Monday, November 30, 2009

USALAMA WA TAIFA NI LAZIMA UBADILIKE, KAMA TUNATAKA TUSALIMIKE! – Sehemu ya 1

Na. M. M. Mwanakijiji


Usalama wa taifa wa nchi yoyote ile duniani ndiyo kinga ya mwisho dhidi ya tishio lolote la uhuru wa taifa hilo. Nitarudia tena kauli hii. Usalama wa taifa wa nchi yoyote ile duniani ndiyo kinga ya mwisho dhidi ya tishio lolote la uhuru wa taifa hilo. Usalama ya usalama wa Tanzania ndiyo kinga ya mwisho ya uhuru wetu na wakati wowote ule idara hiyo inapokuwa katika shaka, shuku, kutokuaminika, wasiwasi, kudhaniwa, tuhuma, au madai hasi basi uhuru wetu uko matatani.

Wengine wanafikiria uhuru wetu unalindwa na Jeshi la Wananchi au na Polisi, hawa ni watekelezaji wa kile ambacho usalama wa taifa umefanya. Pasipo usalama wa taifa kufanya kazi yake vizuri basi vyombo vya ulinzi vinajikuta vinafanya kazi ngumu zaidi ya kutulinda kwani kinga ya mwisho ya usalama wetu iko matatizoni. Bila ya idara yenye nguvu ya usalama wa taifa kazi ya ulinzi wa taifa inakuwa ngumu zaidi kuliko inavyopasa.

Uhuru wa nchi yoyote duniani unaenda sambamba kabisa na uwezo wake katika mambo ya kijasusi.

Ninapozungumzia Usalama wa Taifa ninazungumzia kundi la watu ambao kutokana na nafasi zao wamepewa jukumu la kukusanya, kuchambua, na kuamua juu ya hatua mbalimbali za kuchukuliwa juu ya taarifa za kijasusi ambazo zinatishia maslahi ya taifa letu. Ninazungumzia wale wenye jukumu la kuhakikisha kuwa mipango yoyote, njama yoyote, na mikakati yoyote ya watu wasiotutakia mema inagundulika mapema kabla haijatekelezwa na hatua za kujibu mashambulizi au kuadhibu zinachukuliwa mara moja. Ni watu ambao jukumu lao kubwa ni kutambua taarifa za kijasusi na kuchukua hatua mara moja za kuzuia kitu chochote, mtu yeyote au jambo lolote kuingilia uwepo wa Taifa letu huru, usalama wa watu wake, na usalama wa maslahi yake mahali popote duniani.

Kati ya mambo ambayo yamo moyoni mwangu kwa muda mrefu sasa ni suala hili la usalama wa taifa. Ninapoangalia mambo kadha wa kadha yanayotokea nchini na ambayo yamekwisha tokea nimejifunza mambo fulani ambayo naamini ni muhimu kuwashirikisha ili tuweze kuelewa vita hii dhidi ya ufisadi kwa muda mrefu ujao haitakuwa na mafanikio bila ya kuboresha vyombo kadhaa na cha kwanza miongoni mwao ni Usalama wa Taifa (UwT).

Nimeshaandika mara kadhaa huko nyuma nikiwa mtu wa kwanza kuvunja mwiko wa kuzungumzia usalama wa taifa hadharani na kwa kina, mwiko ambao ninaendelea nao katika sehemu hii ya kwanza ya mabadiliko ya lazima ya “Idara” kama Watanzania tunataka tusalimike. Ningekuwa na uwezo ningewaweka chini wana usalama wote na kuwapatia somo hili la bure ambalo ningedai ni la lazima kabla ya mtu yeyote kula kiapo cha utumishi!

Kwanini mabadiliko ni lazima?

Umuhimu wa kutaka kusababisha mabadiliko ndani ya idara hii nyeti ni mlolongo wa matukio ya kushangaza ambayo kimsingi kabisa yanatishia uhuru wetu kuliko utawala wa kikaburu au mvutano wa mataifa ya Magharibi na Mashariki wakati wa Vita Baridi. Matukio ambayo tunayaita ni “ufisadi” msingi wake na kutokea kwake kumekuja sababu ya kulegalega na kuyumbayumba kwa idara hii nyeti.

Kinachonitisha zaidi ni kuwa hakuna mtu ambaye yuko tayari kuzungumzia mabadiliko haya na kuanza kuyataka yafanyike na hivyo kuendeleza woga wa kutojadili idara hii huku madhara yakiendelea kutokea. Ni sawa na kuogopa kuzungumza au kujadili walinzi wa jengo letu wakati tunaona tunashambuliwa wakati kuna watu wanalipwa kutulinda.

Hivyo, kama kweli tunataka kuushinda ufisadi na kujenga taifa lenye kufuata kweli misingi ya sheria, utawala wa demokrasia na siasa safi hatuna budi kuboresha idara ya usalama wa taifa, kuiimarisha na kuweza kuijenga ili iweze kukabiliana na changamoto za dunia ya leo. Hivyo, kama kweli tunataka kusalimika huko mbeleni hatuna budi kuboresha idara hii ambayo kiukweli kabisa ni moyo wa taifa letu.

Falsafa ya Usalama wa Taifa

Tunaweza kuigawa historia ya falsafa inayoongoza idara yetu ya Usalama wa taifa katika sehemu kubwa tatu ambazo sitaziangalia kwa undani sana (nitawaachia wengine waje kufanya kazi hiyo). Kuna Kipindi cha 1961-1970, kipindi cha 1970-1985, na kipindi cha 1996-Sasa. Vipindi vyote hivi vimeakisi katika utendaji kazi wa idara hii na kwa namna fulani vinaingiliana.

Kipindi cha 1961-1970 (Miaka ya majaribu- Trial Years)

Wakati huu wa historia tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa kadhaa ambazo zilitishia uwepo wa taifa letu na uhuru wetu kwa ujumla. Kilikuwa ni kipindi kigumu zaidi kuongoza. Kwanza, ni kwa sababu nchi yetu ndio imepata uhuru wake na kuwa Jamhuri lakini ikiwa na wataalamu wachache na maafisa wachache wa Usalama wa Taifa ambao walikuwa wamesomea kazi hii. Kilichotegemewa zaidi wakati ule ni ile tunu ya “uzalendo” ambayo watendaji wa kwanza wa serikali yetu iliwaongoza kwani hakukuwa na kitu cha aibu kama kushindwa kulinda uhuru ambao taifa limeupata.

Mapinduzi ya Zanzibar, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na Maasi ya Jeshi ya mwaka 1964 yalikuwa ni kilele cha udhaifu mkubwa na wakati huo huo somo kubwa zaidi la kuelewa jukumu la idara ya usalama wa taifa (wakati huo ikiwa kama chombo kilichojulikana kuwepo bila kuwa idara iliyojulikana dhahiri). Mambo hayo makubwa yalionesha uwepo wa haja ya kuwa na usalama wa taifa uliokomaa, kusambaa na kufanya kazi kwa nguvu zote:

a. Kulinda serikali iliyo madarakani

b. Kumlinda Rais na tishio lolote dhidi ya nafsi yake na ofisi yake

c. Kulinda Nchi kutoka kwa maadui wa nje (hasa Utawala wa Kikaburu wa Afrika ya Kusini)

Hivyo kipindi hiki kwa kweli kilikuwa na matukio ya kushtua na mengine yaliyotokana na uwoga mkubwa hasa baada ya Uasi wa Jeshi. Jambo hili siyo geni kwa nchi changa. Hata Marekani baada ya kupata uhuru wake kwa njia ya Mapinduzi dhidi ya Himaya ya Mwingereza viongozi wake walikuwa na jukumu kubwa sana la kuhakikisha kuwa wanaulinda uhuru huo kwa kuwa na watu wa usalama wa taifa waliokuwa na uwezo na nyenzo za kuilinda nchi yao.

Kama Tanzania chini ya Mwalimu ilivyofanya makosa ya hapa na palekatika usalama wa taifa mwanzoni mwa jamhuri yetu ndivyo hata Marekani taifa lililoundwa kwa misingi ya usawa wa watu wote lilifanya makosa katika sehemu hiyo nyeti, makosa ambayo miaka karibu zaidi ya 200 baadaye Marekani ilifanya tena na kuligharimu taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani matukio ya Septemba 11. Na baada ya hapo Wamarekani wakajikuta wanalazimika kuangalia tena sekta nzima ya ukusanyaji wa habari za kijasusi na suala la usalama wa taifa.

Machafuko ya Rwanda na Burundi mwanzoni mwa miaka ya sitini, mauaji ya Lumumba n.k vyote vilimfanya Mwalimu na uongozi wetu wa awali kuwa na wasiwasi (nervous) na wakati mwingine woga usio na msingi (paranoid) kwa mtu yeyote ambaye alikuwa akionesha dalili ya kuipinga serikali au kuwa mkosoaji sana. Ni njia pia iliyofuatwa na Dr. Hastings Banda wa Malawi na baadhi ya viongozi wa mwanzo wa Afrika na hata sehemu nyingine duniani.

Hivyo, kuangalia idara hii na kufanya mabadiliko siyo jambo la ajabu au mwiko. Hivyo, kipindi hicho cha mwanzo kilikuwa cha mafanikio makubwa lakini pia kikiwa na changamoto ambazo zimeandikwa katika kurasa zisizofutika za historia. Masuala ya kina Kambona, Hanga, kina Bibi Titi Mohammed, n.k yote yanahusiana moja kwa moja na mafanikio na mapungufu ya Idara hii.

Ninaamini miaka ya mwanzo ya nchi yetu taifa letu lilikabiliwa na tishio la ndani zaidi kuliko ya nje na jukumu la kwanza la utawala uliokuwepo ni kuhakikishia kuwa Taifa letu halisambaratiki.

Kipindi cha 1970-1985 – Miaka ya Utukufu (glory years)

Kwa kipimo kikubwa ninaamini Usalama wetu wa taifa ulifanya kazi kubwa zaidi na ya kukumbukwa katika miaka hii 15. Ni miaka ambayo kwanza sheria tuliyoirithi kwa mkoloni ya “Official Secrets” ilifutwa na badala yake sheria ya Usalama wa Taifa ya Mwaka 1970 iliingizwa na kuongoza shughuli za usalama wa taifa.

Tishio kubwa la wakati huu pamoja na matishio ya ndani (halisi au ya kudhaniwa) ni matukio nje ya Tanzania. Kuingia kwa Idi Amin madarakani nchini Uganda na kuendelea kwa majirani zetu kukaliwa na wakoloni kama huko Msumbiji na Zimbabwe na kuendelea kwa utawala wa kikaburu Afrika ya Kusini vilikuwa ni tishio kwa serikali zote za kusini mwa Afrika ambazo zilikuwa zimekwishapata uhuru wake.

Uamuzi wa Tanzania kuongoza harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kukubali kutumiwa kwa ardhi yake na vikosi vya wapigania uhuru vililifanya taifa letu kuwa kama mnyama aliyewekwa alama na wawindaji, adui wa wakoloni, makaburu alikuwa wazi mbele yao.

Ni kutokana na ukweli huo sheria hiyo ya mwaka 1970 iliingiza katika ibara ya 9 kutambua vikundi vya wapigania uhuru na kulinda maslahi yao. Hivyo katika miaka hiyo na chini ya sheria hiyo Usalama wa Taifa wa Tanzania ulikuwa unatumika siyo kulinda maslahi na usalama wa taifa letu tu bali pia kulinda maslahi na usalama wa vikundi vya wapigania uhuru ambavyo tumevitambua hivyo. Kwa misingi hiyo watu wetu wa usalama walikuwa pia wakiangalia usalama wa SWAPO, ANC, FRELIMO, n.k Hili halikuwa jambo dogo.

Ni kutokana na hili mchango wa watu wetu wa Usalama wa Taifa wakati huo unatambulika hata leo katika baadhi ya nchi na unatambulika kwa shukrani. Ilikuwa ni miaka ya utukufu kwani ni pamoja na mchango wetu huo tuliweza kuchangia siyo damu tu kama wengi wanavyojua katika harakati za ukombozi lakini vile vile mchango wa taarifa na habari za kijasusi zilizowezesha vikundi vya wapigania uhuru kufanikisha malengo mbalimbali ambayo hatima yake kwa kiasi kikubwa ilikuwa ni kupatikana kwa utawala wa kidemokrasia na haki ya usawa kwa watu wote wa Afrika ya Kusini pale Nelson Mandela na wenzake walipofunguliwa kutoka katika shimo la giza la gereza la Kisiwa cha Robin walikotumikia jumla ya miaka ma-mia nyingi.

Kipindi cha 1985-1996 – Miaka ya kukosa mwelekeo (Uncertainty Years)

Mojawapo ya mabadiliko makubwa yalitokea baada ya baba wa taifa kung’atuka katika uongozi wa serikali (1985) na baadaye Uenyekiti wa CCM (1990). Kubadilika huku kwa uongozi kulikuwa pia na changamoto ya namna ya pekee kwa usalama wa Taifa. Miaka mitano ya mwanzo tunaye Rais mwingine ambaye kisheria ndio mkuu wa Usalama wa Taifa, lakini kisiasa nguvu zilikuwa kwa Mwenyekiti wa CCM ambaye katika mfumo wa chama kimoja alikuwa na nguvu ya aina ya pekee.

Hivyo, utii (allegiance) ya watu wa usalama wa taifa kama ilivyokuwa kwa maeneo mengine ilikuwa ni ya kuchanganyikiwa kidogo; Kumtii Mwinyi ambaye alikuwa Rais au Nyerere ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama? Je, Rais akifanya mambo fulani yaliyo ndani ya madaraka lakini yakagongana na mtazamo wa Mwenyekiti wa CCM watu wa chini wasimame na nani?

Matokeo yake Usalama wa Taifa ulianza kugawanyika kwa kufuata mwelekeo wa itikadi; kizazi cha zamani kikiwa kinaongozwa na uzalendo wa aina ya pekee na dhana ya kulinda taifa kama miaka ile ya majaribu na utukufu lakini kizazi kipya cha wasomi zaidi kikianza kuona matundu ya mabadiliko ya kiuchumi aliyoyafungulia Mzee Mwinyi.

Ni katika kipindi hiki tunaweza kuona kwa kiasi cha namna fulani kujipanga kwa vikundi ambavyo leo tunaweza kuviita vya kifisadi. Hili lilikuwa linaanza kuonekana zaidi miaka ile mitano ya utawala wa Rais Mwinyi. Katika kipindi hiki viongozi walianza kukaa kwa kujiamini zaidi na hasa baada ya Baba wa Taifa kuachia uenyekiti wa CCM vile vile na hivyo kumpa nguvu zote za kichama na kiserikali Rais Mwinyi.

Matokeo yake ni kuvunjwa rasmi kwa azimio la Arusha, na kuruhusiwa kwa namna ya pekee vitendo vya kifisadi kuanzia uuzaji wa Loliondo na utoroshaji wa dhahabu. Kipindi hiki kwa baadhi ya watu kilikuwa ni cha neema kwani yeyote aliyetaka alipata endapo tu alicheza karata zake vizuri.

Baada ya Afrika ya Kusini kupata utawala wa kidemokrasia na vyama vya ukombozi kutambulika kama vyama vya kisiasa na Tanzania kupunguziwa jukumu la kulinda maslahi ya vyama hivyo, watu wetu wakawa hawana tishio kubwa zaidi la kuangalia zaidi ya kuangalia usalama wa viongozi na serikali iliyoko madarakani na dola (state).

Hii ilikuwa ni miaka ya kukosa mwelekeo kwa sababu adui yetu wakati huo alikuwa ni nani? Vita baridi vilikuwa vimekoma kwa kusambaratika kwa Shirikisho la Kisovieti la Urusi (USSR) na kuibuka kwa Marekani kama Taifa pekee lenye nguvu zaidi duniani; Afrika ya Kusini imerejea katika utawala wa demokrasia, na wimbi la mageuzi ya kisiasa lilikuwa linasambaa katika Afrika. Siyo wimbi la mapinduzi ya kijeshi bali mabadiliko ya kisiasa kwa njia za kidemokrasia.

Je, watu wetu wa Usalama walikuwa wanalinda maslahi ya nani zaidi? Kwa wachache kilikuwa pia ni kipindi cha kuanza kushiriki katika vitendo vya kifisadi. Katika ripoti zinazokuja tutaangalia baadhi ya matukio ya wakati huu ambayo yalifungulia mlango wa ufisadi kuanzia Ikulu hadi nyumba ya mwisho kabisa karibu na shamba la kijiji!

Kipindi cha 1996-Sasa – Miaka ya Aibu (Shameful Years)

Sasa hivi tunaishi katika kipindi cha aibu. Kipindi ambacho nikisikia mtu anajiita mtu wa “usalama” nasikia kukereka (nilitaka nitumie neno jingine hapa!). Si kwamba ninawahukumu wote kuwa wameacha wito wao bali kuna kikundi kati yao ambacho kimeacha suala la usalama wa taifa na badala yake kimebakia kwenye “usalama wa wanasiasa”! Hiki siyo kitu kimoja.

Kundi hili limegeuza “usalama wa taifa” na kuwa usalama wa “chama tawala” na hofu yangu ni kuwa wanatumia muda mwingi kufikiria Tanzania katika mwanga wa siasa za vyama na kusahau kuangalia Tanzania kama jamhuri. Wakati wowote usalama wa taifa unapoacha kuangalia taifa na kuhamisha macho yao kwenye vitu vingine, basi usalama huo wa taifa unakuwa umepotea na ni mabadiliko ya haraka na ya lazima ndiyo yanaweza kurejesha huko.

Miaka hii ya aibu ilianza kwa kuundwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa sheria namba 15 ya Usalama wa Taifa ya 1996 iliyosainiwa na Rais Benjamin Mkapa Januari 20, 1997 kuwa sheria.

Sheria hii ndiyo ilirasmisha uwepo wa idara ya usalama wa taifa na kuwatoa gizani watu waliokuwa wanajulikana uwepo wao lakini pasipo kuonekana. Iliweka msingi wa utendaji kazi wa idara hiyo, utaratibu wake hadi viapo vya wana usalama. Kwa juu juu sheria hii ukiangalia kwa haraka unaweza kufikiri ilikuwa ni nzuri. Kitu kizuri pekee ambacho naweza kusema kiko ndani ya sheria hii (zaidi ya vipengele vyake kadhaa) ni kujenga taasisi rasmi ya usalama wa taifa.

Hata hivyo, mambo mengine yaliyomo katika sheria hiyo ni mambo ambayo mtu yeyote aliyesomea mambo ya ujasusi anaweza kujikuta anahuzunika kwani sheria hii imefungua mwanya wa ufisadi wa kimataifa na kuwafunga kwa minyororo watu wetu wa usalama. Ni sheria mbayo kama ningekuwa na uwezo ningeibadilisha siku ya kwanza Rais Kikwete anaingia madarakani.

Ninaamini kwa moyo wangu wote kuwa sheria hii ilifikiriwa, kutungwa, na kubarikiwa na miungu ya mafisadi! Mtu mwenye akili timamu mwenye kulipenda taifa lake na kujali maslahi ya taifa lake asingeweza kuivumilia iwepo kwa zaidi ya saa moja! Ni sheria inayotishia usalama wetu wa taifa na natumaini kuna mtu ataamka na kutaka kuifanyia mabadiliko ya haraka kama tunataka tusalimike.

Sheria hii kwa maoni yangu ni sawa na mtu ambaye ameamua kulinda mifugo yake, kajenga uzio mkubwa na kaweka lango kuu. Kaajiri na walinzi na kutoa maelekezo ya walinzi kuwa waangalifu. Tatizo ni kuwa baada ya kufanya haya yote, mtu huyo hakuweka lango la kuzuia watu kuingia na hivyo kuacha uzio ukiwa na uwazi huku yeye mwenye akijivunia kuwa amejenga “uzio” mkubwa sana! Anapoamka asubuhi anakuta nusu ya mifugo imetoweka na mlinzi akisimama upande mwingine wa jengo!

Hatuwezi kwenda mbele kama taifa na hasa kukabiliana na changamoto zilizoko mbele yetu na hasa adui yetu mpya ambaye leo hii anatuchezea kama kucheza shere kwa sababu ya udhaifu wa sheria hii. Ni sheria ambayo wapiganaji wa CCM ningetamani wasema tunataka kuifanyia mabadiliko kwani ni mojawapo ya vitu vinavyotengeneza mfumo wa utawala wa kifisadi.

Tutaingalia sheria hiyo ya TISS (Tanzania Intelligence and Security Service) katika sehemu ya pili ya hoja hii. Tutafanya hivyo baada ya kuangalia ni adui gani sasa hivi anayetishia uhuru wetu zaidi na kwanini ni adui wa hatari zaidi kuliko uvamizi wa Nduli au njama za Makaburu wa Afrika ya Kusini.

Usikose sehemu ya pili.

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com

No comments:

Post a Comment