Shule za Msingi ni nguzo kubwa ya maendeleo kielimu katika sehemu mbalimbali hapa nchini na duniani kwa ujumla. Imefahamika na vyombo mbalimbali kuwa bila kuimarisha na kuzijengea mazingira mazuri shule za msingi basi elimu bora itakuwa ni sawa na ndoto isiyotimilika.
Vilevile ni bora kutambua kuwa maendeleo ya kielimu kwa mtu yeyote huanzia shule za msingi. Hivyo kuimarisha mazingira ya shule za Sekondari wakati yale ya shule za msingi ni duni ni sawa na daktari kutibu ugonjwa bila kuzuia chanzo cha ugonjwa huo. Hivyo tusipoweka mazingira mazuri ya shule za msingi, shule za sekondari zitakuwa zinapokea wanafunzi ambao hawatapenda kusoma kwani watahisi kuwa hata sekondari watakutana na mateso yaleyale waliokuwa nayo shule za msingi.
Tabia imejengeka ya vijana na watu mbalimbali waishio mbali na maeneo watokako kujivunia maendeleo ya mahali walipo au wanapoishi bila kujua kuwa wanawajibu wa kujivunia maendeleo ya kule watokako pia.
Ni wajibu wa kila mtu kujua kuwa ana wajibu wa kusaidia shule za msingi katika maeneo atokako ili kuboresha kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa shule hizo. Mazingira ya kusomea kwa shule za msingi yakiboreshwa tutapata watoto watakaopenda shule na kupenda kuendelea na Sekondari pia.
Hivyo kwa kuanzia, elimu inatakiwa ili kuwaelimisha wazee kwa vijana waishio Dar-es-Salaam na Sehemu za jirani kuweza kujitolea ili kusaidia kununua madawati ya shule za Msingi zinazohitaji msaada huo Wilayani Kyela.
Ifahamike kuwa juhudi zinazofanywa na mbunge wa jimbo la Kyela Dk. Harrison Mwakyembe katika kuleta maendeleo yote kwa ujumla ni kubwa mno, hivyo anapaswa kuungwa mkono kwa kuchangia madawati kwa shule za msingi ikiwa ni pamoja na kuunga mkono jitihada zake za kupambana na mafisadi nchini.
Maendeleo ya Wilaya ya Kyela hayataletwa na mtu mwingine yeyote bali na wananchi wake, hasa watokao maeneo hayo japo hawaishi huko kutoka na mgawanyiko wa kazi. Hawa ndio wanaopaswa kuleta maendeleo ya nyumbani kwao na kujivunia hata wawapo sehemu nyingine nchini.
Hivyo kwa ujumbe huu natoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kusomea ya kizazi chetu na Taifa la kesho waweze kuungana na kusaidia madawati kwa ajili ya shule za msingi Wilayani Kyela.
Ni matarajio yangu kuwa mahitaji ya madawati kwa shule za msingi ni makubwa sana hivyo, tukianza mapema kulishughulikia tatizo hili tunaweza kulipunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kulimaliza kabisa.
Hii ni Wilaya yetu, watoto wanaosoma wakiwa wamekaa chini au kwenye mawe ni vijana wetu, kwahiyo kusaidia kuwajengea mazingira mazuri ni jukumu letu na ni kwa faida yetu na vizazi vyetu vya baadaye.
Kila mmoja wetu kwa wakati wake akae chini alifikirie sana suala hili, atafakari kwa mapana na marefu faida atakayoipata yeye binafsi na vijana wetu baada ya kusaidia kuyaboresha mazingira ya kusomea katika shule za msingi.
Umefika wakati sasa kwa kila mmoja wetu kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya Wilaya yetu bila kujali utatoa nini na kiasi gani kwani kutoa ni moyo. Vilevile ukichunguza kwa undani zaidi utagundua kiwango cha vijana wetu wanaoendelea na masomo ya juu kutoka Wilayani Kyela kimepungua na kitaendelea kupungua kama juhudi za makusudi hazitafanywa ili kuboresha mazingira ya kusomea kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.
Fanya utafiti wako binafsi na ung’amue vijana wangapi wanaojiunga na kidato cha Kwanza, Tano, Vyuo na Vyuo vikuu kutoka Wilaya ya Kyela hapo ndipo utagundua kuwa huko tuendako hali itakuwa mbaya zaidi kama hatutachukua tahadhali mapema.
HITIMISHO: Ndugu zangu, tujiandae kufanya kila linalowezekana ili kuokoa hali hii kwa faida yetu wenyewe na vizazi vyetu vya baadaye. Kwa kuanzia hapa tutaendelea kusaidia na mambo mengine ili kuhakikisha kiwango cha wasomi na maendeleo Wilayani Kyela kinakua kila kukicha.
Ewe mwanaKyela saidia madawati kwa shule za msingi Kyela ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mbunge wetu na Serikali kwa ujumla.
Niandikie:
Africarkagema@airtanzania.com
kyela@live.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment