Tuesday, November 24, 2009

Ufisadi chanzo cha wananchi kupoteza imani kwa CCM

NA MWANDISHI WETU
















Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Yusuf Makamba.

Watanzania wanasifika katika bara la Afrika kwa uvumilivu wao hata nyakati zisizoweza kuvumilika. Dhana hii inaweza kuwa ni matunda aliyotuachia Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Dalili za uvumilivu zinaonekaka wakati wa Utawala wa Serikali ya awamu ya nne. Serikali na viongozi wake wamekuwa wanaendesha serikali kinyemela kana kwamba haikuchaguliwa na wananchi.

Mdororo wa uchumi haukuanza leo katika dunia hii. Tofauti ya mdororo wa uchumi unaotuathiri sasa ni kwamba una miale mikali kuliko midororo ya uchumi iliyopita.

Ni katika mvurugano huu wa uchumi, Watanzania walitegemea kwamba viongozi waliowachagua na hatimaye kuunda serikali wangetafuta mbinu mbadala ili kulinasua Taifa na watu wake ili miale ya mdororo wa uchumi uliopo usingewaumiza sana. Matokeo yake ni kwamba wanaongeza joto la miale na waathirika wa miale hiyo ni Watanzania asilimia 85 waliotopea katika ufukara ndio wanaoumia kwenye joto la mdororo huo.

Wizi uliojitokeza na unaofanywa na vigogo wa Serikali ya CCM ni dalili fika zinazoonyesha kuwa maadili na itikadi iliyozoeleka ya CCM vyote hivyo vimewekwa kando.

Watuhumiwa wote wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ni vigogo wa CCM na wale wa serikali yake.

Katika orodha hiyo ya watuhimiwa hakuna hata mwananchi mmoja aliye fukara ametuhumiwa na wala hakuna hata mwanachama mmoja wa vyama vya upinzani amediriki kujihusisha na ufisadi.

Ufisadi wote unaozungumzwa ni wa viongozi wa serikali ambao wamefikishwa mahakamani jambo ambalo Watanzania wanaona ni mchezo wa kuigiza.

Watanzania wanaona ni mchezo wa kuigiza kwa sababu vigogo wote waliofikishwa mahakamani ukijumulisha kile kinachodaiwa wameiba haifiki sh. bilioni 133. Hapa panajitokeza swali ambalo halina majibu kwamba hao wengine ambao wanatuhumiwa kinadharia tu watafikishwa lini mahakamani?

Tanzania inashuhudia amani ya mioyo tuliyorithi kutoka kwa Mwalimu Nyerere imetoweka kabisa. Watanzania wanapozungumza amani sio lazima zilie bunduki.

Ukosefu wa amani ni pamoja na kukosa mitaji, kukosa milo mitatu kutwa, dhuluma, rushwa na ufisadi vikiwa mstari wa mbele kuzidi nchi zote zilizo chini ya jangwa la Sahara.

Kukosekana kwa ajira, kuongezeka kwa ujambazi na ujangili si dalili nzuri ya kudumisha amani katika Taifa. Matatizo haya yote yalipaswa kurekebishwa na serikali.

Viongozi wetu wakiwa chini ya mwamvuli wa Rais Jakaya Kikwete hawaonekani kukemea maovu haya ambayo Watanzania hawakuzoe kuwa nayo.

Wazee wetu kama Peter Kisumo, Pancrasi Ndejembi, Joseph Butiku, Mohamed Raza, John Malecela, wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Waandishi maarufu kama Jenerali Ulimwengu wao wamekuwa wanayavalia njuga maovu yote yanayovurundwa na viongozi wetu kwa bahati mbaya serikali na chama chake imekuwa haitoi msisitizo ili kuafikiana na mawazo hawa.

Kwa mfumo huu wa falsafa na siasa ambazo ni za nadharia tu zimekuwa hazina tija kwa Watanzania. Hotuba za majukwaani zimekuwa haziendani na vitendo na hatimaye kudumaza usalama katika nchi na kuwaacha Watanzania wakijiuliza, wanakokwenda.

Suala zima katika Taifa ni kwamba nchi haina amani kwa sababu, wananchi hawana mlo uliokamilika, mafukara wa kutupwa wakati viongozi wao wanajinafasi kana kwamba wako mbinguni, usalama majumbani umekuwa haupo kwa sababu ya ujambazi uliokirithiri na polisi ina vitendea kazi duni ukifananisha na silaha zilizomo mikoni mwa majambazi.

Tatizo jingine Taifa halijaongeza ajira kwa polisi. Polisi tuliyonayo sasa ni ileile aliyotuachia Mwalimu Nyerere.

Kukosekana kwa utawala bora katika Taifa kumeathiri sana suala zima la usalama katika nchi. Watendaji wa tarafa, mitaa, vitongoji na kata wamekuwa tishio kubwa kwa usalama wa Raia.

Watendaji hawa wanajiita watunza usalama madaraka ambayo hata katika Katiba ya nchi hayapo. Kwa mshangao wa Watanzania wengi watendaji wamekuwa wanachukua sheria mikononi huku wakijua sio stahili yao, lakini wakuu wa mikoa na wilaya licha ya kushindwa kukemea, wamekuwa hawawachukulii sheria za nidhamu hivyo kuhalalisha vitendo vibaya vinavyofanywa na watendaji hao. Ukosefu wa utawala bora na sheria katika Taifa ndio umehatarisha usalama wa nchi.

Dhana ya kudumisha demokrasia endelevu katika Taifa haipo. Serikali pamoja na CCM kama alivyosema Rais Kikwete wakati wa kuadhimisha miaka kumi ya kifo cha Mwalimu Nyerere ni kwamba viongozi wameacha kabisa kusikiliza kero za wananchi na kuwasaidia.

Kinachobaki sasa ni porojo nyingi za siasa zisizokuwa na tija na kujilimbikizia mali ili kuja kugombea uongozi mwaka 2010.

Wanasiasa wengi wamebadili dira na maendeleo ya kisiasa na hatima yake wamegeuza siasa mradi wa kujinufaisha wao na familia zao.

Kwa sababu wakati wanagombea hivyo vyeo vya siasa wanatumia rushwa kwa hiyo wakivipata wanahakikisha fedha yao yote iliyotumika katika rushwa inarudishwa kwa nyakati mbalimbali. Hii ina maana kwamba, maendeleo ya wapiga kura yanawekwa pembeni.

Watanzania ambao kusema kweli wamechoshwa na siasa za CCM zenye poroja nyingi na zisizokuwa na tija. Ili wajinasue kutoka kwenye matatizo hayo wanadhani ni wakati muafaka wa kukiweka Chama Cha Mapinduzi na watafute ustarabu mwingine ambao pengine unaweza ukaleta neema ambayo itawanufaisha wao na vizazi vijavyo.

Suala ni kwamba Siasa za Tanu na CCM zimekuwa katika Tanzania kwa miaka 48 bila maendeleo yoyote kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment