Tuesday, November 24, 2009

Tutaboreshaje elimu katika shule za serikali?

BY BENJAMIN NKONYA

Chimbuko la maendeleo ya elimu nchini ni matokeo ya michakato ya sheria, falsafa na sera zilizoanzishwa katika vipindi mbalimbali kabla na baada ya uhuru. Baada tu ya kupatikana uhuru mwaka 1961, serikali ilitunga sheria ya elimu namba 83 ya mwaka 1962 iliyofuta sheria ya elimu ya mwaka 1927 ambayo iliruhusu utoaji wa elimu na mafunzo kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi, dini na makabila.

Katika sheria hii, serikali iliekeza mitaala, uongozi na ugharamiaji wa elimu na mafunzo ufuate usawa. Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilianzisha falsafa ya elimu ya kujitegemea ambayo ilisababisha mabadiliko makubwa katika sera za jumla za kijamii na kiuchumi.

Falsafa hii, ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndiyo inaweka dira katika mfumo wetu wa elimu hadi leo, inaweka mkazo katika kuondoa matabaka kwenye utoaji wa elimu, utengano (alienation) kati ya shule na jamii na kusaidia kuondoa kasumba ya wasomi ya kujibagua na kutumia elimu waliyoipata kwa manufaa yao binafsi.

Aidha falsafa hii inaelekeza katika kuunganisha nadharia na vitendo, kwa dhana kuwa elimu isipatikane vitabuni tu bali ijumuishe na ile ipatikanayo kutokana na uzoefu wa kutenda au kufanya kazi ya kuongeza tija.

Ili kuhakikisha kwamba haya yanafikiwa na pia kuhakikisha kwamba wanafunzi wanawajibika na upatikanaji wa mahitaji yao, falsafa hii inaelekeza shule kuwa vituo vya kuzalisha mali ili kuchangia gharama za uendeshaji kwa asilimia ishirini na tano. Pia elimu inayotolewa katika ngazi zote iwe na maarifa na stadi za kumwezesha mhitimu kuishi na kufanya kazi yenye manufaa katika jamii.

Katika kutekeleza falsafa hii, shule karibu zote zilitaifishwa na kuendeshwa na serikali kuanzia mwaka 1967. Ili kuondoa aina zote za ubaguzi, serikali ilikubali kugharamia elimu katika ngazi zote. Pamoja na hayo, kila shule ilianzisha mashamba ambayo yalikuwa maarufu kama mashamba ya elimu ya kujitegemea. Hali hii ilimfanya mwanafunzi wa Kitanzania kuwa tayari kujitegemea mara tu baada ya kuhitimu mafunzo ya elimu ya msingi. Kwa hakika falsafa hii ilishabikiwa sana na kila Mtanzania.

Pamoja na uzuri wa falsafa hii, kuna changamoto zilizoukabili mfumo mzima wa elimu katika miaka kumi ya utekelezaji wa falsafa hii. Kama wote tunavyofahamu, katika nusu ya pili ya miaka ya 1970, ubora wa elimu yetu ulishuka sana kiasi kwamba serikali iliruhusu walimu wasio na sifa kuanza kufundisha katika shule za msingi.

Changamoto hii iliambatana na ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia kama vitabu, maabara, maktaba n.k. Sambamba na changamoto hii, ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi halikuenda sambamba na ongezeko la idadi ya vyumba vya madarasa na samani zake, achlia mbali nyumba za waalimu.

Hivyo ililazimu chumba kimoja cha darasa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi inayomfanya mwalimu alimudu darasa kiufundishaji. Pamoja na changamoto hizo, hata suala la usimamizi wa elimu nalo lilikuwa gumu kutokana na shule kuwa nyingi katika mtawanyiko wa kijiografia ambao una ufanisi mdogo. Matokeo ya hali hii ilikuwa ni kushuka kwa elimu kwa haraka sana.

Serikali iling’amua changamoto hizi na kutafuta namna ya kuziondoa ili elimu iendelee kutolewa kwa ubora unaotegemewa. Mwaka 1978 Bunge lilitunga sheria mpya ya elimu namba 25 ambayo, pamoja na mambo mengine, iliruhusu watu binafsi, mashirika ya dini, asasi za kiraia na makampuni kuanzisha, kusajili na kuendesha shule.

Kuanzishwa kwa sheria hii kulianza kuonyesha matumaini ya kunusuru ubora wa elimu kwani shule nyingi binafsi zilionyesha mafanikio. Kuna changamoto kadhaa ambazo zilijitokeza katika miaka kumi na tano ya kwanza ya utekelezaji wa sheria hii.

Changamoto hizi zilirekebishwa kupitia sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995. Hivyo mfumo wetu wa sasa wa utoaji wa elimu na mafunzo nchini unaongozwa na sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995 (iliyopata nguvu kutokana na marekebisho ya sheria ya elimu Na. 25 ya mwaka 1978 iliyorekebishwa kwa sheria Na. 10 ya mwaka 1995), sera ya elimu ya ufundi ya mwaka 1996 na sera ya elimu ya juu ya mwaka 1999.

Pamoja na ukweli kwamba shule za serikali zinaendeshwa kwa kodi za Watanzania pamoja na ufadhili mwingi sana kutoka mashirika mbalimbali ya ndani nje ya nchi, elimu yetu, hasa inayotolewa na shule za serikali, bado ina changamoto nyingi sana katika viashiria vya utoaji (input), mchakato (process) na matokeo (outputs).

Baada ya marekebisho hayo na baada ya sekta binafsi kujiimarisha ipasavyo, Watanzania wameendelea kushuhudia kukua kwa haraka sana kwa elimu katika sekta binafsi licha ya ukweli kwamba shule hizi hazina ruzuku yoyote kutoka serikalini. Sasa ni zaidi ya miaka thelathini tangu kuruhusiwa kwa sekta binafsi kuingia katika utoaji wa elimu.

Pengine ingekuwa busara kudurusu sababu hasa za tofauti hizi na kutafuta namna ambavyo elimu yetu katika sekta ya umma inaweza kuboreshwa.

Ni ukweli usionpingika kwamba gharama za uendeshaji katika shule za serikali ni kubwa kuliko gharama katikashule binafsi. Hii inatokana na ukweli wa kiuchumi kwamba kadri mradi unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo ufanisi kwa kila shilingi inayotumika unavyozidi kushuka. Hali hii inakabili vilivyo shule zetu za serikali.

Moja ya viashiria vya kushuka kwa ufanisi ni hii hali ya waalimu kuwa na malalamiko yasiyoisha kuhusu mapunjo wanayopata katika malipo yao, baadhi ya wanafunzi kuvuka madarasa na vidato bila kujua kusoma na kuandika, kukosekana kwa maabara, maktaba, vitabu na vifaa vingine vya kujifunzia na kufundishia na mambo mengine yanayofanana na hayo.

Sababu nyingine za kudorora kwa elimu katika shule za serikali ni kuingiliwa kupita kiasi na wanasiasa. Utakuta taarifa ya wakaguzi inaonyesha kabisa kwamba shule fulani haitakiwi kusajiliwa kutokana na kutotimiza baadhi ya vigezo vya usajili. Pamoja na taarifa hizo, utakuta mwanasiasa anaingilia kati na kulazimisha shule hiyo isajiliwe.

Hivyo hata uendeshaji wake huenda kisiasa siasa tu bila kujali vigezo muhimu vya uendeshaji wa shule. Utakuta shule ya serikali imesajiliwa lakini haina hata kitabu kimoja wala maabara. Itakuwa ni ajabu isiyo kifani kukuta shule kama hii ikitoa elimu bora.

Hali ni tofauti kabisa katika shule binafsi. Shule hizi husimamiwa na kwa ukaribu sana. Shule hizi hukaguliwa na kusajiliwa baada ya kutimiza vigezo vyote vya usajili. Huwezi kukuta shule binafsi inasajiliwa wakati haina maktaba yenye vitabu au maabara zenye vifaa vyote. Hata baada ya usajili, wakaguzi hufika katika shule hizi mara kwa mara kuangalia kama kila kigezo cha utoaji wa elimu kinazingatiwa.

Sambamba na hili, utakuta mmiliki wa shule hizi anafuatilia kwa karibu sana kila kinachoendelea shuleni na kuhakikisha wanafunzi wake wanapata huduma zinazotakiwa.

Kwaujumla wake ni kwamba shule binafsi huendeshwa kwa kufuata mahitaji ya wateja wake na kutimiza masharti yote yanayowekwa na serikali.

Kurunzi haioni kama itatosha tu kukosoa bila kutoa mapendekezo ya ubereshaji. Njia ya kwanza ni kuondoa siasa katika uendeshajiwa usajili na uendeshaji wa shule.

Hii inaweza kufikiwa kwa njia ya kuifanya idara ya ukaguzi kuwa wakala inayojitegema badala ya hali iliyopo ya kuwa idara katika Wizara Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Itakuwa ni ajabu ya ngariba kujitia suna mwenyewe kama kitengo hiki kitatenda haki hasa wakati shule ya serikali inapofanya makosa.

Njia ya pili ni kuweka ushirikiano kati ya wamiliki wa shule binafsi na serikali ili kuondoa tatizo la kushuka kwa ufanisi wa usimamizi unaotokana na kukua kwa idadi ya shule zinazosimamiwa na mmiliki mmoja.

Katika hali hii, mmiliki wa shule binafsi anaweza kuwekwa kuwa meneja wa shule ya serikali (hasa hizi za kata) iliyo karibu naye. Kama meneja, atahakikisha kwamba anashirikiana na bodi ya shule katika kuhakikisha kwamba shule hii ya kata inatoa elimu bora kama ilivyo shule yake.

Elimu ni mali ya umma na inatakiwa kugharamiwa na umma hata kama inatolewa na shule/chuo binafsi. Kurunzi inaamini kabisa kwamba, tukilizingatia hili, tutakuwa tumekata kabisa mizizi yote ya ufisadi dagaa, papa na nyangumi na tutakuwa tumeenzi na kuhuisha fikra sahihi za Baba yetu wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

No comments:

Post a Comment