwa wawe na uimara wowote ule aidha uimara wa kiuchumi, au uimara wa kielimu au uimara wa kuwa na mshikamano, hivyo basi sera ya ‘’gawanya utawale’’ ikabidi iendelezwe na juu ya hiyo iongezwe sera ya kuwafanya wawe maskini zaidi na pia kuwatenga ama kuwabomolea misingi yote ya maendeleo kwani kama wangekuwa na maendeleo walau nusu tu ya yale yaliyoko kaskazini ingekuwa vigumu kutawalika. Kwa hiyo kwa makusudi kabisa reli ya TAZARA ambayo kimsingi ingekuwa kama ilivyo reli ya kati kwa mikoa ya kusini ikapitishwa porini badala ya kupita Rufiji, Mtwara,Lindi, Songea hadi Itungi Port (Kyela) na kuingia Zambia. Reli ilikwepeshwa maeneo hayo ili tu kuzuia kasi ya maendeleo ya kusini na pia kuzuia kukua kwa uchumi wa kusini.

Kusini ambayo ina rasilimali nyingi na utajiri mwingi kuliko kaskazini na pengine maeneo mengine yote ya nchi hii sasa imekuwa chemi chemi ya kutoa Wamachinga kwa sababu tu watoto wake wamenyimwa elimu. Rasilimali zake zinaoza na huenda siku za usoni watapewa wageni kama ilivyotokea kwa SongoSongo na machimbo ya Alexandrite huko Tunduru.
Baadhi ya wasomi wachache wa kusini walipewa nyadhifa katika serikali ili ziwe kama takrima na uchawi wa kuloga akili zao wasijejali tena maendeleo ya kusini wala kuwahurumia ndugu zao ambao wanahitaji ukombozi kwa njia ya maendeleo.

Niandikie:


kyelacommunity@live.com

WANUFAIKA, WAATHIRIKA NA WANUSURIKA WA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Na. M. M. Mwanakijiji

Katika sehemu ya kwanza tuliangalia kwa ujumla kuwa utawala wa kifisadi unaonekana katika maeneo makubwa matatu yaani kisheria, kiuchumi na kisiasa. Tukatambua kwamba ili utawala wa aina hiyo ufanikiwa ni lazima upenye katika maeneo hayo matatu na mabadiliko yoyote ya kuumomonyoa utawala huo ni lazima yalenge kugusa maeneo hayo matatu. Tumeuangalia kwa nje utawala huo na pole pole katika sehemu hii ya pili tujaribu kuangalia utawala huo kwa karibu na kuangalia ni vitu gani hasa vinaustawisha utawala huo kiasi cha kuweza kutengeneza mfumo unaofanya kazi na watu wakaishi ndani yake na kukubali kama namna ya maisha yao (lifestyle).

Mfumo wa utawala wa kifisadi hausimami hewani na hautokei kama ukungu asubuhi au umande wa alfajiri. Ufisadi hujengwa na kutengenezwa pole pole katika jamii kwa kuanzia katika sehemu au maeneo madogomadogo na pole pole kuanza kupenya kwenye maeneo mbalimbali ya maisha na kuwa ni sehemu ya utamaduni na hatimaye kuwa mfumo uliorasmishwa de facto.

Ufisadi (mfumo) hujengwa na WATU.

Kama nilivyosema hapo juu ufisadi hautokei hivi hivi tu na hatuwezi kumsingizia shetani; ufisadi hujengwa, hupaliliwa, na kulelewa na watu. Lakini siyo watu hivi hivi tu bali kuna mazingira yanayowatengenezea watu hao sababu ya kuanza kujihusisha na vitendo vya kifisadi na matokeo yake kuanza kujenga utamaduni wa kifisadi ambao huanza kuchimbwa na kusimikwa taratibu katika sheria, siasa na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kimaisha kijumla.

Katika mfumo huu wa kifisadi watu hugawanyika katika matabaka kama ilivyo katika mifumo mingine ya kimaisha iliyopo duniani. Kwenye utumwa wapo mabwana na watumwa; kwenye ubepari wapo manyonyaji na wanyonywaji, n.k Kwenye ufisadi kuna matabaka makubwa matatu ambayo yanaingiliana na kuhusiana kila siku na hivyo kuendelea kufanikisha kwa namna ya kila mmoja wao kudumisha na kukoleza mfumo huu dhalimu wa utawala wa kifisadi.

Makundi hayo ni Wanufaika, Waathirika na Wanusurika wa ufisadi. Na ndani ya kila kundi kuna makundi madogo madogo ambayo ndiyo yanaunda kundi hilo kubwa.

WANUFAIKA WA UFISADI

Kundi hili linajumuisha watu wote ambao moja kwa moja (directly) wananufaika na uwepo wa mfumo wa kifisadi. Kama tukitumia mfano wa shamba, basi wanufaika ni wale wakulima waliolima shamba la ufisadi ambamo ndani yake wakapanda mazao mbalimbali. Ni wao ndio huvuna na kunufaika moja kwa moja na mavuno ya matunda ya shamba lao. Siyo tu wao ni wamiliki wa shamba hilo, bali ndio wakulima, wavunaji na walaji wa kwanza wa matunda ya ufisadi. Kundi hili linajumuisha makundi madogo mawili.

WANAONUFAIKA MOJA KWA MOJA

a. watawala serikalini

Hawa ni wale wanaosimama kama wenye madaraka serikalini; ni viongozi wa ngazi za juu katika nafasi mbalimbali kuanzia Ikulu, Mahakama, Majeshi, vyombo vingine vya usalama, n.k Tunapozungumzia watawala hatuzungumzii wafanyakazi wa serikali au maafisa wa ngazi za chini; la hasha! Tunazungumzia kundi lile la watu wenye uamuzi juu ya maisha yetu, sera gani tufuate, tutozwe kodi kiasi gani na tusipolipa tuadhibiweje; hela zetu ziende wapi na kwanini, ni wale wenye uamuzi kwa kweli juu ya hatima ya maisha ya mtu mmoja mmoja kama vile wana uamuzi wa mwisho juu ya maisha ya jamii nzima.

Nilipoliingiza hili neno “watawala wetu” sikuwa namaanisha ni watawala wetu “kisiasa” kama ambavyo tumekuwa tukiwaita zamani tukimaanisha “viongozi” bali ni watawala wetu wa jumla ya maisha yetu. Ni wao ndio wanatuamulia barabara gani zijengwe, shule zetu ziweje, mwekezaji gani apewe nini na kwa muda gani. Hili ndilo kundi la kwanza la wanufaika wa ufisadi. Ukifikiria sana utaona kuwa hawa ndio watu wana nguvu zaidi katika maisha yako kuliko hata familia yako au wale unaowapenda; na yawezekana tunawaona au kuwadhania kuwa wana nguvu kuliko Mungu.

Hawa Watawala wametujaza fikra za kujiona duni na tusiojua kiasi kwamba wametengeneza utegemezi mbaya wa kifikra juu yao. Ndani yetu tumejawa fikra ya “serikali” kama dudu fulani lenye kumiliki maisha yetu na lenye kuamua matokeo ya maisha yetu; dudu hili serikali basi “likisema” au likifanya jambo basi watawaliwa hawana budi kukubali kwani kupinga kokote kule kutaambatana na matokeo mabaya.

Ni roho hii ya kujiamini iliyosababisha kwa muda mrefu watu kukubali maelezo na visingizio vya “serikali” pale ambapo mambo hayaendi sawasawa. Ikafikia mpaka mahali watu walishindwa kuhoji zaidi. Watawala wakapewa ufunguo wa maisha yetu kiasi kwamba katika upotovu wa fikra zao walikuwa ni kama wakoloni tuliowakataa; wakitukebehi hadharani, wakitutukana kama watoto wadogo na wengine hata kutuzaba vibao utadhani vile vya “kelbu” vya mbwa.

Watawala ndio wanufaikaji wa kwanza wa mfumo huu wa kifisadi na kutokana na hilo haiwezekani kwa wao kuubomoa au kuuvunja vunja mfumo unaowahakikishia uwepo wao usiokoma na chakula chao na cha watoto wao. Tukielewa ukweli huu tutambue ni kwanini kundi la wanufaika wa ufisadi walioko serikalini siyo wa kuwategemea kuutokomeza mfumo wa ufisadi. Hawawezi kukata tawi wanalokalia.

b. Chama tawala

Katika mfumo wa ufisadi mahali popote duniani ni chama tawala kilichounda serikali ndiye pia mnufaika wa kwanza na wa moja kwa moja wa mfumo wa utawala wa kifisadi. Ukweli huu ulionekana Mexico chini ya Utawala wa Chama cha Mapinduzi cha Mexico kwa karibu miaka 70, na ni ukweli unaonekana huko Syria chini ya utawala wa Baath, na ndio ulionekana kwa muda mrefu katika utawala wa Kikomunisti wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi. Ni ukweli pia ulionekana kwa miongo karibu minne ya utawala wa chama cha Baath cha Iraq chini ya Sadam Hussein.

Katika mfumo huo wa utawala wa kifisadi mafanikio ya mtu au kikundi cha watu yanahusishwa moja kwa moja na uwepo wao au ushiriki wao katika chama tawala. Kwa wao hao chama tawala ndio mlango rahisi, wa haraka na wa uhakika wa kuwahakikishia mafanikio yao na usalama wa maisha na mali yao. Hivyo, chama tawala katika utawala wa kifisadi hutukuzwa kuliko Bunge, Mahakama, au Urais; chama tawala kiko juu ya vyombo vingine vinavyofanya kazi katika nchi ya utawala wa sheria na demokrasia.

Hivyo, katika mfumo huo wa kifisadia wanachama waandamizi wa chama tawala ndio wanaonesha mafanikio ya mfumo huo. Hawa ndio wabebaji wa kwanza na watetezi wa sera mbalimbali za chama chao na hivyo zawadi ya utii na kujitoa kwao kukitetea chama chao huzaa zawadi ya mafanikio katika mambo mbalimbali. Utawakuta ndio wao wabia wakuu katika makampuni mbalimbali, wananunua viwanja vya ujenzi kwa njia rahisi kuliko mtu mwingine, wanapata taarifa za ndani za mambo mbalimbali yenye manufaa katika biashara zao na hupewa kipaumbele wao na watoto wao (wakati mwingine hata wajukuu) katika nafasi mbalimbali za mafanikio.

Ukitaka kujua kama kweli mfumo wa kifisadi unanufaisha chama tawala, angalia wanachama wake wakuu wana mafanikio gani na jinsi gani wamepata mafanikio hayo, halafu sogea pande zote nne za huyo mwanasiasa na uone jinsi gani watu wa karibu yake nao walivyofanikiwa.

Katika Tanzania basi mfumo huu unanufaisha chama tawala; CCM. Mtu yoyote akitaka kunufaika na kufanikiwa pasipo shaka au kuvutia udadisi usio wa lazima ni lazima ahusiane kwa namna moja au nyingine na Chama cha Mapinduzi. Ukitaka mambo yako “yakunyokee” jiunge nacho; ukitaka usisumbuliwe sana naserikali yake toa michango ya hapa na pale; ukitaka ukumbukwe katika “ufalme” wao hakikisha hukosi unapoitwa na wakubwa wake.

Ukitaka wakutambue uwepo wako jioneshe kuwa ni “mkereketwa”. Nunua nguo kadhaa (na kofia) za kijani na manjano; wakishangilia “CCM, CCM” hakikisha sauti yako ni ya juu zaidi; hata kama unajua kuna madudu ndani ya chama hakikisha “hukichafui” chama bali laumu watu wengine na vitu vingine nje ya chama na ukitetea chama kwa mujibu wa Ibara ya 15:1 ya Katiba ya CCM.

Ukifanya hivyo na kujionesha mapenzi yako yasiyo na shaka kwa CCM basi jiandae kwa neema; jiandae kwa “wema na fadhili” kutoka CCM. Utafanya mambo yako kwa uhakika, utaendesha biashara zako bila kubughudhiwa sana, utawaona na kukutana na vigogo ambao watakufungulia milango ya ajabu ilimradi tu uendelee kutukuza chama tawala.

Na katika hilo utaona kuwa CCM itaendelea kutimiza lengo lake la kushinda uchaguzi na kushika serikali. Wataendelea kutunga na kusimamia sheria ambazo zinawahakikishia kuwa wao ndio watawala milele; hawatabadilisha muundo wa tume ya Uchaguzi ili iwe huru zaidi; hawatabadilisha sheria ya uchaguzi ili kuhakikisha nafasi sawa kwa vyama vyote, hawataruhusu wagombea binafsi, na kwa hakika kabisa watahakikisha kuwa Bunge halipati nguvu ya kuweza kutishia uwepo wa serikali yao madarakani. Itatengeneza mbinu na mikakati ya kushinda chaguzi mbalimbali, haijalishi wanafanya vipi au kwa namna gani. Watashirikiana na watumishi walioko serikalini katika kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa vizuri. Mtumishi yoyote atakayejaribu kuonekana yuko huru au anataka kutoipendelea CCM atapewa onyo lisilo na utata naye atanywea kama jani la mgomba lililokatwa na kutupwa nje katika jua la kiangazi.

WANAONUFAIKA KWA NJIA NYINGINE

Katika mfumo huu wapo wanufaika wengine wa ufisadi ambao kwao mfumo huu unawahakikishia maisha yao na hivyo hawana maslahi ya kuubomoa au kuuvunja vunja. Ni wanufaikaji wa pili wa mfumo wa utawala wa kifisadi na maslahi yao yamefungamana moja kwa moja na uwepo wa mfumo wa utawala wa kifisadi (MUK). Wanufaika hawa wa MUK ndio kwa namna moja wanachochea sana uwepo wa mfumo huu na ni kama mbolea ya kuurutubisha mfumo huo.

a. Wawekezaji wa Kimataifa

Hawa hujionesha kwa kuingiza makampuni ya kibepari ya kimataifa ambayo lengo lake kubwa ni kuchota raslimali kwa ajili ya makampuni yao mama huko kwao. Hawa hawaji kwenye nchi yoyote kirahisi rahisi; wanakuja baada ya kuhakikishiwa mambo kadhaa ambayo hutumika kama chambo cha kuyavutia makampuni haya. Mambo hayo katika Tanzania yamepewa jina la “mazingira ya kuvutia wawekezaji wa kimataifa”.

Sasa mazingira tunayowatengenezea hawa wawekezaji ambao miongoni mwao ni makuwadi wa ufisadi wa kimataifa ni yale ya kuwakaribisha kwenye raslimali zetu muhimu zaidi hasa madini, mafuta, maliasili na fedha. Ili waweze kuingia katika nchi kama ya kwetu tunatakiwa kufungua milango yetu, kuwahakikishia mambo kadha kadha wa kadha kama kusafirisha kwa asilimia mia moja faida wanayopata nchini, kutatua migogoro ya kibiashara katika nchi zao, uwezo wao wa kuajiri watu wa kwao hata katika nafasi kama za kwetu, na kuwahakikishia kuwa ije mvua au jua hatutataifisha au kuingilia kazi za makampuni yao nchini. Na wakati mwingine (kama walivyofanya Bulyanhulu, Buzwagi, Tarime, na sasa Loliondo-kama ilivyokuwa miaka ya tisini) wanataka tuwahakikishie kuwa tuko tayari kuwatimua wananchi wetu (kama nitakavyoonesha hapa chini) kutoka katika ardhi yao ili “kuwapisha wawekezaji”.

Hawa wanapoanza kuzalisha watatumia kila mwanya kutorosha mabilioni ya utajiri wa urithi wa watoto wetu kwenda kwenye nchi zao kujenga maisha ya watu wao kama walivyofanya wakati wa Ukoloni na wakati wa Utumwa. Kama vile makampuni ya watawala wa Kikoloni leo hii makampuni ya kimataifa kutoka kwa nchi zilizoendelea yanaendelea kufanya kitu kile kile nacho ni kupenya katika nchi maskini, kuwaahidi mbingu lakini kuwaacha wakiwa jehanamu.

Nchi yenye kutegemea MUK imejiambia katika fikra zake na kuamini kwa dhati kabisa kuwa bila ya kulegeza masharti na kufungua mlango kwa hawa wawekezaji basi nchi haiendi. Hivyo, kwa jina la “ubinafsishaji” Tanzania ikafungua mlango wake kwenye TTCL, Tanesco, Buhemba, NBC, Dawasco, ATCL, TRL, n.k na kuwakaribisha wageni kuendesha nchi kwa namna ya kushangaza. Na watawala wakithibitisha kuwa wao ni watumishi wazuri wa ufisadi hawafikirii njia nyingine ya kutatua matatizo haya isipokuwa kuendelea kupiga magoti mbele ya mafisadi wa kimataifa kama machangudoa mbele ya wateja wao.

b. Wafanyabiashara wakubwa

Wanufaika wengine wa MUK ni wafanyabiashara wakubwa ambao katika mazingira ya mfumo huu faida yao inahakikishwa. Wafanyabiashara hawa ndio ambao kwa kiasi kikubwa hujijengea utajiri mkubwa na wa haraka haraka wakiwa na uhakika wa usalama wao na wa mali zao. Wafanyabiashara wa aina hii kama wangekuwa na uwezo wangetaka nchi isiwe na sheria yoyote na vitu kama kodi, sheria za mazingira, haki za wafanyakazi n.k zisingekuwepo na wao wangeruhusiwa kufanya wanalotaka.

Lakini kutokana na kuelewa kuwa ufisadi ndio utawala wenyewe basi wafanyabiashara wa aina hii wanatumia mapengo mbalimbali ya kiutawala na kiungozi ambayo yamejitokeza kwa wao kupanua biashara zao mbalimbali na hata kujenga himaya za biashara.

Wanaponogewa na hili utaona kuwa wafanyabiashara hawa wanataka kunufaika mara mbili na hapo hujiingiza kwenye siasa na kuanza pia kushiriki katika kutunga sheria na kusimamia sheria ambazo zinagusa biashara zao. Matokeo yake utakuta wafanyabiashara wamegeuka wanasiasa na katika kofia zao mbili hizo wanauwezo wa kujua na kufanya lolote.

Ni kwa sababu hiyo basi utaona kuwa mahali penye MUK wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wamefungamana sana kama chanda na pete na wanategemeana sana kama vile mti na matawi yake. Mtu yeyote ambaye atajaribu kupendekeza mabadiliko yoyote yale atapata mapingamizi makubwa toka kwa wanasiasa na wafanyabiashara wa aina hii.

Ili kutuliza munkari wa watu wafanyabiashara hawa hujikuta wakimwaga misaada ya hapa na pale ili kupunguza maumivu kwa watu (hasa waathirika). Katika biashara zao watatumia mazingaombwe ya hapa na pale kuendelea kuvutia wateja huku wakichuma faida ambayo ikiangaliwa kwa karibu utaona ni kama kufuru. Lengo lao ni kutengeneza jina jema mbele ya jamii. Lakini hawa hawatapigia kelele mabadiliko ya kiutendaji au kisiasa kwani yaliyopo yanawafaa sana.

Katika MUK wafanyabiashara wakubwa hutengeneza utajiri wa kutisha kwa njia za mchoromchoro, ukwepaji kodi, uvunjaji mbalimbali wa sheria na wanayafanya yote haya wakati mwingine kwa kushirikiana na makuwadi wa ufisadi wa kimataifa (wawekezaji uchwara). Hawa wanasukumwa (kama mabepari wengine) na lengo la kupata faida kwa njia yoyote ile (by any means necessary).

Hata hivyo kundi la wanufaika wa mfumo wa utawala wa kifisadi mahali pote duniani ni dogo sana ukilinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo. Mara zote ni kikundi cha watu wachache lakini chenye nguvu kubwa ya kiuchumi, kisiasa na madaraka.

Vile vile lipo kundi la wanufaika wa mfumo wa ufisadi ambao naweza kuwaita ni machangudoa wa ufisadi. Hawa nimeandika makala inayojitegemea juu yao.

WAATHIRIKA WA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Pamoja na wanufaika wa ufisadi, katika mfumo huu dhalimu wapo waathirika wa mfumo wa ufisadi. Hawa ni wale ambao kutokana na uwepo wa mfumo wa ufisadi wanajikuta wakinyanyaswa katika nchi yao, wakipata kibarua cha ziada kupata nafasi ya kufanikiwa na mara zote huishi kama wahamiaji au wapangaji ambao hutegemea mara zote kupiga magoti na kuomba omba mbele ya wanufaika wa mfumo huu.

Kundi hili mara zote huombea wale wanufaika wa ufisadi watawakumbuka na kuwasaidia au kuwarahisishia kwa namna fulani kupata nafasi ya wao nao kufanikiwa. Kundi hili katika nchi zote duniani ni kubwa zaidi na huundwa na watawaliwa. Hawa ni ndio watu wengi zaidi katika nchi. Tuangalie baadhi ya makundi yanayojikuta yakiathirika katika mfumo huu wa kifisadi.

1. WAKULIMA

Hakuna waathirika wakubwa zaidi wa mfumo wa kifisadi kama wakulima. Hawa ambao ni wengi wanajikuta wanakabiliwa na athari kubwa za ufisadi kwa sababu kubwa tatu. Kwanza, bado wanatumia pembejeo na nguvu kazi ya kijima. Hutumia nguvu nyingi kuzalisha kitu kidogo na wengi wao bado hulima kilimo cha kujikimu (subsistence farming) na ni kile kidogo cha ziada ndio hutegemea kwa mauzo. Pili, wengi wao wako vijijini ambako miundo mbinu ya uhakika bado ni ya kijima. Bado wakulima wetu husafiri umbali mrefu, hutumia muda mwingi, na huhenyeka katika kuhakikisha kuwa mazao yao yana ubora na hatimaye kumfikia mlaji au mnunuzi. Tatu, wakulima wetu wengi bado hawana ufahamu na uelewa wa mahusiano mbalimbali ya siasa, uchumi, maisha, na kilimo chao. Bado wanawategemea wanasiasa kuwaambia nini cha kufanya na jinsi gani ya kukifanya. Matokeo yake wamekuwa wakijikuta wakirubuniwa, kuzugwa na mara kadha wa kadha kuvutiwa na maneno matamu na ahadi hewa.

Mahali pote duniani ambapo mfumo wa kifisadi umekomaa, wakulima hulisha mafisadi na huhimizwa kuzalisha zaidi lakini wakati huo huo kuwekwa nje ya mduara wa madaraka. Huombwa kura zao kila chaguzi zikifika, na husauliwa hadi uchaguzi mwingine. Hawana nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa siasa zao kwani hufanywa duni na watawala na kuoneshwa kuwa wao ni “washamba”. Tumefika mahali ukulima umekuwa ni kama kazi ya fedheha na aibu kiasi kwamba vijana wetu wengi sasa na hata watu wazima hujaribu kutafuta sababu ya kuachana na kilimo na kukimbilia mijini kutafuta shughuli nyingine mbadala ya kilimo.

2. WANAWAKE NA WATOTO

Waathirika wa kwanza wa mfumo huu wa kifisadi ni kundi la kina mama na watoto. Kundi hili linabeba athari za moja kwa moja za ufisadi kwanza kutokana na kutokuwa katika nafasi za juu ya madaraka, biashara, na mahali pa kufanya maamuzi ya kubadili mwelekeo wa taifa na pili kutokana na mfumo dume ambao umejenga utamaduni wa manyanyaso dhidi ya wanawake.

Hatuzungumzii wanawake “wote” kwamba wanapata athari za moja kwa moja kwani wapo wanawake ambao ni sehemu ya wale wanaonufaika na mfumo uliopo sasa; wanawake tunawaozungumzia kwanza ni wale kina mama wa kijijini ambao ndio nguvu kazi kubwa zaidi iliyopo nchini ambayo bado inatumia mbinu na zana za kizamani huku ikiwa imebebeshwa majukumu makubwa ya malezi ya familia.

Kundi hili halina wasomi wengi, na wale wachache waliopo wanajikuta wanaangukia kwenye kundi la tatu la matabaka yaliyopo kwenye MUK. Hili ni kundi la kina mama na kina dada ambao kutokana na matatizo mbalimbali hawakuweza kupata nafasi ya kuendelea na masomo, walijikuta wakianza maisha ya malezi ya watoto mapema, na wale ambao kutokana na tamaduni na mila za mahali walipo wanajikuta hawana sauti ya maamuzi ya mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao.

Japo kuna juhudi katika Tanzania ya kuwaongezea wanawake nguvu zaidi kama vile uanzishwaji wa vyama vya kukopa (SACCOS), benki ya wanawake, asasi mbalimbali n.k bado tunaweza kuona kuwa nguvu ya maamuzi (power to decide) inabakia mikononi mwa watu wachache ambao wengi wao bado wanaangukia katika kundi la wanufaika wa ufisadi. Kina mama hawa kama ilivyo sehemu nyingine zenye MUK huwa wanatulizwa na vitu mbalimbali vinavyowafanya watulie na wasiwe na muda kupiga kelele ya mabadiliko.

Athari zinazowakuta kina mama hawa ni ukosefu wa huduma bora na za kina za kijamii na kimaisha, kuendelea kuishi maisha duni ya kutumia muda mrefu wa siku kutafuta kuni, maji, na chakula, na vile vile kufuatilia maisha ya maendeleo ya familia. Kina mama kama hawa hata wale walioko mjini hujikuta hulazimika hata kujidhalilisha na kujifanya duni ili waweze kuokoa maisha ya familia zao na kutoa msaada wa kifamilia.

Watoto wao wanajikuta wanapata athari za ufisadi kwa sababu vitu vingi ambavyo vingeweza kufanywa na watoto katika kuwaandaa kwa maisha bora vimeachwa kufanywa au kufanywa kiuvivu na kwa uzembe. Nitolee mfano hali ya lishe (nutrition) kwa watoto wetu katika Tanzania katika nchi ambayo ina ubwelele wa nyama, maziwa, samaki, mboga, matunda, na nafaka nyingi tu.

Takwimu mbalimbali za hivi karibuni (angalia ripoti ya REPOA kuhusu lishe kwenye mwanakijiji.com sehemu ya vielelezo) zinaonesha kuwa asilimia 40 ya watoto wetu chini ya miaka mitano wamedumaa – urefu wao hauendeni na umri wao (stunted) na hiyo ni mojawapo ya ishara ya lishe ya kiwango cha chini; asilimia tatu wana uzito wa chini ukilinganisha na urefu wao – dalili ya utapiamlo wa hali ya juu, na karibu asilimia 22 ya watoto wetu wana uzito wa chini ukilinganisha na umri wao – ambayo ni dalili ya ukosefu wa lishe ya kutosha kwa muda mrefu. Takwimu hizo zinaonyesha pia kuwa kuna tofauti kubwa kati ya lishe ya watoto wa mjini na wa kijijini ambapo asilimia 26 ya watoto wa mjini wanaupungufu wa lishe na wamedumaa wakati kule vijijini ni asilimia 41.

Wakati haya tunayaangalia utashangaa kuona nchi yetu ina chakula cha kutosha cha kila aina. Miaka ya zamani tulikuwa na kampeni za “mtu ni afya”, “kuleni chakula bora”, n.k na tulifika mahali tukaweza hata kutoa maziwa kwenye shule zetu za chekechekea hata shule za msingi. Leo hii tukiuliza juu ya mlo kwa watoto wetu jibu la haraka litakuwa ni “hatuna fedha” au “tunatafuta wafadhili”.

Ipo na mifano mingine ya takwimu za afya na masuala mengine ya jamii ambazo zinaonesha jinsi gani watoto wetu wanalipa gharama kubwa ya vitendo vya kifisadi. Matokeo yake huwa tunashangazwa inakuwaje watoto wetu hawafaulu vizuri darasani, na wanafanya vibaya kwenye mitihani tumeshindwa kuoanisha hali ya lishe na ukuaji wa kiakili (cognitive development). Tunafikiri yote haya yanatokea katika ombwe!

3. VIJANA

Mojawapo ya waathirika wakubwa wa mfumo huu ni vijana. Kundi hili lina vijana wa kati ya miaka 18 na 35 na ambao kutokana na sababu mbalimbali wamekosa nafasi ya kujiendeleza kielimu au kuwa katika mazingira ya kupata mafunzo rasmi na hivyo kulazimika kuishi kwa “kujishughulisha” katika kile ambacho kimebatizwa jina la “ajira zisizo rasmi” a.k.a kubangaiza na kuhangaika. Kundi hili la vijana wanatumia nguvu nyingi ya mwili kufanya vitu ambavyo vingetumia mbinu rahisi au utaalamu rahisi, na wakati mwingine wanajikuta wanatumia nguvu zaidi za misulu kuliko za ubongo katika maisha yao.

Hawa (ambao wengine utotoni hawakupata milo mizuri) wanajikuta wamekua kimwili lakini kiakili na kifahamu bado ni watu wa kusukumwa na hisia au nawatu wanaojiita “wataalamu”. Kundi hili ni kundi ambalo ni hatari kwenye taifa lolote lenye mfumo wa utawala wa kifisadi. Kundi hili halihitaji kushawishiwa kuona ubovu wa maisha yao; wanaoishi maisha hayo. Kundi hili haliitaji kuhubiriwa juu ya kile kilicho bora; wanakiona kwa wengine.

Matokeo yake utaona kuwa kundi hili halitoi mchango unaostahili katika kujenga taifa kwani hakuna mtu ambaye anaamini kwa dhati kuwa linamchango; matokeo yake limebakia kuwa ni kundi kubwa lililo nje ya madaraka na nje ya mfumo wa maisha ya kawaida. Mamilioni ya vijana wetu wanajikuta wakizunguka kila kukicha wakitafuta nafasi katika maisha yao. Na mambo yanakuwa mabaya zaidi pale kundi hili linapoanza kuona watawala wanaendelea kujenga mbingu zao hapa hapa duniani huku wao wakiendelea kuwa kituko katika mitaa yao na maeneo yao.

Baadhi yao hulazimika kuanza kuishi maisha ya kujidhalilisha na uhalifu; wanageukia wizi, ubakaji, na uporaji na wengine hasa kina dada hujiingiza katika biashara ya ngono kama hatua za mwisho za kusalimisha utu wao na hadhi yao kama binadamu.

Vijana ndio wanabeba uzito mkubwa wa athari ya utawala wa kifisadi kwani ni hawa ambao wanajikuta wamesukumwa nje ya malango ya mafanikio, na kama ombaomba wanalazimika kukinga mikono yao ili kuweza kupata nafasi ya kula matunda ya urithi wa taifa lao.

4. WENYE KIPATO NA ELIMU YA CHINI

Wananchi wenye kipato cha chini ambao wana elimu duni hujikuta wakiathirika zaidi na ufisadi kwani hawa njozi yao ya maisha ya manufaa na yenye unafuu inabakia katika vichwa vyao lakini isiyotimilika. Hawa hujikuta wakiwa kama abiria wanaoenda uwanja wa ndege kuangalia ndege za walionufaika zikipaa huko wao wameachwa wameduwaa. Hubakia kuambizana tu kuwa “siku moja nikipata nauli na mimi nitaruka”.

Mfumo wa ufisadi huwatengenezea mazingira ya kuwatuliza kwa kuwapa ajira ndogo ndogo, misaada ya hapa na pale na kuwaahidi mema huko mbeleni. Hawa hujikuta wakiambiwa kila siku na watawala kuwa wafanye kazi “kwa bidii na maarifa” bila ya kujiuliza kuwa ulimwengu wa leo kazi hufanywa kwa akili, utaalamu, na weledi wa hali ya juu na maarifa ambayo hubadilika kila kukicha. Matokeo yake kundi hili hujaribu kujiendeleza kwa fani mbalimbali na ujuzi wa aina tofauti lakini wakiamka asubuhi hujikuta wako katika hali ile ile.

WANUSURIKA WA MFUMO WA UFISADI

Vile vile lipo kundi la wanusurika wa MUK. Kundi hili linawajumuisha wale wote ambao kutokana na nafasi zao wanajua madhara ya ufisadi, uovu wa mfumo wa kifisadi na wanajua kabisa kuwa nini kinapaswa kufanyika. Kundi hili linawajumuisha watu ambao wanauwezo wa kubadilisha mambo lakini kutokana na kujikuta wakiwa wananufaika vile vile na mfumo huo hujikuta wakifanya kazi ndani yake kwa manung’uniko na kukerwa nao lakini hawawezi kuuacha kwani kwa kufanya hivyo watajikuta kuwa ni waathirika.

Hawa hawataki kuonekana ni mafisadi na huwabeza mafisadi sirini (siyo hadharani); lakini hawawezi kutoka kwenye mfumo huo wa kifisadi kwani na wao ni wanufaika aidha kutokana na ajira zao, nafasi zao za kisiasa, biashara au mahusiano yao ya karibu na watawala. Wanusurika wa ufisadi ni majeruhi wa mfumo huo lakini wasiopona. Baadhi ya wanusurika wa ufisadi wako katika makundi yafuatayo.

1. WATUMISHI WA UMMA

Hawa ni watumishi ambao wanauona kila kukicha mfumo wa ufisadi ukifanya kazi; ni wao ndio kwa namna ya pekee wanatumika pasipo matakwa yao kuundeleza mfumo huu. Ni hawa ambao kutokana na nafasi zao hutekeleza maagizo na maelekezo mbalimbali hata wakijua kuwa yana matokeo maovu kwa “waathirika”; badala ya kupinga au kuyafichua mambo hayo hujikuta wakikubali (hata kama kwa shingo upande) kupitisha sera, kutekeleza maamuzi ambayo kwa kweli wanajua mioyoni mwao kuwa si yenye maslahi kwa taifa au kwa wananchi moja kwa moja.

Ndio hawa ambao tumeona mambo yao kwenye kashfa za BoT, ni hawa tumewaona kwenye kashfa za ATCL, TRL, Tanesco na kwingine. Hawawezi kuachia nafasi zao kwani ukiwauliza watasema “sasa mimi nile wapi?”

Kwa vile wanajua madudu yanayofanywa na vikaragosi vya ufisadi (mabosi wao) basi hujikuta na wenyewe kutumia nafasi hizo hizo na wao kula. Huandaa visemina uchwara, mikutano ya “tathmini” na kozi za “kujiendeleza” ambazo wakati mwingine hurudiwa kwa jina jingine na kwenye hoteli nyingine. Hujikatia posho za kila namna ilimradi waweza kufuja fedha za umma bila kumuogopa yoyote.

Lakini ni hawa hawa upande mwingine wanachukizwa na vitendo vya ufisadi mkubwa na ndio wamekuwa wa kwanza vile vile kufichua ufisadi mkubwa katika taasisi zao kwani wanajua kabisa na kwa undani mambo yanayofanywa na makuwadi wa ufisadi wenyewe. Katika mikutano mbalimbali na pembeni hulalamika sana juu ya vitendo vya rushwa na milungula ya aina mbalimbali, lakini wakati huo huo na wenyewe hujikuta kupokea au kukubali vitu hivyo ili “maisha” yaende mbele. Hawa kama ingepatikana jinsi ya kuondoa rushwa na kunufaisha maisha yao kihalali wangeachana na vitendo vya kifisadi kwani baadhi yao wanaporudi nyumbani ni watu wa imani, na maadili lakini wanapokuwa kazini au maofisini hujihusisha na vitendo hivyo kwa kisingizio kuwa “kila mtu anafanya hivyo”.

2. VYOMBO VYA HABARI

Kama kuna kitu ambacho ninakielewa vizuri sasa hivi zaidi kuliko miaka karibu minne iliyopita ni kuwa vyombo vya habari vinanufaika na ufisadi lakini kwa namna ya kunusurika. Vyombo hivi hujionesha kuwa vinapigana na ufisadi na vinaandika sana habari ya ufisadi; tatizo ni kuwa ili viendelee kuwepo vinategemea mafisadi hao hao!

Hivyo, utaona baadhi ya magazeti hata ambayo husifiwa kwa kupiga vita ufisadi hutegemea matangazo ya biashara kutoka kwa watawala na wakati mwingine huenda kubembeleza kwa watawala hao hao ili “walete” matangazo kwenye magazeti au vyombo hivyo vya habari. Na watawala wanajua udhaifu huu. Kuna wakati watawala huamua kuvisusia vyombo kadhaa vya habari kwa sababu vinaziandika wizara, idara au vyombo Fulani vibaya na hivyo hawapeleki matangazo yao mbalimbali huko.

Na cha kusikitisha zaidi ni kuwa watawala wale wale ambao ndio wanufaika wa ufisadi wamekamata vile vile vyombo vya habari huku wengine wakiwa na maslahi ya wazi kabisa katika vyombo hivyo. Hawa huajiri waandishi wa habari kufanya kazi ya habari lakini wakati huo huo hupeleka matangazo ya idara, wizara au serikali kwenye vyombo vyao bila ya kutangaza maslahi (without declaring interest).

Sasa, utaona kuwa vyombo vya habari vinanufaika pia kwa namna nyingine; kwa kuandika habari kwa hisia na wakati mwingine kwa kama kuchonganisha. Magazeti haya hupata wasomaji wengi wenye hamu na kiu ya kujua mambo mengi. Mfano mzuri wa jinsi gani magazeti yanacheza mchezo huu ni katika sakata la Mengi na Rostam, na suala la Mwakyembe na Mwakipesile, n.k Ni jambo moja kutoa habari na kuburudisha watu lakini ni jambo jingine kabisa kuchochea ugomvi na wakati huo huo kutengeneza fedha.

Inakuwa kama watu wanaochonganisha watu huku wao wakikaa pembeni kusubiri nani ashinde ili wawe upande wake na waendelee kumchuna.

Vyombo vimenusurika kwa sababu, baadhi yake vingeweza kuendeshwa kwa biashara ya kuuza magazeti na mambo mengine vingekuwa kweli huru na vingependa kuwa hivyo lakini kutokana na ukweli kuwa bado serikali ndiyo yenye biashara kubwa kwenye vyombo hivyo basi vyombo hivyo vya habari hujikuta vinapiga magozi na kucheza ngoma ya mafisadi.

3. TAASISI ZA KIDINI

Kwa muda mrefu taasisi za kidini zimeweza kukua na kunufaishwa sana na mfumo wa kifisadi. Nilipoandika barua yangu ya kwanza kwa wachungaji na makala zilizofuatia baadaye zilikuwa na lengo la kuamsha kundi hili ili watoke katika kile nilichokiita wakati ule “kitanda cha ufisadi” ambao viongozi wetu wa dini na wanasiasa wamelala huku wakijifunika blanketi moja. Kwa muda mrefu viongozi wetu wa dini hawakuwa tayari kuunyoshea mkono utawala wa kifisadi zaidi ya kukiri uwepo wa vitendo vya rushwa na uvunjaji wa sheria wa hapa na pale. Lakini wakati huo huo viongozi hao wa dini na taasisi zao walijua kabisa wakitaka baadhi ya mipango na miradi yao ifanikiwe hawana budi kuimba nyimbo za watawala.

Katika siku za karibuni tumeanza kuona mwamko wa aina yake ambapo viongozi wa dini wakiwa kama watu waliochelewa stesheni ya garimoshi wameanza kudandia mjadala dhidi ya ufisadi kwa namna ya pekee zaidi; kuuita uovu huo kwa jina lake mbele ya watawala.

Jawabu la watawala tuliliona kwenye jaribio la kujaribu kutishia mapato na shughuli za taasisi hizo za kidini katika mapendekezo ya kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini isipokuwa kwa mambo ya ibada. Ile ilikuwa ni kama onyo na sitoshangaa huko mbeleni watawala wakaamua kufanya kweli na hivyo kutishia taasisi hizo za dini kukaa pembeni ya mambo ya siasa.

Pamoja na hilo bado taasisi na viongozi wa kidini hawajaacha kunufaika kwa namna moja au nyingine na mfumo huu wa ufisadi. Ili miradi yao, makanisa, misikiti, mashule na mahospitali yao yafanikiwe na misaada yao isipate shida bandarini ni lazima wawe tayari kula “sahani moja” na watawala.

Lakini viongozi hawa hawa hujikuta wanalazimishwa na ukweli wa mambo kukemea ufisadi hadharani na kuukataa. Lakini jambo moja ambalo hawawezi kulifanya ni kupambana na ufisadi hadharani; hawatoandamana kupinga mafisadi, hawatokataa kuwapigia magoti watawala, na kamwe katika MUK usitarajie viongozi wa dini kuchukua msimamo mkali unaoambatana na vitendo vya kiupingaji ambavyo vina lengo la kuamsha dhamira ya wananchi.

Taasisi hizi za kidini nazo zimenusurika na ufisadi lakini pia zinanufaika na uwepo wake.

4. ASASI MBALIMBALI

Mojawapo ya wanusurika wa ufisadi ni asasi mbalimbali za kijamii. Hizi leo hii zimegeuzwa kuwa mitaji ya kujitengenezea utajiri wa haraka haraka kwa kutumia visingizio vya kutoa misaada au kusaidia jamii. Hivyo, haishangazi kuona kuwa wanufaika wa ufisadi na wao wenyewe wameanzisha asasi zao mbalimbali ambazo zinapokea misaada mbalimbali kama makanisa lakini hizi haziongozwi na imani (japo nyingine ni za kidini); zinaongozwa na kile kinachodhaniwa kuwa ni huruma kwa watu.

Sizijumuishi asasi zote za makanisa au viongozi wote wa dini na kuwaweka kwenye kundi la wasio wa kweli na wenye malengo zaidi ya yale yaliyomo kwenye asasi zao; nazungumzia wale ambao kama wanasiasa waliopotoka au polisi waliopotoka wamejikuta wakitumia nafasi ya uwepo na ukomavu wa mfumo wa kifisadi kujenga na kujijenga wao wenyewe wakitumia shida na mahangaiko ya watu wengine.

Hawa huwa na urafiki wa karibu na wanufaika wa ufisadi na utakuta wakijitangaza aidha kupitia makampuni yao au asasi zao wakigawa misaada ya kila aina na kutoa misaada wakati wa sherehe za kidini na matukio mbalimbali. Lengo lao ni kujenga jina “jema” la asasi, mashirika au makampuni yao mbele ya wananchi na mbele ya watawala. Lakini, wakati huo huo wanatumia kila aina ya ujanja kutumia misaada vibaya na kwa maslahi yao wenyewe nje ya yale ya watu wanaosema wako tayari kuwasaidia.

NI MFUMO WA HATARI

Mfumo huu kwa kila kipimo ni mfumo ambao hatuwezi kuuvumilia, kuuendeleza, wala kuutafutia udhuru wa uwepo wake. Ni mfumo ambao hauna budi kubomolewa na kuvunjwa vunjwa na kutupwa katika shimo la usahaulifu la historia. Ni mfumo ambao hudumaza jamii kubwa huku ukinufaisha kikundi cha watu wachache ambao kutokana na nguvu zao za kisiasa na kiuchumi huharibu hata nafasi ya utawala wa sheria.

Kimsingi kabisa mfumo huu haupatani (incompatible), hauwezi kupatana sasa na hata milele na utawala wa kidemokrasia hauwezi kushikana na utawala wa sheria na kamwe hauwezi kuwa sehemu moja na jamii ya watu walio huru na sawa. Ni mfumo ambao huinua katika jamii tishio kubwa zaidi la mafanikio ya taifa na wananchi, ukiahidi uongo huku ukibeza ukweli, ukigeuza udhalimu kuwa haki na uonevu kuwa maelewano.
Ukweli huo unanifanya niamini kuwa mfumo huu hauwezi kuvunjwa majukwaani, kwa kusoma magazetini au kwa kulumbana mitaani. Mfumo huu hauwezi kuvunjwa na kuharibiwa kwa kuandika na kujadiliana kwenye mitandao ya intaneti au kwa kutumiana barua pepe kusimuliana kilichojiri.

Mfumo wa aina hii huangushwa kisayansi na kitaalamu kwa kutumia nguvu za kisiasa na mikakati yenye matokeo mema. Hauwezi kuangushwa kwa kusubiri bahati itokee. Tutaendelea kuangalia mbele katika masomo mengine zaidi ya huu mfumo.

Thursday, November 19, 2009

Wabunge wamshangaa Rostam

• Kimaro asema anaweweseka kutaka Dowans inunuliwe

na Deogratius Temba

KAULI aliyoitoa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), akiliomba Bunge liunde kamati huru kuchunguza upya sakata la kuhusika kwake na Kampuni ya Richmond Development LLC ili apate nafasi ya kusikilizwa, imewatibua baadhi ya wabunge wa chama chake.

Wabunge hao walisema Rostam anaweweseka na kashfa ya Richmond, na kumtaka akasome vizuri kanuni za Bunge ili ajue kwamba suala likishaamuliwa na Bunge, haliwezi kuundiwa tume nyingine nje ya Bunge.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, James Lembeli (Kahama) na Lucas Selelii (Nzega), walisema Bunge likishahitimisha hoja, haliwezi kurudi nyuma kuijadili upya, na kwamba Rostam anapaswa kufuata kanuni za Bunge.

Kimaro alisema hakuna sheria wala kanuni ya Bunge inayotamka kuwa kamati teule ya Bunge ikifanya kazi yake na Bunge likaridhia, inaweza kuundiwa tena kamati nyingine nje ya Bunge.
“Bunge limeshamaliza kazi yake, hakuna cha kurudia hapo, wala kanuni za Bunge haziruhusu kufanya vile, nafikiri hajakisoma kitabu cha kanuni za Bunge ndiyo maana anaweweseka, vinginevyo asingesema hayo.

“Ninawashauri Watanzania kutojiingiza katika mjadala huo, umeshafungwa na Bunge likatoa mapendekezo yake, na sasa tunaisubiri serikali itekeleze na si mtu mwingine aje tena bungeni kuleta hoja hiyo hiyo, hapana sisi tunapiga hatua nyingine mbele,” alisema.

Alisema kama kuna watu hawakuridhika na kazi iliyofanywa na kamati teule ya Bunge iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, wasifikiri kuwa kuna huruma tena au wakipiga kelele watapata msamaha.

“Tena wasifikiri kuwa kwa kupiga kelele vile serikali inaweza kuifikiria tena Dowans, hilo limepita na serikali haitainunua mitambo hiyo kwani hata sheria hairuhusu. Sheria ya umeme ya mwaka 2008, imeeleza waziwazi kuwa kama kuna watu waliohusika kudai ‘capacity charge’ wasipewe nafasi ya kuiuzia TANESCO umeme,” alisema Kimaro.

Alidai kuwa, kinachomsumbua Rostam hadi kufikia kuliomba Bunge liunde kamati upya, ni kutaka mitambo ya Dowans inunuliwe.

“Mimi ninataka kujua kinachomkera au kinachomfanya aweweseke ni nini? Awaeleze Watanzania waelewe, atumie muda huu kuueleza umma kama ana maslahi gani na Dowans au iliyokuwa Kampuni ya Richmond na si kulitakia Bunge kazi ambayo si yake,” aliongeza Kimaro.
Naye Lembeli, alisema Bunge ni kwa ajili ya Watanzania wote na maamuzi yaliyotoka ni ya wote.
Alisema Rostam hajaonewa na kamati kwani ilitoa ripoti na wabunge wote wa CCM wakaiunga mkono kwa pamoja, kwa hiyo ilifanya kazi yake.

“Tatizo si kuonewa wala kamati teule ya Bunge, Rostam atafute kanuni za Bunge azisome na aelewe zinasemaje, kwanza asiionee kamati, sisi wabunge ndio tuliopitisha ripoti, kama tungeona ina makosa na kubaini kuna mtu ameonewa, tungeikataa.

“Anapotumia muda mwingi kudai kuwa iundwe kamati upya, mara jopo la majaji kuchunguza upya, mbona alishajitokeza mara kadhaa kwenye vyombo vya habari akadai kuwa hausiki? Kwani hilo halitoshi? Mbona maelezo anayoyatoa kwenye magazeti kuwa hakuhusika hayaelezi kama alionewa? Na alionewa wapi?” anahoji Lembeli.

Akizungumzia suala hilo, Selelii, ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo teule, alisema ndoto za Rostam ni za mchana na hazitekelezeki katika Bunge hili na kwa kutumia kanuni hizi za Bunge zilizopo.

“Hizo ni ndoto, tena za mchana, hakuna kitu kama hicho, Bunge lilishafanya kazi yake na kuimaliza, anachokitaka yeye hakiwezekani kwa Bunge la Tanzania, na kama ni kwa Bunge la hapa Tanzania basi si kwa kanuni hizi tulizonazo,” alisema.

Alisisitiza kuwa, siku zote mtu anayetuhumiwa kwa kukosa, hawezi kukubali kosa hata kama atachapwa namna gani, kwa hiyo huo ni ujanja ambao unatumika kujinasua na tuhuma hizo.
Selelii alimtaka Rostam achukue ripoti ya kamati hiyo, aangalie vipengele vyote vinavyomtaja kuwa anahusika na Richmond na Dowans, halafu aende kwenye hoja bila kuzunguka.

“Kama kweli Rostam ana uhakika na hayo malalamiko ambayo anayatoa kila mara na hata kupitia baadhi ya vyombo vya habari, arejee kwenye ripoti yetu ya kamati, asome maeneo yote yanayomgusa na kumhusisha na Richmond na Dowans, halafu ajenge hoja,” alisema Selelii.

Hivi karibuni, Rostam alikaririwa na chombo kimoja cha habari akiliomba Bunge liunde jopo la majaji watatu kuchunguza upya sakata hilo ili kutoa hukumu ya haki.

Siku chache baada ya Rostam kuomba Bunge liunde jopo hilo la majaji, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisisitiza kuwa haiingii akilini, kwa mbunge huyo kutaka uchunguzi wa suala hilo ufanywe na majaji, na juzi mbunge huyo wa Igunga alirejea tena ombi lake la kutaka iundwe tume huru.

“Kwanza, labda nikwambie tu, maamuzi yaliyofikiwa na Bunge katika Richmond hayawezi kuchunguzwa upya na mhimili mwingine wowote wa dola.

“Tunazungumzia kumaliza suala la Richmond si kuanza upya, kama ana pesa zake (Rostam) za kulipa majaji, ni huko huko, lakini hilo haliwezekani,” alisema Sitta.

Alisema ushahidi mbalimbali ulionyesha uhusiano wa mawasiliano ya mbunge huyo na Richmond kisha Dowans.

“Hivi mnataka ushahidi upi zaidi? Ushahidi wa mawasiliano ulionyesha jinsi mtu huyu alivyokuwa akiratibu Richmond kisha Dowans,” aliongeza Spika.

Rostam, mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, amekuwa akitajwa kama mmoja wa vigogo walioshiriki katika kufanikisha Richmond kupewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura katika mazingira tata.

Mkataba na kampuni hiyo yenye taarifa tata kutoka Costa Rica na Marekani, ulisainiwa na TANESCO Juni 23, 2006.

Lakini baada ya kusakamwa kwa muda mrefu, alipopata nafasi katika kikao cha Kamati ya Mzee Mwinyi na wabunge wa CCM, iliripotiwa kuwa Rostam aliongelea kuundwa kwa tume huru kuchunguza kashfa nzima ya Richmond kwa madai ile ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Mwakyembe, ilipotosha.

“Ripoti ya Richmond imeidhalilisha serikali kwa maslahi ya kisiasa. Ili mambo yaishe ni vema uchunguzi huru ukafanyika. Tusipofanya hivyo tutaendelea kuwachanganya wananchi.

“Msimamo wangu tangu kamati teule ya Bunge itoe taarifa yake bungeni, uko pale pale. Ripoti ilijaa upotoshaji na uongo. Nilitaka kuongea bungeni nikazuiwa,” alisema Rostam.

Kamati hiyo teule ilisema katika taarifa yake kuwa, Rostam aliitwa ili aeleze uhusiano wake na Richmond kutokana na kampuni hiyo kutumia anuani ya barua pepe na fax ya Kampuni Caspian na sababu za kuitafutia Richmond kampuni ya ushauri wa mambo ya habari, lakini hakujitokeza.

Rostam alijieleza katika mchango wake wa maandishi wakati wa kujadili ripoti ya Richmond kuwa, Kamati ya Mwakyembe ilimuita kumhoji Desemba 24, mwaka jana wakati ikijua kuwa siku hiyo asingeweza kupatikana kwa sababu ya sikukuu.

Ndege ya Rais wa Tanzania


Ndege ya Rais aina ya Gulfstream 550

Hizi ndio details za gulf stream 550,
Developing nation:
United States of America
Manufacturer/designer:
Gulfstream Aerospace Corporation.
Production line:
Savannah, GA USA.
Type aircraft:
long-range business jet .
First flight:
August 31, 2001.
First delivery:
2003.
Gulfstream G550
Cockpit crew:
2.
Passengers:
14 – 18.
Cabin length:
15,27 m.
Cabin diameter:
2,24 m.
Cabin height:
1,88 m.
Cabin volume:
47,3 m³.
Baggage compartment:
6,4 m³.
Wing span:
28,50 m.
Fuselage length:
29,39 m.
Height:
7,87 m.
Engines:
two Rolls Royce BR710 C4-11 each rated 68.4 kN.
Weight:
- basic operating weight with 4 crew: 21.909 Kg.
- max. zero
-fuel weight: 24.721 Kg.- fuel: 18.733 kg.
- max. payload: 2.812 Kg.
Max. take off weight:
41.277 Kg.
Max. landing weight:
34.156 Kg.
Cruise speed:
946 km/h.
Service ceiling:
12.497 m.
Max. ceiling:
15.545 m.
Max. range:
12.501 km.
Performance:
- take-off run 1.800 m at max. take-off weight.
- landing run 844 m at max. landing weight.

Nadhani kuna umuhimu wa kufahamu haya.

Wednesday, November 18, 2009

KUUELEWA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Na. M. M. Mwanakijiji

Maadui wa Tanzania siyo Rostam, Lowassa, Chenge, Mramba, Yona au mtu yeyote ambaye ameonakana na kutajwa kuwa ni fisadi au kuhusishwa na kashfa za kifisadi. Hawa wote na wengine wengi ambao nimewabatiza majina ya “makuwadi wa ufisadi” na “vikaragosi vya ufisadi” ni matokeo tu ya yule adui yetu namba moja ambaye bila ya kumshughulikia basi juhudi zote za kupigana na “ufisadi” zitakuwa ni kama juhudi za anayezama majini huku kwa hasira akiyapiga ngumi maji hayo ili “kuyakomoa”. Ni zoezi lisilo na tija.

Anayepigana vita dhidi ya ufisadi (awe ndani ya CCM au nje yake) akifikiria kuwa anapigana dhidi ya watu “fulani” basi hajajua uzito wa vita hii iliyo mbele yetu; vita ambayo hatukuitafuta bali tumejikuta tunalazimika kuipigana kwani imeletwa kwetu bila kumchokoza mtu na haitaondoka isipokuwa kwa kuishinda tu.

Tukijifunza katika vita ya Kagera tunaweza kuona kuwa lingekuwa kosa kubwa sana kwa wapiganaji wetu kuwaadhibu wanajeshi wa UPDF (Jeshi la Wananchi wa Uganda) tukifikiria kuwa wao ndio walikuwa adui zetu. Tunaelewa kwamba wanajeshi wale walikuwa wanatekeleza amri ya vita toka kwa amiri Jeshi Mkuu wao wa wakati ule Idi Amin Dada. Sasa kama tungepigana ili kushinda wapiganaji wa Uganda kwenye jukwaa la vita halafu basi tungechekwa na jumuiya ya kimataifa kwa kutokuelewa tulipigana dhidi ya nani hasa.

Adui yetu wakati ule ulikuwa ni utawala wa Nduli Idi Amin na mfumo mzima wa utawala wake uliosababisha sisi twende vitani licha ya juhudi zote za kuepuka vita kuchukuliwa na kushindikana. Ndio sababu wakati wa tangazo la vita kwa Taifa letu Baba wa Taifa aliweka lengo lililokuwa wazi kabisa, kuyarudisha majeshi ya Amin toka ardhi yetu (kama kuwarudisha nyuma makuwadi wa ufisadi), kumkata makali Amin kabisa asiweze kuthubutu kutuvamia na kuwa tishio kwetu tena.(kama kuwakata makali mafisadi wasipate nafasi za kuchukua pesa zetu).

Katika hilo lengo la pili vikosi vyetu vilipewa jukumu la kuhakikisha vinammaliza kabisa adui na kuhakikisha kuwa habakii tena madarakani. Hivyo, tunajifunza kutoka vita vya Uganda kuwa haikutosha kumrudisha adui nyuma au kuyatoa majeshi yake toka ardhi yetu; ilitupasa kuhakikisha kuwa adui hapati tena nafasi ya kuthubutu kutishia mpaka wetu na hivyo licha ya kuingia Uganda hadi Kampala, vikosi vyetu vilisonga mbele hadi Jinja na Entebbe na kusababisha Idi Amin kuachia ngazi na kukimbia taifa lake kwa aibu.

Vikosi vyetu havikuondoka Uganda mara tu baada ya Amin kutoroka bali baadhi ya wapiganaji wetu walibakia Uganda kusaidia katika ujenzi wa taifa hilo na hasa ujenzi wa jeshi jipya lisilokuwa tishio kwa majirani zake kwa kutoa mafunzo na kulinda amani wakati jeshi la Uganda linapangwa upya.

Vita ya ufisadi nayo ni vivyo hivyo. Wale tunaowaita mafisadi, makuwadi wa ufisadi, vikaragosi vya ufisadi ni watumishi wanaofaidika na mfumo wa utawala wa kifisadi. Ndugu zangu, adui nambari moja wa maendeleo na mafanikio ya Watanzania ni mfumo haramu uliotengenezwa na utawala wa kifisadi. Ni lazima kwa mpiganaji yeyote kuelewa mfumo huu unavyofanya kazi kwani wale wote tunaowaita mafisadi leo hii ni matokeo ya mfumo huu wa kiutawala; mfumo ambao ni mchanganyiko wa mifumo midogo midogo ya kisiasa, kiuchumi, na kisheria ambayo msingi wake ni ubinafsi, kutokuwajibika, kulindana, utawala wa hofu, kubebana na kuvumiliana kwa kadiri ya kwamba wanufaikaji ni kikundi cha watu wachache walio katika utawala na wale wanaohusiana nao kwa karibu.


Mfumo wa utawala wa kifisadi ni nini basi?
Ni muungano wa utendaji kazi wa mifumo ya kisiasa, uchumi, na kisheria ambao msingi wake ni kujitajirisha kwa haraka haraka pasipo kuogopa matokeo yake. Mfumo wa kifisadi unahusiana moja kwa moja na utajiri wa “haraka haraka” ambao unafanywa kwa kulainisha utendaji kazi wa vyombo mbalimbali vya dola vyote vikitengeneza kama mwamvuli mkubwa kwa watawala. Lengo kubwa la mfumo huo ni kuwalinda watawala.

“Mfumo” ni nini hasa?
Mfumo yaani “system” kwa kiingereza unaweza kuelezewa kama muunganiko wa michakato, kanuni, shughuli mbalimbali vikifanya kazi kwa pamoja kufikia lengo moja. Neno “system” linatokana na neon la Kigiriki “systema” yaani “kuleta pamoja”. Ndani ya mfumo mmoja mkubwa unaoweza kuzaa mifumo mingine midogo midogo ikifanya kazi mahsusi lakini yote ikitekeleza lengo moja kubwa.

Mfano mzuri hapa ni wa kutumia motokari (gari). Lengo kubwa la gari ni uwezo wake wa kuendeshwa. Hivyo, ukiona gari linakwenda basi unajua kuwa lengo lake limefanikiwa na wakati wowote ukiona gari linazimika zimika au kukwama kwama basi unajua kuna tatizo fulani. Mafundi wa magari wanapoletewa gari bovu wanauliza tatizo nini au dalili gani dereva aliziona. Katika kufanya hivyo fundi-gari anaanza kufikilia ni mfumo gani mdogo (sub-system) wenye tatizo.

Ataangalia mafuta ya breki, mafuta ya injini, maji ya kupoozea, oili n.k na kama gari haliwaki kabisa likiwaswa basi ataangalia kama stata bado inafanya kazi, betri kama bado ina nguvu n.k Ni katika kuiangalia hii mifumo midogo midogo ndivyo anaweza kugundua tatizo na kulishughulikia na hatimaye kulirudisha gari barabarani.

Mfano mwingine mzuri ni wa kuelewa mfumo wa mwanadamu. Mwanadamu ameumbwa akiwa na mifumo mikubwa mikubwa na mingine midogo midogo lakini yote ikifanya kazi kuhakikisha mtu huyo ni hai na anaishi kwa afya. Wengi tunaifahamu mifumo ile mikubwa ya mwili kama Mfumo wa Fahamu (nervous system), mfumo wa chakula (digestive system), mfumo wa Uzazi (Reproductive System), mfumo wa utoaji uchafu mwilini, mfumo wa pumzi, na mfumo wa damu. Ndani ya mifumo hii mikubwa ipo mifumo mingine midogo midogo na yote hii ikifanya kazi “kwa pamoja” inafikia lengo la kutufanya tuwe na afya na kuendelea kuishi.

Kunapotokea tatizo kwenye mfumo wowote kati ya hiyo mtu atajikuta ni mgonjwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia leo hii kunawezesha baadhi ya mifumo kusaidiwa kufanya kazi na mashine mbalimbali.

Madaktari wote na wauguzi na wataalamu mbalimbali wa tiba wanajifunza juu ya mifumo hii na ile mingine na kwa kadiri ya taaluma zao wengine wanajikuta wanasomea zaidi utendaji kazi wa mfumo mmoja maalum na kuwa mabingwa wa eneo hilo. Vivyo hivyo wataalamu wa magari wapo ambao wamekubuhu katika mambo ya umeme wa magari na wengine katika injini n.k

Katika haya yote, mifumo hii inaangaliwa kwa ukaribu wake na ni msingi wa kuelewa utendaji kazi wa gari, kiumbe au kitu chochote kinachohusisha mfumo zaidi ya mmoja. Ni kwa sababu hiyo basi ni muhimu kuelewa kuwa mfumo wa utawala wa kifisadi huundwa na utendaji kazi wa mifumo mikubwa mitatu ambayo ndiyo huwezesha mfumo huo kufanya kazi yake ya kukitengenezea kikundi cha watu wachache utajiri wa haraka haraka bila kuogopa matokeo yake. Kimsingi kabisa, mfumo wa utawala wa kifisadi umejengwa ili kunyonya na kukandamiza.

Ni mifumo ipi inayounda mfumo huu?
Kama nilivyodokeza hapo juu mfumo wa utawala wa kifisadi huundwa na utendaji kazi wa mifumo ya kisiasa, kisheria, na kiuchumi. Mifumo hii mitatu ikifanya kazi kwa pamoja huuisha utawala wa kifisadi, uupa nguvu na kuufanya udumu. Tuangalie mifumo hii mitatu jinsi ilivyo katika Tanzania.

Mfumo wa Kisiasa:
Mfumo wetu wa kisiasa umetengenezwa ili kulinda maslahi ya kikundi cha watu walio madarakani. Haujatengenezwa ili kuruhusu ushindani wa haki wa kisiasa, na hauruhusu changamoto ya kweli ya siasa za kidemokrasia. Utaona kuwa katika mfumo wetu wa kisiasa, katiba ya nchi inaelezea juu ya ujenzi wa taifa la kijamaa na ile ya chama tawala nayo ikisema hivyo hivyo. Hata hivyo hakuna mtu yeyote ndani ya serikali ya sasa au kwenye chama anayeweza kutetea ujamaa leo hii au kutuelezea ni “ujamaa” wa aina gani wanauunda.

Maana yake ni kuwa, watawala waliopo sasa hawajali hasa katiba inasema nini kwani kwao katiba ni kama mapendekezo ya aina fulani tu na siyo mkataba unaowafunga watawala kwa watawaliwa. Leo hii siyo Kikwete, Makamba wala Kingunge wanaoweza kutuambia ni aina gani ya ujamaa wanaoutekeleza kwa mujibu wa Katiba.

Ni mfumo ambao umewekeza nguvu kwenye chama cha kisiasa kiasi kwamba watu wachache kwenye chama hicho wanaweza kutuamulia ni nani anakuwa Rais wetu au Spika wetu wakiamua tu kumvua uanachama. Ni mfumo ambao unafanya geresha ya demokrasia kwa kufanya uchaguzi wa vyama vingi huku mfumo wa sheria walioutengeneza ukizuia kabisa uchaguzi huru na wa haki.

Hivyo, mfumo wa kisiasa wa kwetu ni kiinimacho cha siasa za kidemokrasia kwani ndani yake kuna vizuizi vingi vya utendaji kazi wa demokrasia; kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, matokeo ya uchaguzi wa rais hayawi rasmi hadi tume isiyo huru itangaze, kukataza wagombea huru, ukosefu wa chombo cha kusimamia Bunge, n.k

Mfumo wa Kisheria
Mfumo wetu wa kisheria katika utawala wa kifisadi umeundwa ili kuondoa hasira na siyo kushughulikia tatizo lenyewe hasa linalosumbua jamii. Kwa kiasi kikubwa utaona kuwa sheria mbalimbali zimeundwa zikiwa na majina mazuri na ya kupendeza lakini zikiangaliwa kwa karibu utaona kuwa zimeundwa ili kuwafanya watu wasikasirike sana.

Sheria mbalimbali zilizotungwa kwenye utawala wa kifisadi zimetengenezwa ili kuzuia watu wasijichukulie sheria mikononi lakini wakati huo huo kutoa ulinzi wa aina yake kwa wahalifu wanasiasa.

Mojawapo ya vitu ambavyo vimeondolewa kwenye sheria nyingi ambazo zingeweza kuwakamata wanasiasa na watendaji wazembe ni kile ambacho tunakiita kama “trigger clauses”. Kwamba endapo kitu x kitatokea basi mtu y atachukuliwa hatua zifuatazo. Kwa mfano, endapo mtendaji anatakiwa kutoa maelezo na Mkaguzi Mkuu ya matumizi ya shilingi milioni 300 na akashindwa nini kimtokee? Utaona sheria zetu haziko wazi zaidi ya kumpa CAG uwezo wa kuonesha au kutoa maelekezo kuwa huyo “y” achunguzwe au kuchukuliwa hatua “zinazopasa”.

Utaona kuwa sheria zetu zina matundu ya makusudi kabisa yenye kuzuia utekelezaji wake wa mara moja na hivyo matundu hayo yamekuwa ni kinga kubwa ya makuwadi wa ufisadi kwani wanajua kabisa kuwa mtu akitaka kuzifuata sheria hizo atajikuta anashindwa kabla hajafika mbali.

Hivyo, mfumo wetu wa kisheria umeundwa ili kuzuia hasira lakini kushindwa kuzuia vitendo vya ufisadi uliokubuhu. Mtu yeyote anayesoma sheria ya kupambana na kuzuia rushwa, sheria ya madini, sheria ya usalama wa taifa na sheria ya makosa ya kuhujumu uchumi utaona kuwa watawala wamezitengeneza ili zisifanikiwe. Na hivi karibuni watawala hao hao wamepunguza nguvu ya baadhi ya sheria hizo kwa sababu wanajua akiingia mtu kichaa kwenye ofisi ya DPP kuna watu wengi watatiwa pingu.

Mara zote kwenye utawala wa kifisadi, watawala hutumia mianya mbalimbali kuvuruga utawala wa sheria ili kujikinga na mashtaka huko mbeleni. Ndio maana leo hii tuna mtu ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu kwa miaka 10 na ambaye yeye mwenyewe anashtumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa sheria lakini hakuna mtu mwenye ubavu wa kunyosha kidole na badala yake anakingiwa kifua; ndio maana leo hii baadhi ya “watunga sheria” wetu ndio wale wale wanaotajwa kwenye baadhi ya uvunjaji mkubwa kabisa wa sheria katika jamhuri yetu.

Mfumo wa kiuchumi
Katika utawala wa kifisadi, mfumo wa kiuchumi hufanana na mfumo wa kiuchumi katika utawala wa kidemokrasia. Ukiangalia kwa juu juu mfumo wa kiuchumi unaundwa na taasisi kama zile zilizopo kwenye nchi za kidemokrasia na ukisoma maandishi mbalimbali unaweza kabisa kuamini kuwa mfumo huo wa uchumi katika utawala wa kifisadi unalingana kiutendaji na mfumo wa kiuchumi katika utawala wa kidemokrasia. Hili si kweli.

Unapokuwa na mfumo mbovu wa kisiasa na kisheria, mfumo wa kiuchumi nao hauwezi kuwa salama. Kwa maneno mengine, mfumo wa kiuchumi hauwezi kusalimika pale ambapo mfumo wa kisiasa na ule wa kisheria inapokuwa matatani. Mara zote ubovu wa mfumo wa kisheria na kisiasa huonekana katika ubovu wa mfumo wa kiuchumi.

Katika Tanzania ya leo hii tunaweza kujiuliza ni mfumo wa aina gani wa kiuchumi tunaoufuata? Je ni ubepari au ujamaa? Je ni mchanganyiko wa aina hizo mbili na kwa namna gani? Mara nyingi utamsikia Kikwete na wanasiasa wengine wa CCM wakielezea juu ya “mfumo wa Soko” au mfumo wa “ushindani” je hii kiitikadi ina maana gani? Je, ni mashindano kati ya tajiri na maskini, aliyenacho na asiyenacho, mwanaCCM na asiye mwanaCCM?

Na hata wakati mwingine unaposikia takwimu mbalimbali za kiuchumi toka Benki Kuu hatuna budi kujiuliza hivi ni kweli takwimu hizo ziko sahihi kwa kiasi gani? Kwenye nchi ambayo uzalishaji unafanyika kwa zaidi ya asilimia 90 kwa njia zisizorasmishwa tunaweza vipi kuelezea kwa uhakika hali ya kiuchumi? Kwenye nchi ambapo asilimia zaidi ya 20 (Kikwete hivi karibuni alidai asilimia 30) ya bajeti inaishia kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi, unaweza vipi kuelezea kuwa mfumuko wa bei uko chini ya tarakimu mbili?

Unawezaje kuelezea “kukua kwa uchumi” na ukawa sahihi kwenye taifa ambalo madini yake haijulikani kwa hakika ni kiasi gani kinatolewa nje na mahali ambapo makampuni yanaweza kusafirisha nje faida yao kwa asilimia 100 huku yakitangaza kupata hasara kila mwaka kwa mujibu wa sheria nyingine tuliyowatengenezea?

Tunaweza vipi kupima kwa haki pato la mwananchi wakati sehemu ya pato hilo ni lile linalotokana na rushwa kidogo? Unaposema bei ya kitu (bidhaa au huduma) ni kiasi fulani lakini wakati huo huo mtu anatakiwa kubajeti ndani yake “kitu kidogo” juu ya bei hiyo, mchumi anapopiga hesabu zake anachukulia na hicho “kitu kidogo” ndani au hapana?

Kimsingi utaona kuwa katika mfumo wa utawala wa kifisadi, mfumo wa uchumi ni wa kudanganya. Yaani, taarifa rasmi za kiuchumi haziakisi ukweli hasa wa shughuli za kiuchumi na uwezo wa uchumi huo (kwa uzuri au kwa ubaya). Matokeo yake wakati mwingine watu wanaamini kuwa uchumi wao unafanya kazi vizuri zaidi wakati hiyo “vizuri zaidi” ni kwa sababu ya vitendo vya kifisadi.

Ndio maana kuna baadhi ya watu wanaamini kabisa kuwa endapo ufisadi utapigwa marufuku kabisa na kila mtu kulazimishwa kuishi kwa haki kunaweza kutokea maandamano makubwa sana. Kwani kwa mara ya kwanza, watu watatakiwa kuishi kwa uhalisi wa vipato na matumizi yao.

Sasa basi, tunaweza kuona kuwa mafisadi waliopo sasa ni mazao ya mfumo uliopo sasa hivi. Hata tukiweza kuwaangusha na kuwatia pingu mafisadi wote bado tutakuwa na kizazi kipya cha mafisadi kwani mfumo uliowatengeneza bado upo.

Itakuwa ni sawasawa na kiwanda cha kutengeneza magari; kama kuna mahali ambapo mashine moja haiingizi breki kwa usawa kwenye gari, basi magari yatakayotoka yatakuwa na matatizo na breki zake. Watu watapata ajali na mengine itabidi yaondolewe barabarani. Lakini kama suluhisho ni kuondoa magari mabovu ambayo tunajua yanatoka kwenye kiwanda fulani lakini wakati huo huo kiwanda bado kinatengeneza magari mabovu kwa sababu sehemu ya mashine yake (mfumo wake mmoja au zaidi) imeharibika basi tutakuwa tunacheza “pata potea”.

Suluhisho siyo tu kuondoa magari mabovu barabarani bali vile vile kurekebisha mashine kiwandani ili zisitengeneze gari lenye matatizo ya breki.

Leo hii ninachosikia ni watu kulalamikia “mafisadi” (magari mabovu), watu wanapiga kelele ni kwa kadiri gani mafisadi wameifisadi nchi n.k lakini sijamsikia hata mtu mmoja mwenye ujasiri wa kusema kuwa tatizo letu ni “kiwanda”.

Ndio maana nimesema awali kuwa tatizo letu siyo Rostam, Lowassa, Chenge au Yona; hawa ni dalili tu ambazo tunaweza kuziondoa barabarani. Tutakuwa hatuna hekima kama tunaamini kuwa tukiwaondoa hawa toka madarakani basi ufisadi utakwisha. Tusipobadilisha mfumo wa kiutawala ufisadi tutaendelea kuzalisha mafisadi tu. Haijalishi ni chama gani kiko madarakani.

Ndio sababu, tunapowasikiliza wanaotaka kugombea mwakani hatuna budi kujiuliza na kuwauliza wao, wanampango gani wa kuubadilisha mfumo wa kiutawala wa ufisadi badala ya kuwashughulikia mafisadi wa sasa tu? Watafanya nini kuurekebisha mfumo wetu wa kiutawala ili usitoe mafisadi na vifaranga vyao?

Ni katika kuelewa hili ndipo tunaweza kuelewa kuwa adui yetu wa kwanza kabisa katika vita hii ni mfumo wa utawala wa kifisadi. Lakini ni nani huyu aliyejemedari aliyeuunda, kuupanga, na kuusimamia mfumo huu wa kifisadi kiasi kwamba tunavuna matunda yake machungu leo hii? Ni nani huyo ambaye anapaswa kuzuiliwa asiendelee kutufyatulia matofali ya mchanga mtupu kujengea taifa letu? Wengine, wanafikiria ni mtu mmoja au kikundi cha mafisasdi.

Mimi napendekeza; ni mfumo wa utawala wa Chama cha Mapinduzi. Unabisha?

Niandikie:

mwanakijiji@mwanakijiji.com

Tuesday, November 17, 2009

Mo Ibrahim: Viongozi Afrika hawako makini

MMILIKI wa taasisi ya Mo Ibrahim amesema matatizo yote yanayoikumba nchi za bara la Afrika, ikiwemo vita, njaa na magonjwa, yanatokana na viongozi wake kutokuwa makini na kutofuata misingi ya utawala bora.

"Viongozi wetu wengi si makini na pia hawafuati misingi ya utawala bora na kutokana na haya ndio maana bara hili bado lipo nyuma kiuchumi na linasumbuliwa na matatizo ya njaa, magonjwa na vita," alisema mmiliki huyo, Mo Ibrahim jijini Dar es Salaam juzi katika hafla maalum ya muziki ikiwa ni sehemu ya maadalizi ya mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Mlimani City.

Katika mkutano uliokutanisha viongozi mbalimbali kutoka nchi za bara la Afrika, pamoja na mambo mengine walijadili masuala mbalimbali yakiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa, kilimo na maendeleo ya nchi za Afrika.

Mo Ibrahim, ambaye ni milionea alifafanua kwamba viongozi wa nchi za Afrika ni wepesi wa kuzungumza lakini si watendaji katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.

Alisema kutokana na hali hiyo, Afrika inaonekana ni bara masikini na lenye matatizo mengi ikiwa ni pamoja na vita, njaa na magonjwa.

"Kutokana na rasilimali tulizonazo katika nchi zetu hapa Afrika, hakuna sababu ya kuwa nyuma kiuchumi na wala kukumbwa na matatizo ya magonjwa, vita na njaa. Lakini haya ni kutokana na kutotekelezwa ipasavyo na kwa vitendo mipango ya maendeleo inayokuwa inawekwa na viongozi wetu," alisema

Hata hivyo, Mo Ibrahim alisema bado kuna nafasi kwa viongozi wa Afrika kufanya jitihada zaidi kwa lengo la kufaniksha uchumi wa bara hili ili uachane na utegemezi kwa nchi za barani Ulaya, Amerika na Asia.

"Ni wakati sasa kwa viongozi na Waafrika kujiamini katika mipango yao na kuachana na tabia ya kutegemea kusaidiwa katika kila kitu," alisema tajiri huyo.

"Ni muhimu tukafikiria maisha ya baadaye ya watoto wetu yatakuwaje endapo hali itaendelea kama ilivyo sasa katika bara hili zuri na lililojaa mali."

Monday, November 16, 2009

Selelii awazima Lowassa na Rostam

  • Adai Kikwete alikabidhiwa mapema ripoti ya Richmond
  • Asema kama kumuokoa ni yeye aliyepaswa kufanya hivyo
Na Saed Kubenea
MwanaHALISI

JUHUDI za mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na mwenzake wa Igunga, Rostam Aziz kutaka kujivua na gome la Richmond zimezimwa, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati ya wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichofanyika Dodoma wiki iliyopita, zinamtaja mbunge wa Nzega Lucas Selelii kuwa ndiye aliyezima ndoto za Lowassa na Rostam kujisafisha.

Inaelezwa kwamba Selii alizima ndoto za Rostam na Lowassa baada ya kuanika ushiriki mzima wa wanasiasa hao wawili katika mkataba huo. Mkutano kati ya kamati ya wazee na wabunge ulifanyika siku tatu mfululizo katika ukumbi wa zamani wa Bunge mjini Dodoma.

Akiongea kwa kujiamini na kuchambua hoja moja baada ya nyingine, Selelii alisema Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond ambapo yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wake inaoushahidi kwamba Richmond ni mali ya Rostam.

Kwa upande wa Lowassa, Selelii alisema alibeba kampuni hiyo kwa maslahi ya binafsi ya rafiki yake huyo.

Akiongea baada ya Rostam kukana kumiliki kampuni hiyo na kutaka kuundwa kwa Tume huru kuchunguza mkataba huo, Selelii alisema “Rostam amewadanganya kwa kusema hahusiki na Richmond.”

“Huyu Rostam ndiye aliyetafuta nyumba kwa ajili ya matumizi ya ofisi ya Richmond. Ni yeye aliyelipia pango la nyumba hiyo,” alisema Selelii huku akitolea macho Rostam. Alisema, “Kamati yetu ilihakikishiwa na mtoto wa Mucadam (Hussen Mucadam) ambaye ndiye mwenye nyumba kwamba nyumba iliyotumiwa na Richmond ilipangwa na Rostam.

”Huku wabunge na wajumbe wa kamati ya wazee wakiwa wamepigwa na butwaa, Selelii alisema “hata jopo la waadishi wa habari lililofanya kazi ya kusafisha Richmond lilitafutwa na Rostam.”

Alisema Rostam alifikia hatua ya kutumia waandishi hao wa habari mara baada ya vyombo vya habari kuanza kueleza utata wa mkataba. “Ni huyu Rostam aliyekodisha jopo la waandishi wa habari watatu mashuhuri nchini kwa ajili ya kupoza makali. Tumezungumza na waandishi wa habari hawa mmoja baada mwingine na wote wametuthibitishia hili,” alisema Selelii.

Alitaja hata majina ya waandishi hao kuwa ni Gideon Shoo, Jimmy Mdoe na Salva Rweyemamu ambaye sasa ni mkurugenzi wa mawasiliano ya rais. Tarehe 29 Juni 2006, serikali kupitia Shirika la Umeme la Taifa (Tanesco) ilisaini mkataba wa kufua umeme wa megawati 100 na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) bila kwanza kuhakiki uhalali wa kampuni hiyo.

“Kama hahusiki kwa nini aliwatafuta hawa waandishi wa habari? Kwa nini aliwapa kazi,” alihoji Selelii.Alisema mbali na waandishi wa habari na utafutaji wa nyumba, Kamati Teule iliweza kuthibitisha kwamba baada ya Richmond kuhuisha mkataba wake kwa Dowans, wafanyakazi watatu wa Caspian walionekana katika Dowans.“Kwa maana nyingine, Dowans, Richmond na Caspian ni baba mmoja mama mmoja.”

Alisema Kamati Teule imepata ushahidi kwamba “fedha za Dowans zilihamishiwa katika akaunti ya Caspian; Rostam alikuwa akifuatilia mwenyewe fedha hizo hazina,” alisisitiza Selelii.

Mbunge mmoja wa Bunge la Muungano aliliambia MwanaHALISI kwamba wakati Selelii akieleza wajumbe taarifa hiyo, ukumbi mzima ulikuwa kimya.

“Hata sindano kama ingeanguka, ingeweza kusikika. Nakuambia yule jamaa jinsi alivyokuwa akiongea kwa upole na taratibu, kila mtu alikuwa na shauku ya kumsikiliza,” alisema.

Anasema, “Rostam alikuwa amekaa kimya. Alikuwa kama vile amelowa mvua.”Baada ya kueleza ushiriki wa Rostam Selelii aliyeongea kwa kupanga hoja zake alirukia Makongoro Mahanga, mbunge wa Ukonga, ambaye awali alidai kuwa “ripoti ya Bunge ilikuwa feki.”

Makongoro amesema “ripoti yetu ni feki; Kamati Teule haikumshirikisha Rais Jakaya Kikwete. Haikumueleza; kama angeelezwa angemuokoa Lowassa,” alisema Selelii kwa taratibu. Alisema madai hayo ya Mahanga hayana ukweli, na kwamba yamelenga kuhamishia tatizo kwa wengine. Alihoji: Kama ripoti ilikuwa feki inawezekanaje rais aliyepewa taarifa hiyo kabla ya kuwasilishwa bungeni akaiamini?

Kuhusu Kamati Teule kutomshirikisha rais Kikwete, Selelii alisema kabla ya kamati kuwasilisha ripoti yake bungeni ilikabidhi ripoti kwa rais. Selelii alikuwa akijibu hoja ya Andrew Chenge na Mahanga waliotumia muda mrefu kueleza kikao juu ya kutoshirikishwa rais Kikwete. Alisema, “Rais alikuwapo hapa Dodoma wakati mjadala wa Richmond unafukuta. Tayari alikuwa na ripoti yetu. Sasa kwa nini yeye hakumpa waziri mkuu wake,” alihoji Selelii na kuongeza, “haikuwa kazi ya kamati kumpa ripoti Lowassa.”

Alisema, Rais ana vyombo vya ulinzi na usalama. Je, kama yeye mwenye vyombo hivi hakuona kasoro, nani mwingine mwenye mamlaka ya kudai kuwa ripoti yetu ilikuwa feki,” alihoji.

Akiongea huku akionekana mwenye hasira, lakini kwa taratibu mno, Selelii alisema, “mnaleta umbeya hapa eti rais hakujua haya. Rais tulimpa ripoti hii kabla ya kuwasilisha bungeni.” Taarifa zinasema Selelii alikiambia kikao hicho kwamba Kamati Teule imefanya kazi yake kwa kufuata misingi ya sheria. “Duniani kote mtuhumiwa hawezi kupewa taarifa ya kilichomo katika ushahidi hadi pale suala hilo linapoingia mahakamani. Katika hili Lowassa hana wa kumlaumu,” Selelii alisisitiza.

Baada ya kumaliza kuumbua Mahanga, Selelii aligeukia Sophia Simba ambaye alituhumu Kamati Teule kuwa imemuonea Lowassa na kumvua nguo mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na mumewe Joh Malecela. Katika hilo, Selelii alisema, “Sophia Simba huyu ni mwenyekiti Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT). Pia ni waziri anayesimamia utawara bora,” chanzo cha habari ndani ya kamati kinanukuu Selelii. Anasema, “aliyoyasema hapa hayakustahili kutolewa katika kikao hiki. Haya ni maneno yanayopaswa kutolewa kwenye kitchen party. Nimemsikiliza kwa makini, mheshimiwa Simba amezungumza mambo binafsi yanayohusu mtu binafsi,” alisema.

Mbili, Selii alisema, “Sophia Simba amesema hapa kuwa Lowassa ni mwanamme namba moja. Ni mwanamme wa shoka. Akimaanisha kwamba wanaume wote akiwamo rais, waziri mkuu, wabunge na madiwani siyo kitu. Mimi sikubaliani naye. Labda kama mwanamme wa shoka katika masuala mengine,” alisema kwa kujiamini.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe alikabidhi ripoti ya kamati yake kwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta 31 Desemba 2007.

Mara baada ya Sitta kupokea ripoti ya Mwakyembe aliondoka nchini kwenda Uingereza kuhudhuria mkutano wa Bunge la Jumuiya ya Madola.Taarifa zinasema mara baada ya Sitta kurejea nchini alikabidhi ripoti hiyo kwa rais Kikwete. Hiyo ilikuwa 29 Januari 2008; kabla ya Kikwete kuelekea Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika (AU).

Rais Kikwete alisafiri kuelekea Ethiopia 29 Januari 2007. Alirejea nchini 5 Februari 2008. Lowassa alikabidhiwa ripoti na Sitta 6 Februari 2009.“Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, iwapo nitakupa ripoti hii, sharti nifanye hivyo pia kwa kiongozi wa upinzani,” Sitta alinukuliwa akimueleza Lowassa.

Baada ya Sitta kumkabidhi Lowassa ripoti hiyo, alimkabidhi ripoti hiyo “Kiongozi wa Kambi ya upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed,” taarifa zinaeleza.

Kwa upande wake, Sitta amekana kuwa Rostam aliwahi kuwasuluhisha yeye na Lowassa. “Ni uwongo mtupu. Mimi sijawahi kusuluhishwa na Lowassa. Kwanza, hatukuwa na ugomvi, sasa kwa nini tusulihishwe,” alihoji Sitta. Alisema madai ya Rostam kwamba Sitta alitaka nyumba yenye hadhi Dar es Salaam na Urambo hayana msingi, kwa kuwa suala la makazi ya spika hupangwa na katibu mkuu kiongozi.

SAIDIA MADAWATI SHULE ZA MSINGI WILAYA YA KYELA

Shule za Msingi ni nguzo kubwa ya maendeleo kielimu katika sehemu mbalimbali hapa nchini na duniani kwa ujumla. Imefahamika na vyombo mbalimbali kuwa bila kuimarisha na kuzijengea mazingira mazuri shule za msingi basi elimu bora itakuwa ni sawa na ndoto isiyotimilika.

Vilevile ni bora kutambua kuwa maendeleo ya kielimu kwa mtu yeyote huanzia shule za msingi. Hivyo kuimarisha mazingira ya shule za Sekondari wakati yale ya shule za msingi ni duni ni sawa na daktari kutibu ugonjwa bila kuzuia chanzo cha ugonjwa huo. Hivyo tusipoweka mazingira mazuri ya shule za msingi, shule za sekondari zitakuwa zinapokea wanafunzi ambao hawatapenda kusoma kwani watahisi kuwa hata sekondari watakutana na mateso yaleyale waliokuwa nayo shule za msingi.

Tabia imejengeka ya vijana na watu mbalimbali waishio mbali na maeneo watokako kujivunia maendeleo ya mahali walipo au wanapoishi bila kujua kuwa wanawajibu wa kujivunia maendeleo ya kule watokako pia.

Ni wajibu wa kila mtu kujua kuwa ana wajibu wa kusaidia shule za msingi katika maeneo atokako ili kuboresha kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa shule hizo. Mazingira ya kusomea kwa shule za msingi yakiboreshwa tutapata watoto watakaopenda shule na kupenda kuendelea na Sekondari pia.


Hivyo kwa kuanzia, elimu inatakiwa ili kuwaelimisha wazee kwa vijana waishio Dar-es-Salaam na Sehemu za jirani kuweza kujitolea ili kusaidia kununua madawati ya shule za Msingi zinazohitaji msaada huo Wilayani Kyela.

Ifahamike kuwa juhudi zinazofanywa na mbunge wa jimbo la Kyela Dk. Harrison Mwakyembe katika kuleta maendeleo yote kwa ujumla ni kubwa mno, hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa kuchangia madawati kwa shule za msingi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada zake za kupambana na mafisadi nchini.

Maendeleo ya Wilaya ya Kyela hayataletwa na mtu mwingine yeyote bali na wananchi wake, hasa watokao maeneo hayo japo hawaishi huko kutoka na mgawanyiko wa kazi. Hawa ndio wanaopaswa kuleta maendeleo ya nyumbani kwao na kujivunia hata wawapo sehemu nyingine nchini.

Hivyo kwa ujumbe huu natoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kusomea ya kizazi chetu na Taifa la kesho waweze kuungana na kusaidia madawati kwa ajili ya shule za msingi Wilayani Kyela.

Ni matarajio yangu kuwa mahitaji ya madawati kwa shule za msingi ni makubwa sana hivyo, tukianza mapema kulishughulikia tatizo hili tunaweza kulipunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kulimaliza kabisa.

Hii ni Wilaya yetu, watoto wanaosoma wakiwa wamekaa chini au kwenye mawe ni vijana wetu, kwahiyo kusaidia kuwajengea mazingira mazuri ni jukumu letu na ni kwa faida yetu na vizazi vyetu vya baadaye.

Kila mmoja wetu kwa wakati wake akae chini alifikirie sana suala hili, atafakari kwa mapana na marefu faida atakayoipata yeye binafsi na vijana wetu baada ya kusaidia kuyaboresha mazingira ya kusomea katika shule za msingi.

Umefika wakati sasa kwa kila mmoja wetu kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya yetu bila kujali utatoa nini na kiasi gani kwani kutoa ni moyo. Vilevile ukichunguza kwa undani zaidi utagundua kiwango cha vijana wetu wanaoendelea na masomo ya juu kutoka Wilayani Kyela kimepungua na kitaendelea kupungua kama juhudi za makusudi hazitafanywa ili kuboresha mazingira ya kusomea kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.

Fanya utafiti wako binafsi na ung’amue vijana wangapi wanaojiunga na kidato cha Kwanza, Tano, Vyuo na Vyuo vikuu kutoka Wilaya ya Kyela hapo ndipo utagundua kuwa huko tuendako hali itakuwa mbaya zaidi kama hatutachukua tahadhali mapema.

HITIMISHO: Ndugu zangu, tujiandae kufanya kila linalowezekana ili kuokoa hali hii kwa faida yetu wenyewe na vizazi vyetu vya baadaye. Kwa kuanzia hapa tutaendelea kusaidia na mambo mengine ili kuhakikisha kiwango cha wasomi na maendeleo Wilayani Kyela kinakua kila kukicha.

Ewe mwanaKyela saidia madawati kwa shule za msingi Kyela ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mbunge wetu na Serikali kwa ujumla.


Niandikie:

Africarkagema@airtanzania.com
kyela@live.com