8th October 2009, 07:10 AM
________________________________________
Marehemu baba wa taifa, mwalimu J.K. Nyerere mnamo mwaka 1967 akielezea umuhimu wa kuwa na huduma za maktaba Tanzania alisema “vitabu ni njia muhimu ya kupata maarifa na kujiendeleza. Kutokana na vitabu tunajifunza mbinu na utaalamu mpya wa kufanya kazi zetu za maendeleo. Uzoefu na ugunduzi wote uliowahi kufanywa na mwanadamu unaweza kupatikana kwa kujisomea”
Ni dhahili kwamba maendeleo ya kweli na stamilivu yanapatikana kwa kujisomea. Katika jitihada tunazozifanya kupambana na umaskini ni muhimu pia kuhimiza kujenga utamaduni wa kujisomea. Tukifanikiwa kujenga taifa la watu wanaopenda kujisomea, tutakuwa tumefanikiwa kujenga taifa la watu wanaojua, wadadisi, waelewa na wenye maarifa, hivyo kufanya njia ya kuelekea maendeleo kuwa nyepesi zaidi.
Ni kwa kuzingatia umuhimu wa kujisomea katika kuondoa umasikini na kuleta maendeleo, mwaka huu wadau wa vitabu tumeamua kauli mbiu ya tamasha la kumi na nane la wiki ya vitabu iwe SOMA VITABU, UJIENDELEZE, UJIKOMBOE. Ninaaamini kwamba nchi yoyote haiwezi kujikomboa au kuendelea endapo wananchi wake hawatakuwa na tabia ya kujisomea ili kuwawezesha kuwa na ufahamu mpana zaidi. Ukuaji wa haraka wa uchumi unatokana na kasi ya wananchi kuwa na tabia ya kujisomea. Hata hivyo tabia hii inapaswa kujengeka tangu nyumbani na shuleni hasa katika umri mdogo, ndio maana mwaka huu tumeamua msisitizo uwe kwenye vitabu vya watoto.
Lengo kubwa la mahadhimisho haya hasa ni kuhamasisha kujenga hali ya kupenda kujisomea. Sababu za kutokuwepo kwa ari ya kujisomea zipo nyingi na uwenda nafasi hii haitosherezi kuziorodhesha zote. Napenda kuwaalika nyote, kuungana nasi katika kuhamasisha na kuinua hali ya kujisomea katika jamii yetu.
Miongoni mwa shughuli tulizoandaa kwa ajili ya tamasha hili ni pamoja na maonesho ya vitabu yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mahema ya watoto na watu wazima ya kusomea vitabu, semina, mafunzo ya ukutubi kwa waalimu hamsini kutoka katika shule za msingi za wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro pamoja na kutoa vitabu kwa shule hamsini pia za kutoka wilaya ya Mvomero. Pamoja na shughuli hizo kamati pia imeandaa burudani mbalimbali ili kukuburudisheni wakati wa tamsha.
Kwa niaba ya wadau wote wa sekta ya vitabu Tanzania, napenda kuchukua nafasi hii kuwaalikeni nyote katika shamrashamra za wiki ya vitabu zitakazofanyika kuanzia tarehe 07 mpaka 12 Septemba 2009, Dar es Salaam. Pia napenda kuchua fursa hii kuwakaribisha ndugu zetu waliotoka nje ya nchi ili kushirikiana nasi katika kufanya tamasha letu liwe la mafanikio. Hususan wajumbe wa mabaraza ya maendeleo ya vitabu ya Kenya na Uganda. Karibuni sana na mjisikie mpo nyumbani!
Mwisho napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa taasisi na watu binafsi waliochangia kwa hali na mali kufanikisha tamasha la usomaji la mwaka huu.
Kwenu nyote tunasema asanteni sana.
A.K. Hassan
Mwenyekiti, Tamasha la vitabu 2009
Thursday, October 15, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment