KYELA ni miongoni mwa wilaya saba za Mkoa wa Mbeya. Nyingine ni Rungwe, Ileje, Mbozi, Mbarali, Chunya na Mbeya. Wilaya ya Kyela iko umbali wa kilometa 125 kutoka Makao Makuu ya Mkoa wa Mbeya upande wa Kusini.
Inapakana na Wilaya ya Rungwe kwa upande wa Kaskazini, Wilaya ya Ileje kwa upande wa Magharibi na wilaya za Makete na Ludewa katika Mkoa wa Iringa kwa upande wa Mashariki. Aidha, Wilaya ya Kyela inapakana na nchi ya Malawi na Ziwa Nyasa kwa upande wa Kusini.
Wilaya ya Kyela ina hali ya hewa ya kitropiki, yenye sifa za joto kali na mvua nyingi. Kwa wastani, Kyela ina joto la nyuzi 23 na wastani wa mvua kati ya milimita 2,000 na 3000 kwa mwaka.
Watu wanaoishi katika miji yenye joto, kama Dar es Salaam, hawawezi kupata taabu wanapokuwa Kyela, kutokana na joto kufanana kwa kiasi kikubwa. Joto kali linakuwa katika miezi ya Septemba, Oktoba, Novemba na Desemba na mvua nyingi inanyesha katika miezi ya Machi, Aprili na Mei.
Kutokana na hali ya hewa hii, uoto wa asili wa Wilaya ya Kyela ni wa aina ya nyasi ndefu za savanna zilizo katika mbuga tambarare. Wilaya ya Kyela ina jumla ya kilometa za mraba 1,322 na kati ya hizo, kilometa za mraba 450 zimefunikwa na maji ya Ziwa Nyasa, mito na mabwawa mbalimbali.
Aidha, karibu kilometa za mraba 500 zinafaa na zinatumika kwa kilimo, kilometa za mraba 29 ni misitu na shughuli nyingine zimechukua eneo la kilometa za mraba 343.
Asilimia kubwa ya eneo la Wilaya ya Kyela ni tambarare, yenye mwinuko kati ya mita 400 na mita 600 kutoka usawa wa bahari. Miinuko mikubwa inapatikana sehemu zilizo mpakani mwa wilaya za Ileje na Rungwe katika Kata za Ngana na Busale.
Eneo la utawala Wilaya ya Kyela imegawanyika katika tarafa mbili za Unyakyusa na Ntebela. Tarafa hizi zimegawanyika katika kata 15, vijiji 101 na vitongoji 383. Kata hizi zinazounda Wilaya ya Kyela ni Kyela Mjini, Ikolo, Ngonga, Katumba Songwe, Bujonde, Kajunjumele, Ipinda, Ipande, Mwaya, Lusungo, Matema, Makwale, Ngana, Busale na Ikama.
Halmashauri ya Kyela inaongozwa na madiwani 22, kati ya hao madiwani waliochaguliwa kutoka kwenye kata ni 15 na wa viti maalamu ni sita na Mbunge wa Jimbo la Kyela ni Dk. Harrison Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe alifanikiwa kunyakua jimbo hilo kutoka kwa aliyekuwa Mbunge kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, John Mwakipesile, ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Madiwani wote na Mbunge wametoka Chama tawala cha CCM.
Madiwani hao wa Jimbo la Kyela ni Timon Kisugujila wa Kata ya Makwale, Watson Majuni wa Kata ya Kajunjumele, Stephen Mwangalaba wa Ipande, Moses Mwamaso wa Katumba Songwe, Jacob Mwabusila wa Mwaya, Isaya Mwaipaja wa Lusungo, Paul Mwambafula wa Bujonde na David Mwaikambo wa Ngonga.
Wengine ni Visk Mahenge wa Kyela, Christopher Mullemwa wa Ipinda, Edmaster Mwakibinga wa Ikama, Kaizer Luvanda wa Ngana, Edwin Mwangoka wa Busale, Aleluya Mwakisaje wa Ikolo na Frida Mwampiki wa Matema. Madiwani wa viti maalumu ni Kissa Mwakalukwa, Veronica Kanyanyila, Subilaga Ipopo na Catherine Mwakila.
Hali ya ulinzi na usalama Hali ya ulinzi katika Wilaya ya Kyela ni shwari na mpaka kati ya Tanzania na Malawi ni salama. Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Kyela, Mashimba Hussein Mashimba, alisema mikutano ya mara kwa mara ya ujirani mwema hufanyika, kwa lengo la kuimarisha usalama na utulivu kati ya nchi na nchi.
Katika kipindi cha 2006/2007 kulikuwa na matukio ya ujambazi, hatua zinazostahili zilichukuliwa kudhibiti hali hiyo. “Tunampongeza Meja Jenerali mstaafu Makame Rashid, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, kwa jinsi anavyoshirikiana na uongozi wa wilaya na mkoa huu kuleta utulivu na uhusiano wa karibu wa wananchi wa Tanzania walioko nchini Malawi.” Alisema. Mashimba anasema katika kipindi cha 2006/2007,kulikuwapo na wimbi la wakimbizi kutoka Malawi, Somalia na Ethiopia. Hali hii imedhibitiwa na vyombo vya dola na ni shwari, wakimbizi waliokamatwa walikuwa 149, waliofungwa 109 na walioachiliwa ni 40.
Anasema kamati za Ulinzi na Usalama za kata na vijiji, zimeimarishwa na Ulinzi Shirikishi (Ulinzi wa Umma) umesaidia kupata taarifa mbalimbali za uhalifu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka ya kidola na kwa uongozi wa serikali. “Upo ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vyote vya ulinzi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Takukuru na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Kamati ya Ulinzi na Usalama inakutana kila mwezi na vikao vya dharura inapokuwa lazima,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Utekelezaji wa shughuli za maendeleo Wilaya ya Kyela inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni njia ya kutekeleza kivitendo sera na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali Kuu pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 na Mpango wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUKUTA). Mashimba alisema yote hayo ni mikakati ya kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2005.
Sekta ya elimu Kuna jumla ya shule za awali 85, zenye wanafunzi 4,851 wavulana 2,402 na wasichana 2,449. Mashimba alisema lengo la wilaya hiyo ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwakani kila shule ya msingi iwe na darasa la shule ya awali. Bado shule 14 tu hazijawa na shule za awali.
Wilaya hiyo ina jumla ya shule za msingi 99, zenye idadi ya wanafunzi 52,093, kati ya hao wavulana ni 26,798, sawa na asilimia 51.44 na wasichana ni 25295, sawa na asilimia 48.56. Ingawa Serikali ya Wilaya inafanya jitihada za kuboresha sekta ya elimu. Hata hivyo, zipo kasoro kadhaa zinazoikabili wilaya hiyo.
Mkazi wa Kyela Mjini, Anastazius Mwaijande, alisema kasoro zilizopo katika uboreshaji wa sekta ya elimu ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, vyoo na madawati.
Mkazi huyo alisema upungufu huo mkubwa wa vyumba vya madarasa, umesababisha madhara makubwa ambapo baadhi ya wanafunzi waliofaulu katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana na kutakiwa kujiunga na sekondari mwaka huu, hawajapata nafasi na majina yao yanashikiliwa bila kutangazwa hadi sasa hadi hapo wazazi watakapokamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Serikali wilayani Kyela ilikiri kuwapo kwa upungufu wa vyumba vya madarasa 762, nyumba za walimu 1,114, vyoo 1,788 na madawati 6,218. Elimu ya sekondari Wilaya ya Kyela ina jumla ya shule za sekondari 23, kati ya hizo 21 ni za serikali.
Shule hizo ni KCM, Itope, Ipande, Ikolo, Ipinda, Kyela, Matema Beach, Bujonde, Ngonga, Katumba Songwe, Kajunjumele, Ikama, Lusungo, Kafundo, Makwale, Nkuyu, Ikimba, Itunge, Mwaya, Masukila na Shule ya Wasichana ya Kayuki wilayani Rungwe. Mashimba alisema shule za sekondari za Mwigo na Ngana zinamilikiwa na taasisi zisizo za kiserikali.
Wilaya pia ilitarajia kufungua shule za sekondari, kwa ajili ya kidato cha tano na sita katika kata za Matema na Kyela hivi karibuni, ikiwa ni utekelezaji wa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne, wanaendelea na kidato cha tano.
Essau Mwakapugi ni mkazi wa Ipinda. Akizungumzia maendeleo ya elimu ndani ya Wilaya ya Kyela, yeye alisema anaona kasoro kubwa ipo katika idadi ya watoto wanaoacha shule.
Alisema sababu za watoto kuacha shule ni mimba, utoro wa kawaida, kukosa mahitaji kuugua, kuuguliwa na sababu nyinginezo, ambazo anasema hata hivyo serikali inaweza kuzidhibiti ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaoanza shule wanamaliza ukiondoa sababu zisizoepukika kama vifo.
Hilo la wanafunzi wanaoacha shule, linadhihirishwa na takwimu zilizopo, zinazooonyesha kwamba jumla ya wanafunzi 54 wa shule za msingi wameacha shule kwa mwaka huu, wavulana wakiwa ni 21 na wasichana 33. Katika wasichana, 21 wameacha shule kutokana na kupewa mimba. Kwa upande wa shule za sekondari wanafunzi wote 20 wameacha shule kutokana na mimba. Mwakapugi anasema hali duni ya maisha inachangia wanafunzi kurubuniwa na kupewa mimba.
Mkazi huyo wa Ipinda alilalamikia pia kuwapo kwa madeni makubwa ya walimu. Mashimba alikiri kwamba kumekuwa na madai ya walimu kuanzia mwaka huu, ambapo jumla ya Sh 310,406,492 zinadaiwa, baada ya kulipa Sh 70,368,123, ikiwa Sh 12,903,720 ni za walimu wa sekondari na Sh 297,502,772 ni za walimu wa shule za msingi.
Fedha hizo ni za uhamisho, masomo, likizo, posho za mishahara ya kuanza kazi, posho za kujikimu na matibabu.Sekta ya afya Wilaya ya Kyela ina jumla ya vituo 32 vya kutolea huduma za afya, zikiwamo hospitali mbili, moja ya serikali na nyingine ni ya shirika la dini Matema. Ina kituo kimoja cha afya cha Ipinda na zahanati zipo 29.
Kati ya hizo, 24 zinamilikiwa na Serikali, nne ni za mashirika ya dini moja inamilikiwa na shirika la KCP.Vilevile wilaya inatekeleza Mpango wa Uhai Ulinzi na Maendeleo ya Mama na Mtoto (CSPD) katika vijiji vyake vyote. Wilaya pia ina vituo 14 vya ushauri nasaha na upimaji (VCT) na vituo 30 vya huduma za afya majumbani.
Katika kupambana na Ukimwi, Mashimba alisema Wilaya ya Kyela imeathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Ukimwi, kwani kiwango cha maambukizi kimefikia asilimia 15.8. Wilaya hiyo iliendelea kuongeza juhudi katika mapambano ya Ukimwi, ugonjwa uliotangazwa kuwa janga la taifa.
Wananchi wanaendelea kuhamasishwa kupima kwa hiyari. Tathmini inaonyesha kuwa kabla ya Novemba 2005 ni wananchi 2,000 tu waliojitokeza kupima kwa hiyari, lakini hadi kufikia Desemba 2007 zaidi ya wananchi 16,831 walijitokeza kupima kwa hiyari, kati yao wanawake ni 7513 na wanaume ni 9318. Walioathirika ni 3939, wanawake 1583 na wanaume 2356.
Ipo mikakati ya kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI wilayani ambayo imefanyika kwa kipindi cha mwaka 2007/2008. Mkuu wa Wilaya anaitaka mikakati hiyo kuwa ni pamoja na watumishi wa afya 14 kutoka katika vituo mbalimbali wamepatiwa mafunzo ya ushauri nasaha na upimaji.
Mikakati mingine ni kuanzishwa kwa vituo vipya saba vya ushauri nasaha, kutolewa kwa mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa majumbani, kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, tiba sahihi ya magonjwa ya ngono na elimu ya kuzuia maambukizi imeendelea kutolewa na kamati za UKIMWI za kata na vijiji zimetembelewa na kuimarishwa.
Mashimba alisema pia kuwa huduma kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu yameendelea kutolewa kwa kushirikiana na asasi mbalimbali. Takwimu zinaonyesha kuwa watu 946 wanaendelea na dawa za kupunguza makali ya VVU katika vituo vya Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Matema na pia mashine ya kupima CD4 imepatikana, kwa sasa huduma ya upimaji huo inafanyika wilayani hapo.
Kutokana na juhudi hizo maambukizi mapya ya UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 17 kabla ya Novemba 2005 hadi asilimia 15.8 kwa sasa na wananchi wanaendelea kuelimishwa juu ya kujikinga na ugonjwa huo wa UKIMWI.
Kazi nyingine zilizofanyika ni kutoa elimu ya VVU ngazi zote sehemu chache, kutoa elimu ya umri rika kwa shule na nje ya shule, kutoa mafunzo kwa Kamati ya Ukimwi ya Wilaya, na kamati za Ukimwi katika kata, kutoa elimu kwa waelimishaji rika 40 nje ya shule na kusimamia mipango shirikishi jamii katika kata 10.
Ugonjwa wa malaria Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, idadi ya watu waliougua malaria mwaka 2007 chini ya miaka mitano ni 53,427 na zaidi ya miaka mitano ni 24,620, jumla ni 78,047.
Vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria ni 119. Chini ya miaka mitano ni 72 na zaidi ya miaka mitano ni 47, sawa na asilimia 0.15 ya waliougua malaria. Hata hivyo, wilaya hiyo imeendelea kuweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoa dawa mpya ya malaria (Alu), kuendelea kuelimisha jamii jinsi ya kujilinda na maambukizi ya ugonjwa wa malaria, ikiwa ni pamoja na kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa pamoja na hati punguzo kwa watoto na mama wajawazito.
Kwa upande wa ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, Mashimba alisema wilaya hiyo ina mpango wa kujenga vituo vya afya kwa kila kata na zahanati kwa kila kijiji kwa mujibu wa agizo la serikali. Alisema malengo ya wilaya ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Malengo ya muda mfupi ni kutoa agizo kwa kila kijiji kisicho na kituo cha kutolea huduma, kutenga eneo la kujenga zahanati. Tayari kila kijiji kimeshatenga eneo hilo.
Malengo ya muda wa kati ni kila kata itenge eneo la kujenga kituo cha afya, kujenga vituo vya afya saba ifikapo 2010, kuipa hadhi zahanati ya KCM iwe kituo cha afya ifikapo 2010 na kujenga zahanati mpya 15 ifikapo 2010.
Mashimba alitaja malengo ya muda mrefu kuwa ni kujenga zahanati mpya 56 ifikapo 2015 na kujenga vituo vya afya ifikapo 2015
Mpango huo tayari umeandaliwa na elimu na hamasa imeshatolewa kwa kila kijiji. Mashimba alisema wananchi wameufurahia mpango huo na kwamba tayari imeshapitishwa katika vikao vyote vya halmashauri.
Alisema mipango yote ya utekelezaji imeshakamilika kwa kuzingatia kuwa ujenzi huo kwa sehemu kubwa utafanywa na wananchi. Kwa kushirikiana na mipango ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Huduma za maji Wilaya ya Kyela ina jumla ya miradi ya maji ya mserereko mitano ambayo ni Kanga, Ngamanga, Ngana, Makwale, Sinyanga na mradi wa msukumo wa pampu mmoja katika Kijiji cha Lema.
Miradi hii inahudumia vijiji 82 kati ya vijiji 101 vilivyomo wilayani, ambapo eneo la mtandao wa maji ni asilimia 80 na wakazi wake wanaopata maji safi na salama ni asilimia 67 tu. Hii inatokana na ongezeko la watumia maji pamoja na muda wa usanifu wa miradi mingi kupita.
Pamoja na miradi hii ya maji ya bomba, wilaya hii ina jumla ya visima 63 vya pampu za mkono na visima vitano vya umeme. Kwa mwaka 2007-2008, kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa miradi ya maji ya bomba tiririka ambapo miradi ya Lema, Ngana, Makwale na Sinyanga imekarabatiwa. Ujenzi wa visima ulifanyika na jumla ya visima virefu saba na visima vifupi 17 vimechimbwa.
Lakini pia upimaji, usanifu na ujenzi wa chanzo umefanyika na kazi ya kuweka bomba kuu na ujenzi wa tangi lenye ujazo wa mita za ujazo 45 unaendelea katika Kijiji cha Ikombe. Mkuu wa Wilaya anasema mikutano ya hadhara imefanyika katika vijiji vyote 101 ambayo ilikuwa ni kuihamasisha jamii ya kutunza na kuendesha miradi ya maji.
Alisema ili kutumia vizuri mvua zinazonyesha idara ilipanga kuanzisha uvunaji wa maji kwenye shule tano na zahanati tano ambapo kwa kipindi hiki Shule ya Sekondari Kyela imeshaanza kutumia teknolojia hiyo. Mpango huo utaendelea kwa mwaka huu.
Mamlaka ya Maji mjini na Mamlaka ya maji mji mdogo Kasumulu zimeanzishwa na zimeshaanza kufanya kazi, mikutano imefanyika katika vijiji tisa kata za Ngana na Ipande ambavyo vinazunguka vyanzo vya maji ili jamii ione umuhimu na wajibu wa kulinda na kutunza mazingira ya vyanzo vya maji. Anasema vijiji vyote vimeelekezwa namna ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kusaini mkataba maalumu.
Kilimo na mifugo Karibu asilimia 80 ya wakazi wa Kyela wanategemea kilimo kwa kipato, ustawi na maendeleo yao. Mazao ya chakula yanayostawishwa wilayani humo ni mpunga, mahindi, ndizi, mihogo, viazi na mazao jamii ya mikunde. Mazao ya biashara ni pamoja na kakao, michikichi, korosho na mpunga.
Hali ya hewa kwa maana ya mvua zilizonyesha msimu wa kilimo 2007/08 ilikuwa nzuri kwa ustawi wa mazao mbalimbali na hasa mpunga kutokana na mtawanyiko wake mzuri. Matumizi ya mbolea yameongezeka miongoni mwa wakulima. Tathmini ya miaka miwili (2005-2007) inaonyesha kwamba jumla ya tani 459.4 zimetumika ukilinganisha na tani 166.75 zilizotumika kabla ya Novemba. 2005.
Hii ni sawa na ongezeko la tani 292.7 kwa kipindi cha awamu hii ya nne. Wilaya hiyo kwa mara nyingine tena katika kipindi cha miaka miwili imeshuhudia uharibifu wa viwavi jeshi wa hapa na pale katika mazao ya mahindi na mpunga. Hata hivyo, safari hii uharibifu haukuwa mbaya sana kutokana na ukweli kwamba mashamba mengi yalikuwa hayajapandwa bado.
Aidha mvua nyingi zilinyesha baadaye na kusaidia kuangamiza wadudu hao, sambamba na juhudi za idara. Dawa aina ya Dursban ilisambazwa na idara katika maeneo mbalimbali kwa tahadhari ya wadudu hao.
Kwa upande wa chakula, Mashimba alisema katika kipindi cha 2007/08 hali ya upatikanaji wa chakula kwa jumla ilikuwa ya wastani licha ya bei za vyakula kupanda mara kwa mara.
Hata hivyo mazao mengine kama mhogo na ndizi toka ndani na nje ya wilaya pamoja na mazao ya biashara, kwa maana ya kokoa na mawese yalisaidia sana katika kuboresha hali ya upatikanaji wa chakula.
Alisema pamoja na kukumbwa na hali mbaya ya hewa, wilaya hiyo iliongeza uzalishaji wa mazao ya biashara hususani kokoa na korosho. Kiwango cha uzalishaji wa kokoa kilipanda kwa asilimia 17 kutoka tani 4,000 kwa mwaka 2005, hadi tani 4,830 kwa mwaka 2007.
Kwa upande wa korosho kiwango kiliongezeka kwa asilimia 40 kutoka tani 300 mwaka 2005, hadi tani 496 kwa mwaka 2007. Sababu kubwa zilizochangia ongezeko hili ni mafunzo kwa wakulima kupita ziara mbalimbali za kuongeza ujuzi na mafunzo kwa njia ya mashamba darasa.
Hadi sasa mashamba darasa matatu ya kakao yanaendelea kuendeshwa katika kata ya Bujonde na mengine 23 ya mpunga na 3 ya mahindi yamepangwa kuendeshwa kwa mwaka huu wa 2007/08.
Wilaya pia imeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 200 mwishoni mwa mwaka 2005 hadi hekta 240 mwaka 2007.Skimu za kisasa za umwagiliaji zimeanzishwa katika kipindi cha miaka miwili hii. Skimu hizo ni Ngana ambayo mfereji mkuu umekamilika, Ikumbilo ambayo kazi ya ujenzi wa mifereji mikuu miwili ya umwagiliaji inaendelea kujengwa na ule wa Makwale ambao kwa sasa uko kwenye upembuzi yakinifu.
Miradi hii ikikamilika itawezesha kilimo cha mpunga, kulimwa kwa misimu miwili kwa mwaka katika maeneo hayo, hivyo kuongeza uzalishaji wa kilimo cha mpunga wilayani. Kwa upande wa mifugo, wilaya ina ng’ombe wa asili wapatao 37,200 na chotara 4,485, nguruwe 7,606, mbuzi 1,820, kondoo 2,100 na kuku 142,000.
Hata hivyo, baadhi ya wakulima wilayani Kyela wanaeleza kutoridhishwa na usimamizi wa shughuli za kilimo. Sarah Mwamboneke wa Kasumulu anasema kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa kilimo lakini pia vitendea kazi na fedha za mtaji kwa ajili ya kilimo.
Alisema pia kuna uzito kwa wakulima na wananchi kwa ujumla katika kupokea mabadiliko yakiwamo ya kilimo bora na ufugaji wa kisasa, uhaba wa miundombinu ya kilimo na hasa inayohusiana na kilimo cha umwagiliaji, uhaba wa zana na pembejeo za kilimo na hasa kilimo cha mpunga (zana za kupandia na mbolea za aina zote) na umasikini miongoni mwa wakulima wengi hupunguza kasi ya kupokea teknolojia za kisasa.
Mwamboneke anaeleza kukerwa pia na mafuriko ya mara kwa mara na hivyo kuleta athari kwa wakulima. Kwa mwaka jana mwezi Machi hadi Aprili 2008, jumla ya hekari 386.12 zimeathirika na mafuriko kati ya hekari 13,496 ambayo ni sawa na asilimia 2.9.
Mpango wa kuanzisha Benki ya Wananchi Kyela Wilaya ya Kyela ina mpango wa kuanzisha Benki ya Wananchi, mchakato wa uanzishaji ulishaanza tangu mwaka juzi kwa timu ya watu saba, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya kwenda Wilaya ya Mbinga kujifunza.
Lengo kubwa la benki hiyo ni kujibu matatizo ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa kawaida vijijini (mikopo ya fedha).Faida za benki hiyo ni wananchi wa Kyela, ndiyo watakuwa wamiliki wa benki hiyo, hivyo faida itakayotokana na biashara ya kibenki itawarudia wananchi wa Kyela kwa maana ya kupata gawio.
Lakini pia itakuwa imesogeza mfumo wa huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi wa kawaida vijijini, wananchi wa kawaida vijijini, watanufaika na huduma za kifedha zitakazotolewa na benki hiyo kwa njia ya mikopo ya aina mbalimbali, utunzaji wa fedha zao, utumaji na upokeaji wa fedha kutoka na kwenda maeneo mbalimbali pamoja na huduma za bima.
Mikopo kwa wajasiriamali, Wilaya ya Kyela ilitoa mikopo kwa wajasiriamali 326 kupitia Benki ya NMB kiasi cha Sh 216,533,335. Mikopo yote ilitakiwa iwe imerudishwa kufikia Juni 6, 2008.
Wajasiriamali 105 tayari wamerejesha mikopo yao kiasi cha Sh 160,200,165. Mpaka sasa wajasiriamali 221 bado hawajarejesha mikopo yao yenye thamani ya Sh 56,333,169. Hata hivyo juhudi za kufuatilia mikopo hiyo inaendelea kwa ushirikiano na watendaji wa kata, vijiji na vitongoji ili wajasiriamali wengine wapewe mikopo hiyo.
Uboreshaji wa Barabara, Wilaya ya Kyela ina mtandao wa barabara kuu na zile za vijiji. Barabara ya kitaifa ina urefu wa jumla ya kilometa 38 ambayo ipo katika kiwango cha lami.
Hali ya ubora wa barabara ya kitaifa ni kilometa 31 ipo katika hali nzuri, kilometa saba ni ya wastani na hakuna sehemu iliyokuwa mbaya. Barabara ya kimkoa ina jumla ya urefu wa kilometa 93, ambayo ni ya changarawe. Hali ya barabara ya kimkoa ni kilometa 46 ipo katika hali nzuri, kilometa 40 ni ya wastani na kilometa saba ni mbaya.
Barabara za Wilaya ya Kyela zina jumla ya urefu wa kilometa 201. Kati ya hizo kilometa 0.5 ipo katika kiwango cha lami, kilometa 95.3 ni za changarawe na kilometa 105.2 ni za udongo. Mashimba alisema Wilaya ya Kyela ina barabara za vijijini zenye jumla ya urefu wa kilometa 178 ambazo ni za udongo.
Kwa taarifa hii tunategemea kupata taarifa ya Mwaka 2008/2009 kutoka kwa mkuu wa Wilaya Mpya ili tujue maendeleo kwa Mwaka huo. Tutawaletea taarifaa hizi hapa hapa. Vilevile ukiwa na maoni au mawazo yoyote usisite kuwasiliana na Kyela Community Initiatives.
''Kyela Community Initiatives kwa maendeleo ya Kyela na Watu wake.''
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Napenda kuwakumbusha wananchi wa Kyela kuwa tarehe 25.10.2009 ni siku muhimu sana kuwachagua wale watakaotuongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo katika uchaguzi wa Serikali za mitaa. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kutambua kuwa rushwa ni adui wa haki hututakiwi kutoa wala kupokea rushwa.
ReplyDeleteVilevile tunapashwa kuhamasishana ili ikifika siku hiyo watu wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kupiga kura.
Ukiwa kama mdau wa maendeleo ya wilaya ya Kyela na vitongoji vyake inakubidi kutambua kuwa bila wewe Kyela haitaendelea hata kidogo. Kuchagua mtu kwa kuangalia ametoa nini kwako na kusahau kuwa huyu mtu atakusaidia nini wewe binafsi na jamii nzima ya Kyela huku hakutatusaidia.
Tumchague mtu kwa sifa zake na uwezo wake wa kuleta maendeleo katika maeneo yake. Tambua kuwa kama mtu hawezi kusimamia maendeleo katika eneo lake asichaguliwe kuwa kiongozi.
Nawatakia maadalizi mema kuelekea uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Ndugu,
ReplyDeleteKagema,
Kwanza nakupongeza kwa jitihada zako za dhati juu ya kusimamia na kufungua hii blog inayo husu maendeleo ya wilaya yetu.Hata kama tusha wahi kujadili swala hili,lakini swala ya kutoa muda na kukusanya taarifa mbalimbali toka vyanzo mbali mbali kwa ajili ya jamii kubwa na hasa kama ya wana kyela si jambo dogo.Ni rahisi kuona taarifa zimeandikwa lakini jinsi ya kuzipata ni kazi tofauti.
Ndugu wenzangu,
Ninaamini ya kwamba itatusaidia wana kyela tunaoishi ndani na nje ya kyela,kuunganisha mawazo yetu ya nini kifanyike ili kuleta maendeleo ndani ya wilaya yetu.
Nimeweza kuingia(log in) ndani ya tovoti hii (http://kyelacommunity.blogspot.com), na kwa ufupi ina toa picha ya mapema ya khali ya kyela jinsi ilivyo kwa sasa,ki elimu,utawala ,siasa na maendeleo ya wilaya yetu.
Tuna kazi kubwa ya kuhamasishana kwaajili ya maendeleo ya wilaya yetu,kwani si wengine wanao takiwa kufanya kwa ajili yetu,bali ni sisi wenyewe kwa ujumla wetu ndio askari pekee tunaotakiwa kuikomboa kyela.
Nina penda kuwashauri wenzangu,kwamba lugha na mawazo ya busara,unyenyekuvu na upole ndio yawe msingi wa kubeba ujumbe tofauti tofauti,badala ya kujenga ubishani,ushindani,kubaguana na hata kudharauliana kwa aina yoyote,kwani mara nyingi uwa hatufanani kimtazamo.
Bado nazidi kupongeza wana kyela tena ,na kuwatia moyo,kwamba tuipatapo tuvuti hii ambayo ipo kwaajili yetu,basi tuifungue na tuyasome yale yaliyoandikwa,kwani ndiyo yatakayo tupa kuyajua yaliyopo sasa, hivyo kutupa Mwanga wa nini cha kuchangia.
Asanteni sana,na Mungu awabariki.
Amos M Phillip