Friday, November 27, 2009

Vivutio vya Mbeya vina nafasi kubwa kukuza uchumi

Na Mwadishi WetuMh. Profesa Mark Mwandosya akitembelea maporomoko ya Malamba wilayani Rungwe ambayo ni mojawapo ya vivutio kibao vya utalii mkoani Mbeya.

JIJI la Mbeya lina vitongoji vingi vyenye utajiri. Lina vivutio vingi kwa wageni waliopata fursa ya kulitembelea. Mbeya ina safu za milima iliyosheheni rasilimali za urithi tangu zama za kale. Rasilimali hizo ni pamoja na misitu mikubwa iliyo hifadhi wanyama na ndege wazuri wa kuvutia.

Mbeya ni Mkoa ulioandika historia ya maajabu katika bara la Afrika na ulimwenguni, tangu kilipodondoka kimondo. Kimondo hicho kilidondoka katika Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya.Vivutio vingine vinavyoipamba Mbeya ni mabwawa yenye matukio ya maajabu, kwa mfano bwawa lililopo Masoko, jirani na kilele cha Mlima Rungwe.

Pia, Ziwa Ngozi na Daraja la Mungu ni baadhi ya vivutio vinavyotengeneza historia ya pekee ya Mbeya na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Ziwa Nyasa ni kivutio kingine, ambapo watu kutoka mataifa mbalimbali hufika kujionea ziwa hilo lenye hadhi kubwa katika bara la Afrika.

Wageni mbalimbali hufika wilayani Kyela kujionea mandhari ya ziwa hilo, ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika. Ziwa hilo pia lipo katika nchi tatu za Malawi, Msumbiji na Tanzania. Wananchi wa nchi hizo na wageni wengine, hunufaika na Ziwa Nyasa kwa uvuvi wa samaki na viumbe wengine waishio majini, kwa ajili ya chakula na biashara.

Ziwa hilo pia limerahisisha usafiri kati ya bandari za Mbamba Bay na Itungi. Lakini, jambo kubwa la kujivunia katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni kuwapo kwa pango la Matema na Hoteli ya Matema. Hoteli hiyo ya ufukweni imeboresha mazingira ya ufukwe wa Matema na kuufanya kuwa sehemu ya kuvutia kwa wageni wanaofika hapo.

Matema ni eneo tulivu, lenye mandhari mwanana na mimea ya rangi ya kijani kibichi, iliyopambwa na safu za milima. Milima hiyo imesheheni misitu, inayopatikana ndege wazuri wa angani. Wageni wanaotembelea hotelini hapo, huvutiwa na mandhari hiyo. Hoteli ya Matema ipo katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Eneo hilo lilikuwa pori, lakini sasa limegeuka kuwa lulu kwa watu wa makabila tofauti ya ndani na nje ya nchi.

Eneo hilo limejaa utulivu na lina sauti za ndege. Baadhi ya wageni waliowahi kutembelea eneo hilo, wanadiriki kulifananisha na bustani ya Edeni. Kanisa la Uinjilisti lenye makao yake makuu Mbalizi, Mbeya Vijijini, ndicho chanzo cha kuwapo kwa hoteli hiyo, maarufu kama Matema Lake Shore Resort.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Kanisa hilo, Mchungaji Marcus Lrhner, anasema kuwa Kanisa la Uinjilisti lilifanya utafiti na kugundua kuwa eneo hilo linafaa kuweka vivutio na vivutio hivyo vinaweza kukuza sekta ya utalii nchini. Anasema kumekuwa na mafanikio kutokana na kuwapo kwa kivutio hicho.

Mafanikio hayo yanatokana na juhudi za kanisa hilo, kwa kupitia wafadhili wake, ambao kwa miaka nane sasa wamekuwa wakijitahidi kutunza mazingira. Mchungaji Lehner anasema kwamba utafiti uliofanywa pia ulizingatia kuwapo kwa eneo zuri la kuogelea, lenye mchanga safi na mzuri. Anasema Lake Shore Resort inatoa huduma za kulala na chakula cha asili, kinachoandaliwa kwa muda maalumu (kwa oda).

Pia, ina nyumba mbalimbali zenye jumla ya vyumba 22, ikiwamo vyumba vya kujihudumia (self contained) na vyumba vya vitanda viwili hadi vitano. Zipo pia nyumba za ghorofa, zinazomwezesha mgeni kutazama vizuri ziwa, lilivyo na umbo lake, kabla ya kutumia usafiri wa boti, wa miguu au gari. Huduma hizo pia hupatikana hapo.

Matema ipo katika eneo la Kaskazini, mwishoni mwa Ziwa Nyasa, ndani ya Wilaya ya Kyela. Ziwa lina upana wa wastani kilomita 60 na urefu wastani kilomita 550. Lipo kwenye Bonde la Ufa katika Afrika Mashariki na lina ujazo wa mita 500 kutoka usawa wa bahari. Ufukwe wa Matema unapambwa na safu za mlima Livingstone, wenye urefu wa mita 3,000.

No comments:

Post a Comment