Wednesday, November 25, 2009

Kawambwa ahimiza ujenzi wa Kiwanja cha ndege Songwe

na Gordon Kalulunga, Mbeya


WAZIRI wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, amehamasisha ukamilishaji wa Kiwanja cha Ndege cha Songwe, kilichopo mkoani Mbeya, baada ya kutembelea uwanja huo na kuukagua, kisha kuzungumza na mkandarasi na mhandisi mshauri wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini uwanjani hapo.

Kawambwa alitembelea na kuukagua uwanja huo juzi na kuwahimiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mkandarasi Kampuni ya Kundan Singh Construction Ltd ya nchini Kenya na mhandisi mshauri kutoka Falme za Kiarabu kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo unakamilika mapema iwezekanavyo.

Waziri huyo alisema kuwa kwa sababu awali kikwazo cha uendelezaji wa ujenzi wa uwanja huo kilikuwa ni kutolipwa malipo ya awali mkandarasi anayejenga uwanja huo, lakini kwa sasa tayari serikali imekwisha kulipa deni hilo, hivyo hatarajii kuendelea kusuasua kwa ujenzi katika kiwanja hicho.

“'Kwa sababu serikali imelipa fedha zote za malipo ya awali kwa mkandarasi, hivyo hatutarajii kuona ujenzi wa uwanja huu ukisuasua kama mwanzo, maana kikwazo kilikuwa ni fedha,”' alisema Waziri Kawambwa.

Aidha, alifafanua kuwa ifikapo Januari mwaka 2010 anatarajia kupata taarifa nzuri zaidi za maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, ambao ni tegemeo kubwa la wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na taifa kwa ujumla.

“'Kwa kipindi cha mwaka wa bajeti 2008/2009 serikali imetenga sh bilioni 18 kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa kiwanja hiki ambacho kina umuhimu sana kwa taifa letu, hivyo ni muhimi pia nanyi kama wataalamu mkaona kuwa ni jinsi gani serikali ilivyoupa kipaumbele uwanja huu,” alisema Kawambwa kwa matumaini ya kumalizika kwa uwanja huo kama matarajio ya serikali yalivyo.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho mbele ya Waziri huyo wa Miundombinu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Prosper Tesha, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Uhandisi, White Majula, alisema mkandarasi tayari amemaliza kukata na kujaza udongo njia za kuruka na kutua ndege ambazo waziri alizitembelea na kuzikagua.

“Maeneo yote ya usalama katika njia ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa mita 1,800 tayari mkandarasi ameyakamilisha kwa asilimia 65 na amekamilisha kazi ya ufungaji wa mitambo ya kusaga mawe kwa ajili ya kokoto na ameanza kufunga mtambo wa lami,” alisema Majula.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya uhakika vya habari, imeelezwa kuwa kampuni hiyo kutoka Falme za Kiarabu tayari imelipwa shilingi bilioni 3.1, ambapo kiwango hicho cha fedha kinajumuisha gharama za kazi za kufanya marejeo ya usanifu wa njia za kuruka na kutua ndege pia usimamizi wa utekelezaji wa ujenzi unaoendelea.

Kandarasi ya kumalizia kazi za ujenzi wa kiwanja hicho cha Songwe ilisainiwa Septemba 12 mwaka 2008 na kukabidhiwa Oktoba 19, mwaka huo huo, inatakiwa kazi hiyo ikamilike kwa kipindi cha miezi 18 kwa gharama ya sh bilioni 32.

No comments:

Post a Comment