Friday, November 20, 2009

Umasikini wa Tanzania ni wa Kujitakia

Africar T Kagema

UNDP inatoa taarifa juu ya "The concentrated poverty". Yaani umaskini wa kutisha, kwa bahati mbaya Tanzania ni moja ya nchi zilizo chini ya mstari mwekundu wa umaskini ambao wao wanaita "below poverty level" au absolutely poverty". Huu ni umaskini unaozidi kawaida ya umaskini, waweza kuita umaskini sana, au umaskini zaidi, ama umaskini mno, lakini yote hayo yanaashiria neno moja tu nalo ni kwamba umaskini unaoikabili nchi yetu ni sawa kabisa na ugonjwa wa ukimwi kwa maana ya kwamba umaskini wetu sasa hautibiki.

KATIKA kuufafanua umaskini, mtu aweza kuuweka ama kuugawanya katika mafungu mawili, umaskini wa nchi (au taifa) na umaskini wa watu au "mass poverty" yaani walio wengi katika ujumla wao. Enzi za mkoloni nchi yetu ilikuwa na umaskini wa watu tu yaani "individuals" lakini haikuwa na umaskini wa dola kama uliopo sasa ambapo takribani asilimia 50 ya bajeti ya serikali inatoka kwa wahisani.

Katika uhalisi wa mambo nchi yetu ni ombaomba, hata wanaodai Mkapa amerudisha heshima ya Tanzania kimataifa sijui wanatumia vigezo gani kwani katika ukweli wa maisha hakuna omba omba yeyote aliyepata kuheshimika. Heshima ya Tanzania italetwa kwa kujitegemea na kujitosheleza, kwanza kwa chakula na baadaye kwa mahitaji mengine, yaliyo muhimu kwa taifa. Enzi za mkoloni Tanganyika ilikuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa mkonge ambapo ilitoa asilimia 28 ya mahitaji ya dunia ukiacha mazao mengine kama nyonyo, karanga, pamba na ngozi, na kahawa.

Kwa mapato hayo serikali ya mkoloni haikuwa lofa iliweza kujenga mabarabara, njia za mawasiliano, na kutoa elimu bora kwa hao waliobahatika kusoma. Kwa maneno mengine walau serikali iliweza kujitegemea, lakini sasa kila kitu kiko nyang'anyang'a na hoi bin taabani. Hakuna mradi wowote wa kitaifa ambao ungeweza kutoa ajira ya maelfu kama ukoloni, hakuna watu wabunifu ndani ya hiyo kada ya watawala badala yake umahili wao uko kwenye kudhibiti wapinzani na kuendesha mizengwe ya kuwawezesha kubaki madarakani. Wao watawala, ushindi wanaouona muhimu ni ule tu wa uchaguzi mkuu. Ule ukweli kwamba wao baada ya kuwashinda wapinzani, nao wameshindwa na umaskini hawaujali wala hawaoni aibu.

Inapotokea kwamba dola imekuwa maskini hadi kuendeshwa kwa misaada toka nje ya nchi na watu (wananchi) nao wakawa maskini hadi kufikia kiwango cha kushindwa kufanya lolote na kubaki kama walemavu kungojea kudra za Mungu basi hapo kuna tatizo mara mbili yaani tatizo la umaskini na tatizo la watu wenyewe. Lakini papo hapo viongozi wakuu wa serikali wanapokuwa ni matajiri kuliko serikali yao, basi hapo ndipo kinapoinuka kitendawili cha uongozi bora.

Mawaziri walio matajiri, wakuu wa mikoa walio tajiri, makatibu wakuu walio tajiri, na wabunge walio tajiri, je, wamefanya biashara gani madarakani hadi wakaupata utajiri walio nao? Kisha je wameulipia kodi ya mapato? Maana inaonyesha kwa utajiri wao basi wanavyo vyanzo vya uhakika vya mapato na kwa kuwa katika nchi yetu kuna sera ya kutoza kodi ya mapato (wakati mwingine hata kabla ya mtu hajapata) basi na wao watoe mchanganuo wao kuthibitisha kwamba nao ni raia wema wanaoilipa serikali mapato sawa na sheria za nchi zinavyoagiza!!

Kitendawili hiki ni kigumu kuteguliwa ingawa jibu lake liko wazi, kitendawili chenyewe ni kwamba hapa kuna nchi yenye rasilimali za kila namna lakini bado nchi hiyo ni maskini ya kupindukia duniani, nchi hiyo ilipotawaliwa na Wakoloni haikuwa maskini kama ilivyotawaliwa na watawala waliopo sasa, wakati nchi ni maskini, na watu ni maskini mno. Viongozi ni matajiri wa kupindukia. Je kuna mchezo gani umechezwa kuyaleta haya? Jibu wanalo wenyewe watawala, wanajua jinsi walivyofanya hata kuupata utajiri walio nao sasa isipokuwa wanajifanya hawajui wafanye nini ili kuondoa umaskini kwa nchi yao na watu wao, kwa kuwa akili yao imeishia kujitajirisha wao na siyo nchi. Vijana wapatao laki nne wanamaliza elimu ya msingi kila mwaka lakini uongozi uliopo madarakani haujui ufanye nini au uwapeleke wapi,hivyo baada ya kutoka darasani wanaishia "vijiweni".

Viwanda vingi vimekufa, na mashirika ya umma mengi yameanguka waliokuwa wafanyakazi nao inabidi waungane kwenye vijiwe na vijana wao wanaotoka darasani hadi vijiweni. Kutokana kukosekana sera ya uhakika ya kilimo, kilimo kimebaki duni toka enzi za Mwalimu Nyerere hadi sasa na kwa uduni huo.Kilimo kimejiunga kwenye siasa na kutengenezewa majina mazuri ya kisiasa kama ‘’KILIMO KWANZA’’ wakati uhalisia sio huo. Tumebaki kudanganyana tu ili mradi siku iende. Hakuna elimu ya kuwaelimisha wananchi hasa vijana wajue umuhimu wa kilimo. Mikopo ya Kikwete inatolewa kwa wafanyabiashara badala ya wakulima, na wafanyabiashara wenyewe sio wahitaji halisi wa mikopo hiyo kwania tayari walishakuwa na mitaji ya kutosha. Wakulima wanaachwa kama walivyo, vijana wanaona kilimo kama hakiwezekani kwani hakiwaondoi katika dimbwi la umasikini wa kutupwa. Wakulima hawapendelewi wala hawajengewi mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao kama wanavyofanyiwa wafanyabiashara, hivyo vijana wanaona ni bora kufanya biashara ili wajiingize kwenye mazingira mazuri kuliko kiliko kulimo. Kizazi kipya cha vijana wanakimbia kilimo vijijini na kuja mjini kubahatisha maisha mapya. Wale vijana wanaozaliwa mijini, wao wanakimbilia majuu (wanazamia meli), kizazi cha kale cha wakulima kinazeeka na kudhoofu na hakuna wa kuziba pengo, hivyo usemi wa kwamba Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi umebaki kauli za maandishi tu, lakini katika uhalisi wa mambo Tanzania haina wakulima ndiyo maana ni nchi inayoumwa njaa kila mwaka. Pia Tanzania si nchi ya wafanyakazi maana hakuna kazi nyingi za kufanya kwa sababu hakuna viwanda wala makampuni au mashirika ya kutoa ajira.

Yale yaliyokuwepo yameuawa na watawala waliopo madarakani. Sasa inabidi wote wenye kutazama mambo katika umakini wajiulize nchi ambayo imepukutisha maelfu ya askari wake toka jeshini baada ya kulazimishwa na sera za IMF za kuwa na jeshi dogo, na hivyo kuwalazimisha askari hao kujiunga na walalahoi wengine vijiweni, nchi ambayo imeua mfumo wake wa elimu na kuwafanya vijana wake wasipate elimu ya kuwasaidia kuishi badala yake vijana wake wakawa na elimu ya nadharia ambayo baada ya mtu kumaliza shule (kutoka darasani) anashindwa kuitumia (to apply) aidha hapo kijijini au mjini, mwisho anaishia kijiweni kuvuta bangi au kulamba unga. Ndio vijana hawa wanalaghaiwa na wafanyabiashara wakubwa kujiingiza katika biashara haramu.

Nchi ambayo inashindwa kuzalisha kizazi kipya cha wakulima na waliopo inawaacha wawe wachovu zaidi kwa kuvuruga mfumo wa masoko ya mazao yao na kuwasababishia umaskini usiomithilika, nchi ambayo haina mpango wowote wa kuongeza ajira kwa maelfu ya wananchi wake, nchi ambayo imeua mfumo wa utoaji haki na kusababisha magereza kufurika wafungwa na mahabusu, nchi ambayo haina mikakati yoyote ya kuwatumia wafungwa kuzalisha mali ili kujikimu wawapo magerezani badala ya kutegemea pesa kutoka serikalini, na mahakama zake kuwa na mafuriko ya kesi za jinai. Je nchi ya namna hiyo ina uhakika gani wa kudumisha amani yake wakati inayaacha mabomu yanayongojea wakati wake ufike yalipuke?

Kwa hakika nchi yetu ni mfano wa mtu anayetembea sambamba na gema ambaye kuna uwezekano wa kutumbukia wakati wowote. Hata hivyo ieleweke wazi kwamba tatizo la umaskini ni matokeo tu ya uzembe wa watawala, endapo nchi itapata utawala ulio makini na ulio dhamiria kuondoa tatizo hili, umaskini wa Tanzania unaweza kufutika baada ya muda mfupi na Tanzania ikawa miongoni mwa nchi tajiri na zenye uchumi imara au "economic giant" katika dunia hii.

Mtu hawezi kuamini akielezwa kwamba umaskini wa Tanzania ni sera ya makusudi kabisa ambayo lengo lake kuu ni kudhibiti wananchi na kuwawezesha watawala kuendelea kudumu madarakani hadi siku ya kufa. Watawala wa nchi hii wanajua wazi kwamba wakiwaondoa watu wao katika dimbwi la umasikini hawawezi kutawalika na pia hawawezi kuburuzwa, kwa hiyo umaskini ni silaha yao nzuri ya kuendelea kutawala.

Fikiria kama Watanzania wangekuwa na elimu, shibe, na utajiri, ni wazi kwamba asingekuweko mgombea yeyote wa ubunge, urais, au udiwani wa kuhonga watu soda, pilau, khanga au pombe za kienyeji. Pasingekuweko na mtu wa kuuza shahada yake ya kupigia kura kwa Tshs: 2,000. Hapo ndipo yangekuweko mashindano ya sera na programu za kuendeleza nchi, majimbo, maeneo, au mitaa.

Kwa ajili hiyo umaskini kama ulivyo katika nchi hii ni kikwazo cha mengi, ni kikwazo dhidi ya demokrasia, ni kikwazo dhidi ya utawala bora kutokana na ukweli kwamba wezi wa mali za umma na walaji rushwa na mafisadi ndio wenye tabia za kuwanunua wapiga kura walio hoi kwa njaa na umaskini wa kupindukia. Pia umaskini ni kikwazo dhidi ya mabadiliko yoyote.

Sasa kwa bahati mbaya tatizo la umaskini haliwezi kuondoshwa na utawala unaoona kwamba kuwatawala watu masikini ni raha zaidi kuliko kuwatawala watu walioridhika kimaisha, wakoloni walijitahidi kuwagawa wananchi ili wabaki hawaelewani kati ya walionacho na wasionacho, waliosoma na wasiosoma ili wapate kinga ya kuwafanya waendelee kutawala bila shida. Wao walihakikisha wananchi wanaowatawala wanabaki wajinga. Wagonjwa, na maskini ili wasiwe na ubavu wa kuwaondoa madarakani. Cha kushangaza ni kwamba takribani miaka 48 (2009-1961) tangu tupate uhuru wetu kutoka kwa Mwingereza watawala wetu bado wanaendeleza mbinu za wakoloni za kutawala za kutufanya tuwe wajinga, masikini na tunaosumbuliwa na magonjwa kila wakati.

Kwa mfano Maasi ya Maji Maji 1905-1907 yalifanya Mjerumani kuyaelewa makabila ya kusini kwamba ni ya watu jeuri na wagumu kutawalika endapo wataachiwa kutulia pasipo kuvurugwa na njaa, umaskini au magonjwa alichokifanya ni kutokupeleka maendeleo makubwa kama vile reli, shule, na mahospitali makubwa. Serikali ya TANU pia ilifuata nyayo za Mjerumani, ilijua wazi kwamba watu wa kusini, Wangoni, Wapangwa, wamatengo, Wamakua, Wamwera, Wanyasa, Wamakonde, Wayao, na Warufiji kwa asili yao ni watu jeuri na wagumu kuburuzwa endapo wataachiwa wawe na uimara wowote ule aidha uimara wa kiuchumi, au uimara wa kielimu au uimara wa kuwa na mshikamano, hivyo basi sera ya ‘’gawanya utawale’’ ikabidi iendelezwe na juu ya hiyo iongezwe sera ya kuwafanya wawe maskini zaidi na pia kuwatenga ama kuwabomolea misingi yote ya maendeleo kwani kama wangekuwa na maendeleo walau nusu tu ya yale yaliyoko kaskazini ingekuwa vigumu kutawalika. Kwa hiyo kwa makusudi kabisa reli ya TAZARA ambayo kimsingi ingekuwa kama ilivyo reli ya kati kwa mikoa ya kusini ikapitishwa porini badala ya kupita Rufiji, Mtwara,Lindi, Songea hadi Itungi Port (Kyela) na kuingia Zambia. Reli ilikwepeshwa maeneo hayo ili tu kuzuia kasi ya maendeleo ya kusini na pia kuzuia kukua kwa uchumi wa kusini.

Kusini ambayo ina rasilimali nyingi na utajiri mwingi kuliko kaskazini na pengine maeneo mengine yote ya nchi hii sasa imekuwa chemi chemi ya kutoa Wamachinga kwa sababu tu watoto wake wamenyimwa elimu. Rasilimali zake zinaoza na huenda siku za usoni watapewa wageni kama ilivyotokea kwa SongoSongo na machimbo ya Alexandrite huko Tunduru.
Baadhi ya wasomi wachache wa kusini walipewa nyadhifa katika serikali ili ziwe kama takrima na uchawi wa kuloga akili zao wasijejali tena maendeleo ya kusini wala kuwahurumia ndugu zao ambao wanahitaji ukombozi kwa njia ya maendeleo.

Niandikie:


kyelacommunity@live.com

No comments:

Post a Comment