Tuesday, October 13, 2009

Halmashauri zashauriwa kuelimisha sera ya wazee


na Moses Ng?wat, Mbeya


HALMASHAURI za wilaya katika Mkoa wa Mbeya zimeshauri kuongeza juhudi ya kupeleka elimu ya sera ya wazee ili jamii iweze kuitambu na kutoa ushirikiano katika mipango madhubuti ya kuwapatia huduma muhimu.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya uangalizi wa wazee mkoani Mbeya (MOPEC), Christian Chakudika, katika mkutano uliowakutanisha wazee pamoja na watendaji wa serikali za mitaa na wataalamu wa kada mbalimbali kutoka kata tano za halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Alisema kama viongozi wa ngazi za kata na vijiji wataelimishwa zaidi juu ya sera ya taifa ya wazee ya mwaka 2003 itasaidia katika mipango ya maendeleo kwenye halmashauri hizo.

Aliongeza kuwa sera ya taifa inaeleza bayana umuhimu wa makundi maalumu ndani ya jamii kama wazee hivyo ni jukumu la kila halmashauri za wilaya kuhakikisha zinaweka kipaumbele kwa kundi hilo hususan wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Chakudika aliongeza kuwa ni jukumu la kila mdau wa maendeleo kutambua na kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa huduma na stahiki za wazee kama ilivyoainishwa katika miongozo mingine kama Mkukuta.

Alisema ushirikiano wa dhati kwa wadau hao wakiwemo viongozi wa ngazi za kata na vijiji utachangia kwa kiasi kikubwa kushawishi uboreshaji wa sera na utekelezaji wake kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, kata, wilaya hadi mkoa.

Mwenyekiti wa MOPEC, Anyaghile Luvanda, alisema ili chombo hicho cha kutetea maslahi ya wazee kiwe endelevu ni lazima makundi mengine ya jamii hasa wale walio chini au kukaribia miaka 60 wapewe elimu zaidi ya sera ya wazee ili washiriki kikamilifu katika kutoa mchango kwenye kundi hilo.

No comments:

Post a Comment