Wednesday, October 28, 2009

Mwakyembe ataka Hosea asijihami

Tuesday, 27 October 2009 15:12

*Asema hawezi kuwaziba midomo wabunge
*Asisitiza chanzo ni kashfa ya Richmond

Na John Daniel, Dodoma

MBUNGE wa Kyela. Dkt. Harison Mwakyembe, (CCM), amemshukia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dkt. Edward Hosea na kumtaka aache mara moja kutafuta njia ya kujihami kwa kuwahoji ili kuwaziba midomo wabunge badala yake izingatie utawala wa sheria.

Dkt. Mwakyembe aliyeongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya kampuni tata ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, na kumtuhumu Dkt. Hosea kwa kuisafisha, anaungana na mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo kuhusisha kashfa hito na hatua ya TAKUKURU kuwahoji wabunge kuhusiana na posho wanazopokea.

Madai ya wabunge hao yamekuja wakati TAKUKURU ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge ikiwatuhumu kupokea posho mara mbili kutoka serikalini na kwenye mashirika ya umma, huku wakiwa wameshalipwa na ofisi ya Bunge.

Tofauti na Bw. Shelukindo aliyekiri kuhojiwa na kutoa ushirikiano, Dkt. Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema hawezi kukubali kuhojiwa na TAKUKURU kwa sasa hadi hapo serikali itakapomaliza kutekeleza maamizio 23 ya Kamati Teule ya Bunge, mojawapo likiitaka kumwajibisha Dkt. Hosea.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari wa Bunge jana, Dkt. Mwakyembe alisema amesikitishwa na kitendo cha TAKUKURU kuwaita wabunge katika kundi kwa kuwapigia simu kuwahoji kuhusu malipo ya posho ya vikao mbalimbali hukutaasisi hiyo, nayo ikiwa inawalipa wabunge pale inapokutana nao Dar es Salaam.

“Leo nimesoma gazeti moja (Sio Majira) likiwa limeandika habari kwamba sijui Mwakyembe amechanganyikiwa, ameitwa na TAKUKURU ameomba hifadhi, kwanza hili ni gazeti la mafisadi na si mara ya kwanza kuandika habari kama hizi, gazeti hili linamilikiwa na mafisadi.

"Waandishi wa (hilo gazeti) wapo hapa, tuambieni Kagoda ni nani, Richmond ni nani, hili gazeti linamilikiwa na mafisadi na mnawajua, sina haja ya kuwataja na tulishawataja,” alisema.

Mbunge huyo aliongeza: “Lakini ninachotaka niseme ni kwamba kwa muda wa karibu mwezi sasa, TAKUKURU wamekuwa wakiwaita wabunge kwa makundi tena kwa kuwapigia simu, na mimi walinipigia simu nikiwa jimboni, nikakataa kwenda sasa huo ni ujasiri kwa sababu bado tunasubiri utekelezaji wa serikali kuhusu TAKUKURU katika suala la Richmond, hatujapata majibu hayo, huyo huyo anayetakiwa kushuguhulikiwa (Dkt. Hosea) anatuita eti kutuhoji,” alisema Dkt. Mwakyembe na kuongeza.

“Huo siyo utawala wa sheria, hili ni bunge la tisa lakini hata sisi tumekuta wabunge wakilipwa posho au kuandaliwa chakula, sisi tunawapokea mawaziri kila siku katika maeneo yetu hatujawahi kusema kwamba leo tusimwandalie chakula kwa kuwaamelipwa, hapana. Hata wao TAKUKURU wametuita pale Dar es Salaam walitulipa posho tena mpaka ya kulala, yapo masuala mazito ambayo tunataka TAKUKURU wawasaidie Watanzania si michezo michezo hii,” alisema.

Alisema fedha zinazotumika katika fungu hilo hupitishwa bungeni kila mwaka kwa jina la hospitality (takrima) na kwamba ni jambo la kawaida kumkarimia mgeni anapokutembelea na kwamba kama mtu hapendi kufanya hivyo halazimishwi lakini kuwahoji wabunge juu ya malipo hayo ni kutaka kuwaziba midomo ili wawe na hofu kuhoji utekelezaji wa serikali kuhusu mkuu wa TAKUKURU.

“Mimi waliniita na nimekataa kwenda sasa kama wana hoja waende mahakamani tutakutana huko na nitawaumbua huko,” alisema Dkt. Mwakyembe. Alisema yeye kama mbunge mwana taaluma ya sheria hawezi kukubali kuona watu wanatumia baadhi ya vyombo vya habari kuendelea kupotosha ukweli kwa maslahi yao na kuwaomba wanahabari kusaidia jamii kuelewa hoja za msingi za taifa badala ya baadhiyao kupotosha ukweli kwa maslahi yao.

“Eti mafisadi wanataka kuniangusha kule jimboni kwangu, najua leo kuna ndege imepeleka magazeti ya fulani Kyela na kugawa bure, lakini nawaambia wananchi ni waelewa, mafisadi kuning’oa Kyela itawabidi wao na wake zao wapige kambi na wahamie Kyela kwa miaka mitano,” alisema Dkt. Mwakyembe.

Kauli hizo za Dkt. Mwakyembe zimekuja siku mbili baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuishtumu TAKUKURU kupitia gazeti kuwa inadhalilisha wabunge kwa kuwahoji bila kufuata taratibu, ikiwamo kuifahamisha ofisi yake.

Lakini taasisi hiyo kwa upande wake inasema ilipata baraka za bunge kufanya hivyo na wabunge wanastahili kuitikia wito kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Malumbano hayo yanaendelea wakati Mkutano wa 17 wa Bunge unaotarajia kuhitimisha kashfa ya Richmond kwa serikali kueleza ilivyotekeleza maazimio 23 ya bunge ukiendelea.

Tuesday, October 27, 2009

Urafiki wa Lowassa, JK usiingilie urais-Wabunge

*Selelii, Kimaro wataka afikishwe kortini
*Walaumu serikali kwa kutoa majibu ya ovyo
*Lowassa: Sizungumzi na vyombo vya habari

Waandishi Wetu, Dar, Dodoma

Majira26 October 2009

WAKATI mkutano wa bunge unaanza leo, mzimu wa mkataba tata wa Richmond umeendelea kumwandama aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa baada ya baadhi ya wabunge kudai kuwa anastahili kuchukuliwa hatua zaidi ya ile ya kujiuzulu kutokana na kutajwa kwake katika kashfa hiyo.

Wabunge hao kwa nyakati tofauti wamesema kuwa urafiki ambao Bw. Lowassa alisema upo baina yake na Rais Jakaya Kikiwete usiingilie urais, serikali na uiachwe ifanye kazi yake kwa kumchukulia hatua kutokana na kuliingizia taifa hasara.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Nzega, Bw. Lucas Seleli Bw. Selelii alisema kutochukuliwa hatua za kisheria kwa Bw. Lowassa kunatokana na urafiki uliopo kati rais Kikwete na mbunge huyo wa Monduli.

Alisema Rais Kikwete anapaswa kuamua kusuka au kunyoa kwa kuacha urafiki na kufuata sheria za nchi kwa kumfikisha Bw. Lowassa katika vyombo vya sheria, kwani alionekana wazi kushiriki kupitisha mkataba huo tata.

"Tulipokuwa tukijadili taarifa ya Kamati Teule ya Bunge tulibaini kuwa bila shaka alishiriki katika uamuzi huo, hivyo tulimwambia apime akapima, akaamua kujiuzulu. Huu ulikuwa ni uamuzi wake binafsi lakini sisi hatukuishia hapo.

"Tuliacha na serikali nayo iamue nini cha kufanya lakini hadi sasa imekuwa ikitupatia majibu ya ovyo ovyo tu, tunajua hawa watu ni marafiki tangu muda mrefu lakini urafiki na urais ni kitu tofauti. Hapa ni kazi wanatakiwa kuweka urafiki pembeni na kuwatumikia wananchi," alisema Bw. Selelii.

Alisema kama kweli nchi inafuata sheria na utawala bora, serikali inatakiwa kumshtaki Bw. Lowassa kutokana na kosa alilofanya kwani limekuwa likiipotezea nchi pato kubwa hadi sasa.

Alisema kuwa sheria ni sawa na moto, kwa kuwa moto unaweza kuundaa mwenywe lakini ukakuunguza.

Alisema katika mkutano wa 17 unaoanza leo mjini Dodoma wamekamia kumaliza suala hilo na kuhakikisha kuwa sheria inachukuwa mkondo wake kwa kuwachukiliwa hatua watu wote walihusika katika mkataba huo tata.

Kauli ya Selilii imekuja siku moja baada ya gazeti moja kutoa vielelezo vinavyoonesha jinsi Bw. Lowassa alivyohusika kushinikiza kusainiwa kwa Mkataba wa Richnond.

Lakini Bw. Lowassa alipoulizwa hakuwa tayari kuzungumza na gazeti hili. "Sikusikia vizuri swali lako kwa kuwa simu inakatakata, lakini siko tayari kuzungumza na vyombo vya habari kwa sasa hadi hapo nitakapopanga," alisema Bw. Lowassa na kukata simu.

Mapema, Mbunge wa Vunjo, Bw. Aloyce Kimaro naye aliungana na Bw. Selelii, akisema kuwa Rais Kikiwete anatakiwa kuuweka pembeni urafiki wao na kuchukua uamuzi utakaowafurahisha wananchi waliomweka madarakani.

Alisema Rais anatakiwa kukumbuka kuwa madaraka aliyonayo ni ya milele na yanagharimiwa na wananchi, hivyo hatakiwi kufanya machezo kwa kuchanganya urafiki na madaraka hayo, kwani kutomchukulia hatua Bw. Lowassa ni sawa na kuwadharau wananchi anaowangoza.

"Iwapo atachukua uamuzi mzito wa kumfikisha Bw. Lowassa katika vyombo vya sheria utakuwa si uamuzi wake bali ni wa wananchi kwa kuwa cheo hicho si mali ya Lowassa au ya Kikwete bali ni mali ya wananchi," alisema Bw. Kimaro.

Alisema hadi sasa hajui ni kwa nini rais anakuwa mzito katika kutoa maamuzi katika jambo hilo kwani mapendekezo ya Kamati Teule ya Bunge na maoni ya wabunge yako wazi.

Mwansheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Tindu Lisu, alihoji, "Lowassa mwenye alishasema kuwa urafiki wake na Rais Kikwete haukuanzia barabarani, sasa kwenye mazingira ya aina hiyo anaweza kumshitaki?

"Mtu wa kumshitaki mahakamani ni DPP (Mwendesha Mashitaka wa Serikali) ambaye anachaguliwa na Rais, na rais ni rafiki yake Bw. Lowassa, sasa hatawezaje kumshitaki katika mazingira hayo." alihoji Bw Lissu.

Alisisitiza kuwa Rais akitaka anaweza kumfikisha, Bw. Lowassa, katika vyombo vya sheria kujibu mashitaka ya kutumia vibaya ofisi yake.

"Kuna ushahidi mkubwa unaoonesha jinsi Bw. Lowassa alivyohusika, ukisoma ripoti yote ya Dkt. Mwakyembe (Harrison) utaona inavyoeleza wazi jinsi alivyohusika...barua zipo nyingi zinazothibitisha alivyoshiriki," alisema na kuongeza kuwa;

"Lowassa ni rafiki wa karibu wa Rais Kikwete, bado ana nguvu serikalini ndiyo maana haguswi."Alisema hata makosa aliyofanya Bw. Lowassa yakifumbiwa macho lakini baadaye anaweza kushitakiwa. "Makosa yanayomkabili ni ya jinai ambayo hayafi hadi baada ya miaka 60," alisema na kufafanua kuwa hata serikali zijazo zinaweza kumfikisha mahakamani.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond, Dkt. Mwakyembe alisema yeye kama mwenyekiti hawezi kusema lolote kuhusu taarifa hiyo bali anasubiri kile kitakachowasilishwa na serikali.

“Unajua mimi nilikuwa mwenyekiti wa kamati sasa siwezi kusema lolote, waache Wabunge wengine waseme, mimi nikisema inaweza kutafsiriwa vibaya kwa kuwa nilikuwa mwenyekiti,” alisema Dkt. Mwakyembe.

Kauli hizo za wabunge zimekuja wakati serikali inatarajia kuwasilisha taarifa yake ya utekelezaji ya maazimio 23 ya Bunge kuhusu Richmond muda wowote kuanzia leo.
__________________

Nadharia 30 za Ufisadi

Africar T Kagema

Habari hii imeandikwa kwenye mitandao mbalimbali ingawaje chanzo kinaonekana kuwa ni kutoka kwa mwanafunzi mmoja ambaye amejipambanua kuwa ni "mwanaharakati, anayesomea Uongozi huko Ohio). Nimezileta hapa ili agalau wadau mpate chachu ya kuchambua zaidi na kutafakali jinsi ya kupambana na watu kama hawa kabla hawajafikia kukomaa.

NADHARIA THELATHINI KUHUSU UFISADI:
UNAVYOJITENGENEZA, KUJILINDA, NA NAMNA YA KUPAMBANA NAO.

Nadharia hii imeandikwa baada ya kutafakari matukio mbali mbali duniani yaliyotokea katika vipindi mbalimbali vya historia. Nadharia hii inajaribu kuchambua ufisadi pamoja na adhari zake na namna ya kupambana nao. Mwandishi alipoandika nadharia hii hakusoma kitabu au kazi ya mtu yeyote; wala hakuandika kwa mtiririko maalumu; bali alijaribu kutafakari na kuyaandika mawazo yake kama yalivyojitokeza ili kuchokoza mjadala, utafiti, au mchango zaidi kutoka kwa watu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wasomi, wataalamu wa sayansi ya jamii, na wahanga wa ufisadi. Lakini pamoja na kwamba nadharia hii ni ya awali, naamini inaweza kuwasaidia wana jamii kuufahamu kidogo ufisadi ulivyo na kufikiria namna ya kujipanga kupambana nao. Kwa watafiti na wasomi, itakuwa ni nafasi nzuri ya kuchambua zaidi, kutafiti na kuelimisha jamii zaidi juu ya adui huyu mkubwa wa mwanadamu.

1. Ufisadi ni aina fulani ya tabia inayojitengeneza ndani ya moyo wa mtu mwenye asili ya uchoyo na ubinafsi.

2. Ufisadi huanza kidogo kidogo katika maisha ya watu, hasa wale wanaopenda daima kuweka maslahi yao binafsi mbele zaidi kuliko ya wengine.

3. Kama haupigwi vita mapema katika jamii, ufisadi unakua na kujieneneza; na kasi ya kukua kwake inaongezeka kama kuna watu wanaoshabikia ‘mafanikio’ yanayotokana na ufisadi huo.

4. Ufisadi ulioachiliwa (ama kwa sababu ya hofu, kuoneana aibu, au vinginevyo) hujiimarisha kwa kujitengenezea mtandao wake mwenyewe.

5. Mtandao wa ufisadi usipovunjwa mapema hukomaa na kutengeneza tabaka la mafisadi katika jamii, ambao hutafuta namna ya kuhalalisha ‘matunda’ ya ufisadi wao.

6. Mojawapo ya njia inayotumika kuhalalisha matunda ya ufisadi ni kusaidia katika jamii, kutoa michango katika jamii au vyama, kuwekeza katika biashara, kusaidia wanasiasa kushinda uchaguzi, au kuingia serikalini; na ikibidi husaidia mafisadi wenzao kuingia kwenye siasa au shughuli nyingine muhimu.

7. Wakati wote, tabaka la mafisadi huteteana kwa siri, lakini wakishajiona wamekomaa hukosa aibu hivyo huteteana kwa wazi. Na kwa hiyo fisadi mmoja hawezi kumwadhibu fisadi mwingine isipokuwa wamekosana katika mambo au maslahi yao

8. Ufisadi uliojitengenezea tabaka huwa ni ngome ngumu kuivunja, kwani unatafuta mbinu zote kujilinda, kujitanua, na kujihalalisha.

9. Ufisadi uliokomaa hauna huruma, aibu, wala staha. Na unakuwa mkali kwa wale wanaojaribu kuupiga vita.

10. Mbinu kubwa ya ufisadi ni kusema uongo, kutumia vitisho, au kutumia nguvu yoyote ilioyokaribu nao (ya kipesa, kicheo, kichawi, kisilaha, kisiasa, kijeshi, kikabila, n.k.).

11. Mbinu ya uongo ikishindwa, vitisho vinatumiwa, vitisho vikishindwa nguvu hutumika kutetea maslahi yao.

12. Ufisadi ukipigiwa sana kelele na wananchi, unajipaka chokaa nyeupe kwa nje na kujifanya unaongoka, na hivyo kuwahadaa wananchi; kwa namna hiyo ufisadi hautenganishwi na unafiki.

13. Unafiki wa mafisadi una mbinu tatu. Mbinu ya kwanza ni ya kujisafisha kwa juu juu pasipo toba la kweli. Hilo lisiposaidia, mbinu ya pili hutumika ambayo ni kuwachafua watu wengine waliosafi ili kuiaminisha jamii kuwa kila mmoja ni fisadi hivyo wasifuatwefuatwe. Hilo lisipofaa, mbinu nyingine hutumika ambayo ni ya kuwachafua baadhi ya mafisadi wenzao wachache, na hasa waliobainika, ili watolewe kafara na wengine wapate kupona. Mbinu zote zikishindikana, mafisadi wanaweza kudhuru watu ili kujitetea.

14. Mtandao wa ufisadi unaweza ukawa wa sehemu moja kijiografia; au ukasambaa nchi nzima, na hata kuchukua sura ya kimataifa. Na unapovuka mipaka kuingia nchi nyingine, unatumia hila ya kuhadaa na kuwalainisha watu mashuhuri wa nchi au sehemu husika.

15. Kama jamii ya wapenda HAKI na KWELI isipojizatiti na kupambana na ufisadi, na ukiachiwa utawale jamii kama unavyopenda, matokeo katika jamii yanakuwa ni mabaya sana. Jamii inakuwa mtumwa wa ufisadi, na mafisadi wanakuwa kama wafalme wa kudumu.

16. Ufisadi unajidhihirisha katika sura mbalimbali kama vile rushwa kubwa na ndogo, ukandamizaji wa wanyonge, unyonyaji, kikundi kimoja kunyanyasa kingine, ubabe wa kiuchumi au kisiasa, biashara haramu (kama vile ya utumwa, madawa ya kulevya, bidhaa feki, biashara ya magendo, n.k.), uporaji wa mali na haki za wengine, demokrasia bandia, utawala mbovu, udikiteta, ajira mbaya kama vile ya watoto, n.k.

17. Baadhi ya matokeo mabaya ya ufisadi ni kuongezeka unyonge na umasikini; kuporomoka maadili; chuki za kitabaka, kisiasa, kikabila, au kivikundi; vita vya wenyewe kwa wenyewe; mauaji ya kikabila, kikoo, au kisiasa; kukosa kuaminiana katika jamii, ukoloni wa sura mbali mbali, maisha ya wasiwasi, n.k.

18. Kwa mantiki hiyo, ufisadi sio kitu cha kuchekea kabisa (hata kama unafanywa na ndugu wa kuzaliwa). Ni janga, aibu, na hatari kwa jamii au nchi yeyote ile. Pia ni ugonjwa mbaya unaoua kabisa maadili ya jamii, kwa maana vizazi vipya vinakosa mifano mizuri ya kuiga; pia vinakosa maongozi sahihi, licha ya kukosa haki zao za msingi na msaada wa kweli.

19. Lakini jamii pia lazima ifahamu kuwa ufisadi uliokomaa hauwezi kujiondoa wenyewe, maana unajikita kama ufalme mdogo ndani ya jamii. Ili kupambana nao, umoja wa wananchi, nguvu, busara, na maarifa yanahitajika.

20. Ufisadi hauwezi kupigwa vita na mafisadi, bali utapigwa vita na watu walio safi, wapenda maendeleo, haki, na kweli. Mwenye madoa ya kifisadi akipigana na mafisadi ataumbuliwa; ndio maana si rahisi kwa asiyesafi kupambana na mafisadi.

21. Vita ya kupambana na ufisadi inatoka ndani ya moyo wa dhati wa mpenda haki, amani, na maendeleo ya watu; inahitaji uvumilivu, ni vita ya muda wote, haitafuti mafanikio binafsi.

22. Vita ya kupambana na ufisadi inahitaji viongozi safi, wenye maono safi, wenye uadilifu, wanaoweze kuelezea umma malengo yao na kuhamasisha haki na kweli, na wanaoonyesha mfano wa kweli kupitia maisha yao wenyewe.

23. Vita ya kupambana na ufisadi sio lele mama, ina hitaji kujitolea kwa hali ya juu. Lakini matunda yake ni mazuri, yanaleta faraja kwenye jamii, na yanadumu kwa muda mrefu.

24. Kila mwana jamii aukemee ufisadi wakati wote na mahali popote anapouona, pasipo kujali kama ungemletea yeye faida fulani.

25. Viongozi wa taasisi zote za jamii, serikali, kidini, na kitaaluma wapige vita ufisadi wa namna zote, na wahamasishe watu wao kuupiga vita ufisadi. Wanapofanya hivyo wajisafishe kwanza ili wawe mfano kwa wananchi wao wenyewe.

26. Vyombo vya habari vina nafasi kubwa kusaidia wananchi katika vita hii, kwa kuendelea kufichua vitendo vya ufisadi, kuandika taarifa kwa busara, na kuhamasisha haki, kweli, na uadilifu katika jamii.

27. Inawezekana kupambana na kuushinda ufisadi, unyonge, na umasikini kama wanajamii wakimaanisha na wakikusudia kujiletea maendeleo ya haki na kweli.

28. Ikumbukwe kuwa ufisadi hauwezi kujiondoa wenyewe; wala malalamiko tu na kusimanga mafisadi haviwezi kuuondoa ufisadi. Wala ushabiki tu wa juu juu hauwezi kuuondoa ufisadi. Kinachohitajika ni juhudi na nguvu za dhati na za pamoja kati ya wananchi na viongozi wao, pamoja na taasisi za dini na zile zinazotetea haki za watu.

29. Kwa kuwa ufisadi unatumia mwanya wowote na hasa udhaifu fulani katika jamii, ni vema kuhakikisha kuwa maeneo yote ya kijamii yanaboreshwa (kama vile sheria za nchi na serikali za mitaa, kanuni na taratibu za taasisi, utendaji wa vyombo vya kusimamia haki na sheria, utawala bora, utendaji wa vyombo vya habari, demokrasia na ushirikishwaji umma, maadili ya viongozi, n.k.)

30. Ili kusaidia vizazi vijavyo, elimu na itolewe kuanzia ngazi ya shule za msingi. Elimu hiyo ilenge kuwasaidia vijana kuwa waadilifu, kuuchukia na kupambana na ufisadi. Kama vile tunavyopambana kulinda mazingira yetu, ni lazima kupambana pia kulinda jamii zetu na utu wetu. Mazingira ni muhimu, lakini ni kweli pia kuwa utu wetu ni muhimu zaidi. Maana utu wetu ukiharibiwa, na jamii ikiharibiwa na ufisadi, je mazingira hayo yatamsaidia nani?

Imeandikwa na mtanzania - mkereketwa wa haki na kweli, mwanafunzi wa uongozi, Ohio, Marekani.

Monday, October 26, 2009

Matokeo Serikali za Mitaa: CCM yafanya kufuru

• Yarejesha mitaa mingi iliyoshikiliwa na CUF D'Salaam-Tanzania Daima

na Waandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi mkubwa katika matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika nchini juzi.

Mkoani Dar es Salaam, chama hicho tawala kimeibuka na ushindi mnono kwa kupata viti 402 kati ya 448, sawa na asilimia 91, huku wapinzani wakiambulia viti 40, sawa na asilimia tisa tu.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema ushindi huo ni mkubwa ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi huo mwaka 2004 ambapo CCM ilipata viti 307 kati ya 387, sawa na asilimia 79, huku kambi ya upinzani ikiambulia viti 80, sawa na asilimia 20.

Alisema matokeo ya vitongiji sita, yamefutwa na kupangiwa tarehe nyingine za uchaguzi kutokana na wagombea kufariki dunia ghafla na maeneo mengine uchaguzi huo kufutwa kutokana na kuvurugika kwa taratibu za uchaguzi.

Hata hivyo, Guninita alisema matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa leo.

Kutoka mkoani Iringa, inaripotiwa kuwa CHADEMA, imefanikiwa kushinda mtaa mmoja wa Kihesa Kilolo "B", kwenye Kata ya Mtwivila Manispaa ya Iringa baada ya kuzoa kura zote kuanzia wajumbe wa mtaa hadi nafasi ya mwenyekiti.

Wakati CHADEMA ikiambulia mtaa huo mmoja, CCM imeshinda katika mitaa 13 kati ya 14 ya manispaa hiyo.

Hata hivyo, wafuasi wengi wa vyama vya upinzani, walipinga matokeo hayo kwa kuzomea, kwa madai kuwa CCM ilifanya hujuma kuhakikisha inashinda uchaguzi huo.

Kutoka mkoani Morogoro, CCM imeshinda mitaa 259 kati ya 274, iliyopo katika Manispaa ya Morogoro Mjini.
Vyama vingine na idadi ya mitaa waliyoshinda kwenye mabano ni CUF (10), TLP (4) na CHADEMA mtaa mmoja.
Hata hivyo katika matokeo ya jumla, vyama vya upinzani vimefanikiwa kuongeza viti witatu zaidi kutoka 12 ilivyopata mwaka 2004 hadi 15 vya mwaka huu.

Kutoka Kahama, mkoani Shinyanga, inaripotiwa kuwa Mtaa wa Korogwe, Kata ya Kahama anapoishi Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Hamis Mgeja, umechukuliwa na CHADEMA.

Habari kutoka Shinyanga, zilisema kuwa licha ya kampeni kubwa zilizofanywa na mwenyekiti huyo akiambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Zainabu Kawawa, mgombea Leonard Mayala wa CHADEMA, aliibuka kidedea kwa kupata kura 214, dhidi ya Amos Maganga wa CCM aliyeambulia kura 156.

Kushindwa kwa CCM katika mtaa huo, kumetokana na mizengwe iliyofanywa na chama hicho wakati wa kura za maoni, jambo ambalo liliwakasirisha wapiga kura, hivyo kuamua kuiadhibu CCM kwa kuichagua CHADEMA.

Mkoani Mbeya, taarifa zinasema CHADEMA, imeonyesha taswira ya kulitwaa Jimbo la Mbeya Vijijini katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kupata ushindi mnono katika vijiji vya Mbalizi na Ilembo ambavyo ni ngome ya CCM.

Katibu wa chama hicho Wilaya ya Mbeya Vijijini, Ipyana Seme, alisema mbali na ushindi katika vijiji hivyo, CHADEMA imeshinda vitongoji vya Ndola, Maguzi, Mlimareli na Tunduma Road vilivyopo katika Kijiji cha Mbalizi.Hata hivyo, matokeo ya jumla katika Wilaya ya Mbeya Vijijini, yanaonyesha CCM imepata viti 169, CHADEMA 6 na NCCR –Mageuzi kiti kimoja kati ya 180.

Mbali ya taarifa za matokeo, uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu ambapo watu 30 kutoka mkoani Dar es Salaam, Pwani na Mwanza, wanashikiliwa na polisi kwa madai ya kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa watu 18 walikamatwa katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mrisho Nyembo ambaye anadaiwa kusababisha vurugu zilizowajeruhi askari polisi mwenye namba E.6401 S/SGT Salaika Zomboko Kiborongwa, D.9490 D/CPL Lucas, F.80884 PC Sultani Bugoro, WP 3706 PC Asha na E.2122 D/C Hashimu.

Wengine ni Msafiri Gasper (31), Seif Ally Masoud (44), Khadija Salum (18), Bakari Hamisi (27), Rashid Hamad (25), Riziki Hamad (23), Hamis Amir (38) na Cleophace Barongo (45).

Kwa mujibu wa Kova, wengine ni Philipo Mikorogoro, Said Rashid (51), Hamisi Lupamba (45), Suleiman Kitamba (35), Funua Ally Funua (33), Gilbert Mushi na Azimio Milinga (39).

Hata hivyo, Kova hakuwataja watuhumiwa wengine wawili akisema bado uchunguzi dhidi yao unaendelea.

Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya vurugu katika vituo vya kupigia kura na kujihusisha na vitendo vya uharibifu wa mali.

Aidha, Kova alisema baadhi walikamatwa na vitabu vya orodha ya kupiga kura na kutumia majina mawili tofauti wakati wa kupiga kura.

Kutoka mkoani Pwani, watu watano wanashikiliwa na polisi kutokana na kufanya vurugu zilizoibuka katika maeneo mbalimbali ya uchaguzi.

Mmoja kati ya watuhumiwa hao, anadaiwa kulipiga teke sanduku la kupigia kura na kupasuka hatimaye kura kutawanyika na kusababisha uchaguzi huo kusitishwa hadi hapo utakapotangazwa tena.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma, aliwaambia waandishi wa habari mjini Kibaha kuwa, tukio hilo la kupiga teke limetokea katika Kijiji cha Mgomba, wilayani Rufiji.

Alimtaja anayetuhumiwa kupiga teke sanduku hilo kuwa ni David Malecela (41).

Wengine ni Hassan Hafif (53), Ramadhani Hojaj (45), Mwajabu Mnete na Marvelous Sylvester (30).

Kutoka mkoani Mwanza, inaripotiwa kuwa polisi lililazimika kutumia nguvu ya ziada kwa kufyatua risasi za moto katika vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi katika eneo la Machinjoni, Wilaya ya Nyamagana.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi nchini, Jamal Rwambow (RPC), alimtaja aliyepigwa risasi na kujeruhiwa kuwa ni Emmanuel Tungaraza (17).

“Polisi tulilazimika kutumia risasi kutuliza ghasia hizo, na katika matumizi hayo ya risasi, kijana mmoja alijeruhiwa maeneo ya tumboni, lakini hali yake inaendelea vizuri na kuna watu saba tumewakamata kutokana na vurugu hizo,” alisema Kamanda Rwambow.

Alisema, katika vurugu hizo, gari binafsi la Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Mwatex (OCS), lilipigwa mawe na wafuasi wa vyama vya siasa na kuharibika vibaya. “Mambo yalikuwa mabaya sana katika maeneo haya ya Machinjioni na Mahina shuleni... OCS wa Mwatex gari lake lilipondwa mawe na kuvunjwa vioo, lakini tunashukuru hakukutokea madhara zaidi,” alisema.

Alitaja maeneo mengine yaliyogubikwa na vurugu mkoani humo kuwa ni Wilaya ya Geita, Katoro na Rwamgasa na Kisiwa cha Nyakanyasi Chifunfu ambapo zilitokea vurugu baada ya mfuasi mmoja kutaka kubeba masanduku yote ya kura ili yasihesabiwe.

Taarifa hii imeripotiwa na Ghisa Abby na Anitha Challi, Morogoro, Francis Godwin, Iringa, Herman Meza, Shinyanga, Julieth Mkireri, Pwani na Andrew Chale, Dar.

Hivi ndivyo Lowassa alishiriki Richmond

Na Mwandishi wetu -Nipashe

26th October 2009

Nyaraka zaonyesha kila hatua aliweka mikono yake
Uthibitisho wa kuibeba Richmond watolewa peupe
Kumbe ndiye aliipora Tanesco kazi ya kusaka mzabuni

Wizara ya Nishari na Madini ilisubiri maamuzi yake .


Kilio cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, bungeni kwamba alidhalilishwa sana kwa kuhusishwa na mkataba tata wa kampuni ya Richmond, si lolote wala chochote baada ya uchunguzi wa kina wa nyaraka uliofanywa na gazeti hili kubaini kwamba alihusika vilivyo katika mchakato mzima wa zabuni hiyo.


Nyaraka kadhaa ambazo Nipashe imeziona, zimethibitisha si tu ushiriki wa Lowassa katika mchakato huo, bali alikuwa anatoa maelekezo ya nini kifanyike kwa kila hatua.


Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha, alibakia kuwa kama karani tu wa kutekeleza maagizo ya Lowassa, kila hatua alikuwa anaamua Lowassa na kuifanya Wizara ya Nishati na Madini kutekeleza kile alichotaka kiongozi huyo aliyejiuzulu Februari mwaka jana huku akilalamika kwamba ameonewa kwa kuzushiwa mambo kuhusu kashfa ya Richmond.


Akitii maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu Lowassa, Dk. Msabaha, naye alimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Athur Mwakapugi, Juni 21, 2006 akimwagiza atekeleze maagizo wa Waziri Mkuu ya kusaini mkataba na Richmond.


Kwa kifupi barua hiyo inasomeka hivi…“Iagize Tanesco iingie mkataba na kampuni ya Richmond kwa ajili ya umeme wa kukodisha haraka iwezekanavyo. Nakuletea nakala ya kibali kilichotolewa kutoka ofisi ya Mhe. Waziri Mkuu kwa kumbukumbu za Wizara.”


Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, Katibu Mkuu huyo, wakati huo, Arthur Mwakapugi, baada ya kupata maelekezo toka kwa waziri wake, naye alitoa maagizo siku hiyo hiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura, akimwagiza kuhakikisha shirika hilo linaingia mkataba na Richmond.


Maelezo hayo ambayo aliyaandika kwa mkono yalisomeka kwa kifupi... “Andaa barua kwa Mwenyekiti wa Tanesco kumuagiza waingie mkataba na Richmond.”


Taarifa zinaonyesha kuwa baada kampuni ya Richmond Development Company LLC kuingia mkataba na Tanesco Juni 23, 2006 na baada ya siku kusonga mbele bila kuwepo kwa dalili yoyote ya kupatikana kwa umeme wake katika kipindi cha siku 60 kama walivyosema wenyewe, maneno yalianza kuzagaa miongoni mwa wananchi, vyombo vya habari na hata baadhi ya wabunge, hivyo Lowassa akahisi kuwa kazi aliyokuwa ameisimamia kwa nguvu zote amechemsha na hivyo kutoa maelekezo mapya.


Katika maelekezo hayo, Lowassa kwa barua yake kwenda kwa Waziri Msahaba alisema: “Kama unavyofahamu yapo maneno mengi sana yanasemwa kuhusu uwezo wa kampuni tajwa (yaani Richmond) kuagiza Gas Turbines kama alivyopewa mkataba na Tanesco baada ya kushinda zabuni. Yameandikiwa pia kwenye Gazeti la Thisday la jana (20.09.06).

“Inawezekana hivi vikawa ni vita vya kibiashara. Lakini kwa sababu ya meneno hayo yanasemwa na watu wengi na tofauti ni vizuri UKAJIRIDHISHA kwamba kampuni hii itaweza kutekeleza kazi hiyo. Kama utaona shaka lolote ni vizuri kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu mapema ili tuweze kuchukua hatua zinazopasa mara moja.”

Aidha, Lowassa akijua kwamba kuna jambo linazidi kuumuka juu ya Richmond, katika barua hiyo ya Septemba 21, 2006 alijipa moyo akisema: “Kwa upande mwingine kwa kuwa malipo yake ni kwa L/C hawezi kupata nafasi ya ‘kuturusha’. Ila unachoweza kufanya ni kuweka utaratibu wa kumfuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba analeta ‘turbines’ hizo zenye kiwango na kwa wakati. Napenda kupata taarifa za ufuatiliaji wa suala hili kila siku; bila kukosa.”

Ushiriki wa Lowassa haukuishia kwenye barua hiyo aliyoandika na kuisaini mwenyewe Septemba 21, 2006 tu; bali ushiriki wake mwingine unaonekana katika waraka wa Waziri Msabaha, aliyegeuzwa karani katika mchakato mzima huo, kwenda kwa Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco, Balozi Flugence Kazaura.

Dk. Msabaha anamtaarifu Balozi Kazaura kuwa suala la kushughulikia mashine za umeme wa kukodi limekwisha kushughulikiwa na Waziri Mkuu Lowassa.

Katika barua hiyo ambayo pia Nipashe ilifanikiwa kuiona ya Aprili 12, 2006 inasema ifuatavyo:

“Nadhani hatukuelewana vizuri. Suala la kushughulikia gas turbines za kukodisha lilishashughulikiwa na Mhe. Waziri Mkuu, ambaye aliunda Kamati ya wataalam watatu – KM- Hazina, KM Nishati na AG. Nia ni kuliondoa suala zima kwenye mikono ya Menejimenti ya Tanesco ambayo imeshindwa kulishughulikia kwa ufanisi.”

Kwa barua hiyo, si tu kwamba Dk. Msahaba aliweka wazi msimamo wa Lowassa katika suala zima la ukodishaji wa mitambo hiyo, bali pia alionyesha jinsi ilikuwa imekubalika kuwaweka pembeni Tanesco ambao walikuwa ni wataalam wa mitambo hiyo kuliko mtu mwingine yeyote kwenye masuala ya uzalishaji umeme.

“Waache Kamati iliyoteuliwa kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na BODI yako na wataalam wa Tanesco kwa kadri watakavyoona inafaa. Pasiwe tena na picha kama vile Menejimenti ya Tanesco imerejeshewa kazi hiyo, maana huko kutakuwa ni kukiuka maagizo ya Mhe. Waziri Mkuu,” kwa kauli hiyo ni dhahiri Lowassa alikuwa ndiye anayejua mwelekeo wa kile alichokuwa anakitaka.

Mikono ya Lowassa katika sakata la Richmond haipo tu kwenye kumwagiza Dk. Msabaha na Kamati ya Makatibu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini pia inaonekana jinsi alivyobariki mapendekezo ya Timu ya Majadilino ya Serikali (GNT) iliyojadiliana na Richmond.

Kwa mujibu wa barua nyingine ya Waziri Msabaha ambayo pia Nipashe imefanikiwa kuiona ya Juni 17, 2006 siku sita tu kabla ya mkataba wa Richmond kusainiwa, inaonyesha alivyoelezwa hatua kwa hatua za majadiliano baina ya GNT na Richamond na jinsi utekelezaji wa mkataba utakavyokuwa.

Katika barua hiyo, Lowassa alielezwa gharama za kuleta mitambo hiyo na mpangilio mzima wa kuileta kwa awamu tatu, kwa kuonyesha alivyokuwa amelipa suala hilo kipaumbele, Juni 21, 2006 Lowassa kupitia kwa Katibu wake, aliyetambulika kama B. Olekuyan, alimtaarifu Katibu wa Waziri wa Nishati na Madini majibu ya bosi wake.

Majibu yalisema ifuatavyo: “Mheshimwa Waziri Mkuu amekubali mapandekezo na ushauri wa Mheshimiwa Waziri. Tafadhali mjulishe.”

Kwa kasi ya ajabu, siku hiyo hiyo, Dk. Msabaha akiwa anafanyia kazi majibu ya Lowassa, alimwagiza Katibu Mkuu wake, Arthur Mwakapugi, hatua za kuchukua juu mkataba wa Richmond.

“Serikali imekubali mapandekezo ya Wizara kuwa Tanesco iagizwe kuingia mkataba wa kuleta Gas Turbines za kukodisha za jumla ya MW 105.6 na kampuni ya Richmond kwa mtiririko uliopendekezwa katika makubaliano kati ya Kampuni ya Richmond ya Marekani na GNT,” ilisema barua hiyo na kuongeza kuwa:

“Iagize Tanesco iingie mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya umeme wa kukodisha haraka iwezekanavyo. Nakuletea kibali kilichotolewa kutoka kwa Ofisi ya Mhe. Waziri Mkuu kwa kumbukumbu za Wizara.”

Mwakapugi naye kwa kasi kama ya Waziri Msabaha, siku hiyo hiyo, aliagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco aagize Tanesco waingie mkataba na Richmond. Mkataba ambao kwa mujibu wa kumbukumbu za Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mchakato wa mkataba wa Richmond, ulisainiwa usiku kwa haraka hizo hizo siku mbili baadaye.

Mikono ya Lowassa pia ilionekana kwenye mkataba wa Richmond kama waraka wa ndani wa Waziri Msabaha kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara akieleza kuwa Waziri Mkuu ameamrisha Richmond wapewe dili nyingine ya kuzalisha megawati 40 za umeme.

Waraka huo wa Julai 13, 2006 baada ya kusainiwa kwa mkataba wa Richmond na Tanesco, unasema:

“Nimezungumza tena na Mheshimiwa Waziri Mkuu leo juu ya bei ya mitambo ya Aggreko. Msimamo ni uleule niliokueleza awali na ameagiza tuulize Richmond kama anaweza kutoa 40 MW kwa bei isiyozidi ile ile ya 4.99 cents per kwh na kama tunaweza kuipata basi achukuliwe Richmond.”

Kwa maelekezo ya Lowassa, Msabaha katika barua hiyo kwa Katibu Mkuu alisema:

“Nimempigia simu Mohamed Gire wa kampuni ya Richmond juu ya upatikanaji wa hizo MW 40. Gire amekubali kuwa anaweza kutoa MW 40 za ziada ifikapo Septemba na kwa bei hiyo ya USD cents 4.99 @ kwh. Amesema hatahitaji majadiliano mapya. Inatosha kama ataandikiwa barua tu ya nyongeza MW 40.”

Kwa mtiririko mzima wa kusakwa kwa Richmond, hakuna hata hatua moja ambayo Lowassa anaweza kudai hakuhusika katika mchakato mzima, na kama vile Dk. Msabaha alikuwa anajua kitakachotokea wakati wote alionyesha kwamba alikuwa akifanyia kazi maelekezo ya bosi wake, yaani Lowassa.

Kuna habari kwamba wakati Serikali itakapowasilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimo ya Bunge juu ya Richmond, hoja ya kutaka kusafishwa kwa Lowassa itaibuka ikilenga kuionyesha kwamba alionewa na Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mchakato wa mkataba wa Richmond na Tanesco

''Ni wazi kuwa Watanzania sasa hatudanganyiki kwani eulewa wetu ni mkubwa''

Friday, October 23, 2009

Wapenda maendeleo tusaidieni- Paroko wa Kyela

Na Pd. Raphael Kilumanga, Mbeya

PAROKO wa Parokia ya Mtakatifu Mathias Mulumba, Kyela katika Jimbo Katoliki la Mbeya, amewapongeza waamini wake kwa kujitolea kutumia nguvu zao kujenga kanisa na akatoa wito kwa wenye mapenzi mema kuwaunga mkono kwa hali na mali kukamilisha ujenzi huo.

Paroko huyo Padre Paul Mwanyalila, alitoa pongezi na wito huo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi parokiani kwake juma lililopita.

Alisema moyo waliouonesha waamini wa parokia hiyo katika kujiletea maendeleo, hauna budi kuigwa na jamii nzima kwani mtu anayeonesha bidii mwenyewe ni rahisi kusaidiwa pale nguvu zake zinapoishia.

Alisema waamini hao wamechangia nguvukazi na mali zao kwa ujenzi wa kanisa ambalo kwa mujibu wa tathmini za mwaka 1996, linagharimu jumla ya shilingi milioni 146/= za Kitanzania.

"Gharama hiyo ilikuwa kwa kipindi hicho na ni wazi kwamba sasa zimepanda," alisema.

Alitoa wito kwa Serikali, makanisa, mashirika na asasi za kidini na za kibinafsi; pamoja na watu wote wenye mapenzi mema na hasa wazawa wa Kyela popote walipo, kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha ujenzi huo.

Parokia ya Mtakatifu Mathias Mulumba, Kyela, ina waamini takribani 6000 na vigango zaidi ya14. Ilianzishwa mwaka 1968.

Ujenzi huo utakapokamilika, kanisa hilo litamudu kuhudumia waamni 1200.

Serikali, asasi na wafadhili mbalimbali wamekuwa wakisisitiza jamii kuchangia kwa juhudi katika kujiletea maendeleo na huku wakisema wako tayari kuwasaidia pale ambapo juhudi za kujiletea maendeleo zimekwama badala ya kutaka watu kutaka kusaidiwa kila kitu.

Hivi sasa ujenzi huo uko kaika hatua za kukamilisha msingi na kunyanyua ukuta.
Kwa yeyote mwenye mapenzi mema aliyeguswa na ombi hili, na kupenda kuunga mkono juhudi za waamini hao, atume mchango au msaada wake kwa: Paroko,


Parokia ya Kyela,
S.L.P. 170.
KYELA.

Tujikumbushe ya Richmond Tarehe 6 Feb, 2008

MUHTASARI (EXECUTIVE SUMMARY) WA TAARIFA YA KAMATI TEULE ILIYOUNDWA NA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 13 NOVEMBA, 2007 KUCHUNGUZA MCHAKATO WA ZABUNI YA UZALISHAJI UMEME WA DHARURA ULIOIPA USHINDI RICHMOND DEVELOPMENT COMPANY LLC YA HOUSTON, TEXAS, MAREKANI MWAKA 2006.

1.0 UTANGULIZIMheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 119 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007, naomba kutoa taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa tarehe 13 Novemba, 2007 na Bunge hili Tukufu kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura uliofanyika mapema mwaka 2006 na kuipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas, Marekani.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kwa niaba ya wajumbe wenzangu wa Kamati Teule kukupongeza wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwa uamuzi wa kuunda kamati hii maalum kwa lengo la kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya kikatiba ya Bunge katika kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake kwa niaba ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule kuwasilishwa na kuafikiwa na Bunge, uliwateua Wabunge watano wafuatao kuunda Kamati Teule ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 104(3) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2004:

(a) Mhe. Dk. Harrison George Mwakyembe, Mb
(b) Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya, Mb
(c) Mhe. Mohamed Habib Juma Mnyaa, Mb
(d) Mhe. Lucas Lumambo Selelii, Mb
(e) Mhe. Herbert James Mntangi, Mb

1.2 Hadidu za Rejea.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Novemba, 2007 uliipa Kamati Teule siku thelathini kukamilisha kazi yake na Hadidu za Rejea zifuatazo kwa ajili ya kutekeleza kazi hiyo ya uchunguzi:

1. Kubainisha Richmond Development Company LLC ni kina nani, na ni kampuni ya shughuli zipi na hivyo kupima uwezo wake kupatiwa zabuni ya kuleta nchini na kujenga mtambo wa umeme wa gesi wa MW 100;

2. Kutathmini mchakato mzima wa jinsi zabuni waliyoshinda Richmond ilivyoshughulikiwa kuanzia Kamati ya Zabuni hadi mwisho ili kujiridhisha kuwa sheria, taratibu, miiko na maadili ya zabuni yanayotawala zabuni za aina hiyo vilifuatwa au vipi;

3. Kutathmini mkataba baina ya Richmond Development Company LLC na TANESCO ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa masharti ya mkataba huo ukizingatia gharama na masharti mengine ukilinganisha na masharti yaliyomo katika mikataba ya aina hiyo iliyoafikiwa na TANESCO/Serikali;

4. Kubainisha huduma na misaada mbalimbali waliyopewa Richmond kama vile kufunguliwa Letter of Credit na kupima uhalali wake;

5. Kuziangalia na kuzitolea maoni taarifa za TAKUKURU, PPRA na taarifa zozote nyingine zilizoangalia utaratibu wa zabuni ya Richmond; na6. Kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na mchakato mzima wa Richmond ili kutoa mapendekezo ya kuboresha taratibu za zabuni kwa siku zijazo, kwa maslahi ya Taifa letu.

1.3 Utekelezaji wa Majukumu

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 104(3) ya Kanuni za Bunge, Toleo la mwaka 2004, wajumbe walinichagua kuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule. Aidha Mhe. Eng. Stella Manyanya (Mb) alichaguliwa kuwa Makamu mwenyekiti wa Kamati. Nakuomba, Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii ya awali kuwashukuru wajumbe wa Kamati kwa imani kubwa waliyotuonyesha mimi na Mhe. Eng. Manyanya ya kutuchagua kwa kauli moja kuiongoza Kamati Teule ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ilianza kazi yake mara moja kwa kukusanya na kuzisoma nyaraka mbalimbali za msingi kama vile Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC, Sheria ya Ununuzi wa Umma (Public Procurement Act) ya Mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005, taarifa ya uchunguzi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakati huo ikiitwa TAKURU, na taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority-PPRA) kuhusu suala hilo.

Vilevile, Kamati Teule ilianza kuandaa hati (summons) kwa mujibu wa vifungu 13(1) na 14(1) na (2) vya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ya Mwaka 1988 (Sura ya 296) za kuita mashahidi mbalimbali waliohusika kwa njia moja au nyingine katika mchakato wa zabuni hiyo ya uzalishaji wa umeme wa dharura.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 15 Disemba, 2007 jumla ya mashahidi 46 walihojiwa na maswali 2061 kuulizwa. Pamoja na Kamati Teule kutumia vyombo vya habari kuwatia moyo watu wenye ushahidi kuhusu suala hili ili wajitokeze na kuieleza Kamati Teule, hakuna shahidi hata mmoja aliyekuja kwa hiari yake mwenyewe bila kupelekewa hati ya kuitwa. Aidha, mashahidi wote waliotuletea maelezo kimaandishi kwa njia ya simu au barua, hawakuweka majina yao wala anuani zao, hivyo kuipa Kamati Teule wakati mgumu kufuatilia kauli zao.

Mheshimiwa Spika, matokeo haya yanaonesha hali halisi iliyopo Tanzania, hali ya uoga na ya kutojiamini inayowakumba Watanzania walio wengi wanapotakiwa kuelezea kwa uwazi maneno yale yale wanayoyanong'ona pembeni kwa hamasa kubwa. Kwa mtindo huu Taifa letu linaweza kuishia kuwa la walalamishi wasio na ujasiri wala dhamira ya dhati ya kukemea maovu pale inapobidi.Mheshimiwa Spika, mashahidi wengi walioitwa kwa hati hususan kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Katiba na Sheria walionyesha hofu, mashaka na hali ya kutojiamini kwa kutoa majibu yaliyofanana ya kiitifaki-itifaki na yaliyokosa mvuto na ushawishi wa kawaida mithili ya watu walioketishwa pamoja na kukaririshwa hoja za kujibu. Wataalam wa TANESCO, mathalan, waliikataa Richmond Development Company LLC mara tatu wakati wa kutathmini zabuni ya umeme wa dharura, kwa hoja za kitaalam kuwa haifai kwa vigezo vyote muhimu. Walipofika mbele ya Kamati Teule, wakawa wapambe nambari moja wa kampuni hiyo, wote wakiimba sifa za kulazimisha za kampuni hiyo!

Aidha, nyaraka nyingi ambazo Kamati Teule ilizipata toka Serikalini na taasisi mbali mbali, zilikuwa nakala zilizokosa mtiririko wa kimasijala. Kamati Teule ilipodai nyaraka halisi kulinganisha na nakala ilizokuwa nazo, ilipewa majalada yaliyoonyesha dalili zote za kukarabatiwa.

Mheshimiwa Spika, hali hii ilijitokeza zaidi kwa TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini. Jalada halisi kutoka TANESCO lilichukua siku tatu kuifikia Ofisi Ndogo ya Bunge likiwa na nyaraka zenye namba zilizokosa mtiririko stahili. Wizara ya Nishati na Madini ndiyo iliyotia fora kwa kumtuma Msaidizi wa Katibu Mkuu, Ndugu Julius Sarota tarehe 18 Disemba 2007 akiwa na maagizo ya kuwafungulia Wajumbe wa Kamati Teule kurasa maalum tu na si nyinginezo hivyo kuinyima Kamati Teule mtiririko halisi wa mawasiliano. Kamati Teule haikuridhishwa na utaratibu huo, hivyo ilimtaka Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu aondoke na majalada yake na kumpelekea hati ya kuitwa Katibu Mkuu, Ndugu Arthur Mwakapugi afike yeye mwenyewe na majalada hayo.

Tarehe 19 Disemba 2007 Katibu Mkuu huyo kwa maneno mengi na ya kuzunguka alithibitisha kuwa alichokifanya Msaidizi wake yalikuwa maelekezo ya Wizara. Kwa kuzingatia uhaba wa muda wa kukamilisha kazi ya Kamati Teule na kwamba suala hilo tayari lilikuwa limechukua siku tatu nzima za Kamati Teule, ugeni wa Katibu Mkuu huyo katika Wizara hiyo na katika masuala ya Bunge na uwezekano uliokuwepo kwa Kamati Teule kupata taarifa za ziada kupitia njia nyingine, Kamati Teule iliamua kusonga mbele na kumuacha Katibu Mkuu huyo na siri kubwa za Wizara yake.

Mheshimiwa Spika, ni kutokana na changamoto hizo Kamati Teule ikaona kuwa ni vyema baadhi ya Wajumbe wake waende Houston, Texas, Marekani ili kupata taarifa za kina na za ziada kuhusu suala hilo. Kamati Teule inakushukuru sana Mhe. Spika kwa kuzielewa changamoto zilizokuwa zinaikabili Kamati Teule na kuwawezesha Wajumbe watatu kwenda Washington DC kukutana na maafisa wa Ubalozi wetu, na Houston Texas kukutana na wamiliki wa Richmond Development Company LLC.

Mheshimiwa Spika, wajumbe hao walioondoka Dar-es Salaam kwenda Marekani tarehe 10 Disemba 2007 ni:

(a) Mhe. Eng. Stella Martin Manyanya, Mb
(b) Mhe. Lucas Lumambo Selelii, Mb
(c) Mhe. Mohamed Habib Juma Mnyaa, Mb, na
(d) Ndugu Anselm L. Mrema (Katibu wa Kamati)

Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Disemba 2007 Kamati Teule ilikuandikia barua kukuomba uiongezee muda kwa sababu kuu mbili: Kwanza, Wajumbe watatu kati ya watano na Katibu wa Kamati Teule walikuwa nchini Marekani kuanzia tarehe 10 Disemba 2007 kujiridhisha na taarifa mbalimbali ambazo Kamati Teule ilizipata kuhusu Richmond Development Company LLC. Kwa kuwa Wajumbe hao walikuwa wanategemea kurejea nchini tarehe 15 Disemba 2007 siku ambayo Kamati Teule ilitakiwa kuwasilisha taarifa yake na kwa kuwa taarifa ambazo wangezipata Marekani zingetakiwa kuingizwa kwenye taarifa ya Kamati Teule na hata kubadilisha baadhi ya masuala katika taarifa hiyo, muda wa ziada ulihitajika.

Pili, baada ya uchambuzi wa kina wa ushahidi wa maandishi na wa mdomo uliotolewa mbele ya Kamati Teule chini ya kiapo, Kamati Teule iligundua kuwepo kwa mgongano wa ushahidi, hivyo kutia mashaka juu ya dhamira ya baadhi ya mashahidi. Kamati Teule iliona umuhimu wa kuwaita tena baadhi ya mashahidi kuthibitisha kauli zao, na hata kuwachukulia hatua za kisheria baadhi yao ambao wangeendelea kusema uongo chini ya kiapo ili kulinda heshima ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, uliuona umuhimu wa kuiongezea muda Kamati Teule, hivyo tarehe 13 Disemba 2007 ukaridhia ombi la Kamati Teule na kuweka tarehe 31 Disemba 2007 kuwa tarehe ya kuwasilisha taarifa ya uchunguzi. Tunakushukuru sana kwa hatua hiyo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2007 siku ilipowasilisha taarifa yake kwako, Kamati Teule ilikuwa imewahoji jumla ya mashahidi 75 na kuuliza maswali 2717 na kuzipitia nyaraka na kumbukumbu 104. Mashahidi 4 kati ya hao walikuja kwa hiari yao bila kupelekewa hati za kuitwa. Mashahidi 7 waliitwa mara mbili. Mashahidi wawili, Ndugu Daniel Yona na Mhe. Rostam Aziz, (Mb) walipelekewa hati za kuitwa mbele ya Kamati Teule lakini hawakufika kwa maelezo kwamba walikuwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Ndugu Daniel Yona alitakiwa na Kamati Teule atoe maelezo kuhusu msingi wa uamuzi wake wa kuipa Richmond Development Company LLC, haki maalum ya kipekee (exclusive right) ya miezi 18 kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza mwaka 2004 wakati huo akiwa Waziri wa Nishati na Madini. Maelezo ya ziada ya mradi huu nitayatoa baadaye.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mhe. Rostam Aziz alitakiwa atoe maelezo kuhusu uhusiano wake na Kampuni za Richmond Development Company LLC na Dowans Holdings S.A baada ya mashahidi kadhaa kudai kuwa ana uhusiano nazo. Aidha, alitakiwa na Kamati Teule aeleze kwa nini anwani ya barua pepe ya kampuni yake ya Caspian Construction Ltd ilitumiwa na Dowans. Kamati Teule ilitaka vilevile kupata ufafanuzi kutoka kwake kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa kampuni yake wanaosemekana kuwa ni watumishi vilevile wa Dowans Holdings S.A.

Mheshimiwa Spika, leo tunapowasilisha taarifa hii mbele ya Bunge lako tukufu, tunajisikia kuutua mzigo mzito sana ulioanza kutuelemea kutokana na kuzongwa kila kukicha na kila aina ya uzushi, uchochezi, uchonganishi na hata vitisho. Tumezushiwa kuhongwa magari ya kifahari na fedha taslimu; tumetuhumiwa kuendesha vita dhidi ya Waislamu na mara nyingine tuhuma hiyo ikageuka kuwa vita dhidi ya Wakristo ndani ya Serikali; tumesingiziwa kuibadilisha taarifa yetu mara mbili, baadhi wakisema kwa ushawishi wa fedha, wengine wakidai kwa shinikizo la Mhe. Spika na wengine kwa shinikizo la Waziri Mkuu; tumeshuhudia pilikapilika za usiku na mchana za kujipanga na kuwashawishi baadhi ya Mawaziri na Wabunge kuikana taarifa hii na mapendekezo yake kiasi cha wengine wetu kujiuliza: kulikoni mtu asiye na hatia kuweweseka?

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya wajumbe wenzangu wa Kamati Teule, kukuhakikishia wewe binafsi na Bunge lako tukufu kuwa tumekamilisha kazi tuliyopewa kwa uaminifu na ujasiri mkubwa, dhamira safi, moyo wa uzalendo na kwa kumtanguliza mbele Mwenyezi Mungu katika kila tulilolifanya. Tulichukua kila tahadhari tusibanwe na mgongano wowote wa kimaslahi kiasi kwamba mjumbe mwenzetu, Mhe. Eng. Stella Manyanya, mwajiriwa wa muda mrefu wa TANESCO ambaye alikuwa kwenye likizo isiyo na malipo, akaamua kukatisha ajira yake kwa kujiuzuru. Aidha, tunakuhakikishia Mheshimiwa Spika kuwa hatukupokea senti tano ya mtu wala baiskeli yake. Mwenye ushahidi tofauti, basi alithibitishie Bunge hili tukufu. Mimi na wajumbe wenzangu wa Kamati Teule tuko tayari kuwajibika kisiasa.

2.0 UKAME NA TATIZO LA UZALISHAJI UMEME NCHINI

Mheshimiwa Spika, kwa takribani miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2002 nchi yetu ilikumbwa na tatizo la ukosefu wa mvua za kutosha. Athari za tatizo hilo hasa katika uzalishaji umeme, zilianza kuonekana mwaka 2004, na kufikia mwishoni mwa mwaka 2005 ikawa dhahiri kwamba nchi ilikuwa inaelekea kwenye janga kubwa la upungufu wa umeme. Mahitaji ya mitambo ya gesi ya kuzalishia umeme wa dharura yakajitokeza.

Kutokana na hali hiyo, mwezi Disemba 2005 TANESCO iliiomba Serikali kufikiria na kuidhinisha mpango wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kwa kutumia gesi kutoka kwenye makampuni yanayofahamika kwa biashara hiyo chini ya Mikataba ya kuuziana umeme kwa muda usiopungua miezi kumi na mbili.

Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Disemba 2005 Serikali ilikubali ombi hilo na kuiruhusu TANESCO kuwasiliana moja kwa moja na kampuni ya SONGAS iliyopo nchini kuhusu mahitaji hayo ya dharura. Bila kuchelewa TANESCO wakawasiliana na SONGAS ambayo ikaanza mara moja kuandaa makisio ya mradi huo. Tarehe 11 Januari 2006, CDC Globeleq, kampuni mama ya SONGAS, iliwasilisha TANESCO makisio ya kukodisha mitambo ya gesi ya kuzalisha umeme wa MW 74 ambayo ingefungwa Ubungo na kuanza kuzalisha umeme katikati ya mwezi Aprili 2006.

Tarehe 13 Januari 2006 Bodi ya Zabuni ya TANESCO ilianza kujadili zabuni hiyo ya CDC Globeleq na siku sita baadaye, yaani tarehe 19 Januari 2006, Bodi hiyo ikathibitisha mapendekezo ya zabuni hiyo na kuingia katika majadiliano na CDC Globeleq. Tarehe 30 Januari, 2006 Bodi ya Zabuni ya TANESCO iliyakubali mapendekezo ya Kamati ya Tathmini ya kuingia mkataba wa uzalishaji umeme kwa miaka mitano au mitatu kama ifuatavyo: (i) miaka mitano kwa bei ya senti za Kimarekani 3.2/kWh; au (ii) miaka mitatu kwa bei ya senti za Kimarekani 5.3/kWh. Chini ya mpango huo, mitambo hiyo ya kuzalisha umeme ingekuwa mali ya TANESCO baada ya kipindi cha kukodi kumalizika.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi pamoja na mapendekezo ya Wizara ya Nishati na Madini yaliwasilishwa na kujadiliwa katika Kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 10 Februari 2006, yaani siku nne baada ya kuanza mgao wa umeme kwa mikoa yote ya Tanzania Bara inayounganishwa na Gridi ya Taifa. Pamoja na mambo mengine, Baraza la Mawaziri liliweka msimamo wa Serikali wazi kuwa CDC Globeleq ikubali kuiuzia Serikali mitambo yake au iikodishe Serikali kwa bei ambayo Serikali ingeridhika nayo na siyo kwa kipindi cha miaka mitano bali kipindi kile tu cha matatizo ya umeme kutokana na ukame.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri haukuwa makini. Kwani siku hiyo hiyo ya tarehe 10 Februari 2006, Wizara ya Nishati na Madini, badala ya kuwatumia ujumbe sahihi CDC Globeleq kuwa Serikali inataka wabadilishe masharti yao kama nilivyokwishaeleza, ikapeleka ujumbe tofauti kabisa kuwa Serikali inafuta mpango wa kukodisha mitambo kutoka kwao.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kumhoji aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kipindi hicho Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha, (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ndugu Arthur Mwakapugi kwa muda mrefu na katika siku nne tofauti, Kamati Teule ilishindwa kupata majibu ya uhakika kwa maswali yake manne:

(i) Je, kulikuwa na kikao kingine cha Baraza la Mawaziri siku hiyo hiyo ya tarehe 10 Februari, 2006 kilichotengua maamuzi yake ya awali ya siku hiyo hiyo?

(ii) Ikiwa jibu ni hapana, kwa nini Wizara ilipeleka CDC Globeleq ujumbe tofauti na ule ulioagizwa na Baraza la Mawaziri?

(iii) Kwa nini Wizara isitume barua hiyo baada ya kushindwa kuwashawishi CDC Globeleq kubadilisha masharti yao?

(iv) Maamuzi kama hayo, siku nne ndani ya mgao wa umeme wa nchi nzima na katika kipindi ambacho Serikali haikuwa na mkakati mbadala uliokuwa umeiva kama wa CDC Globeleq, hayo kweli yalikuwa maamuzi makini ya kunufaisha Taifa?

Mheshimiwa Spika, kutokana na msimamo huo mpya wa Wizara, TANESCO ikaachana na mpango wa kukodisha mitambo na kuelekeza nguvu zake kwenye kununua mitambo mipya ya kuzalishia umeme. Hivyo, tarehe 20 Februari 2006, TANESCO iliwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini mpango wa ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa mitambo ya kuzalishia umeme wanaofahamika duniani chini ya utaratibu unaotambuliwa kama international shopping chini ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake.

Hatua hiyo ikafuatiwa na kikao cha Waziri wa Nishati na Madini na watendaji wa Wizara na TANESCO tarehe 21 Februari 2006 ambacho Waziri alikitumia kusisitiza kuwa mpango wa Serikali si kukodisha mitambo bali kununua na kuiagiza TANESCO kutangaza zabuni mara moja. Waziri alitaka tangazo la zabuni lichapishwe magazetini siku ya Alhamisi tarehe 23 Februari 2006 na kuwapa TANESCO masharti yafuatayo:

(i) zabuni ifunguliwe baada ya siku 10 (yaani tarehe 6 Machi 2006);

(ii) tathmini ya zabuni ifanyike kwa siku mbili (tarehe 7 - 8 Machi 2006).

2.1 Maandalizi ya Zabuni

Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Februari 2006 TANESCO iliomba idhini ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kutangaza zabuni hiyo kwa muda wa siku 10 badala ya siku 45 zinazoainishwa katika Kanuni za Ununuzi. Tarehe hiyo hiyo ya 22 Februari 2006, PPRA ikaijibu TANESCO kwa kuitahadharisha kuwa utaratibu huo utakuwa kinyume cha taratibu na Kanuni za ununuzi. Muda wa siku 10 hautoshi kuitisha zabuni ya kimataifa na kuweza kupata wazabuni wenye sifa zinazohitajika.

Mamlaka ikaishauri TANESCO kuwa badala ya kutumia njia ya kutangaza zabuni ya kimataifa (international competitive tendering) itumie njia mbadala ya ununuzi wa kimataifa (international shopping) ambapo makampuni mengi yanayotengeneza mitambo ya kuzalisha umeme yanaalikwa na "kuyashindanisha kwa kuyaomba yawasilishe zabuni zao badala ya kutangaza kwani utaratibu huo ungesaidia kuondoa makampuni ya kati yasiyohusika na uzalishaji umeme".
Mheshimiwa Spika, tarehe hiyo hiyo 22 Februari, 2006 TANESCO ikaiarifu Wizara kuhusu ushauri wa PPRA. Wizara ikaukataa na kuiagiza TANESCO kutekeleza agizo la Waziri bila kukosa kwa kuitangaza zabuni hiyo. Zabuni hiyo ikatangazwa kwa utaratibu wa ndani tarehe 23 Februari 2006. Hatua hiyo iliishitua PPRA ambayo iliiandikia barua TANESCO kuelezea kushangazwa kwake na hatua ya shirika hilo kukaidi ushauri wa kitaalamu na wa kisheria. PPRA ikasisitiza kuwa, njia pekee kwa TANESCO kupata wazabuni wazuri na wenye sifa stahili katika kipindi kifupi ni kutumia utaratibu ilioupendekeza wa international shopping.

Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji umeme nchini iliendelea kuwa tete na kulazimu kikao cha Baraza la Mawaziri kufanyika tarehe 23 Februari 2006, na kuagiza utaratibu wa haraka (fast track) wa kukodi mitambo ya kuzalishia umeme wa dharura ufanyike. Katika kutekeleza maamuzi hayo, Baraza liliagiza kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005 zizingatiwe. Pamoja na msisitizo huo wa Baraza la Mawaziri, Wizara ya Nishati na Madini ikaendelea kuishinikiza TANESCO kufuata maagizo ya Wizara na si vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, TANESCO ikionyesha dhahiri kusukumwa tu na Wizara, ikaiandikia tena PPRA Jumapili tarehe 26 Februari 2006 kuelezea kuwa sasa imeagizwa na Serikali kuitangaza zabuni hiyo magazetini, hivyo mamlaka hiyo ya udhibiti wa ununuzi wa umma itoe idhini ya kutangaza zabuni ya kimataifa kwa siku chache kuliko zilizowekwa na sheria. TANESCO huku ikijua kabisa kuwa PPRA isingeweza kuipata na kuijibu barua hiyo Jumapili, ikatangaza zabuni hiyo magazetini tarehe 27 Februari 2006 na kuwataka wazabuni wawasilishe zabuni zao tarehe 6 Machi 2006 yaani siku 10 baada ya kuchukua nyaraka za zabuni tarehe 24 Februari 2006.

Tarehe 1 Machi 2006 PPRA ikaijibu TANESCO kuwa pamoja na kuendelea na zabuni hiyo, isingekuwa rahisi kwa Shirika hilo la umeme la Taifa kupata mzabuni anayefaa katika kipindi hicho kifupi cha siku 10. Hata hivyo PPRA ikaitaka TANESCO kuufuatilia utaratibu mzima wa zabuni hiyo kwa karibu ili kuhakikisha kuwa taratibu zinafuatwa, ili kuepusha malamiko yasiyo ya msingi kutoka kwa wazabuni.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuipongeza PPRA kwa kuonyesha subira ya hali ya juu, uwazi na ukweli wa kitaaluma, Kamati Teule ilishindwa kubaini moja kwa moja chanzo cha ujasiri wa kiburi ndani ya Wizara ya Nishati na Madini kiasi cha kupindisha maamuzi ya Baraza la Mawaziri kama tulivyoona na kukaidi ushauri wa Mamlaka iliyowekwa kisheria. Aidha Kamati Teule ilishangazwa na Ofisi ya Waziri Mkuu iliyokuwa ikifuatilia kwa karibu sana mchakato huo, kushindwa kukemea ukaidi huo wa Wizara ya Nishati na Madini.

2.2 Mchakato wa Zabuni ndani ya TANESCO

Mheshimiwa Spika, hadi muda wa zabuni ulipoongezwa, yaani tarehe 20 Machi 2006, jumla ya wazabuni ishirini na sita (26) walinunua nyaraka za zabuni zilizouzwa kwa fedha isiyorejesheka (non refundable) ya Dola za Kimarekani 100. Ni wazabuni wanane (8) tu ndio waliorudisha nyaraka za zabuni hiyo kama ifuatavyo:

(i) M/S Aggreko International Projects Ltd ya Uarabuni,

(ii) M/S Quantus ya Ujerumani,

(iii) M/S APGUM Co. Ltd ya Ujerumani,

(iv) M/S Globeleq Ltd ya Kanada,

(v) M/S Real Energy Projects ya Uingereza,

(vi) M/S Renco SPA ya Italia,

(vii) M/S Richmond Development Company LLC ya Marekani, na

(viii) M/S GAPCO(T) Ltd ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, zabuni zikafunguliwa na wazabuni wote wanane waliorudisha nyaraka zao za zabuni waliwakilishwa kwenye ufunguzi. TANESCO ikaunda Kamati ya Kutathmini Zabuni iliyokuwa na wajumbe 12, kati yao wanane walitoka TANESCO, wawili kutoka kampuni ya ushauri ya Lahmeyer International, mmoja kutoka Wizara ya Fedha na mwingine Wizara ya Nishati na Madini. Kamati hiyo ilipewa wiki moja tu kumaliza kazi yake na kuiwasilisha taarifa ya tathmini kwenye Bodi ya Zabuni ya TANESCO tarehe 28 Machi, 2006.

2.3 Vigezo vya Tathmini (Preliminary Evaluation)

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Tathmini ikitumia vigezo mahsusi karibu ya 30 vya kupima uwezo wa mzabuni, ikathibitisha kuwa hakuna mzabuni hata mmoja kati ya wanane aliyetimiza au kukidhi vigezo vya zabuni vilivyowekwa. Kutokana na hali ya kutisha ya ukosefu wa umeme nchini, Kamati ya Tathmini ikalazimika kuondoa zaidi ya nusu ya vigezo na kubakiza tisa tu ilivyoviona muhimu sana kwa ngazi ile ya uchambuzi ili kumpata mshindi katika kundihilo la wazabuni wanane. Vigezo vilivyobakizwa ni:

(i) Muda wa kuleta mtambo na kuanza kazi,

(ii) Dhamana ya zabuni (Tender Security),

(iii) Uwepo wa mtambo tayari kuletwa Tanzania,

(iv) Uzoefu wa mzabuni kutekeleza miradi/ kuendesha mitambo ya aina hiyo,

(v) Uzoefu na sifa za kitaaluma/ kiufundi za mzabuni,

(vi) Viambatisho vya idhini ya kisheria kuweza kufanya maamuzi ya mwisho (Power of Attorney),

(vii) Uwepo wa maelezo ya lazima ya kiufundi,

(viii) Ujazaji fomu ya zabuni kikamilifu, na

(ix) Mchanganuo wa bei/ gharama ya umeme.

Mheshimiwa Spika, wazabuni wote wanane wakafanyiwa tathmini ya pili kwa kuzingatia vigezo hivyo tisa tu. Hata hivyo matokeo yakawa yale yale. Wazabuni wote wanane wakashindwa kukidhi vigezo hivyo vichache.Mheshimiwa Spika, nyaraka tulizozipata kutoka TANESCO zinaonyesha maeneo mbalimbali ya udhaifu miongoni mwa wazabuni hao kama ifuatavyo:-

i) M/S Aggreko International Projects Ltd ya Uarabuni ilikutwa na maeneo 7 yenye mapungufu,(ii) M/S Renco SPA ya Italia maeneo 9,

(iii) M/S APGUM Co. Ltd ya Ujerumani maeneo 12,

(iv) M/S GAPCO(T) Ltd ya Tanzania maeneo 13,

(v) M/S Globeleq Ltd ya Kanada maeneo 14,

(vi) M/S Real Energy Projects ya Uingereza maeneo 15,

(vii) M/S Quantus ya Ujerumani maeneo 16, na

(viii) M/S Richmond Development Company LLC ya Marekani ilikutwa na maeneo 17 yenye mapungufu.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Tathmini haikuona busara kutangaza kuwa imeshindikana kabisa kumpata mshindi. Hivyo, ikapunguza vigezo zaidi na kubakiza vitano tu kama ifuatavyo:

(i) muda ambao mtambo utaanza kazi,

(ii) uwepo wa mtambo tayari kuletwa Tanzania,

(iii) uzoefu wa mzabuni kutekeleza miradi/kuendesha mitambo ya aina hiyo,

(iv) uzoefu na sifa za kitaaluma/ kiufundi za mzabuni, na

(v) uwepo wa maelezo ya lazima ya kiufundi.

Katika hatua hii wazabuni wanne (4) wakashindwa kukidhi vigezo vichache vilivyobakizwa, hivyo kushindwa kufuzu kuingia hatua ya pili ya kufanyiwa tathmini ya kina (detailed evaluation). Wazabuni wengine wanne wakaonekana kuwa na afadhali kidogo na kuruhusiwa kuingia hatua ya pili ya kufanyiwa tathmini ya kina. Nao ni:

(i) M/S Real Energy Projects ya Uingereza,

(ii) M/S Renco SPA ya Italia,

(iii) M/S GAPCO(T) Ltd ya Tanzania, na

(iv) M/S Richmond Development Company LLC ya Marekani.

Mheshimiwa Spika, tathmini ya kina ya wazabuni hao wanne walioonekana afadhali kidogo, ilionyesha kuwa Richmond Development Company LLC ya Marekani bado ilikuwa na mapungufu mengi yaani 13 kupita wazabuni wengine watatu. M/s Renco SPA ya Italia ilifuatia kwa kuwa na mapungufu 10; M/s GAPCO (T) Ltd ya Tanzania mapungufu 9 na M/s Real Energy Project ya Uingereza mapungufu 8. Kamati ya Tathmini iliwasilisha matokeo ya tathmini kwa Bodi ya Zabuni ya TANESCO ikielezea kwamba hakuna mzabuni hata mmoja aliyetimiza masharti, hivyo wote walikosa sifa za kupata zabuni. Hivyo Kamati ikashauri zabuni itangazwe upya.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Zabuni ya TANESCO baada ya kuridhia mapendekezo hayo, iliyawasilisha kwenye Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO tarehe 30 Machi 2006. Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ilipitia tathmini nzima na kuamua kwa kauli moja kuishauri Serikali kurejea kwenye ushauri wa PPRA wa kutumia njia ya international shopping ili kupata quotations moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa mitambo ya kuzalishia umeme kwa gesi.

Kesho yake, yaani tarehe 1 Aprili 2006 Waziri wa Nishati na Madini, wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha, (Mb.) akionesha dhahiri kutotaka njia ya international shopping kutumika, akawaita wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO na kuwaagiza wahakikishe kuwa Bodi ya Zabuni ya shirika inawaita tena wazabuni wote waliojitokeza awali na makampuni mengine yoyote yenye uwezo wa kuingiza nchini mitambo hiyo. Aidha, Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha, (Mb.) alisisitiza kwa barua kwamba:"Mshindi wa tenda ya ununuzi wa mitambo mipya atajulikana baada ya idhini ya Serikali kutolewa. Composition ya wajumbe wa TANESCO Tender Board ibadilishwe na kuimarishwa kwa kuwa na wajumbe wenye uwezo na ni pro-active".

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa agizo hili la Waziri lilikuwa batili kwani Sheria ya Ununuzi wa Umma haimpi Waziri mamlaka ya kuingilia uteuzi wa Wajumbe wa Bodi za Zabuni za mashirika yaliyo chini ya Wizara yake. Agizo hilo la Waziri likafuatiwa na uamuzi wa Waziri Mkuu wa kuliondoa suala hilo mikononi mwa TANESCO na kulikabidhi kwa Kamati Maalum iliyokuwa inaundwa na Katibu Mkuu (Hazina), Katibu Mkuu (Nishati) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tarehe 13 Aprili 2006, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TANESCO wakati huo, Bw. Adriaan Van De Merwe, akaiondoa TANESCO rasmi kutoka kwenye mchakato huo kwa kumtumia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini nyaraka zote kuhusu zabuni yenyewe na uchambuzi wote uliofanywa na TANESCO.

2.4 Mchakato wa Zabuni Ndani ya Wizara

Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Aprili 2006, Wizara ya Nishati na Madini iliamua kuunda timu ya wataalamu ili ichague mzabuni mmoja kati ya wanane walioshiriki kwenye zabuni na kufanya naye majadiliano ya mkataba. Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ilikuwa tayari imejiandaa na kamati zake zifuatazo: Kamati ya Makatibu Wakuu, Kamati ya Watalaam na Kamati ya Serikali ya Majadiliano.Kamati ya Makatibu Wakuu iliundwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 10 Februari 2006, ikiwajumuisha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kamati hii ilipewa jukumu la kusimamia mchakato mzima wa zabuni. Ili kuharakisha zoezi hilo, Serikali iliunda Kamati ya Wataalam (Team of Experts) ili kuisaidia kwa karibu Kamati ya Makatibu Wakuu.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule iligundua kuwa Kamati ya Wataalam ndiyo iliyokuwa inafanya maamuzi ya msingi katika mchakato huu na iliyokuwa na mawasiliano ya karibu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, kwani kufuatana na ushahidi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ndugu Gray Mgonja, Kamati ya Makatibu Wakuu ilikutana mara moja tu toka iundwe.

Kazi ya kwanza ya Kamati hiyo ya Wataalam ilikuwa ni kupitia upya na kuichambua tathmini iliyofanywa na TANESCO. Kazi ya pili ya Kamati hiyo ilikuwa ni kumpata mzabuni ambaye angeweza kutekeleza mradi huo wa umeme wa dharura kwa haraka. Katika kutekeleza majukumu yake, Kamati hiyo ikatupilia mbali vigezo vya msingi vilivyotumika na Kamati ya Tathmini ya TANESCO na kuweka vipya ambavyo, kwa maoni ya Kamati Teule, vilifanana na vigezo vya mchezo wa zamani wa watoto wa sadakarawe: "mwenye kupata apate, mwenye kukosa akose".

Mheshimiwa Spika, vigezo hivyo vilikuwa:

(i) Uwepo wa mitambo yenyewe pamoja na mitambo ya akiba,

(ii) Uunganishwaji wake kwenye gridi ya Taifa,

(iii) Hali ya usalama wa mitambo yenyewe kwa kulinganisha na usalama wa gridi ya Taifa,

(iv) Muda wa kuleta mitambo, na

(v) Bei ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa maoni ya Kamati Teule vigezo hivyo vilikuwa haviendani na uzito na utaalam wa kazi iliyokusudiwa. Pia vilikuwa vinatoa mwanya bayana kwa wazabuni hata walio dhaifu kupenyezwa.

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Wataalamu ikawaalika wazabuni wote 8 kwa usaili wa kuwapima kufuatana na vigezo hivyo vipya. Mzabuni mmoja kati ya wazabuni wanane, M/S GAPCO (T) Ltd hakushiriki. Baada ya usaili huo, Kamati hiyo ikapata wazabuni wanne ambao walionesha kukidhi vigezo hivyo vipya. Wazabuni hao ni: Richmond Development Company LLC, Renco SPA,

Aggreko International Projects Ltd na APGUM Co. Ltd.Aggreko International Projects Ltd walidai kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 40 kwa senti za Kimarekani 6.0/kWh; Renco SPA walidai kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 60 kwa senti 10.0/kWh; Richmond Development Company LLC alidai kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 100 kwa senti 4.99/kWh; na APGUM Co. Ltd ilidai kuwa na uwezo kuzalisha umeme wa MW 100 kwa senti za Kimarekani 5.4/kWh.

Mheshimiwa Spika, kutokana na madai hayo ambayo hayakuwa na uthibitisho, Kamati ya Wataalamu ikaipendekeza Richmond Development Company LLC kuingia kwenye majadiliano ya mkataba na Serikali. Katika kuhalalisha ushindi huo wa Richmond Development Company LLC wajumbe wote wa Kamati hiyo ya wataalamu, Waziri wa Nishati na Madini aliyetangulia Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb), Waziri wa sasa wa Wizara hiyo, Mhe. Nazir Karamagi (Mb), Katibu Mkuu wake, Ndugu Arthur Mwakapugi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Johnson Mwanyika, (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ndugu Gray Mgonja na maafisa wote waandamizi wa Serikali na TANESCO waliotoa ushahidi mbele ya Kamati Teule, walitoa kauli zilizofanana mithili ya wimbo maarufu kuhusu sifa za Richmond Development Company LLC zilizoifanya ishinde, kuwa:

(i) kwanza, bei yake ya umeme ilikuwa chini kupita makampuni mengine;

(ii) pili, kampuni hiyo ilikuwa na ubia na kampuni kubwa na maarufu duniani ya Pratt & Whitney ya Marekani inayotengeneza mitambo mbalimbali ya umeme; na

(iii) tatu, iliwasilisha pendekezo lake kama mwendelezaji miradi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na wimbo huo wa Richmond kunoga, Kamati Teule ilishangazwa na udhaifu mkubwa wa hoja hizo uliokuwa haulingani kabisa na ujuzi na uzoefu walionao watendaji wa TANESCO na Serikali, hivyo kujenga hisia kuwa Richmond Development Company LLC ilibebwa. Kwa mfano, hoja ya kwanza inayohusu bei iliyopendekezwa na Richmond Development Company LLC kuwa ilikuwa ndogo, haijitoshelezi. Je, Kamati hiyo ililinganisha bei hiyo na kigezo kipi? Kwani katika kuangalia kumbukumbu za mchakato wa majadiliano, Kamati hiyo haikuwa na kiwango chochote cha makadirio ya bei ya umeme wa kukodi ambacho kingetumika kama kigezo cha kupima unafuu huo kama ulikuwepo badala ya kulinganisha na bei kubwa za makampuni ambayo yalikwisha tubebesha mzigo mkubwa wa malipo hapo awali.

Aidha, Kamati Teule ilipata tetesi na baadaye ushahidi kuwa Richmond Development Company LLC ilikuwa na wapambe ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO waliokuwa wanaipa taarifa (insider dealing). Mfano mdogo tu ni wa Ndugu Mohamed Saleh, aliyekuwa Mkurugenzi wa Usambazaji wa TANESCO na rafiki wa karibu wa wamiliki wa Richmond Development Company LLC. Alishiriki kwenye Kamati ya Wataalam na Kamati ya Serikali ya Majadiliano. Alipostaafu tu TANESCO, akawa mmoja wa wahandisi waandamizi wa DOWANS HOLDINGS S.A iliyochukua majukumu ya Richmond Development Company LLC.

Pili, Mheshimiwa Spika, hoja ya kwamba kampuni hiyo ilikuwa na ubia na kampuni kubwa ya Pratt & Whitney, haikuwa ya kweli. Katika mchakato wote wa zabuni ndani ya TANESCO, moja ya masuala kadhaa yaliyoifanya Richmond Development Company LLC isitiwe maanani, ni ukosefu wa ushahidi wa kisheria wa ubia (consortium agreement) kati yake na Pratt & Whitney. Baada ya kubanwa na Kamati Teule kuhusu ushahidi wa mahusiano wa kampuni hizo mbili, Wajumbe wa Kamati ya Wataalamu waliwasilisha mbele ya Kamati Teule ushahidi wa aina mbili: kwanza business card ya mzungu mmoja aliyejulikana kwa jina la John Perun aliyejiita mwakilishi wa Pratt & Whitney, na pili, kivuli cha mkataba wa kurasa nne kati ya Richmond Development Company LLC na Pratt & Whitney wa kubadilishana taarifa na siyo kuzalisha umeme. Aidha mkataba huo ulikuwa haujathibitishwa na wakili au shahidi yeyote wa kuaminika kuwa mkataba halali. Kamati Teule imesikitishwa na kushangazwa kwa kiwango cha chini cha umakini kilichoonyeshwa na wataalam wetu hususan kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kushughulikia suala hili.

Mheshimiwa Spika, viongozi wote wa Serikali waliohojiwa na Kamati Teule walisisitiza kuwa uamuzi wa kuipa Richmond Development Company LLC kazi hiyo ya kuzalisha umeme wa dharura, ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na madai ya kampuni hiyo kuwa na ubia na kampuni maarufu ya Pratt & Whitney. Hivyo basi, ushahidi wa uhusiano wa kisheria wa Kampuni hizo mbili, ulikuwa suala la msingi ambalo wataalamu wetu waliwajibika kulipa uzito ili kulinda maslahi ya nchi.

Katika tovuti yake (http://www.rdevco.com/) Richmond Development Company LLC ilikuwa inajitangaza kimataifa kuwa kampuni yenye miradi mikubwa Tanzania ya ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha michezo, ujenzi wa bomba la mafuta la kilometa 1,150 na ukarabati wa viwanja kadhaa vya ndege. Kamati Teule ilishindwa kuelewa kwa nini Kamati ya Wataalam haikuihoji Richmond Development Company LLC kuhusu uongo huo bayana ambao ulikuwa ushahidi wa kutosha kuipotezea sifa za kuwa mzabuni.

Hoja ya tatu, Mheshimiwa Spika, ya kwamba Richmond Development Company LLC ni mwendelezaji miradi, ilitakiwa vile vile ifanyiwe kazi badala ya kuiamini tu. Wizara ya Nishati na Madini haiwezi kukwepa lawama kwa kufumbia macho ukweli kuwa Richmond Development Company LLC ilishakuwa na Mkataba na Wizara hiyo uliosainiwa tarehe 30 Juni 2004, Mkataba uliovunjika mwezi Januari 2006 kwa kampuni hiyo ya Kimarekani iliyojitambulisha kama mwendelezaji miradi kushindwa kutekeleza sehemu yake ya mkataba. Wizara inaelewa fika kuwa kampuni hiyo ilishindwa utekelezaji kutokana na kuyumba kifedha. Mwendelezaji miradi gani ambaye anashindwa kumudu hata fedha ya kununulia maafisa wake tiketi ya ndege kutoka Dar-es-Salaam hadi Afrika Kusini na kurejea, kama ilivyoelezwa na Mkurugenzi wa Tanzania Green Company Ltd?

Mheshimiwa Spika kama tulivyodokeza hapo awali, baada ya Kamati ya Wataalam kumaliza kazi yake na kuwasilisha taarifa Serikalini, Kamati ya Serikali ya Majadiliano (Government Negotiation Team) ikiwa na wajumbe kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha, Benki Kuu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikaanza mchakato wa majadiliano ya mkataba na Richmond Development Company LLC.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyotokea kwa Kamati ya Wataalam, Government Negotiation Team vile vile haikufanya kazi ya kuridhisha japokuwa ilikuwa na uwakilishi mpana. Kwa mfano, suala la kukosekana kwa consortium agreement kati ya Richmond Development Company LLC na Pratt & Whitney halikuwasumbua kabisa wajumbe wa Kamati ya Serikali ya Majadiliano. Wajumbe hao, akiwemo mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waliichukulia business card ya Bwana John Perun na mkataba wa kubadilishana taarifa kati ya kampuni hizo mbili kuwa ushahidi wa kutosha wa ubia au ushirikiano. GNT ilishindwa hata kusisitiza kuwa ubia wa kampuni hizo uwekwe wazi katika mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Cpompant LLC.

Aidha, kwa kuelewa kuwa Richmond Development Company LLC haikufanyiwa uchunguzi wa awali (due diligence) GNT ilishindwa kupendekeza kwa Serikali umuhimu wa kuifanyia Kampuni hiyo uchunguzi baada ya kuiteua (post-qualification) kujua uwezo wake kifedha, kiutendaji, kiutalaam na kiuzoefu. Katika mahojiano na Wajumbe wa GNT, Kamati Teule iligundua kuwa masuala mengi waliyapitisha kwa mazoea tu, baadhi ya wajumbe wake wakiamini kuwa mikataba ya aina hiyo inatoka Benki ya Dunia na vipengele vyake havibadiliki. GNT ilifika mahali ikakubali bila vigezo vya kueleweka kwamba Richmond Development Company LLC ikichelewesha utekelezaji wa mradi itailipa TANESCO faini ya Dola za Kimarekani 10,000 au sh. milioni 12.5 tu kwa siku, lakini Richmond itaidai TANESCO ilipe Dola za Kimarekani 121,811 au sh. milioni 152 kila siku hadi mwisho wa mkataba kama gharama za kudumu za uwezo wa mitambo yao (capacity charges), wazalishe umeme, wasizalishe! Haiingii akilini!Mheshimiwa Spika, tarehe 19 Juni, 2006, Bodi ya Zabuni ya TANESCO ilikutana na kupitisha uamuzi rasmi wa kufuta zabuni waliyokuwa wanashughulikia awali na kutangaza kuwa "TANESCO isihusishwe na mkataba wowote utakaotokana na nyaraka za zabuni waliyoifuta".

Lakini siku hiyo hiyo ya tarehe 19 Juni 2006, Waziri wa Nishati na Madini alimwandikia Waziri Mkuu dokezo kuwa majadiliano ya awali na Richmond Development Company LLC yamekamilika hivyo Serikali iiteue kampuni hiyo kwa lengo la kuingia mkataba na TANESCO wa kuzalisha umeme wa dharura kwa miaka miwili. Sehemu ya barua hiyo inasomeka:"Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) inayojumuisha wataalam kutoka Wizara Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Benki Kuu na TANESCO ilifanya majadiliano na Richmond Development Company LLC ya Houston, Marekani kutoka tarehe 8 hadi 16 Juni 2006, kwa kuzingatia maelekezo yako."

Mheshimiwa Spika, tarehe 21 Juni 2006, Katibu wa Waziri Mkuu Ndugu B. Olekuyan aliiandikia Wizara ya Nishati na Madini kuitaarifu kuwa Mhe. Waziri Mkuu amekubali mapendekezo na ushauri wa Waziri wa Nishati na Madini kama ulivyokuwa umeletwa.

Siku hiyo hiyo tarehe 21 Juni 2006, Waziri wa Nishati na Madini akamwandikia dokezo Katibu Mkuu wake aiagize TANESCO iingie mkataba mara moja na Richmond Development Company LLC baada ya Waziri Mkuu kuidhinisha mapendekezo ya Wizara. Muda mfupi baadaye, kwa kutekeleza agizo la Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini akamwandikia barua Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Balozi Fulgence Kazaura kumwagiza ahakikishe kuwa TANESCO inasaini mkataba na Richmond Development Company LLC.

Mheshimiwa Spika, Ijumaa ya tarehe 23 Juni 2006, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa TANESCO, Bwana Johannes .G. Lottering, aliitwa Wizara ya Nishati na Madini na kuagizwa kusaini Mkataba huo kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC. Pamoja na kusita kwake, hatimaye alisaini mkataba huo.

Kamati Teule inaelewa hisia walizokuwa nazo viongozi wa ngazi mbalimbali wa TANESCO kutokana na uongozi wa kiimla wa Wizara ukipata nguvu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Tulichokiona awali kwa maana ya mchakato wa Zabuni kuchukuliwa na Wizara, ulikuwa ukiukwaji wa sheria na utaratibu mzima wa uwajibikaji. Pamoja na dharura iliyokuwa inaikabili Taifa, Serikali haiwezi kuwa kinara wa kuvunja sheria za nchi. Ni maoni ya Kamati Teule kuwa Wizara ilikiuka siyo tu masharti ya sheria na kanuni za ununuzi wa umma, bali vilevile maagizo mbalimbali ya Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule isingelikerwa sana na matukio haya kama Wizara ambayo ni taasisi ya ununuzi (procurement entity) kama ilivyo TANESCO, ingemalizia mchakato wake kwa kusaini mkataba huo yenyewe. Kuishinikiza TANESCO kusaini mkataba ambao vyombo vyake halali vilikuwa havijaupitia, ni udanganyifu, upotoshaji wa hali ya juu wa taratibu za kazi na sheria na udhalilishaji wa vyombo vya maamuzi ndani ya TANESCO. Inashangaza kuwa baada ya kudhalishwa na Wizara kwa kiwango hicho, chombo kikuu cha maamuzi cha TANESCO, yaani Bodi ya Wakurugenzi, hakikuchukua hatua ya heshima ya kujiuzulu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyodokeza awali, Kamati Teule ilishindwa kubaini moja kwa moja chanzo cha ujasiri wa kiburi ndani ya Wizara ya Nishati na Madini kiasi cha kupindisha maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote, kukaidi ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma mara tatu mfululizo na kinyume na maagizo ya Baraza la Mawaziri yaliyotaka Sheria ya Ununuzi wa Umma izingatiwe, kukiuka sheria kwa makusudi kwa kuingilia mchakato wa zabuni wa taasisi nyingine ya ununuzi, kuvipuuza vyombo vya ndani vya maamuzi vya TANESCO (Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Zabuni n.k), kuilazimisha Bodi ya Menejimenti ya TANESCO kuridhia maamuzi yaliyofanywa na Wizara ya kuibeba Richmond Development Company LLC kinyume cha sheria na taratibu, n.k. Aidha Kamati Teule ilishangazwa na Ofisi ya Waziri Mkuu iliyokuwa ikifuatilia kwa karibu mchakato huo, kushindwa kukemea ukaidi huo wa Wizara ya Nishati na Madini.

Baadhi ya mashahidi, wakiwemo waandishi wa habari mashuhuri nchini, waliinyooshea kidole Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa msingi wa ubabe uliokithiri wa Wizara ya Nishati na Madini katika kuibeba Richmond. Aidha baadhi ya nyaraka ambazo Kamati Teule ilipata katika uchunguzi wake zilionesha kuwa maelekezo na maamuzi mengi ya msingi yalikuwa yanafanywa na Waziri Mkuu badala ya Wizara.

Mfano ni barua kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda kwa Waziri Mkuu tuliyoinukuu ukurasa wa 31 wa taarifa hii, ikitamka wazi kuwa GNT ilifanya majadiliano na Richmond Development Company LLC tarehe 8 hadi 16 Juni 2006 "kwa kuzingatia maelekezo" ya Waziri Mkuu.

Vilevile, Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Julai 2006 Waziri wa Nishati na Madini akamwandikia Katibu Mkuu wake kuwa, "Nimezungumza tena na Mheshimiwa Waziri Mkuu leo juu ya bei ya mitambo ya Aggreko. Msimamo ni ule ule niliokueleza awali na ameagiza tuulizie Richmond kama anaweza kutoa 40 MW kwa bei isiyozidi ile ile ya 4.99 cents per kWh na kama tunaweza kuipata basi achukuliwe Richmond".

Mheshimiwa Spika, ushiriki huu wa karibu wa Waziri Mkuu katika kila hatua ya zabuni ya umeme wa dharura, si lazima uwe ushahidi wa kwamba kiongozi huyo wa kitaifa alihusika katika kuibeba Richmond. Unaweza pia ukawa ushahidi wa staili yake ya kawaida kabisa ya uongozi katika kufuatilia masuala yote ya kitaifa kwa karibu sana tukizingatia kwamba nchi wakati huo ilikuwa katika kipindi kigumu sana cha ukosefu wa umeme. Watu pekee waliokuwa wanaujua ukweli wenyewe, ukweli ambao ungeipa Kamati Teule msingi wa kumhoji Waziri Mkuu kwa kiapo, walikuwa watatu: Waziri Dk. Msabaha (Mb), Katibu Mkuu Mwakapugi na Mwenyekiti wa Bodi Balozi Kazaura.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ikawaita kwa mara ya pili Dk. Msabaha (Mb) na Ndugu Mwakapugi kwa mahojiano zaidi. Wote wawili, wakiwa ndani ya kiapo, walikataa katakata kupokea maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu ya kuipa Richmond upendeleo. Lakini Mhe. Dk. Msabaha (Mb), baada ya mahojiano chini ya kiapo, akaiuma sikio Kamati Teule kuwa katika suala hilo yeye atakuwa kondoo wa kafara tu au, kwa maneno yake mwenyewe, "Bangusilo" kwa lugha ya Kizaramo. Maelezo hayo ya ziada nje ya kiapo ya Mheshimiwa Waziri yaliyotoa ujumbe kuwa "si yeye ila mkuu wake wa kazi", yalioana na maelezo aliyoyatoa Balozi Kazaura nje ya kiapo tarehe 30 Novemba, 2007. Mara baada ya kumaliza mahojiano kwa kiapo na Kamati Teule, Balozi akatoa maelezo ya ziada kuwa Richmond ilikuwa mradi wa "Bwana Mkubwa" na "mshiriki wake mkubwa kibiashara", akimaanisha Mhe. Waziri Mkuu na Mhe. Rostam Aziz (Mb).

Mheshimiwa Spika, tumelazimika kueleza hata mambo tuliyoelezwa kwa siri kiungwana (in confidence) kutokana na uzito wa suala lenyewe na dhamana kubwa tuliyopewa na Bunge ya kuelezea kilichotokea kwa uwazi na ukweli. Lakini ushahidi huu wa ziada na nje ya kiapo wa viongozi hawa wawili, haukutoa msaada stahili kwa Kamati Teule kwa kuwa msingi wa maamuzi yote ya Bunge si minong'ono au tetesi, bali taarifa zenye uthibitisho halisi. Ni dhahiri kuwa, kwa watumishi hao "waaminifu" wa Serikali, isingelikuwa rahisi kumtaja Waziri Mkuu chini ya kiapo. Hatua hiyo inahitaji ujasiri mkubwa na uzalendo wa hali ya juu.

Pamoja na woga uliokuwa dhahiri wa watumishi hao, ushahidi wa maandishi, wa mdomo na kimazingira ambao Kamati Teule iliupata kutoka kwa mashahidi mbalimbali, unamhusisha Waziri Mkuu na mchakato wa maamuzi katika suala hili la Richmond.

Mheshimiwa Spika, uvumi wa kuhusika kwa Waziri Mkuu na baadhi ya washiriki wake wa karibu katika suala hili la Richmond umeenea sehemu nyingi nchini kwa kiwango cha kushangaza. Kamati Teule inaelewa kuwa uvumi huo unaweza kuwa umechangiwa na mahasimu wake kisiasa, lakini uharaka, urahisi na wepesi wa wananchi kuziamini tetesi hizo, unazua maswali mengi kuhusu imani, taswira, na heshima aliyojijengea yeye mwenyewe katika jamii.

3.0 MKATABA KATI YA TANESCO NA RICHMOND DEVELOPMENTCOMPANY LLC

3.1 Maudhui na Utekelezaji wa Mkataba

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoona awali, Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC hatimaye ulisainiwa na pande zinazohusika Jijini Dar-es-Salaam tarehe 23 Juni 2006. Madhumuni ya Mkataba yameainishwa wazi katika Utangulizi wa Mkataba kuwa ni kusambaza umeme wa dharura kwa kutumia mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme wa MW 105.6 kutokana na gesi.

Madhumuni ya msingi ya Mkataba huu yalikuwa kuzalisha na kusambaza umeme wa dharura (emergency power supply) katika kipindi cha ukame kilicholikumba Taifa. Ndiyo maana tangazo la awali la zabuni la TANESCO liliweka kipindi kifupi cha miezi 12 tu cha kutumia umeme huo wa dharura na muda huo ungeweza kuongezwa kutegemea hali ya uzalishaji umeme nchini. Lakini Mkataba huo umeongeza muda kutoka miezi 12 hadi 24 na kuifanya dhana ya "umeme wa dharura" ipotee kabisa katika mradi huo.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule haikuona mantiki ya kuongeza muda mapema hadi miaka miwili wakati fursa ya kuongeza muda baada ya mwaka mmoja ilikuwepo kutegemeana na hali ya mvua nchini. Uamuzi wa kuongeza muda kabla ya kutathmini hali ya mvua na upatikanaji maji kwenye mabwawa yetu ya kuzalishia umeme, ulikosa uzalendo na hauwezi kukwepa tuhuma ya ufisadi. Uamuzi huo umeibebesha nchi gharama kubwa zisizo za lazima kwani miezi sita tu baada ya kusaini Mkataba huo, mabwawa ya kuzalishia umeme nchini yalikuwa yameshajaa.Hivyo,

Mheshimiwa Spika, tunalazimika chini ya Mkataba huo kulipia, mbali na gharama ya umeme wenyewe, uwepo wa mitambo hiyo nchini (capacity charges) kwa gharama ya sh. milioni 152 kila siku kwa miaka miwili mfululizo badala ya mwaka mmoja. Aidha kutokana na mabwawa yetu kuzalisha umeme usio na gharama kubwa, mitambo hiyo ya kukodisha ambayo umeme wake ni aghali hutumika chini kabisa ya kiwango kilichokusudiwa (underutilisation).

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule inasisitiza kuwa udharura wa mradi huu ulimalizika pale mabwawa yetu yalipoanza kujaa maji polepole kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha nchini mwishoni mwa Disemba, 2006 na kufikia kilele stahili mapema mwezi Februari 2007. Hivyo kitendo cha Wizara kuikubalia kampuni iliyoshindwa kutekeleza sehemu yake ya Mkataba kwa wakati muafaka, Richmond Development Company LLC, kuyahamishia majukumu yake kwa kampuni nyingine ya Dowans Holdings S.A. bila kuufanyia Mkataba huo marekebisho stahili ya kuipunguzia nchi mzigo wa malipo, hakikuwa cha kizalendo bali cha kukidhi maslahi binafsi ya kibiashara.

Mheshimiwa Spika, mbali na hoja hiyo, tulikuwa na fursa ya wazi ya kuuvunja mkataba huo bila madhara yoyote ya kisheria chini ya kifungu cha 12.3 cha Mkataba. Tarehe 27 Oktoba, 2006 TANESCO ilichukua hatua ya kwanza kuelekea huko kwa kuitumia Richmond Development Company LLC taarifa ya tahadhari (Default Notice) iliyoelezea mapungufu ya Richmond yalitohitaji majibu ya uhakika: kushindwa kwa kampuni hiyo kusafirisha angalau mtambo wa kwanza wa wastani wa unit 22 kW kuja Tanzania; kushindwa kwa kampuni hiyo kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo ya utekelezaji wa mradi; uwepo wa kampuni hiyo Marekani kihalali; uwezo wa kampuni hiyo kitaalamu na kifedha kuweza kutekeleza Mkataba huo wa umeme wa dharura katika muda muafaka.

Mheshimiwa Spika, kimya cha Richmond kikailazimu TANESCO kuiandikia tena kampuni hiyo tarehe 17 na 23 Novemba 2006 kuikumbusha kuhusu hoja zake za awali ambazo hazikujibiwa na kudai maelezo kuhusu taarifa za kwamba kampuni hiyo haikuwa na mahusiano na Pratt & Whitney iliyotegemewa sana kubeba sehemu kubwa ya majukumu ya mradi.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini haikufurahishwa na mwelekeo huo wa TANESCO wa kuvunja Mkataba huo licha ya kwamba hali ya maji nchini ilizidi kuwa nzuri na kampuni hiyo ya Marekani ilikuwa haionyeshi dalili ya kuweza kutekeleza mradi huo kinyume na makubaliano. Aidha, TANESCO ilikuwa imepata uthibitisho usio na shaka kutoka kampuni mashuhuri ya mawakili ya Virginia, Marekani iitwayo Hunton & Williams LLP kwamba Richmond Development Company LLC ilikuwa kampuni ya mkobani (brief-case company).

Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Nazir Karamagi (Mb), kupitia kwa Kamishna wa Nishati, Ndugu Bashir Mrindoko, akamtaka Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO ajieleze kulikoni anaitumia Richmond taarifa za tahadhari zenye mwelekeo wa kuvunja mkataba. Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO akajieleza kwa barua aliyomwandikia Waziri moja kwa moja yenye Kumb. Na. MD/003 ya tarehe 23 Novemba, 2006.

Mheshimiwa Spika, siku tano tu baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kujieleza, yaani tarehe 28 Novemba 2006, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi Kazaura, alimtaarifu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kwa barua kwamba asubuhi ya siku hiyo alikuwa kapigiwa simu na Waziri Karamagi akiwa Jijini Calgary, Canada akimuarifu kwamba Richmond Development Company LLC walikuwa wanataka kuhamisha majukumu yao yaliyobaki katika Mkataba wa uletaji mitambo na uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni nyingine. Kufuatana na barua ya Balozi Kazaura yenye Kumb. Na. SEC.216/C/RDC ya tarehe 28 Novemba, 2006, Mheshimiwa Waziri aliagiza, pamoja na mambo mengine, kuwa TANESCO iangalie kama Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC unaruhusu kukabidhi majukumu kwa kampuni nyingine.

Mheshimiwa Spika, siku hiyo hiyo ya tarehe 28 Novemba 2006, uongozi wa TANESCO ulimshauri Mwenyekiti wa Bodi amtaarifu Mhe. Waziri kwamba Kifungu cha 15.12 cha Mkataba huo hakiruhusu kukabidhi majukumu ya Mkataba kwa Kampuni nyingine isipokuwa kwa maafikiano ya pande mbili za Mkataba. Hatimaye, siku sita baadaye, yaani tarehe 4 Disemba 2006, TANESCO ikapokea barua kutoka kwa Richmond Development Company LLC ikielezea makusudio ya Richmond kuhamisha majukumu yake yote ndani ya Mkataba huo kwenda kwa Dowans Holdings, S.A.

Siku hiyo hiyo TANESCO ikaijibu Richmond kwamba haikuwa tayari kuridhia pendekezo hilo kwa sababu kuu tatu:

(i) Kifungu 15.12 cha Mkataba kinataka kuwepo kwa makubaliano ya pamoja ya kimaandishi (written mutual agreement) kutoka kwa wahusika wote wa Mkataba (Parties) kabla ya kufikiwa uamuzi wa kuhamisha Mkataba.

(ii) Richmond Development Company LLC haijatoa sababu zozote za msingi kwa pendekezo hilo la kuhamisha Mkataba.

(iii) TANESCO haifahamu historia, uzoefu wala uwezo wa kifedha wa hao wanaopendekezwa kuhamishiwa Mkataba.

Aidha, TANESCO ilikumbushia barua zake za awali ilizoiandikia Richmond Development Company LLC kuhusu ukiukwaji wa masharti ya Mkataba, lakini Richmond haikuzijibu. Hivyo, TANESCO ikataka ipate kwanza majibu ya masuala yote iliyoyaainisha kabla ya kufikiria kuridhia pendekezo la kuhamisha Mkataba huo.

Mheshimiwa Spika, kama kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO ikashinikizwa kukubaliana na ombi la Richmond hata kabla kampuni hiyo ya Kimarekani haijajibu hoja za msingi za TANESCO. Tarehe 21 Disemba 2006 TANESCO ikaiandikia barua Richmond Development Company LLC kukubali pendekezo la kuhamisha majukumu yake kwa Dowans Holdings, S.A.Uamuzi huo wa kuruhusu uhaulishwaji wa Mkataba kipindi ambacho nchi ilikuwa imeondokana na hali ya dharura, tena kwa masharti yaleyale ya kulaliwa yanayoweza kukubalika pale tu ambapo nchi imebanwa kweli kweli na tatizo, ulimfedhehesha hata Mkurugenzi Mwendeshaji wa Dowans Holdings S.A., Bw. Guy Piccard, raia wa Kanada, alipohojiwa na Kamati Teule tarehe 27 Disemba, 2007. Bw. Piccard haoni kwa nini mkataba huo usiangaliwe upya kutokana na mazingira ya udharura kutokuwepo.

3.2 Mzigo wa Malipo wa TANESCO

Mheshimiwa Spika, nimeeleza awali kuwa mbali na kulipia gharama ya umeme wenyewe, TANESCO inawajibika chini ya Mkataba huo kulipa gharama za uwezo wa mitambo (capacity charges) ambazo ni sh. milioni 152 kila siku hadi mwisho wa Mkataba. Aidha, chini ya Mkataba huo, TANESCO inabebeshwa mzingo wote wa kodi, malipo na gharama mbalimbali zinazoweza kumkabili mwekezaji! Kifungu cha 3.4 cha Mkataba wa TANESCO na Richmond kinasema:"

All taxes and charges arising in relation to the importation and exportation of the plant, equipment, tools, spare parts, consumables, testing and monitoring equipment or in connection with the supplier's performance of its obligations under this Agreement generally that become due in accordance with the laws of Tanzania shall be paid for by TANESCO at its sole cost and expense".

Mheshimiwa Spika, Tafsiri ya jumla ya kifungu hiki cha Mkataba ni kwamba: kodi na ada zote zinazohusiana na uingizaji ndani ya nchi na usafirishaji nje ya nchi wa mitambo yote, vifaa, vipuli n.k. na gharama zote zinazohusiana na utekelezaji wa wajibu wa Richmond (sasa Dowans) chini ya Mkataba, yaani gharama za uendeshaji (operations), za matengenezo (maintenance) ya mitambo na gharama ya gesi inayotumika kuzalishia umeme, ni wajibu wa TANESCO kuzibeba!

Mheshimiwa Spika, mzigo mkubwa ambao TANESCO inabeba chini ya mkataba na Richmond (sasa Dowans) unajirudia katika mikataba mingine kati ya TANESCO na makampuni mengine ya umeme kama vile IPTL, AGGREKO, ALSTOM na SONGAS ambayo kwa ujumla yanachukua sehemu kubwa ya mapato ya shirika hilo, hivyo kuvuruga kabisa mizania yake. Kwa wigo wa tafsiri wa mikataba hii inayotuumiza kwa kujitakia, TANESCO inawajibika kuwalipia hawa wanaojiita wawekezaji hata gharama za bima na ada za mawakili wao!

Mheshimiwa Spika, tumefikishwa hapa tulipofika na mikataba mibovu, maamuzi ya kiimla na papara ya baadhi ya watendaji waandamizi wa Serikali wasiozingatia maslahi ya muda mrefu ya Taifa. Net Group Solution (PTY) ambayo kwa kiwango kikubwa imechangia sana katika kuidumaza TANESCO kiutaalamu na kifedha, iliingizwa TANESCO kwa ubabe bila kujali hoja za msingi za wataalamu na wafanyakazi wa TANESCO. Matokeo yake wote tunayaelewa. Vivyo hivyo, Richmond Development Company LLC, kampuni isiyo na rekodi yoyote ya kiufundi hata ya kuchomeka "bulb" kwenye kishikio chake, ikapewa mradi mkubwa na Serikali wa kuzalisha umeme wa dharura bila kujali kuhusu ufanisi wake tena katika kipindi ambacho nchi ilikuwa gizani! Huu ni ujasiri wa kifisadi.

4.0 UTEKELEZAJI WA MRADI

4.1 Barua ya Dhamana ya Benki (Letter of Credit)

Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa haraka wa mradi wa umeme wa dharura, Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC, ulitoa fursa ya kufunguliwa kwa Barua ya Dhamana ya Benki (Letter of Credit), kwa kifupi nitaiita LC, kwa madhumuni ya kulipia gharama za maandalizi na za usafirishaji wa mitambo ya uzalishaji wa umeme huo wa dharura. Mkataba ulitaka TANESCO, Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na Richmond Development Company LLC waketi pamoja kukubaliana masharti ya LC hiyo.

Mheshimiwa Spika, vyombo hivyo vya Serikali vilikaa tarehe 7 Julai, 2006 baada ya kupokea mapendekezo kutoka Richmond Development Company LLC ya namna ambavyo ingetaka ilipwe. Vyombo hivyo vya Serikali vikarekebisha kidogo madai ya Richmond na kuamua kuwa kampuni hiyo ilipwe Dola za Kimarekani 30,000,000 (milioni thelathini), sawa na asilimia 30 ya thamani ya malipo ya Mkataba kwa kipindi cha miaka miwili kwa masharti kwamba: asilimia 12 ya fedha hizo ilipwe kama malipo ya awali (Advance Payment) baada ya kuwasilishwa hati ya madai (Invoice), hati ya Uthibitisho wa Udhamini wa Benki (Bank Guarantee) kwa TANESCO na uthibitisho wa kusafirisha mitambo kuleta Tanzania; asilimia 10 ilipwe baada ya kuwasilishwa hati za kusafirishia mitambo kwa mpangilio wa awamu; asilimia 8 ilipwe mara baada ya uzinduzi wa mitambo.

Mheshimiwa Spika, siku tatu baadaye Richmond Development Company LLC ikataka masharti hayo yarekebishwe ili kuipa kampuni hiyo unafuu zaidi, wazo ambalo TANESCO ililikataa kwa kuhofia kuwa kampuni hiyo ingeweza kupotea baada ya kupata malipo ya awali yasiyo na masharti magumu. Tarehe 27 Julai, 2007 Wizara ya Nishati na Madini ikaingilia kati mvutano huo na kuitisha kikao kilichosimamiwa na Waziri Mhe. Dr. Ibrahim Msabaha, Mb kama Mwenyekiti. Kikao hiki kilihusisha wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, TANESCO, Benki Kuu ya Tanzania, Mwakilishi kutoka CTI na Richmond Development Company LLC. Kama ilivyokuwa kwa kikao cha tarehe 7 Julai, 2006, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wala mwakilishi wake hakuhudhuria.

Mheshimiwa Spika, kikao hiki kikaamua kurekebishwa kwa masharti ya LC kama ilivyopendekezwa na Richmond Development Company LLC. Baadhi ya marekebisho yalikuwa:

(i) Kampuni hiyo ilipwe asilimia 17.5 ya jumla ya thamani ya Mkataba baada ya Benki ya kampuni hiyo kupokea hati za usafirishaji wa mitambo (shipping documents), hati ya bima, orodha ya vifungashio (packing list), hati za uasili wa bidhaa (Certificate of origin), hati za upangaji wa mizigo (packing lists), pamoja na hati ya madai (Invoice) kwa mtambo wa MW 22.

(ii) Kampuni hiyo ilipwe vilevile asilimia 17.5 ya jumla ya thamani ya Mkataba baada ya TANESCO kutoa hati ya uthibitisho ya mitambo kuwasili eneo la kazi (Ubungo, Dar-es-Salaam).

4.2 Mchakato wa Kufungua Barua ya Dhamana ya Benki

Mheshimiwa Spika, baada ya makubaliano hayo, tarehe 23 Agosti, 2006 TANESCO iliiomba Citibank (Tanzania) kufungua LC kwa ajili ya Richmond Development Company LLC yenye thamani ya Dola za Kimarekani 30,696,598.00. Siku hiyo hiyo ya terehe 23 Agosti 2006, Citibank (Tanzania) iliwajulisha TANESCO kwamba isingeweza kufungua LC kwa ajili ya Richmond Development Company LLC, kutokana na kile walichoeleza kuwa ni kutopata muda wa kutosha kuchunguza kwa kina uwezo wa mteja anayehusishwa na dhamana ya malipo hayo (due diligence) kabla ya kuingia Mkataba huo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukataliwa na Citibank, TANESCO waliiomba Benki ya CRDB kufungua Barua ya Dhamana ya Benki hiyo kwa masharti sawa na yale yaliyopelekwa Citibank (Tanzania). Tarehe 25 Agosti, 2006 CRDB ikafanya mawasiliano Citibank (New York). Lakini tarehe 2 Septemba 2006, Citibank (New York) ikaifahamisha CRDB kuwa wao pia wasingeweza kushiriki katika kufungua LC kwa Richmond Development Company LLC kutokana na mahitaji ya lazima ya kuzingatiwa chini ya Kifungu Namba 7 cha Kanuni za UCP 500. Kifungu hicho ndicho kilichowafanya Citibank (Tanzania) kukataa kufungua Barua kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, kitendo cha benki hizo mbili za Kimarekani kukataa kufungua LC kwa jili ya kampuni ya Kimarekani, kilitosha kuzua wasiwasi wa msingi kuhusu kampuni hiyo. Kwa kuwa Watanzania tuliishaamua kufa na Richmond, tukasonga mbele! Hivyo, tarehe 2 Septemba 2006, CRDB ikafungua upya LC kwa ajili ya Richmond Development Company LLC kupitia Benki nyingine ya nje iitwayo HSBC kwa masharti yale yale ambayo CRDB ilipokea kutoka TANESCO. Hatimaye HSBC ikafungua LC kwa ajili ya kampuni hiyo lakini kwa kutumia jina lingine la RDEVCO na siyo Richmond Development Company LLC!

4.3 Maombi ya Mapya ya Richmond kubadilisha tena Masharti ya LLC.

Mheshimiwa Spika, baada ya LC kufunguliwa na kuthibitishwa uwajibikaji kwa utekelezaji wa masharti ya Mkataba ulianza rasmi. Hata hivyo, tarehe 4 Oktoba 2006, Richmond Development Company LLC kwa mara nyingine tena, iliipelekea TANESCO maombi ya kutaka kuifanyia marekebisho ya LC kwamba:-

(i) LC iruhusu malipo ya awali (upfront payment) ya Dola za Kimarekani milioni 10;

(ii) Richmond Development Company LLC iruhusiwe kusafirisha mtambo wa kwanza kwa njia ya ndege kwa gharama ya Dola za Kimarekani 5,696,568.00;

(iii) Asilimia 50 ya Barua ya Dhamana ya Benki ilipwe baada ya uthibitisho kutoka TANESCO juu ya kupokelewa kwa mitambo nchini.

Mheshimiwa Spika, tarehe hiyo hiyo ya 4 Oktoba, 2006 Wizara ya Nishati na Madini ikaitisha kikao kujadili maombi hayo. Kikao hiki kilichohudhuriwa na wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini, TANESCO, Benki ya CRDB na Richmond Development Company LLC, kikakubali maombi yote ya Richmond Development Company LLC na kuagiza kuwa hatua za utekelezaji zifuatie mara moja.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba mchakato mzima ulitawaliwa na udharura, Kamati Teule haielewi ni vipi Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa ikitekeleza kila pendekezo jipya lililotolewa na Richmond Development Company LLC bila kujali madhara ambayo yangewea kutokea pindi kampuni hiyo ingelipwa na kuingia mitini.Mheshimiwa Spika, baada ya kubaini kwamba mapendekezo hayo mapya ya kuibeba Richmond yalikuwa nje ya masharti ya LC yaliyoainishwa katika Mkataba wa malipo kati ya TANESCO, Benki Kuu ya Tanzania, Wizara ya Fedha na CRDB Bank, Wizara ya Nishati na Madini ikaijulisha Wizara ya Fedha kuhusu maamuzi mapya ya LC kutokana na maombi ya Richmond Development Company LLC.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha haikuridhishwa na mapendekezo yaliyotolewa kwani malipo yoyote ya awali kutoka fungu maalum la Multilateral Debt Relief Initiative ni lazima yafanyike kwa uthibitisho wa kuridhisha. Sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ndugu Gray Mgonja, inasema::

"... tunaona kuwa tofauti na taarifa zilizotolewa wakati wa majadiliano ya Mkataba kuwa mkandarasi aliyechaguliwa alikuwa na vifaa tayari kuvileta nchini, sasa ni wazi kuwa si hivyo.

Kama unavyojua, msingi wa malipo kuhusu mitambo ya kununua au kukodisha chini ya Mradi wa Nishati ya Dharura unaofadhiliwa kupitia IMF MDRI, ni mkataba unaotokana na majadiliano.
Napenda kupendekeza kuwa malipo yoyote ya awali kutoka akaunti ya MDRI lazima yaandamane na dhamana ya kuridhisha kutoka kwa mkandarasi. Sharti hili linaonyesha kutokuzingatiwa chini ya mapendekezo yenu".

Mheshimiwa Spika, pamoja na maelekezo na ushauri huu wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini siku hiyo hiyo ikaiandikia barua TANESCO kuitaka itekeleze maombi ya Richmond Development Company LLC mara moja kubadilisha masharti ya malipo:-

" . . . I wish to inform you that the proposed amendments to the existing Letter of Credit are acceptable and you are advised to liaise with CRDB Bank to effect the changes as soon as is practical. . . ." Barua ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini (Kumb. Na. CBD.214/324/01 ya tarehe 6/10/2006) inasomeka.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule imejiuliza bila kupata majibu: Ni nini kilifanyika hadi Wizara ya Nishati na Madini ikatoa kauli hii ambayo ni tofauti kabisa na ushauri ilioupata kutoka Wizara ya Fedha? Nini msingi wa ukereketwa au ufukukutwa bayana wa Wizara ya Nishati na Madini kuhusu Richmond?

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maagizo ya Wizara, TANESCO iliiandikia barua Benki ya CRDB tarehe 6 Oktoba, 2006 kuitaka kufanya mabadiliko hayo mapya kwenye LC ya Richmond. Tarehe 9 Oktoba, 2006 Benki ya CRDB iliijibu TANESCO na kuikumbusha kwamba LC inasimamiwa na makubaliano ya pamoja chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania. Kwa msingi huo TANESCO ikatakiwa kufuata taratibu kwa kuiomba Benki Kuu ya Tanzania kibali cha kufanya marekebisho katika Kifungu 1(a) cha Mkataba wa makubaliano ya taratibu za malipo ili kuwezesha maombi yaliyopendekezwa kufanyiwa kazi. Jibu hilo likailazimu TANESCO kufuta maombi hayo.

Mheshimiwa Spika, hadi LC hiyo ya Richmond inaisha muda wake (tarehe 30 Novemba, 2006), kampuni hiyo ya Kimarekani haikuweza kutekeleza sharti hata moja na hivyo kushindwa kuchukua fedha kama ilivyokuwa imepangwa. Swali linalojitokeza ni: Iwapo CRDB ingekubali kubadilisha masharti ya LC na kuipa Richmond Development Company LLC fedha ilizoomba bila kibali cha Benki Kuu ya Tanzania; Je, Richmond ingeleta nchini mitambo kama ilivyokusudiwa au ingekuwa ni hasara kwa Taifa?Kwa upande mwingine, mchakato mzima wa Richmond Development Company LLC wa kutaka kufanya mabadiliko katika Barua ya Dhamana ya Benki mara kwa mara unadhihirisha nia yao ya kutaka kupata mtaji. Pia inadhihirisha kwamba Richmond Development Company, LLC haikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza Mkataba huu kinyume na tamko kwenye Mkataba kuwa:-"The Supplier (i.e. Richmond) has the equipment and the financial and technical capability to construct, install, commission, operate and maintain such a plant as required by TANESCO". (Msambazaji (yaani Richmond) ana vifaa na uwezo wa kifedha na wa kitaalam kujenga, kusimika, kuiwasha, kuendesha na kuendeleza mtambo huo kama TANESCO inavyohitaji.)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo Kamati Teule ilijiuliza maswali yafuatayo:-

(i) Je, utafiti ulifanywa kufahamu gharama halisi za mitambo mipya kutoka kwa watengenezaji wenyewe bila ya kupitia kwa mawakala? Kamati Teule ilibaini kuwa zoezi hilo liliwahi kufanyika mwaka 1998 tu ambapo Wizara ya Nishati na Madini ilitoa kazi hiyo kwa wataalam wa sekta (consultants) na kufanikisha kugundua kuwa bei ya mitambo ya umeme ya IPTL (400 MW) ambayo ilitakiwa kuuzwa kwa Dola za Kimarekani milioni 150 (Tsh. 187.5 bilioni) bei yake halisi ilikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 85 (Tsh.106.2 bilioni) tu na hivyo kupata kigezo cha kukataa bei yao. Hivyo basi, kutokana uzoefu huo, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na TANESCO walitakiwa kufuatilia bei hizo za mitambo na pia makadirio ya kazi za ujenzi ili kupata picha ya gharama halisi ya mradi jambo, ambalo halikufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa viongozi wa Wizara na TANESCO kushindwa kujua bei halisi ya mitambo kutoka kwa watengenezaji wenyewe kwa takribani miaka 10 huku wakisafiri kwenda nje ya nchi kila kukicha kwa mikutano, warsha, makongamano, n.k, na kwa Wizara kung'ang'ania kutumia mawakala badala ya watengenezaji wa mitambo, nchi yetu imegeuzwa gulio la wajanja kuikamua na kuwabebesha wananchi mzigo wa kodi.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ilipotembelea Marekani, iliamua kuwatembelea baadhi ya watengenezaji wa mitambo ya uzalishaji wa umeme huko huko Houston Marekani kujua bei za mitambo yao. Mmoja wa watengenezaji wenye jina kubwa duniani, Kawasaki Gas Turbines – Americas, anatengeneza na kuuza Mtambo mpya aina ya GPB180 wenye uwezo wa kuzalisha MW 17.5 kwa Dola za Kimarekani 7.5 milioni (Tsh. 9.4 bilioni). Mawakala huwa wanatuletea mitambo ya aina hiyo hiyo kwa bei mara mbili ya bei halisi.

(ii) Iwapo TANESCO au Serikali iliweza kufungua LC ya Dola za Kimarekani 30,696,598; je, fedha hizo zisingeweza kutosheleza kununua mitambo mipya ya uzalishaji umeme, na mitambo hiyo kubakia mali ya TANESCO, badala ya kuingia katika Mikataba ya ghali ya kukodisha mitambo?

Aidha, taarifa za watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini kwamba wakati wa kipindi cha mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura kulikuwa na ugumu wa kupatikana mitambo ya umeme wa dharura zimethibitishwa na Kamati Teule kuwa sio za kweli.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba kulikuwa na ukame, lakini ukame huo haukuwa wa mitambo ya kuzalisha umeme kwani mitambo hiyo hutengenezwa muda wote na sio kwa kutegemea mvua. Aidha, utafiti wetu umebaini kuwa katika kipindi hicho cha matatizo ya umeme nchini, kampuni zote za kutengeneza mitambo hiyo ya umeme zilikuwa zina mitambo kadhaa ikisubiri wateja. Kawasaki ilikuwa na mitambo 8 ya kisasa tena yenye kutumia gesi na dizeli (dual fuel plant). Serikali nyingi, ikiwemo ya Nigeria, ni wateja wazuri wa kampuni hiyo ambao huteremshiwa bei kwa mtambo moja hadi Dola za Kimarekani milioni 6.7 milioni badala ya Dola za Kimarekani milioni 7.5 bei ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, kwa thamani ya LC iliyofunguliwa kwa Richmond Development Company LLC ya Dola za Kimarekani milioni 30.7 au Tsh 38.4 bilioni, TANESCO ingeweza kununua mitambo mipya yote minne pamoja na kumudu kulipia gharama za kusafirisha kwa meli hadi Dar-es-Salaam. Hivyo ili zipatikane MW 105.6 zilizohitajiwa na TANESCO ingehitajika mitambo sita (6) ambayo ni sawa sawa Dola za Kimarekani milioni 45 au Tsh. 56.25 bilioni badala ya Dola za Kimarekani milioni 87 au Tsh. 108.7 bilioni tulizobebeshwa na Richmond Development Company LLC.

Mheshimiwa Spika, Je, si dhahiri kuwa hii ndiyo ilikuwa nia ya Richmond Development Company LLC, yaani kupata fedha za malipo ya awali (advance payment) ili ikatununulie mtambo mmoja na kuja kutukodisha sisi wenyewe, hivyo kufaidika na capacity charge ya kila mwezi kwa Mkataba wa miaka miwili? Kwa mtambo mmoja wa MW 22, capacity charge ni Dola za Kimarekani takriban 730,871 au Tsh. Milioni 913.6 kwa mwezi, hivyo kwa miezi 24 ni wastani wa Dola za Kimarekani 17,540,912 au Tsh. Bilioni 21.9.

(iii) Kwa kuwa thamani ya LC inalipwa kama malipo ya awali (advance payment), Je, hii si sawa na kutoa mkopo kwa Richmond Development Company LLC? Kamati Teule inaona kwamba hiyo ni sawa na kutoa mkopo usio na riba kwa mfanyabiashara wa nje ili awe mwekezaji.

(iv) Kwa nini katika Mkataba wa Richmond Development Company LLC kifungu cha kufidia malipo ya awali (advance payment) ya LC hakikuwekwa bayana ndani ya Mkataba tofauti na Mikataba mingine, badala yake ikawekwa fursa ya kujadiliana na mkandarasi? Kamati Teule haioni sababu yeyote ya msingi mbali na wahusika kujiwekea fursa ya kukidhi maslahi yao binafsi.

3.0 5.0 TAARIFA ZA PPRA na TAKURU

3.1 5.1 Taarifa ya PPRA
3.2
3.3 Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali wa kuipa Richmond Development Company LLC zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa MW 105.6 na baadaye kuingia mkataba na TANESCO, ulizua mjadala wa manung'uniko ya wananchi wa kada mbalimbali walioshuhudia kushindwa kwa kampuni hiyo kutekeleza mradi huo katika muda muafaka. Umma wa Watanzania wa kawaida, wanasiasa, wasomi, wanataaluma, wanahabari, na wadau mbalimbali hawakusita kuilalamikia Serikali kwa uteuzi huo wa Richmond ambao walihisi kuwa uligubikwa na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi.

3.4 Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ambayo sasa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa mamlaka ya kisheria ambayo taasisi hizi inayo, zikaamua kulichunguza suala hili.
3.5
3.6 Mheshimiwa Spika, kwa ujumla PPRA ilifanya uchunguzi makini na wa kina kujua kama Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma zilifuatwa. Taarifa hiyo imebainisha wazi kuwa pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kuiokoa nchi kutokana na hali mbaya ya umeme, mchakato mzima wa zabuni ulikiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2005 kama tulivyoelezea kwa kina sehemu ya pili ya taarifa hii fupi. Kwa ujumla Kamati Teule imeridhishwa na taarifa ya PPRA ambayo imeandikwa kitaalamu ikiwa na vielelezo vya wazi ambavyo Mamlaka imevitumia.

5.2 Taarrifa ya TAKURU

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla uchunguzi uliofanywa na TAKURU, ambao taarifa yake unadai kuwa ulikuwa wa "kina na wenye umakini wa hali ya juu'' ulibaini kwamba:-
• Mchakato wa kumpata mzabuni ulikuwa wa wazi na shindanishi;
• Hakuna ushahidi uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe na hata kupokea kamisheni. Pia hakuna ushahidi uliopatikana wa Afisa yeyote Serikalini kumiliki hisa au kuwa na madaraka katika Richmond Development Company LLC;
• Kamati maalum iliyoundwa haikupata muda wa kutosha kuifanyia uchambuzi wa kina Richmond Development Company LLC ili kufahamu uwezo wake kiufundi na kifedha na badala yake ilitegemea uwezo wa Kampuni ya Pratt & Whitney kama kigezo cha kuipatia Richmond zabuni;
• Utafiti wa kina haukufanywa kutambua uwezo wa Kampuni ambayo ingepaswa kusimamia shughuli za Richmond Development Company LLC yaani Richmond Development Company (T) Ltd; na
• Mapungufu machache yalikuwepo lakini ya "kawaida kiutendaji" na hayakuhusisha rushwa au manufaa ya aina yeyote ile kwa watendaji wa Serikali na wala hakuna hasara iliyosababishwa na mapungufu hayo.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule ilishindwa kuona mantiki ya matokeo ya uchunguzi wa TAKURU kama ifuatavyo:-
(i) Mchakato ambao TAKURU imedai kuwa ulikuwa wa wazi na shindanishi uliendeshwa na Wizara ya Nishati na Madini bila kuzingatia taratibu za sheria na kanuni za ununuzi wa umma.Kamati Teule imeshindwa kuelewa ni mbinu zipi taasisi hii ilitumia katika kueleza kuwa mchakato wa zabuni ulifanywa kwa uwazi na kuwa shindanishi. Je, uwazi gani na ushindanishi gani ulikuwepo kwa Wizara ya Nishati na Madini ikishirikiana kwa karibu na Ofisi ya Waziri Mkuu, kusitisha mchakato wa zabuni ndani ya TANESCO na kuunda chombo kipya nje ya taratibu ili kumteua mzabuni kwa niaba ya TANESCO?

(ii) Hoja ya TAKURU kuwa kulikuwa na mapungufu, lakini mapungufu hayo yalikuwa ya kawaida ambayo hayajengi makosa ya jinai haina msingi. Kwa Wizara kuilazimisha taasisi nyingine ya ununuzi, yaani TANESCO, kusaini Mkataba ambao haukupitishwa na vyombo vyake vya maamuzi; kwa kampuni hiyo ya Kimarekani kujitambulisha kwa majina mbalimbali katika mchakato huo: mara Richmond Development Company LLC, mara RDC, RDVECO, na mara nyingine RDEVCO; yote haya kwa TAKURU ni makosa ya "kawaida ya kiutendaji"?

(iii) Taarifa ya TAKURU imeeleza kwamba Richmond DevelopmentCompany LLC ilikuwa ifunguliwe Letter of Credit yenye thamani ya Dola za Kimarekani 30,696,598.00. Sawa, lakini TAKURU haikuona jitihada za kampuni hiyo kujaribu kubadilisha masharti ya LC hiyo mara ratu? TAKURU haikushangazwa na benki za Kimarekani kukataa kuihudumia kampuni ya Kimarekani? TAKURU haikushangazwa na kiherehere cha Wizara ya Nishati na Madini kutekeleza matakwa na kampuni hiyo hata pale ambapo yalikwenda kinyume na makubaliano ya msingi?

(iii) TAKURU haikuona hasara ambayo nchi ilipata kutokana na zabuni hiyo wakati kila mwananchi aliona hasara bayana kwa nchi kukosa umeme kwa kipindi kirefu na kuathiri uzalishaji mali na huduma za lazima nchini.

(iv) TAKURU iliamini kuwa hakukuwa na uzembe. Je, kwa Wizara na watendaji mbalimbali wa Serikali kuamini kuwa Richmond Development Company LLC na Pratt & Whitney zilikuwa na ubia bila kudai nyaraka za ubia; kwa viongozi wa Serikali kumwona tu mzungu na business card yake, na kuamini moja kwa moja kuwa ni mwakilishi wa Pratt & Whitney wakati siyo; kwa Serikali kuamua kusaini Mkataba na kampuni ambayo haijafanyiwa uchunguzi wa kina kujiridhisha kuwa si kampuni hewa au ya mkobani; hivyo vyote kweli si uzembe?

(v) Pamoja na kuwajibika kisheria kujisajili kwenye Bodi ya Usajili ya Makandarasi, na wahandisi wake kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Richmond Development Company LLC haikufanya hivyo na ililindwa na Wizara ya Nishati na Madini kubaki kama ilivyokuwa! Hilo nalo TAKURU haikuliona?

(vi) Richmond Development Company LLC, haikuwa na nyaraka zozote za kikampuni kuonyesha kuwa imesajiliwa Marekani, haikuwa na uthibitisho wa kibenki kuwa ina fedha kuendesha mradi wa umeme ili kupata sifa ya uwekezaji nchini, haikuwa na Business Plan iliyoandaliwa vizuri na kwa uangalifu, klakini ikapata huduma ya haraka Kituo chetu cha Uwekezaji na kupewa Certificate of Incentives.

Mheshimiwa Spika, ikizingatiwa kuwa TAKURU ni taasisi nyeti Kitaifa ambayo ina uwezo wa kutosha kitaaluma, kifedha na kirasilimali watu katika kufuatilia masuala mbalimbali ya uchunguzi, haikuwatendea haki Watanzania kwa kazi ya ubabaishaji iliyofanya.Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa TAKURU ndugu Alex Mfungo aliitetea Taasisi yake mbele ya Kamati Teule kuwa ilifanya uchunguzi kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1971 iliyokuwa na mapungufu mengi na kwamba ilikuwa vigumu sana kuthibitisha madai ya rushwa yaliyokuwa yanalalamikiwa na wananchi

Mheshimiwa Spika, pamoja na utetezi huo, bado TAKURU haikufanya kazi iliyotegemewa na wananchi kufanya ya kufichua uovu. Ilichofanya ni kuuficha ukweli kwa hoja za ubabaishaji.
5.3
5.4
5.5
5.6
5.3 Vyombo vya Habari – Magazeti
5.7Mheshimiwa Spika, vyombo vya habari hususan magazeti vilifanya kazi kubwa na ya ziada katika kutafuta ukweli kuhusu suala hili. Ni vyombo hivi vya habari kupitia makala mbalimbali, tahariri na taarifa maalum, vilivyoamsha shauku ya wananchi kuhusu suala hili.Naomba kuchukua fursa hii, Mheshimiwa Spika, kuvipongeza vyombo vyote vya habari, wamiliki wake, wahariri, waandishi wa habari, watangazaji na wapiga picha kwa ujasiri na moyo wa kizalendo katika kupambana na kila aina ya ufisadi kwa kutumia kalamu.

Mheshimiwa Spika, ufuatiliaji wa karibu wa vyombo vya habari kuhusu suala hili ulikuwa moja ya sababu kubwa kwa Richmond Development Company LLC kujitoa mapema kwenye Mkataba huo. Mmiliki wa Kampuni hiyo Bw. Mohammed A. Gire alikiri mbele ya Ujumbe wa Kamati Teule uliotembelea Houston, Texas, Marekani kuwa moja ya sababu zilizoifanya kampuni yake kusitisha shughuli zake ni kutokana na kuandamwa kwa kuandikwa kila siku na vyombo vya habari vya Tanzania. Ikamlazimu kuajiri kampuni ya G&S Media Consultancy ili kupunguza makali ya maumivu aliyokuwa anayapata, haikusaidia.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule inakumbushia ahadi ya Serikali ya kuanzisha mafunzo maalum ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuwawezesha wanahabari kuongeza ujuzi na kujenga uzoefu wa kuhoji na kuandika habari za uchunguzi wenye kina stahili, shughuli ambayo ni sehemu muhimu ya kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini.

6.0 RICHMOND DEVELOPMENT COMPANY LLC NI KINA NANI?
6.1 Utambulisho wake Kisheria

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura unaielezea kwenye utangulizi Richmond Development Company LLC kuwa ni kampuni iliyosajiliwa chini ya sheria za Jimbo la Texas, Marekani na yenye anuani ifuatayo: 5825 Schumacher, Houston Texas 77057, Marekani. Aidha, kifungu cha 5.1 (a) cha Mkataba huo kinatoa maelezo ya ziada kuhusu Richmond Development Company LLC kuwa ni kampuni yenye ukomo wa hisa (limited by shares) ambayo uwepo wake Tanzania haukinzani na sheria za nchi. Kifungu hicho kidogo kinamalizia kwa kutamka bayana kuwa kampuni hiyo ina nguvu na mamlaka yote stahili ya kikampuni (all requisite corporate power and authority) ya kumiliki au kukodisha na kutumia mali zake na kuendesha biashara zake kama ilivyokusudiwa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo sura ya Richmond Development Company LLC kama ilivyoainishwa katika Mkataba huo wa kisheria uliotiwa saini kwa upande wa TANESCO na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa TANESCO, Johannes G. Lottering na kushuhudiwa na aliyekuwa Kaimu Katibu (Ag. Company Secretary) wa TANESCO, Godson Makia na kwa upande wa Richmond na Meneja wake, Mohamed Gire na kushuhudiwa na wakili maarufu nchini, Dr. Ringo Tenga ambaye alijitambulisha katika mkataba huo kama Katibu wa Richmond Development Company LLC.6.2 Hadhi ya Richmond kisheria/kikampuni Marekani
Mheshimiwa Spika, uchunguzi wa kina uliofanywa na Kamati Teule ndani na nje ya nchi na kwa msaada mkubwa wa Ubalozi wa Tanzania Washington D.C na Wizara yetu ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, umetoa picha tofauti kabisa na ile iliyomo kwenye mkataba huo. Kamati Teule imejiridhisha kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC iliyokuwa imesajiliwa Jimbo la Texas wakati wa kusaini mkataba huo au iliyosajiliwa baada ya mkataba huo hadi tunapowasilisha ripoti hii kwa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 31 Disemba, 2007.

Hitimisho tulilofikia linashabihiana kwa vigezo vyote na ushauri wa kitaalamu uliotolewa na kampuni mashuhuri ya mawakili ya Virginia, Marekani inayoitwa Hunton & Williams LLP kwa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO mwezi Oktoba 2006. Katika ripoti yake yenye jumla ya kurasa 19, kampuni hiyo ya mawakili imetamka bayana kuwa hakuna kampuni yenye jina la Richmond Development Company LLC kwenye masijala ya Katibu wa Jimbo la Texas ambaye moja ya majukumu yake ni sawa na ya Msajili wa Makampuni wa Tanzania.

Hunton & Williams LLP wameituhumu Richmond Development Company LLC kwa upotoshaji wa hadhi yake kikampuni (misrepresentation of its corporate status) na kutoa tamko lisilo sahihi (incorrect statement) kuhusu hadhi yake chini ya sheria za Texas. Ukaguzi wa kumbukumbu za Katibu wa Jimbo la Texas uliofanywa na kampuni hiyo ya mawakili Oktoba 2006, ulionesha kuwa hakuna kampuni yenye jina la "Richmond Development Company LLC" iliyokuwa imeanzishwa na kuendesha shughuli zake jimboni Texas wakati huo.

Mheshimiwa Spika, aidha, tarehe 10 Oktoba, 2006 gazeti la kila siku la Kiingereza linalochapishwa hapa nchini, The Citizen, lilimkariri afisa mmoja katika Jimbo la Texas, Bw. William Pate, akisema makampuni yote yanayofanya biashara halali jimboni humo yana kumbukumbu zake katika ofisi ya Katibu wa Jimbo la Texas. Alisema ofisi hiyo haina taarifa au kumbukumbu zozote kuhusu kampuni hiyo inayojiita Richmond Development Company LLC.

Wajumbe wa Kamati Teule waliotembelea Marekani kati ya tarehe 10 na 16 Disemba, 2007 waliambiwa na Bwana Mohamed Gire, kuwa Richmond Development Company LLC ni jina mbadala la biashara la kampuni yake iitwayo RDEVCO LLC. Bwana Gire ambaye aliamua mkutano wake na Wajumbe wa Kamati Teule ufanyike ofisini kwa wanasheria wake, Duane Morris LLP waliopo 3200 Southwest Freeway, suite 3150, jijini Houston, alisisitiza kuwa sheria za Texas zinawaruhusu wafanyabiashara na makampuni kutumia majina mbadala au tofauti na yale yaliyopo kisheria kwa sababu za kibiashara. Kamati Teule iliyazingatia maelezo ya Bwana Gire kwa lengo la kuyafanyia kazi.

Ni kweli kabisa kuwa majimbo mengi Marekani, likiwemo la Texas, yanaruhusu matumizi ya majina mbadala katika biashara au huduma. Kwa Kiingereza majina hayo yanaitwa "assumed names" au "dba", kwa kirefu: "doing business as". Katika nchi nyingine nyingi kama vile Tanzania, Uingereza, Ireland, Australia na baadhi ya majimbo ya Marekani na sehemu za Kanada, neno linalotumika zaidi ni "t/a", yaani "trading as".

Mheshimiwa Spika, katika nchi zote hizo, sheria zinaweka taratibu za kuzingatia ili kuepusha vitendo vya kitapeli katika matumizi ya majina mbadala ya kibiashara. Nchini Tanzania na nchi zingine za Jumuiya ya Madola, zipo sheria maalum za usajili wa majina ya biashara tu ambapo kampuni au mfanyabiashara au mtu yeyote yule ambaye kwa sababu za kibiashara au vinginevyo, asingependa kutumia jina lake halali katika biashara fulani, anaweza kusajili jina mbadala kwa biashara hiyo bila kulazimika kuunda kampuni tofauti. Majina mbadala ya kibiashara hapa kwetu Tanzania yanasajiliwa chini ya Sheria ya Usajili wa Majina ya Biashara (Business Names (Registration) Ordinance) Sura ya 213.

Nchini Marekani vilevile, huwezi ukakurupuka tu na kuanza kutumia jina mbadala la biashara bila kupitia usajili maalum ambao unawawezesha watu wengine kukagua jalada la majina hayo mbadala kwa lengo la kupata utambulisho kamili wa wanayoyatumia. Vilevile, sheria zinalazimu majina hayo kuchapishwa magazetini kwa lengo la kuutaarifu umma. Lengo, kama tulivyodokeza awali, ni kulinda raia wema dhidi ya vitendo vya udanganyifu.

Katika Jimbo la Texas ambako Bwana Gire anaishi, ni kosa la jinai kutumia jina mbadala bila kulisajili. Usajili wa jina mbadala unadumu kwa miaka mitano ambapo mtumiaji lazima asajili jina hilo upya kati ya tarehe 1 Januari na 31 Disemba ya mwaka wa tano.

Sasa je, ni kweli kwamba jina la Richmond Development Company LLC ni jina mbadala la kampuni ya Bwana Gire iitwayo RDEVCO LLC? Je, jina hilo lilisajiliwa ipasavyo? Katika kujibu maswali hayo mbele ya mawakili wake wawili, Bwana Gire aliwakabidhi Wajumbe wa Kamati Teule hati ya uthibitisho ya Harris County, Texas ambayo kwa maoni yake, ilikuwa inathibitisha kuwa Richmond Development Company LLC ni jina mbadala la biashara!

Kamati Teule imeikagua hati hiyo kwa kina na kuona kuwa badala ya kumsaidia Bwana Gire, inazidi kuthibitisha kuwa si mfanyabiashara mwadilifu ila tapeli kwa sababu kuu mbili:

(a) Mbali na kwamba hati hiyo ya Bwana Gire ni kivuli tu au nakala ya "hati" halisi (kama ipo), nakala ambayo haina uthibitisho wowote wa uhalali na uhalisia wake, ilikuwa ina saini ya afisa mmoja tu badala ya wawili walioainishwa katika hati hiyo;

(b) Badala ya hati hiyo kutamka kuwa RDEVCO LLC imesajili jina la Richmond Development Company LLC kama Bwana Gire alivyotaka Kamati Teule ielewe, hadithi mpya kabisa inaanzishwa kuwa Richmond Development Company ni jina mbadala lililosajiliwa na Richmond Development Company LLC! La kushangaza ni kuwa katika baadhi ya barua zake alizoiandikia TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Gire anatamka kuwa Richmond Development Company ni jina mbadala la biashara la RDEVCO LLC.

Mheshimiwa Spika, mtu anaweza akadanganyika akafikiri kuwa kiwango hiki cha ubabaishaji hakithibitishi utapeli pekee, bali vilevile elimu duni ya mmiliki wa kampuni hizo, Bwana Gire, inayomfanya asione hatari kubwa anayojitwalia ya hata kumfikisha jela kwa udanganyifu. Lakini kwa mfanyabiashara mzoefu aliyejizungushia mawakili wa kumtetea mambo yakimwendea mrama, anajua analolifanya. Hivyo basi, Richmond Development Company LLC ni kampuni ya kimakusudi, ya kimkakati ambayo haikamatiki, haishitakiki, haipigiki faini na haiadhibiki kwa lolote lile itakalolifanya kwani haina uhai wa kikampuni (corporate personality).

Mheshimiwa Spika, pamoja na Bwana Gire kuamua kufanyia mkutano wake na Wajumbe wa Kamati Teule ofisini kwa wanasheria wake na si kazini kwake mwenyewe, Wajumbe walihakikisha kuwa wanatembelea mtaa unaotajwa kwenye mkataba kuwa ofisi za Richmond Development Company LLC, yaani 5825 Schumacher, Houston Texas, 77057, USA. Anuani hiyo ikawafikisha kwenye jengo lenye jina la Richmond Printing LLC, jina walilothibitisha kuwa la kampuni iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Kampuni yenye Ukomo wa Hisa ya Texas (Texas Limited Liability Company Act) tarehe 1 Agosti, 1994 kwa madhumuni ya kuendesha biashara ya uchapishaji na biashara zingine zinazoruhusiwa na sheria kwa kampuni ya aina hiyo. Kampuni hiyo ilianzishwa ikiwa na mwanahisa na meneja mmoja tu kwa jina Mohamed Gire.

Aidha, Wajumbe wa Kamati Teule wakatambua kuwa jengo hilo la Richmond Printing LLC linatumiwa vilevile kama ofisi za RDEVCO LLC, kampuni ambayo ilisajiliwa chini ya sheria hiyo hiyo ya Texas tarehe 11 Septemba, 2003 ikiwa na madhumuni mapana ya kujishughulisha na "biashara yoyote halali". Kampuni hiyo vilevile ilianzishwa ikiwa na mwanahisa na meneja mmoja tu kwa jina Mohamed Gire. Tunalazimika kusema kuwa jengo hilo vilevile ni "makao makuu" ya kampuni hewa ya Richmond Development Company LLC.

Licha ya kutumia jengo moja, kampuni zote hizo zinamhusu mtu mmoja, Mohamed Gire, na zinatumia anuani moja. Kutokana na uchambuzi huu, ni wazi kuwa maelezo yaliyomo kwenye utangulizi wa Mkataba kati ya Richmond Development Company LLC na TANESCO kuwa chombo hicho cha biashara cha Bw. Gire ni "kampuni iliyosajiliwa chini ya sheria za Jimbo la Texas", si sahihi hata kidogo.

6.3 Hadhi ya Richmond kisheria/ kikampuni Tanzania

Mheshimiwa Spika, Richmond Development Company LLC si jina geni Tanzania. Jina hilo lilianza kusikika nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na kwa kishindo likihusishwa na mradi mkubwa wa takriban shilingi bilioni 400 wa ujenzi wa bomba la mafuta la urefu wa kilometa 1,150 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Mheshimiwa Spika, katika barua yake ya kujitambulisha iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) tarehe 28 Mei, 2003, Richmond Development Company wakati huo ikijiita kwa kifupi RDC, ikajitambulisha kuwa kampuni yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika miradi ya nishati na kwamba imekamilisha miradi mbalimbali ya aina hiyo kwa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 500 katika nchi zinazoendelea. Kutokana na wasifu huo, TPDC ikawapa RDC nakala ya ripoti ya upembuzi yakinifu iliyofanywa na kampuni ya COWIconsult (Tanzania) Consulting Engineers and Planners Ltd mwaka 1997 ili kupata taarifa za awali kuhusu mradi huo. Aidha Wizara ya Nishati na Madini ikairuhusu RDC kuleta mapendekezo ya awali kuhusu mradi huo.

Mapema mwezi Oktoba, 2003 Wizara ikapokea mapendekezo ya awali ya mradi kutoka RDC ambayo yalipitiwa na wataalamu wa Wizara na TPDC na kukutwa na mapungufu mengi yakiwemo: kukosekana kwa tathmini za kifedha na za kiuchumi za mradi, kukosekana kwa tathmini za mazingira, na kukosekana kwa mpango wa kuwapa makazi waathirika katika njia ya bomba. Kutokana na mapungufu hayo, Wizara ikasita kuipa RDC mradi huo muhimu na kuitaka kampuni hiyo kwanza irekebishe mapungufu yote yaliyojitokeza. RDC nayo ikaweka sharti la kupewa upendeleo wa kutoruhusu kampuni nyingine kwenye mradi huo kwa kipindi maalum (exclusivity period) ili kukamilisha kazi hiyo bila wasiwasi wa kunyang'anywa mradi.

Mheshimiwa Spika, tarehe 30 Juni, 2004 Mhe. Daniel Yona, wakati huo Waziri wa Nishati na Madini na Bwana Mohamed Gire, wakati huo akijiita Mwenyekiti wa RDC, wakasaini mkataba wa awali (Memorandum of Understanding) ulioipa RDC exclusivity period ya miezi 18 kufanya upembuzi yakinifu wa kina. Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, uliitaka RDC kuipa Wizara ripoti za maendeleo ya utekelezaji wa mradi kila baada ya miezi sita na uliipa Wizara jukumu la kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa na RDC mara baada ya zoezi la upembuzi yakinifu wa kina kufanikishwa.

Mheshimiwa Spika, tangu mkataba huo usainiwe, RDC haikuonekana tena ikijishughulisha na utekelezaji wa sehemu yake ya mkataba. Kumbukumbu za mawasiliano kati ya Wizara na kampuni hiyo, zimetawaliwa na malalamiko ya watendaji wa Wizara kuhusu ubabaishaji wa RDC. Hatimaye tarehe 9 Januari, 2006, Ndugu. Bashir J. Mrindoko, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, akaiandikia barua RDC kuitaarifu kuwa mkataba kati yake na Wizara kuhusu bomba la mafuta ulikoma tarehe 30 Disemba, 2005 na wawekezaji wengine sasa wanapewa fursa kuendelea na mradi huo.

Sehemu ya barua ya Katibu Mkuu inasomeka hivi: "The Ministry of Energy and Minineral (sic) notes with regret that throughout the 18 month exclusivity period, in spite of several reminders, the Richmond Development Company failed to honor its obligations as provided for in Art.2.1 and 2.2 of the Memorandum". (Wizara inasikitika kuwa kwa kipindi chote cha miezi 18 ya upendeleo, Richmond Development Company, pamoja na kukumbushwa mara kwa mara, ilishindwa kuheshimu wajibu wake kama ulivyoainishwa katika Ibara ya 2.1 na 2.2 ya Mkataba).
Mheshimiwa Spika, naomba turejee kwenye hoja ya awali ya kupima ukweli uliomo kwenye kifungu cha 5.1 (a) cha Mkataba kati ya TANESCO na kampuni hiyo ya Richmond tulichokinukuu awali kinachosema Richmond Development Company LLC ni kampuni yenye ukomo wa hisa ambayo uwepo wake Tanzania haukinzani na sheria za nchi na kwamba kampuni hiyo ina nguvu na mamlaka yote stahili ya kikampuni ya kumiliki au kukodisha na kutumia mali zake na kuendesha biashara zake nchini.

Katika kupima ukweli wa kauli hizo ndani ya mkataba, kikwazo kikubwa cha mwanzo ambacho Kamati Teule ilikipata kilikuwa ni msingi wa kuichunguza Richmond Development Company LLC kama kampuni wakati uhalali wake kama kampuni huko ilikotoka unabishaniwa au kwa lugha iliyonyooka, haupo. Richmond Development Company LLC, kwa maneno mengine, si kampuni ya mchana bali ya usiku, kampuni ya mfukoni au ya sanduku la barua (mail box company)! Hiyo ndiyo kampuni ambayo shirika la umma, TANESCO, iliingia nayo mkataba wa mabilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kampuni ya wanasheria ya Kimarekani ya Hunton & Wiliams LLP iliyopewa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kuichunguza Richmond Development Company LLC, kama tulivyoeleza hapo awali, inathibitisha kuwa tarehe 23 Juni, 2006 siku ambayo mkataba huo ulisainiwa, Richmond Development Company LLC haikuwa na nguvu za kisheria wala mamlaka yoyote ya kikampuni kuiwezesha kuendesha shughuli zake Tanzania.

Kamati inaamini kuwa wamiliki au waendeshaji wa kampuni hiyo wanaotambulishwa kwenye tovuti ya kampuni hiyo (http://www.rdevco.com/), Bwana Mohamed A. Gire na Dk. Mohammed S. Huque, waliliona tatizo hilo na kuamua siku 19 tu baada ya kusainiwa kwa Mkataba huo kusajili kampuni mpya kwa jina la Richmond Development Company (T) Limited yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo mpya ilisajiliwa tarehe 12 Julai, 2006 na kupewa Hati ya Usajili nambari 57014 ikiwa na wanahisa wawili, kwa majina:

1. Richmond Development Company LLC yenye anuani ya 5825 Schumecher (tunadhani ni Schumacher), Houston – Texas 778057, USA (hisa 750,000) na

2. Naeem Gire wa S.L.P. 1998, Dar es Salaam (hisa 250,000).

Mheshimiwa Spika, kwa kusajili kampuni hiyo mpya, ni dhahiri kuwa wamiliki wa kampuni hiyo walitaka wasibanwe na Kifungu cha 434 cha Sheria ya Makampuni ya Tanzania (Na. 12 ya 2002) kinachotamka wazi kuwa kampuni zote za nje ambazo zinaanzisha ndani ya nchi mahali pa biashara (a place of business), zinawajibika kuwasilisha kwa Msajili wa Makampuni taarifa mbalimbali za kampuni ndani ya siku 30 toka zianzishe mahali pa biashara, kama vile: sheria au mkataba unaoelezea muundo wa kampuni (charter, statutes or memorandum and articles of association); orodha ya wakurugenzi na katibu wa kampuni; anuani kamili ya ofisi kuu ya kampuni; na nakala ya taarifa ya mahesabu ya kampuni na shughuli za kampuni.

Mheshimiwa Spika, kwa kutekeleza masharti yote chini ya kifungu cha 434 cha Sheria ya Makampuni ya 2002, kampuni ya nje itathibitishwa na Msajili wa Makampuni kuwa imetimiza masharti. Uthibitisho huo utakuwa ushahidi kamili wa usajili wa kampuni hiyo ya kigeni nchini ambao utaipa kampuni hiyo haki sawa na kampuni iliyosajiliwa Tanzania katika kumiliki ardhi. Ni dhahiri kuwa taarifa zinazodaiwa chini ya kifungu hicho cha sheria zisingeweza kutolewa na Richmond Development Company LLC, kwa sababu kampuni hiyo isiyo na usajili stahili Marekani haiwezi kuwa nazo.

Pamoja na juhudi hizo za wamiliki wa kampuni ya Richmond, Kamati Teule ilibaini kutokana na ushauri mbalimbali iliopata wa kisheria, kuwa tatizo la uhalali wa Richmond ya Tanzania lilikuwa palepale kwani kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Makampuni kinataka watu wawili au zaidi kuwa na uwezo wa kufungua kampuni. Kwa kuwa mmoja wa wanahisa waliofungua kampuni hiyo ya Richmond ya Tanzania ni Richmond Development Company LLC ya Marekani (yenye asilimia 75 ya hisa zote za kampuni hiyo iliyosajiliwa Tanzania) na kwa kuwa kampuni hiyo ya kimarekani haijasajiliwa Marekani wala hapa Tanzania kwa mujibu wa kifungu cha 434 cha Sheria ya Makampuni na kwa kuwa, kutokana na hiyo sababu, kampuni hiyo ya kimarekani haina nguvu wala mamlaka stahili ya kikampuni, Richmond Development Company (T) Limited ina mwanahisa mmoja tu kwa jina Naeem Gire, hali ambayo haikubaliki kisheria.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa picha iliyojengwa kwenye mkataba tunaouongelea hapa kuhusu hadhi na uhalali wa Richmond Development Company LLC nchini Tanzania ilikuwa ya kisanii, ya uongo na isiyo na msingi wowote kisheria. Kinachosikitisha hapa ni kuwa mwezi Februari, 2006, yaani mwezi moja tu baada ya Wizara ya Nishati na Madini kuiandikia barua Richmond Development Company LLC kuwa haina imani nayo, "kampuni" hiyo ya Bwana Gire, ikajitosa kwenye zabuni nyingine ya Wizara hiyohiyo ya Nishati na Madini, zabuni ya kuingiza nchini jenereta za kuzalishia umeme wa dharura wa Megawati 100.

6.4 Uwezo wa Richmond Kifedha, Kitaalamu, Kiutendaji

Mheshimiwa Spika, tumeeleza kuwa Richmond Development Company LLC iliweza kuaminiwa na Serikali kufanya upembuzi yakinifu wa kina wa mradi wa bomba la mafuta la Dar es Salaam hadi Mwanza kwa kujitambulisha kuwa:
(a) Kampuni hiyo ina uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 25 katika kuendeleza miradi ya nishati;(b) Kampuni hiyo inaaminiwa na taasisi mbalimbali za biashara na fedha za Marekani na ina mahusiano ya karibu na Serikali ya Marekani;
(c) Kampuni hiyo imekamilisha miradi mikubwa ifuatayo duniani: kituo cha umeme cha MW 130 cha Gaziantep, Uturuki (gharama za mradi $117 milioni) na utafutaji wa mafuta na gesi kusini mashariki mwa Ulaya ($150 million).

Mheshimiwa Spika, Serikali ingejaribu kuzichunguza sifa hizo za rejareja za Richmond Development Company LLC hata kwa kuuandikia Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam au kukagua tovuti yake (http://www.rdevco.com/), ukweli ungelidhihirika kuwa "kampuni" hiyo si chochote wala lolote. Tovuti yake yenyewe imesheheni makosa madogo madogo ya Kiingereza na kupambwa na taarifa za juu juu za miradi ambayo "kampuni" hiyo inadai kuitekeleza, hivyo kuzua maswali mengi na hali inayoashiria upeo mdogo kielimu wa wamiliki wa kampuni hiyo.

Kwa mfano ukurasa wa kwanza wa tovuti hiyo iliyoandaliwa mwaka 2004 unabeba dhamira mbili za "kampuni", lakini dhamira ya kwanza haieleweki, inahitaji mpangilio mpya wa sentensi kwa Kiingereza sanifu. Mbali na makosa madogo madogo ya kisarufi na mpangilio, ambayo yamepamba kurasa zote 11 za tovuti hiyo, ukurasa wa 7 unaorodhesha miradi mbalimbali ambayo "kampuni" hiyo ilikuwa inatekeleza: ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo unaoweza kuchukua watazamani 65,000; ujenzi wa bomba la mafuta la kilometa 1,150 na ukarabati wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini Tanzania. Miradi yote hiyo ilikuwa porojo tupu ambazo watendaji wetu Serikalini hawakustahili kuzifumbia macho.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyotarajiwa, "kampuni" hiyo ikashindwa kutekeleza sehemu yake ya mkataba. Mashahidi kadhaa walioongea na Kamati Teule wakati wa uchunguzi, walisema ingelikuwa maajabu kwa "kampuni" ya aina hiyo iliyokuwa haina uwezo kifedha hata wa kuwasafirisha wawakilishi wao kwenda Afrika ya Kusini kwa mazungumzo ya kutafuta fedha za mradi, kampuni iliyokuwa haina uelewa stahili wa masuala ya nishati na iliyokosa rekodi nzuri ya utendaji, kufanikisha mradi huo.

Kwa hali ya kawaida, kampuni yoyote inayoshindwa kutekeleza masharti ya mkataba na Serikali, inalazimika kukaa pembeni kwa muda kusubiri angalau mapungufu yake yasahaulike kidogo. Aidha muda ambao kampuni hiyo itakuwa imekaa pembeni utachukuliwa na waungwana kuwa wa kujisahihisha, wa kurekebisha mapungufu na kuweza kuaminiwa tena. Lakini si kawaida kwa kampuni iliyoshindwa kutekeleza kazi moja ya mteja kurejea muda mfupi baadaye kutafuta kazi nyingine tena yenye unyeti mkubwa kwa mteja huyohuyo bila kigugumizi wala soni.

Hivyo basi, Mheshimiwa Spika, kwa Richmond Development Company LLC kuingia kwenye mchakato wa zabuni nyingine ya Wizara ya Nishati na Madini hata kabla wino kwenye barua iliyoandikiwa na Wizara ikilalamikia utendaji kazi wake haujakauka sawasawa, na kwa Wizara kufumbia macho ubabaishaji bayana wa "kampuni" hiyo na kuiruhusu kushiriki kwenye zabuni ya umeme wa dharura inayohitaji uzoefu maalum bila wasiwasi wa madhara ambayo yangeweza kutokea kwa Taifa, hisia za maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wa Serikali hazikwepeki.

7.0 HITIMISHO NA MAPENDEKEZO

7.1 Hitimisho

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule imeuchambua kwa kina mchakato mzima wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura ulioipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas, Marekani mapema mwaka 2006 ili kuzitolea majibu yaliyokamilika hadidu rejea zote sita ambazo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samuel J. Sitta(Mb), aliipa Kamati Teule tarehe 15 Novemba, 2007 mjini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kurasa zote 165 za Taarifa kubwa ya Uchunguzi ya Kamati Teule ambayo inatokana na kazi kubwa ya kuwahoji jumla ya mashahidi 75, kuwauliza maswali 2,717 na kupitia nyaraka 104, zimebeba ushahidi usio na mashaka yoyote kwamba Wizara ya Nishati na Madini, iliibeba Richmond Development Company LLC kutoka mwanzo wa mchakato wa zabuni hadi mwisho. Kwa kufanya hivyo Wizara, kwa kutokufuata misingi ya utawala bora, ikachangia kwa kiasi kikubwa urefushaji wa mgao wa umeme ulioathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii nchini.

Kamati Teule imeridhika kuwa ukiukwaji huo unaweza kuwa ulichangiwa na hoja ya kukidhi maslahi binafsi. Pengine ndiyo sababu ya Wizara hii kuonyesha tabia ambayo haikuonyeshwa na Wizara zingine ya kukataa katakata kuiruhusu Kamati Teule kuona majalada ya Wizara hiyo yenye mawasiliano kuhusu zabuni hiyo.Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari tu, tumeonyesha katika Sehemu ya Pili ya Taarifa hii jinsi Wizara ya Nishati na Madini ilivyopindisha maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwa kusitisha mpango uliokuwa umekaribia utekelezaji wa kuzalisha umeme kupitia mitambo ya kukodi ya kampuni ya CDC Globeleq bila kuufikisha ujumbe wa Serikali kwa kampuni hiyo wa kurekebisha masharti yao ili mradi huo utekelezwe. Hayo yamefanyika siku ileile Baraza la Mawaziri limetoa maagizo na siku nne baada ya kuanza mgao wa umeme kwa mikoa yote ya Tanzania Bara inayounganishwa na Gridi na Taifa.

Tumeonesha vilevile maamuzi yenye jeuri na kiburi ya kukiuka kwa makusudi Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni zake za mwaka 2005, licha ya Baraza la Mawaziri kusisitiza kwamba Sheria ya Ununuzi wa Umma na kanuni zake izingatiwe. Kama vile Wizara hiyo haihusiki kabisa na utawala wa sheria na utawala bora, ikailazimisha TANESCO isiheshimu ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na kuingilia mchakato wa zabuni wa procurement entity nyingine kwa kuiweka pembeni Bodi ya Zabuni ya TANESCO, kuiagiza TANESCO ivunje sheria kwa kuwabadilisha wajumbe wa Bodi yake ya Zabuni na Wizara kufanya maamuzi ya ununuzi kwa niaba ya TANESCO na kuulazimisha uongozi wake kusaini mkataba na kampuni ambayo TANESCO waliikataa mara tatu kwa vigezo vya kitaalamu kuwa haifai kwa kazi hiyo. Huo ulikuwa udhalilishaji mkubwa wa viongozi na watendaji ndani ya TANESCO.Mheshimiwa Spika, tumebainisha kuwa mwezi mmoja tu kabla ya hiyo zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura, Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa imeiandikia Richmond Development Company LLC kuitaarifu kuwa imeshindwa kutekeleza mkataba baina yake na Wizara kuhusu mradi wa bomba la mafuta. Kimya cha Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC, kuliipa Kamati Teule mashaka kuhusu uadilifu wa viongozi wa Wizara hiyo.

Tumeonyesha vilevile kuwa Richmond Development Company LLC ilikingiwa kifua na kufunguliwa kila mlango na Wizara: majaribio ya Richmond Development Company LLC kubadilisha masharti ya Barua ya Dhamana ya Benki (LC) yaliungwa mkono na Wizara ya Nishati na Madini kwa hamasa kubwa kiasi cha kupuuza maelekezo ya Wizara ya Fedha kwa kulazimisha kufanya mabadiliko katika LC hiyo nje ya mkataba wa makubaliano wa fedha kwenye akaunti ya escrow.(Tumenukuu na kuambatanisha kwenye Taarifa hii barua mbili zilizoandikwa na Wizara hizi mbili tarehe 6 Oktoba, 2006 zikionesha hamasa iliyoigubika Wizara ya Nishati na Madini kuisadia Richmond bila hata kujali maslahi ya Taifa). Tumeonyesha hata jinsi Richmond Development Company LLC ilivyoanza kazi bila kujiandikisha Bodi ya Usajili ya Makandarasi na wahandisi wake kuacha kujiandikisha Bodi ya Usajili ya Wahandisi na jinsi Wizara ya Nishati na Madini ilivyokuwa wima kuitetea kampuni hiyo ya Kimarekani. Aidha, Kamati Teule imejionea jinsi Richmond Development Company (T) Ltd, kampuni tanzu ya Richmond Development Company LLC, ilivyopata Cetificate of Incentives kutoka Tanzania Investment Centre bila kukidhi masharti ya msingi kama vile ushahidi wa mtaji wa kutosha kutekeleza mradi.

Hatimaye, Mheshimiwa Spika, TANESCO walipotaka kuuvunja mkataba kati yao na Richmond Development Company LLC kwa kampuni hiyo ya Kimarekani kushindwa kutekeleza sehemu yake ya mkataba na kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu hadhi ya kampuni hiyo, ni Wizara ya Nishati na Madini iliyoingilia kati na, bila aibu, "kuwezesha" mkataba huo urithiwe na kampuni nyingine katika kipindi ambacho nchi ilikuwa haihitaji kabisa umeme wa ziada licha ya kuwepo fursa za wazi kisheria kwa TANESCO kuvunja mkataba huo bila ya athari za hasara zozote.

Mheshimiwa Spika, ubebwaji wa Richmond Development Company LLC na Wizara ya Nishati na Madini ulichangiwa na kurahisishwa zaidi na ukosefu wa umakini wa maafisa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao, badala ya kuwa washauri wa sheria wa Serikali, wanageuka kuwa wasindikazaji! Taarifa hii imesheheni mifano ya matukio mbalimbali ya majadiliano ambayo Mwanasheria wa Serikali au wawakilishi wake hawafiki, hivyo kukosa uelewa mpana wa michakato mbalimbali. Hata wakifika, mchango wao wa kuilinda nchi dhidi ya vifungu vya sheria vya kutumaliza, hauonekani.

Mheshimiwa Spika, katika suala hili la Richmond Development Company LLC, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilichangia sana kulea ubabaishaji kwa kutohudhuria vikao vya majadiliano na kufumbia macho dosari bayana au pengine kutojali. Mahojiano ya Kamati Teule na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwakilishi wake kwenye majadiliano ya mikataba, yanajieleza yenyewe katika Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) za tarehe 30 Novemba, 2006 na tarehe 5 Disemba, 2007. Ulikuwa wajibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kugundua kuwa Richmond Development Company LLC si kampuni yenye ukomo wa hisa; ulikuwa wajibu wa Ofisi ya Mwansheria Mkuu wa Serikali kuieleza Wizara ya Nishati na Madini kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma inataka kampuni inayoshinda kwa kigezo cha bei ya chini kufanyiwa post qualification, uchunguzi wa kina baada ya kuteuliwa; ulikuwa wajibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuishauri Serikali kuwa business card na karatasi walizoonesha Richmond Development Company LLC haviwezi kuwa mbadala wa consortium agreement kati yake na Pratt & Whitney ya utekelezaji wa mradi huo wa umeme.

Mheshimiwa Spika, utetezi mkuu uliotolewa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini ni kwamba nchi ilikuwa katika dharura, hivyo ilibidi Wizara ichukue hatua ilizochukua na kwamba kanuni ya 42 ya Public Procurement (Goods, Works, Non-consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender) Regulations, 2005 inairuhusu Wizara kuingilia kati mchakato kwenye taasisi yake. Kamati Teule iliyakataa maelezo haya kwani yanapotosha maana halisi ya emergency procurement chini ya Kanuni ya 42. Ni kweli kuwa kanuni hiyo inatoa mwanya na uhuru mpana zaidi wa maamuzi, lakini uhuru huo ni kwa taasisi yenyewe. Ni makosa kwa taasisi moja ya ununuzi (procurement entity) kuingilia maamuzi ya procurement entity nyingine kwa kisingizio cha dharura kama Wizara ya Nishati na Madini ilivyofanya. Ikiwa Wizara ilitaka ifanye kazi hiyo yenyewe, kwa nini basi isisaini mkataba na Richmond Development Company LLC yenyewe as a procurement entity, badala yake kuibambikizia TANESCO mzigo ambao haukuwa wake?

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule sasa inaelewa chimbuko la tabia mbaya iliyoenea nchini ya ajali ikitokea watu kukimbilia kusaidia. Lakini si wote wenye dhamira ya kusaidia, kuokoa. Baadhi yao lengo kuu ni kuiba, kupora! Viongozi tunaobuni miradi kutokana na majanga ya kitaifa, hatuna tofauti na watu wanaokimbilia ajali kama waokoaji kumbe wezi. Ukame nchini ulitabirika, lakini hatukuchukua hatua mapema pengine kwa kusubiri janga kubwa litokee ili kupata fursa ya miradi ya akina Richmond.

Mheshimiwa Spika, Kamati Teule iliyaona mawasiliano ya karibu kati ya Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini katika hatua mbalimbali za zabuni hiyo. Kwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini aliyekuwepo awali, Mhe.Dk. Ibrahim Msabaha(Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndugu Arthur Mwakapugi, hawakukiri kutumwa au kuagizwa kuibeba kampuni hiyo ya Kimarekani, kwa mfumo wa uongozi na utawala bora wanawajibika wenyewe kama ambavyo Waziri Mkuu atapimwa wadau kivyake.

Mheshimiwa Spika, ifikapo mwaka 2025, Tanzania inatakiwa iwe imeondoka kwenye kundi la nchi za kipato cha chini (low-income countries) na kuingia katika kundi la nchi za kipato cha kati (middle-income countries). Kipato cha Watanzania kinategemewa kupanda kutoka Dola za Kimarekani 210 kwa mwaka kilichopo sasa hadi Dola za Kimarekani 3,420 kwa mwaka. Kwa fedha ya Tanzania ni kutoka sh. 262,500/= hadi sh. 4,275,000/= kwa mwaka. Kama Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyosema: maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana, kila mtu atimize wajibu wake.

Moja ya sifa kuu za nchi za kipato cha kati ni kilimo cha kisasa na maendeleo ya kati ya viwanda, shughuli ambazo haziendi bila nishati ya kutosha na ya bei nafuu. Msingi wa kujenga uwezo wa kutosha wa nishati ili kuendeshea viwanda, unatakiwa uanze kujengwa sasa na si baadaye. Kamati Teule inakubaliana na ushauri uliotolewa na Kamati ya Uwekezaji na Biashara katika Taarifa yake kwa Bunge kwa mwaka 2006 kuwa Serikali sasa iandae mpango madhubuti wa muda wa kati na muda mrefu (power system master plan) ukionesha ni namna gani nchi itatekeleza na kukabiliana na tatizo la mfumo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa umeme.Mheshimiwa Spika, mpango wa aina hii utaipunguzia Serikali gharama ya kuingia mikataba ya dharura mara kwa mara kila kukitokea ukame. Aidha mpango huo ujumuishe pamoja miradi kama ya Stieglers George ya kuzalisha umeme wa MW 2100 na zaidi, makaa ya mawe ya Mchuchuma, umeme wa nishati ya gesi asilia, upepo, jua, taka n.k. Hapo tutakuwa tumejijengea msingi mzuri wa kupokea changamoto za maendeleo ya nchi za kipato cha kati.

7.2 Mapendekezo ya Kamati Teule

Mheshimiwa Spika, Kutokana na uchunguzi wa kina tuliuainisha katika taarifa hii, Kamati Teule imejiridhisha na hivyo inatamka bayana mbele ya Bunge Tukufu kuwa mchakato wa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wa MW 100, uliopelekea Richmond Development Company LLC kuteuliwa na hivyo kusaini mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tarehe 23 Juni 2006 na baadaye kurithiwa na Dowans Holdings S.A tarehe 23 Desemba 2006, uligubikwa na vitendo vya ukiukwaji taratibu, kanuni na sheria za nchi na hivyo kujenga kiwingu cha mashaka ya upendeleo, ubadhirifu na rushwa ambavyo vimechangia kumuongezea mwananchi mzigo wa gharama za umeme. Aidha, Kamati Teule imethibitisha bila ya shaka lolote kuwa uteuzi wa Kampuni dhaifu kifedha, kiufundi na kiuzoefu na ambayo haina usajili Marekani wala Tanzania kama kampuni yenye ukomo wa hisa, yaani Richmond Development Company LLC, ulitokana na kubebwa bila woga wala aibu na viongozi waandamizi wa Serikali. Kutokana na msingi huo Kamati Teule inapendekeza yafuatayo:

(1) Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 (Public Procurement Act, 2004) haina nguvu ya kutosha ya kuiwezesha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha kwamba Ununuzi wa Umma unaboreshwa kwa kuongeza ushindani wa ukweli na uwazi na hivyo kuipa Serikali thamani halisi ya pesa zake. Kamati Teule inapendekeza kwamba sheria hii ipitiwe upya ili kuiboresha kwa kuipa Mamlaka nguvu zaidi za udhibiti na uwezo wa kuchukua hatua pale Sheria na Kanuni zinapokiukwa, badala ya kutoa ushauri tu kama ilivyo sasa.

(2) Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma isiwajibike Wizara ya Fedha ambayo nayo ni taasisi ya ununuzi (procurement entity) badala yake iwe chombo huru kinachowajibika Ofisi ya Rais na taarifa zake kuwasilishwa Bungeni.

(3) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A, kama ilivyo mikataba kati ya TANESCO na IPTL, SONGAS, AGGREKO na Alstom Power Rentals inatoa unafuu usiostahili kwa makampuni hayo ya umeme na kuiumiza TANESCO na hatimaye watumiaji na walipa kodi kimapato, k.m mikataba hiyo kuwa na vipengele vya kuibana TANESCO kuyalipia makampuni hayo kodi zinazohusika na uendeshaji (operations), matengenezo/marekebisho ya mara kwa mara ya mitambo (maintenance) gharama za bima, ada za mawakili na washauri elekezi (consultants) gharama za mafuta na gesi ya kuendeshea mitambo, gharama za ukodishaji mitambo (capacity charges) ambazo TANESCO hulipa kila mwezi si chini ya wastani wa shilingi bilioni 2 kwa kila kampuni, izalishe au isizalishe umeme. Kamati Teule inatoa rai kwa Serikali kuwa mikataba yote hii ipitiwe upya mapema iwezekanavyo kama ambavyo mikataba ya madini inavyopitiwa upya sasa na Serikali. Bila kufanya hivyo, mzigo mkubwa wa gharama za umeme utawaelemea wananchi na kushindwa kufikia azma ya Serikali ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

(4) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC ulikuwa wa uzalishaji umeme wa dharura kipindi ambacho nchi ilikuwa katika hali ngumu ya ukame uliokausha mabwawa yote ya kuzalishia umeme. Kamati Teule inaitaka Serikali kutathmini upya uhalali wa kuwepo na kuendelea kuwepo na mkataba huo kutokana na udanganyifu bayana uliofanywa na Richmond Development Company LLC kuhusu uwezo wake kifedha, kiufundi, na uzoefu wake katika masuala ya uzalishaji umeme; usajili na uwepo wake kisheria kama kampuni halali yenye ukomo wa hisa nchini Marekani na Tanzania; uhusiano wake kisheria na Kampuni kubwa ya Kimataifa ya Pratt & Whitney na utambulisho wa Mzungu mmoja kwa jina la John Perun kama mwakilishi wa Pratt & Whitney, mambo ambayo Kampuni hiyo kubwa ya Kimataifa imeyakanusha vikali.

(5) Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC na sasa Dowans Holdings S.A umesheheni makosa mengi ya kisheria yanayoashiria udhaifu mkubwa wa kitaalamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au ukosefu wa umakini ama ubinafsi katika kuiwakilisha Serikali. Kwa mfano, kushindwa kutambua ukosefu wa sifa za kikampuni za Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kuifanyia kampuni hiyo ukaguzi wa awali (due deligence) au ukaguzi baada ya uteuzi (post qualification); kushindwa kutambua tofauti kati ya consortium agreement na proprietary information agreement; kushindwa kuona dosari kisheria za proprietary information agreement; kushindwa kuona tofauti kisheria kati ya Richmond Development Company LLC, RDEVCO,RDVECO na RDC, majina ambayo wamiliki wa Richmond Development Company LLC walikuwa wanayatumia kwa kubadilisha badilisha (interchangerbly) kwa makusudi; kushindwa kuwashauri Wajumbe wa GNT kwamba business card si mbadala wa hati mahsusi kisheria; kushindwa kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa muhtasari wa majadiliano kati ya Kamati ya Serikali ya Majadiliano (GNT) na Richmond Development Company LLC ambao ulizingatia baadhi ya maslahi ya nchi, uwe sehemu ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC; kushindwa kuishauri Serikali kutumia fursa iliyokuwepo wazi ya kuvunja Mkataba baada ya Richmond Development Company LLC kushindwa kutekeleza sehemu yake ya Mkataba; kushindwa kuhudhuria idadi kubwa ya vikao muhimu vya majadiliano;n.k. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye katika majadiliano yake na Kamati Teule alionyesha kutokuelewa kabisa kilichokuwa kinatendeka na wasaidizi wake, na mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Wakili wa Serikali Donald Chidowu, ambaye ushiriki wake katika GNT haukuwa na tija yeyote, wawajibishwe na Mamlaka ya juu ya nchi kwa kuchangia kuiingiza nchi katika mkataba wa aibu.

(6) Katika mikataba yote na makampuni ya nje Serikali ihakikishe kuwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) inatumika kikamilifu katika kupata taarifa kamili za kampuni hizo, kama vile wanahisa, mitaji na anwani. Aidha, Ofisi zetu za Ubalozi zilizo sehemu mbalimbali duniani zihusishwe katika majadiliano na makampuni yanayotoka nje ya nchi kwa lengo la kupata taarifa zao za msingi na kuboresha nguvu ya hoja ya Serikali.

(7) Madhumuni ya Mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company LLC yalikuwa kuzalisha umeme wa dharura kwa kipindi cha miezi kumi na mbili (12) tu.

Muda huo ungeweza kuongezwa baada ya kutathmini hali ya ongezeko la maji katika mabwawa ya kuzalishia umeme nchini. Kabla ya muda wa tathmini hiyo haujafikiwa, wakati majadiliano yakiendelea GNT ikaongezea Richmond Development Company LLC muda wa kukodi mitambo hiyo kuwa miaka miwili (2). Kamati Teule haikuona vielelezo vyovyote vilivyojenga uhalali kwa GNT kuongeza muda huo. Uamuzi huo umeliongezea Taifa mzigo mkubwa wa gharama zisizokuwa za lazima. Mathalan, kwa upande wa capacity charges tu, TANESCO itailipa Dowans Holdings S.A jumla ya shilingi bilioni 54.8 kwa kipindi kilichongezwa cha mwaka mmoja. Aidha, GNT ilishindwa kutambua ulaghai wa Richmond Development Company LLC kuhusu mwakilishi wa Pratt & Whitney na hivyo kuamini karatasi ambayo ilikuwa haijathibitishwa na mawakili na diskette zenye picha za mitambo ya Pratt & Whitney, vielelezo ambavyo Kamati Teule imegundua na kuthibitisha kuwa vilikuwa vya kugushi. Vilevile, bila kujali kwamba TANESCO ingelezimika kuilipa Richmond Development Company LLC shilingi milioni 152 kwa siku kama gharama ya kuweka vifaa vyao nchini, GNT ikakubali kilegelege kuitoza Richmond Development Company LLC shilingi milioni 12 tu kwa siku kama fidia kwa ucheleweshaji wa kuanza kuzalisha umeme kulingana na tarehe iliyokubalika kwenye mkataba. Kamati Teule inapendekeza kuwa Wajumbe wote wa GNT ambao ni maafisa waandamizi wa Serikali wawajibishwe mara moja kwa kushindwa kutumia elimu na ujuzi wao kulinda maslahi ya Taifa.

(8) Pamoja na Uongozi wa TANESCO kubainisha mapungufu ya Richmond Development Company LLC na kutoa notisi tarehe 27 Octoba 2006 ya kusitisha Mkataba tena kwa ushauri mahsusi kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Mawakili, Wizara ya Nishati na Madini haikuupenda mwelekeo huo hivyo tarehe 28 Novemba 2006 baadaye Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Nazir Karamagi, Mb akiwa nje ya nchi Calgary, Canada alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Balozi Kazaura kuangalia uwezekano wa kuhaulisha Mkataba wa Richmond kwa kampuni nyingine. Siku tano baada ya mawasiliano hayo, yaani tarehe 4 Desemba 2006, TANESCO ikapokea barua kutoka Richmond Development Company LLC ikielezea nia ya kampuni hiyo kutumia haki yake chini ya kifungu 15.12 cha mkataba ili kuhamisha majukumu yake ndani ya mkataba kwenda kwa kampuni mpya ya Dowans Holdings S.A. Kamati Teule ilipata taarifa za ndani ya Wizara na TANESCO kuwa viongozi wa Wizara kama kawaida yao waliishinikiza TANESCO kuridhia ombi hilo la Richmond Development Company LLC kuhaulisha mkataba kwa Dowans Holdings S.A. TANESCO ikalazimika kuridhia uhaulishaji wa mkataba huu badala ya kutumia fursa iliyokuwepo ya kusitisha mkataba baada ya kutoa notisi ya siku thelathini. Kamati Teule inaamini kwamba uamuzi wa Wizara ya Nishati na Madini kuizuia TANESCO isitumie fursa ya kusitisha mkataba huo, unaashiria jinsi viongozi wetu wanavyojali zaidi faida na maslahi ya makampuni ya nje kuliko maslahi mapana ya Taifa. Tarehe 3 Desemba TANESCO kama ilivyoagizwa ikaridhia uhaulishwaji wa mkataba huo lakini kipindi ambacho hali ya maji katika mabwawa yetu ya kuzalishia umeme ilishaanza kurejea kuwa ya kawaida. Uamuzi huo umeingizia Taifa hasara kubwa. Hivyo basi Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Nazir Karamagi, Mb aliyeshabikia sana uhaulishaji huo, awajibishwe.

(9) Matokeo ya uchunguzi ya Kamati Teule kama yalivyoainishwa hapo juu yanadhihirisha wazi jinsi Taifa lilivyotumbukizwa kwenye hasara kubwa kutokana na mkataba huo wa Richmond Development Company LLC na Dowans Holdings S.A, kinyume na taarifa iliyotolewa na TAKUKURU (wakati huo TAKURU) kwamba Taifa halikupata hasara yoyote. Taarifa ya TAKUKURU ililenga kuficha ukweli (white wash) hivyo ikaishia kujikanganya kwa kukiri kuwepo kwa mapungufu lakini yasiyokuwa na athari. Taarifa hiyo imemong'onyoa kwa kiasi kiasi kikubwa hadhi na heshima ya chombo hiki muhimu cha kitaifa kilichopewa dhamana ya kupambana na rushwa na sio kuipamba ili kurejesha heshima ya umma katika taasisi hiyo. Kamati teule inapendekeza mabadiliko ya haraka ya uongozi wa taasisi hiyo.

(10) Taratibu za malipo ya madai ya mkataba wa umeme wa dharura zinafanywa kupitia Barua ya Dhamana ya Benki iliyofunguliwa kati ya TANESCO na benki ya CRDB ya dola za Kimarekani milioni 30,696,598 iliyofunguliwa tarehe 27 Desemba 2006. Kamati Teule imethibitisha kwamba hadi kufikia tarehe 19 Juni 2007 malipo yaliyolipwa na Benki Kuu yamefikia Dola za Kimarekani 35,561,598 kiasi hicho ni zaidi ya Barua ya Dhamana ya Benki kwa dola za kimarekani milioni 4,565,000 wastani wa shilingi bilioni 5.7. Kamati Teule inashangaa ni vipi Benki Kuu iidhinishe malipo hayonje ya Barua ya Dhamana ya Benki iliyofunguliwa kati ya TANESCO, CRDB Bank na Dowans Holdings S.A. Kwa kuwa Benki Kuu ndio msimamizi mkuu wa akaunti maalum (Escrow Account), Gavana wa Benki Kuu pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wachunguze kwa makini uhalali wa malipo hayo na kuhakikisha kwamba udhaifu wa namna hii haujitokezi tena hapo baadaye.

(11) Wakati umefika sasa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 (Public Leadership Code of Ethics Act) ifanyiwe marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaonekana wa kawaida sasa wa viongozi waandamizi wenye dhamana kisiasa kuendelea na biashara zao wakiwa madarakani, hivyo kuwaweka kwenye mtihani mkubwa wa mgongano wa kimaslahi katika maamuzi yao. Tufike mahali ambapo sheria iwalazimu kuchagua kati ya Utumishi wa Umma au biashara binafsi. Viongozi waandamizi wenye dhamana kisiasa (mawaziri na kuendelea) kuendelea na biashara zao wakiwa madarakani hivyo kuwaweka kwenye mtihani mgumu wa mgongano wa kimaslahi.

(12) Serikali iondokane kabisa na utaratibu wa kutumia mawakala katika ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini na kuhakikisha kuwa Wizara husika ina taarifa za bei halisi ya mitambo kila wakati ili kujiepusha na mchezo wa kawaida wa mawakala kupandisha bei mara mbili au zaidi ya bei halisi. Kamati Teule ilishuhudia bei za mitambo hiyo jijini Houston, Texas Marekani kwa watengenezaji kiwandani ikiwemo kampuni ya Kawasaki Gas Turbines – Americas ambayo iko chini ikilinganishwa na bei zinazotolewa na mawakala hao, jambo ambalo lingeiwezesha Serikali kununua na kumiliki badala ya kukodi kwa muda mfupi na kwa gharama kubwa. Mathalan, MW 105 zingepatikana kwa kununua mitambo sita ya MW 17,5 kila mmoja kwa gharama ya shilingi bilioni 56.25 badala ya shilingi bilioni 108.7 tulizotandikwa na Richmond Development Company LLC mitambo hiyo ikibaki mali ya wakodishaji. Kwa kumalizia Kamati Teule ilithibitisha kwamba kauli iliyokuwa inatolewa mara kwa mara na baadhi ya viongozi wote tuliowahoji kwamba kipindi hicho cha ukame haikuwa rahisi kupata mitambo hiyo na ilikuwa ikigombaniwa na nchi nyingi kauli hiyo ilikuwa sio ya ukweli na upotoshaji mkubwa.

(13) Utaratibu tuliourithi kutoka kwa wakoloni na kuuzoea wa kuiona mikataba ya kibiashara kuwa ni siri hata kwa walipa kodi wenyewe na kuwa uwanja wa pekee wa watendaji, ambao Waziri wa Mipango Uchumi na Uwezeshaji Mhe. Dk Juma Ngasongwa (Mb) aliusifia bungeni tarehe 19 Aprili 2007 kuwa best practice wakati akijibu swali la Mhe. Masolwa C. Masolwa (Mb) Mbunge wa Bububu, umepitwa na wakati na unakiuka misingi ya demokrasia na uwajibikaji. Matokeo ya utaratibu huu ni kuwepo kwa mikataba mibovu inayoficha vipengele vinavyoibebesha Taifa mizigo mikubwa ya gharama zisizokuwa za lazima kama tulivyoainisha katika pendekezo namba 3 hapo juu. Kamati Teule inatoa wito kwa Serikali kuondokana na utaratibu huu usio na tija kwa kuzihusisha Kamati za Kudumu za Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo. Aidha, Kamati Teule inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba mikubwa nay a muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba iliyofichika.

(14) Pamoja na dharura iliyokuwa inalikabili Taifa, Serikali haiwezi kuwa kinara wa uvunjaji wa taratibu, kanuni na sheria za nchi kwa makusudi. Kamati Teule imeanisha katika taarifa hii vitendo vya ubabe, ujeuri na kiburi vilivyofanywa na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini alimradi kampuni waliyoitaka iteuliwe kiasi cha kupindisha hata maamuzi ya Baraza la Mawaziri bila wasiwasi wowote, kukaidi ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma mara tatu mfululizo na kinyume na maagizo ya Baraza la Mawaziri lililotaka Sheria ya Ununuzi wa Umma izingatiwe, kukiuka sheria kwa makusudi kwa kuingilia mchakato wa zabuni wa taasisi nyingine ya ununuzi, kuvipuuza vyombo vya ndani vya maamuzi vya TANESCO (Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Zabuni n.k), kuilazimisha Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuridhia maamuzi yaliyofanywa na Wizara ya kuibeba Richmond Development Company LLC kinyume cha sheria na taratibu n.k. Wizara hiyo katika kuibeba Richmond Development Company LLC ilifikia hatua ya kupotosha kwa makusudi ushauri wa Wizara ya Fedha uliozuia malipo ya awali ya Dola za Kimarekani Milioni 10 katika Barua ya Dhamana ya Benki ya Richmond Development company LLC. Siku iliyopotosha ilikuwa tarehe 6 Octoba 2006. Kamati Teule inapendekeza kwamba Waziri wa Nishati na Madini wa wakati huo Mhe. Dk. Ibrahim Msabaha (Mb) na Katibu Mkuu Ndugu Arthur Mwakapugi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu kwa kuliingiza Taifa kwa makusudi kwenye mkataba na kampuni ya mfukoni ambao umesababisha hasara kubwa kwa nchi. Aidha Kamishna wa Nishati Ndugu Bashir Mrindoko naye achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kushindwa kumshauri Katibu Mkuu mpya wa Wizara kuhusu udhaifu wa Richmond Development Company LLC ambao ulijulikana dhahiri na Wizara toka mwaka 2004 kwenye mkataba wa Bomba la Mafuta. Ndugu Mrindoko ndiye aliyeiandikia barua kampuni hiyo kusitisha mkataba wake na Serikali mwezi mmoja tu kabla ya mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura haujaanza.

(15) Utaratibu wa kuteua wakurugenzi na makamishna katika Wizara kuwa wajumbe wa bodi za wakurugenzi za mashirika yaliyo chini ya Wizara, unazua mgongano wa kimaslahi, kudhoofisha usimamizi na uwajibikaji, hivyo Serikali iupige marufuku mara moja. Mfano Kamishna wa Nishati ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ambaye alishiriki kwenye kikao kilichowakataa wazabuni wote kuwa hawafai na kuishauri Serikali vilivyo, aliporejea Wizarani alishiriki katika kutengua maamuzi ya Bodi ya TANESCO.

(16) Uhuru mkubwa ambao viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini waliutumia bila wasiwasi katika kuhakikisha kwamba kampuni waliyoitaka, Richmond Development Company LLC, inapewa zabuni ya umeme wa dharura; maelekezo ya mara kwa mara ya Waziri Mkuu kwa Wizara katika kila hatua ya mchakato huo; upendeleo wa dhahiri ambao Richmond Development Company LLC iliupata kutoka taasisi mbalimbali za Serikali k.m Kituo cha uwekezaji (TIC) ambacho kilifikia hatua ya kufumbia macho baadhi ya taratibu zake za msingi ili kuipa kampuni tanzu ya Richmond Development Company LLC cheti cha uwekezaji haraka iwezekanavyo; kutotimiza masharti ya Bodi za Makandarasi na Wahandisi na Wizara ya Nishati na Madini kuikingia kifua kampuni hiyo isichukuliwe hatua za kisheria; uteuzi wa mwisho wa Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kufanywa na Waziri Mkuu mwenyewe tarehe 21 Juni 2006; uamuzi wa kuiteua Richmond Development Company LLC kuwa mkandarasi kusafishwa na TAKURU ( sasa TAKUKURU) kuwa ulikuwa wa wazi na wa haki; uamuzi wa Serikali kuizuia TANESCO isivunje mkataba na kampuni hiyo licha ya sababu zote kisheria kuwepo, ni baadhi tu ya viashiria vya nguvu kubwa iliyo juu ya Wizara ya Nishati na Madini kutumika katika suala hili na Kamati Teule kutokana na ushahidi wa kimaandishi, kimazingira na wa mdomo, inaiona nguvu hiyo kuwa ni Waziri Mkuu.

Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inatamka wazi kuwa Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Kamati Teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa hizo zinazomgusa moja kwa moja Mhe. Waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond Development Company LLC. Hata hivyo Kamati Teule imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge letu Tukufu. Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge. Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake. Kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia Kamati Teule ya Bunge ilifadhaishwa sana na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ya kukaidi amri ya kuwasilisha nyaraka zinazohitajika na Kamati Teule.

Kamati Teule inaliomba Bunge litafakari kitendo cha aina hii na kufikiria hatua za kuchukua dhidi ya watendaji wa namna hiyo.

7.0 SHUKRANI

Mheshimiwa Spika, naomba kurudia kukushukuru wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwa kutupa heshima hii kubwa ya kuunda Kamati Teule ya Bunge.

Pia napenda kuishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano wake mzuri ambao uliiwezesha Kamati hii kupata taarifa mbalimbali. Vilevile naushukuru Ubalozi wa Tanzania wa Washington D.C, Marekani kwa kuwawezesha baadhi ya Wajumbe wa Kamati hii waliosafiri kwenda Marekani kufanya kazi yao kwa ufanisi. Nakishukuru Chama cha Uwekezaji cha Watanzania waishio Marekani (Tanzanian American Investment Forum- TAIF) chini ya Mwenyekiti wake Dk. Lenard Tenende kwa mapokezi mazuri ya Wajumbe wa Kamati Teule walipozuru Houston, Texas - Marekani.

Mheshimiwa Spika, naomba vilevile nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara, Mhe. William Shellukindo (Mb) na wajumbe wake wote kwa kusimama kidete kuhakikisha kuwa kamati yao inapata majibu kupitia kamati Teule ya Bunge.Shukrani za pekee na pongezi ziwaendee waandishi wa habari na vyombo vyao walioweka maslahi binafsi pembeni na kupiga kelele kwa nguvu zao zote kuhusu mwenendo uliokuwa hauridhishi wa mchakato wa zabuni ya umeme wa dharura. Kwa niaba ya Kamati Teule naomba, Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpa pole mwandishi mahiri na jasiri Saed Kubenea na mwenzake Ndimara Tegambwage kwa mkasa wa kushambuliwa na kuumizwa vibaya na watu tunaoamini hawafai kuitwa Watanzania.

Vilevile shukrani zetu ziende kwa Watanzania na watu wote wenye nia njema na nchi hii waliotuunga mkono kwa kutupa taarifa mbalimbali, maoni kwa njia ya barua pepe, simu n.k.

Kwa kumalizia namshukuru Katibu wa Bunge Ndg. Damian S.L Foka kwa kuisadia Kamati hii kufanya kazi vizuri. Aidha, shukrani za pekee zinatolewa kwa Katibu wa Kamati hii Ndg. Anselm Mrema akishirikiana na Ndg. Emmanuel Mpanda, Ndg. Lina Kitosi na Ndg. Nenelwa Mwihambi kwa kuisaidia Kamati kufanikisha kumaliza kazi hii kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.Mhe. Dk. Harrison G. Mwakyembe
MWENYEKITI
KAMATI TEULE YA BUNGE
06 Februari 2008