MMILIKI wa taasisi ya Mo Ibrahim amesema matatizo yote yanayoikumba nchi za bara la Afrika, ikiwemo vita, njaa na magonjwa, yanatokana na viongozi wake kutokuwa makini na kutofuata misingi ya utawala bora.
"Viongozi wetu wengi si makini na pia hawafuati misingi ya utawala bora na kutokana na haya ndio maana bara hili bado lipo nyuma kiuchumi na linasumbuliwa na matatizo ya njaa, magonjwa na vita," alisema mmiliki huyo, Mo Ibrahim jijini Dar es Salaam juzi katika hafla maalum ya muziki ikiwa ni sehemu ya maadalizi ya mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Katika mkutano uliokutanisha viongozi mbalimbali kutoka nchi za bara la Afrika, pamoja na mambo mengine walijadili masuala mbalimbali yakiwemo ya mabadiliko ya hali ya hewa, kilimo na maendeleo ya nchi za Afrika.
Mo Ibrahim, ambaye ni milionea alifafanua kwamba viongozi wa nchi za Afrika ni wepesi wa kuzungumza lakini si watendaji katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.
Alisema kutokana na hali hiyo, Afrika inaonekana ni bara masikini na lenye matatizo mengi ikiwa ni pamoja na vita, njaa na magonjwa.
"Kutokana na rasilimali tulizonazo katika nchi zetu hapa Afrika, hakuna sababu ya kuwa nyuma kiuchumi na wala kukumbwa na matatizo ya magonjwa, vita na njaa. Lakini haya ni kutokana na kutotekelezwa ipasavyo na kwa vitendo mipango ya maendeleo inayokuwa inawekwa na viongozi wetu," alisema
Hata hivyo, Mo Ibrahim alisema bado kuna nafasi kwa viongozi wa Afrika kufanya jitihada zaidi kwa lengo la kufaniksha uchumi wa bara hili ili uachane na utegemezi kwa nchi za barani Ulaya, Amerika na Asia.
"Ni wakati sasa kwa viongozi na Waafrika kujiamini katika mipango yao na kuachana na tabia ya kutegemea kusaidiwa katika kila kitu," alisema tajiri huyo.
"Ni muhimu tukafikiria maisha ya baadaye ya watoto wetu yatakuwaje endapo hali itaendelea kama ilivyo sasa katika bara hili zuri na lililojaa mali."
Tuesday, November 17, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment