Friday, November 27, 2009

Ziwa Ngozi linalodaiwa kuhamishwa kwa jiwe la moto

Na Thobias Mwanakatwe

Tanzania ni nchi iliyobahatika kuwa na maziwa mengi hata hivyo kila ziwa lina historia yake jinsi lilivyojitokeza kwa maana ya chanzo chake.

Ziwa Ngozi lililoko Rungwe ni moja ya maziwa ambayo wenyeji huogopa kulitembelea kutokana na imani walizonazo. Mwandishi Wetu, Thobias Mwanakatwe, anaandika zaidi.

Yapo maziwa au maeneo ambayo ukianza kusimuliwa historia yake unaweza kabisa ukakata tamaa hata kulitembelea hasa kutokana na maajabu yaliyopo katika ziwa hilo.

Mojawapo ya maeneo yenye historia ya maajabu ni ziwa Ngozi lililopo katika kijiji cha Mbeye One wilayani Rungwe katika mkoa wa Mbeya.

``Mimi sijawahi kufika huko lakini siwezi kwenda kule kunatisha,`` anasema Uswege Mwakimbete alipoulizwa kama amewahi kufika kwenye ziwa hilo.

Ziwa hilo liko urefu wa mita 150 kutoka kilele cha milima inayozunguka ziwa , ambapo kutoka usawa wa maji kina cha maji ni urefu wa mita 73 na ukubwa wa eneo lenye maji ni kilomita sita hadi 10 za mraba na lina ukubwa wa kilometa za mraba 3.75.

Wataalam wanaeleza kuwa ziwa hilo limetokana na volkano , limezungukwa na misitu mizuri ya asili ya kitropiki hali nzuri ya hewa na tulivu.

Ili kulifikia ziwa hilo unalazimika kutembea kwa mwendo wa kati ya dakika 45 na saa 1 kutoka kijijini Mbeye One ambacho kipo barabara kuu ya Mbeya-Kyela.

Pia kutoka katika kilele cha milima inayozunguka ziwa hilo unalazimika kushuka kwa zaidi ya dakika 45 huku ukilazimika kushuka kwa kutumia mizizi migumu ya miti ya asili iliyopo katika msitu mnene kwasababu ya mteremko mkali kuelekea katika ziwa hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbeye One, Watson Mwakalinga anasema kuwa ziwa hilo liligunduliwa mwaka 1925 ambapo anasema kuwa ziwa hilo lilihama kutoka katika kijiji cha Mwakaleli wilayani humo baada ya kudaiwa kuwa baada ya kuchomwa na jiwe la moto na wakazi wa kijiji hicho.

Anasema ziwa hilo la maajabu lilichomwa moto na wakazi wa kijiji cha Mwakaleli kwasababu lilikuwa likileta mikosi mingi kijijini hapo ikiwemo watu kufa kila mara hali iliyowalazimu wazee wa kijiji hicho kufanya uchunguzi na kubaini kuwa kunasababishwa na ziwa hilo la Ngozi.

Hata hivyo unapowauliza wataalam wa masuala ya mazingira wanasema kisayansi ziwa haliwezi kuhama.

``Kwa vile ziwa hili halikuwepo pengine wangesema kuwa halikuwepo mpaka volkano hiyo ilipokuwepo lakini ziwa haliwezi kuhama,`` anasema Prof .William Rugumamu , wa Idara ya Jiografia toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwakalinga anasema kuwa maajaabu ambayo yametokana na imani za kishirikina yanayodaiwa kuwepo katika ziwa hilo ni pamoja na watu wanaofika huku kudaiwa kupotea, sauti za vikohozi vya watu wasioonekana pamoja na miujiza ya watu wanaotwanga mahindi lakini hawaonekani.

Anasema mbali ya maajabu mengine ya imani za kishirikina yaliyokuwepo, anasema kuwa ziwa hilo linatabia ya kubadilika rangi ambapo anasema ziwa hilo limekuwa likigeuka rangi mara kwa mara na kuwa na rangi za kijani, bluu, nyeusi na nyeupe.

Anasema kubadilika kwa maji katika ziwa hilo kimsingi wananchi wameshindwa kufahamu kunatokana na nini ingawa waatalam waliowahi kufika kijijini hapo wanadai kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa ya eneo hilo.

Prof. Rugumamu anasema hali ya kubadilika rangi kwenye ziwa Ngozi siyo kitu cha ajabu kwani ni hali inajitokeza kwenye maji ya bahari ambapo anasema wakati mwingine huweza kuonekana rangi ya bluu au rangi ya upinde kutegemeana na hali ya jua.

`Kwenye maji ya bahari hali ya maji kubadilika ni jambo la kawaida pengine watu hawawi makini kuangalia tu,`` anasema Prof. Rugumamu ambaye ni mtaalam wa masuala ya mazingira na hali ya udongo.

Hata hivyo unapofika eneo hilo misitu inayozunguka ziwa hilo ina hali nzuri pamoja na baadhi ya wanyama wakiwemo chui na nyani, ingawa ni nadra sana kuwaona chui katika misitu hiyo kwa kuwa wanajificha na hawajawahi kuleta madhara kwa binadamu.

Anasema kutokana na maajabu hayo, wakazi wa kijiji hicho walikuwa wakiogopa kabisa kufika katika ziwa hilo kutokana na maajabu hayo yaliyokuwa yakisemwa.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mbeye 1, George Mbepe (65), anasema awali walikuwa wanahofia kufika katika ziwa hilo kutokana na madai ya kuwapo kwa imani za kishirikina.

``Kulikuwa na imani kuwa mtu akija huku atasikia vikohozi vya watu wasioonekana huku wengine wakitwanga mahindi, lakini hawaonekani,`` alisema na kuongeza kuwa imani hizo zilisababisha watu wasifikirie kwenda katika ziwa hilo .

Hata hivyo anasema, kuwa kutokana na maji hayo kuonekana yanafaa, yamekuwa yakitumiwa kama mradi na vijana ambao wamekuwa wakiuza kati ya shilingi 300 na 500 kwa lita.

Wakazi wa Kijiji hicho, wanaamini maji ya ziwa hilo hutumika kama dawa kwa ajili ya kutibu watoto ambao wamekuwa wakistuka nyakati za usiku na kwamba pindi wanaponywesha maji hayo hali hiyo inakoma mara moja.

Prof .Rugumamu anasema kuwa hakuna maelezo yoyote ya kisayansi ya Ngozi kuwa na uwezo wa kuponya magonjwa lakini anasema wenyeji kwenye maji mengi yanayotokana na volkano wamekuwa na imani za aina hiyo.

``Hata sehemu nyingi ambako yanatoka maji moto yanayotokana na volkano watu wanaamini hiyo lakini hiyo ni imani tu, anasema .``

Ziwa hilo liliwahi kupandikizwa samaki aina ya perege mwaka 2001, hata hivyo hadi sasa hawajafanikiwa kuvua samaki hata mmoja kutokana na ukosefu wa vifaa vya uvuvi pamoja na ugumu wa kufika katika ziwa hilo .

Hata hivyo imani hizo za kishirikina za wakazi wa Kijiji hicho zilifikia tamati mwanzoni mwa mwaka huu baada ya timu ya watafiti wa Kimataifa kutoka nchi za Ufaransa, Uingereza na Ubelgiji kufanikiwa kufika katika ziwa hilo na kufanikiwa kuingia ndani ya ziwa hilo na kuchota udongo kwa ajili ya kufanya utafiti wa kisayansi kuhusiana na ziwa hilo pamoja na mazingira yanayolizunguka.

Watafiti hao walibaini kuwa ziwa hilo lina umri wa zaidi ya miaka 40,000.Ingawaje wataalam wengine wanasema kuwa ziwa hilo linaweza kuwa lilikuwepo hata miaka milioni 2 iliyopita.

Kuna baadhi ya watalii wamekuwa wakitembelea ziwa hilo ambapo hulipia kiasi cha Sh 2,000 kwenda kuliona .

Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema kuwa kiasi kinachotozwa cha sh.2,000 hakitoshi bali wangetozwa zaidi.

``Watalii walitakiwa kutozwa shilingi 10,000 na watanzania walipe shilingi 2,000 ili mapato yatokanayo na shughuli za utalii yaweze kutumika kwa shughuli za maendeleo katika Kijiji na wilaya,`` anasema Jackson Mwakabuta,mkazi wa kijiji hicho.

Mwakabuta anasema kuwa idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii wilayani humo haitoshelezi, ambapo alisema kuwa kuna haja ya kufanyika kwa juhudi za makusudi kutangaza vivutio vilivyopo nchini pamoja na kuwahamasisha Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii badala ya kuwategemea wageni tu.

Mbali ya ziwa hilo kukosa watalii wanaotembelea kuangalia vivutio vilivyopo, pia wakazi wa Kijiji cha Mbeye One, wameshindwa kuendesha shughuli za uvuvi kutoka katika ziwa hilo kutokana na ukosefu wa vifaa vya uvuvi pamoja na ugumu wa kufika katika ziwa hilo la shimo ambalo limezungukwa na milima.

Wananchi hao wanaiomba serikali iwasaidia kupata boti itakayotumika kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo, ambapo alisema kuwa kuanza kwa shughuli za uvuvi kutasaidia kukuza uchumi wa kijiji hicho na hivyo kuinua maisha ya wananchi .

Mwambata wa Ubalozi wa Ufaransa nchini, Dk. Raymond Latest ambaye alikuwa pamoja na timu ya utafiti wa ziwa hilo anasema kuwa wilaya ya Rungwe ina vivutio vizuri vya utalii kuliko mkoa wa Arusha lakini havifahamiki kutokana kwa kutotangazwa.

Anasema awali kabla hajafika nchini, alikuwa akiifahamu zaidi nchi ya Kenya ambayo imekuwa ikijitangaza zaidi kwenye utalii, lakini alipofika nchini akagundua kuwa Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ikiwamo misitu ya asili kuliko nchi yoyote ya Afrika Mashariki.

Dk.Latest anasema vivutio hivyo vikitangazwa vizuri vitaweza kuchangia kukuza pato la Taifa kupitia sekta ya Utalii.

Akilizungumzia ziwa Ngozi, Dk. Latest alisema kuwa amevutiwa na ziwa hilo lililozungukwa na milima na kuonekana lipo shimoni pamoja na kuzungukwa na misitu ya asili, ambapo alisema kuwa atahakikisha anaitangaza wilaya ya Rungwe ili iweze kufikiwa na watalii wengi kutoka nchini Ufaransa na watalii waweze kujionea maajabu ya wilaya hiyo.

Kiongozi wa timu ya watafiti, Dk. David Williamson kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema hiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kufika katika ziwa hilo kwa lengo la kufanya utafiti ili kujua umri wa ziwa hilo, mabadiliko ya hali hewa na mazingira pamoja na kufahamu volkano ndogo ya mwisho ililipuka lini. Na kama maji ya ziwa hilo yanafaa kwa matumizi ya binadamu.

Dk. Williamson anasema kuwa ziwa ngozi ni moja kati ya maziwa 10 ya volkano yaliyopo wilayani Rungwe ambayo wanafanyia utafiti wa kisayansi, aliyataja maziwa mengine kuwa ni pamoja na Ndwati, Kisiba, Chungululu, Ikapu, Itamba, Asoko, Ilamba, Kingili, Katubwi na Itende.

Utafiti wao unajumuisha uchukuaji wa vumbi na tope lililopo chini ya ziwa hilo vitu ambavyo vitasaidia katika utafiti wao.

Katika utafiti wao wa awali waligundua kuwa kina cha maji katika ziwa hilo kinazidi kupungua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mmonyoko wa udongo na kwamba hali hiyo inahatarisha uwepo wa ziwa hilo kwa miaka ijayo.

Akieleza sababu za kuchukua tope lililochini ya ziwa hilo , alisema kuwa wanaamini kuwa tope lililoganda ndani ya maji linakuwa na mkusanyiko wa tabaka mbalimbali za taka, udongo na kwamba kiasi wanachochukuwa kitawawezesha kujua mambo muhimu wanayoyahitaji katika utafiti wao.

Mtafiti mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,Edister Abdallah anasema kuwa utafiti huo utasaidia wakazi wanaosihi kuzunguka ziwa hilo kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kushiriki katika kuhifadhi mazingira ya eneo hilo na wilaya ya Rungwe na hivyo kufanya uwepo wa ziwa hilo kuwa endelevu.

Anasema kuwa juhudi za dhati zinapaswa kuchukuliwa ili kuwajengea wananchi utamaduni wa kutunza mazingira tofauti na ilivyo sasa ambapo wananchi hawaoni wajibu wao wa kushiriki katika kutunza na kuhifadhi mazingira ambayo ni muhimu katika maisha ya mwanadamu na viumbe hai.

Alisema kuwa wananchi wakipatiwa elimu na kujua umuhimu wa kuhifadhi mazingira kila mmoja atatimiza wajibu wake kwa kutunza mazingira.

Anaongeza kuwa ukosefu wa elimu umekuwa ukisababisha wananchi wengi washiriki katika uharibifu wa mazingira bila wao kujua au wengine kuharibu kwa makusudi bila kujua athari za baadaye za uharibifu huo.

Naye Mshauri wa Sekta ya Wanyamapori mkoa, Stanley Munisi anasema mkoa wa Mbeya unao vivutio vingi vya kitaalam, lakini vingi bado havijatangazwa na kwamba hivyo ipo mikakati ya kuanza kuzitangaza.

No comments:

Post a Comment