• Mkutano wa Bunge, serikali, TANESCO wakatisha tamaa
na Sauli Giliard na Deogratius Temba
KIKAO cha pamoja kati ya serikali, Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, kimebaini kwamba ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la mgawo wa umeme nchini utapatikana baada ya muda mrefu.
Ukweli huo mchungu kuhusu mgawo wa nishati hiyo unaoweza kuendelea kulikabili taifa mara kwa mara, ulibainishwa jana wakati pande hizo tatu zilipozungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kikao chao.
Hata hivyo, matumaini pekee ambayo yanaweza kulinusuru taifa katika kipindi kifupi kijacho, ni kukamilika kwa miradi kadhaa ya kuzalisha umeme kama ile ya Tegeta ya kuzalisha megawati 45 na majadiliano yanayoendelea kati ya serikali na kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL yenye uwezo wa kutoa megawati 100.
Akizungumza katika mkutano huo wa pamoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini ya Bunge, William Shellukindo (CCM), alikiri kwamba, uchunguzi uliofanywa na wajumbe watatu wa kamati hiyo waliotembelea mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Hale na Pangani umebainisha kwamba, mgawo huo haujasababishwa kwa namna yoyote na vitendo vya hujuma.
“Tulipanga kukutana nao ili tupate maelezo ya kutosha juu ya mgawo huu wa umeme, katika taarifa za pande zote hizi tumeona kuwa kuna sababu mbili zinazosababisha mgawo huu kutokea, ambazo ni mitambo ya kuzalisha umeme ya Hale, Kihansi na Pangani kuharibika na kukosekana kwa maji ya kutosha ya kuzalisha umeme,” alisema Shellukindo ambaye kamati yake imekuwa na msimamo mkali dhidi ya maamuzi kadhaa ya menejimenti ya TANESCO kuhusu namna inavyosimamia utoaji wa huduma ya nishati hiyo muhimu.
Alisema kamati hiyo ililazimika kupata majibu ya kuridhisha kutokana na kwamba katika bajeti ya mwaka wa fedha 2009/10, Bunge liliridhia na kuidhinisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Pamoja na kukiri kwamba, kikao chao kilibaini kuwa, tatizo la umeme litaendelea kulisumbua taifa kwa kipindi kirefu zaidi, Shellukindo alisema suala la kuitaka serikali kuinunua mitambo ya Dowans halikuwa sehemu za ajenda walizozijadili.
“Suala la Dowans halikuwa ajenda ya kukutana hapa, lengo letu lilikuwa ni kupokea taarifa ya TANESCO. Hapa hakuna Dowans, tulishaizika tangu Machi mwaka huu, halina kazi tena,” alisema Shellukindo.
Hata hivyo, baada ya Shellukindo kusema kwamba sakata la Dowans limekwishazikwa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima aliyekuwapo katika mkutano huo aliongeza kuwa, serikali haina mpango tena wa kununua mitambo hiyo ya kufufua umeme ya Dowans, lakini endapo mtu binafsi atainunua na kuiuzia TANESCO umeme kwa sheria ya sasa, itakubali.
Katika hilo, Malima alisema kwa sheria za sasa, TANESCO ina uwezo wa kununua umeme kutoka katika makampuni na taasisi binafsi ili iweze kukidhi mahitaji yake ya kuhakikisha kuwa nishati hiyo inakuwepo wakati wote nchini.
Akizungumzia hatua ambazo serikali imechukua kutafuta mbadala wa mitambo hiyo ya Dowans, Malima alisema mchakato wa kuagiza mingine yenye uwezo wa kuzalisha megawati 160 imeshaanza na inategemea kuwasili nchini katika kipindi cha miezi 12 ijayo.
Katika hili, Malima alisema matokeo hayo yanatokana na mchakato ambao ulianza Aprili, mwaka huu kwa kutangaza zabuni na kufanya mchujo, baada ya uamuzi wa kuinunua mitambo ya Dowans kukwama.
Kwa upande wake, akizungumzia sababu zilizolifikisha taifa hapa lilipo sasa, Shellukindo, alibainisha ya kuwa, mgawo wa sasa unatokana na upungufu wa megawati 72 ambao kamati yake iliridhika na sababu za kitaalamu kutoka serikalini na TANESCO.
Mbunge huyo alitaja sababu sita za kuwepo kwa upungufu huo kuwa ni kutokana na kuharibika mtambo wa Songas UGT1 wenye uwezo wa kuzalisha megawati 20, mtambo mmoja wa Kihansi unaotoa megawati 60 na Hale uliokuwa unazalisha megawati nane.
Mbali na mitambo hiyo kuharibika, alisema uhaba mkubwa wa mvua mwaka huu umechangia kwa kiasi kikubwa maji kupungua katika vituo vya kuzalishia umeme vya Kihansi na Pangani.
Alieleza sababu nyingine kuwa ni kukosekana kwa uwezo wa kuzalisha umeme wa akiba (Reserve Margin) pamoja na kuchelewa kukamilika kwa mtambo wa gesi wa Tegeta ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 45 na ambao unatarajia kuanza kazi mwezi ujao.
Taarifa ya kamati hiyo, ilionyesha kuwa, kituo cha Kihansi kilichotakiwa kuzalisha megawati 180, kwa sasa kinazalisha megawati 120 ambazo kutokana na upungufu wa maji, umeme unaozalishwa ni megawati 80-85, wakati kituo cha Hale kilichotakiwa kizalishe megawati 21, kwa sasa hakizalishi kabisa kutokana na kuharibika kwa mashine ya kuzalisha.
Shellukindo aliitaka serikali kutotegemea vyanzo vya sasa vya umeme na badala yake itafute mbadala kwani hali ya hewa inaathiri umeme unaozalishwa kwa kutumia nguvu za maji.
Aliishauri kuipitia Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, kuona namna ya kuondoa urasimu uliopo ili usiathiri manunuzi ya mitambo miwili itakayozalisha umeme wa jumla ya Megawati 160, katika majiji ya Dar es Salaam na Mwanza.
Wakati Shellukindo akitoa rai hiyo, kumbukumbu zinaonyesha kuwa, miongoni mwa sababu ambazo zilisababisha Bunge kuitia misukosuko serikali, wakati wa sakata la Richmond mwaka jana ni uamuzi wake wa kuamua kutumia utaratibu uliokuwa ukijaribu kukwepa ukiritimba wa sheria ya manunuzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Malima ambaye mara kwa mara alisisitiza mitambo ya sasa haiendani na kasi ya ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi, alibainisha kuwa, hatua zinazochukuliwa kulinusuru taifa kutoka katika hali ya sasa ni matengenezo ya mtambo wa Tegeta ambao unatarajiwa kukamilika Novemba.
Aliongeza kuwa, mtambo wa Songas, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 20, utakamilishwa mapema iwezekanavyo wakati ule wa Kihansi wa megawati 60 na Hale wa megawati nane, inatarajiwa kuanza kazi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Licha ya mategemeo hayo, Malima alionya kuwa mitambo hiyo ya Kihansi na Hale itaanza kazi kutokana na hali halisi ya hali ya hewa kwani mvua zinazotarajiwa kunyesha mwezi ujao, ndizo zitakazotoa mustakabali wa mitambo hiyo kuanza uzalishaji.
Pamoja na hofu hiyo, Malima alisema hatma nyingine ya kupata umeme na kuliondoa taifa katika hali ya giza, inategemea mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya serikali na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na endapo muafaka utafikiwa, megawati 100 zitapatikana.
Katika hali ambayo haikutarajiwa katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, alishindwa kujibu maswali ya waandishi wa habari waliomtaka kutoa ufafanuzi wa kauli zake alizozitoa Machi mwaka huu kuwa, serikali isiponunua mitambo ya Dowans, nchi itaingia gizani mwishoni mwa mwaka na wananchi wasimlaumu kwa hilo.
Baada ya kuulizwa swali hilo, Dk. Rashid alisita kujibu na kunyamaza kimya, hatua iliyowafanya waandishi kumshinikiza kuelezea suala hilo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Malima aliingilia kati kwa kujibu kuwa alifanya utabiri wa nyota ulioegemea katika utaalamu wa kisayansi na ambao matokeo yake yamethibitisha kwamba alikuwa sahihi.
“Mkurugenzi alituandikia mwezi Februari mwaka huu akitoa mapendekezo ya kitaalamu kuwa serikalini tusipochukua hatua za haraka, nchi inaweza kuingia gizani mwishoni mwa mwaka kutokana na uwezekano wa kutokea kwa ukame na tumeuona,” alisema Malima.
Alisema ni wazi kuwa wataalamu wa masuala ya umeme waliliona tatizo mapema na kutoa ushauri wao wa kitaalamu, hivyo serikali ilipaswa kuzingatia.
Mapema mwaka huu, dhamira ya serikali kupitia TANESCO kutaka kununua mitambo ya Dowans, iliibua mjadala mkali miongoni mwa Watanzania, huku wakionyesha shaka kuhusu uamuzi huo.
Mjadala huo ulitokana na malumbano ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Shellukindo na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma, iliyo chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA).
Kutokana na mjadala huo uliochukua mwelekeo wa kupinga ununuzi wa mitambo hiyo, hatimaye TANESCO ilitangaza kuondoa nia yake hiyo kwa kile ilichoeleza kuwa mjadala wake umechukua sura ya kisiasa kuliko kuzingatia utaalam.
Tuesday, October 13, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment