Thursday, November 26, 2009

Jamani hatupungi mashetani hapa, tunasoma

Na Brandy Nelson, Chunya
Wanafunzi wakiwa darasani wakiendelea na masomo


HADI kufikia mwaka 2000 kijiji cha Udinde kilikuwa na shule moja ya msingi iitwayo Udinde iliyochukua watoto kutoka vitongoji vya jirani pia, lakini ulipoanzishwa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) mwaka 2002 ilionekana haja ya kufanya maboresho.

Shule hiyo ilipachuliwa ikazaa shule nyingine ya msingi katika kitongoji cha Iboma mwaka 2003.

Uamuzi wa kujenga shule nyingine, mbali ya kufanya maboresho ulilenga pia kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali wa kilomita 10.

Serikali ya kijiji hicho kilichopo kata ya Kapalala tarafa ya Kwimba wilaya ya Chunya mkoani Mbeya ikitumia pesa zilizotokana na Mmem ilifanikiwa kujenga darasa moja tu na hadi sasa halijakamilika wala halijaongezwa darasa jingine wala vyoo na nyumba za mwalimu.

“Shule hii ilimegwa kutoka shule ya msingi Udinde ambapo hapa Iboma tuliletwa walimu watatu na mazingira yenyewe ni kama haya unavyoyaona. Wazazi walichangia kujenga darasa hili moja na serikali kupitia Mmem ikamalizia paa ingawa darasa lenyewe bado halina sifa ya kuwa darasa kwani halijakamilika,” anasema mwalimu Albert Juakali ambaye alikutwa akifundisha hisabati wanafunzi wa darasa la kwanza.

Uamuzi wa haraka uliofanywa na walimu ni kuhamishia ‘mikoba’ yao kwenye mti wa mbuyu ulio jirani na kuweka mbao. Upande mmoja wanakaa darasa la kwanza, halafu upande mwingine darasa la pili, la tatu, la nne, la tano nk. Wakati wa juakali shida na wakati wa mvua ni likizo.

Mwenye masikitiko zaidi ni mwalimu mkuu wa shule, Onesmo Mdamu ambaye anasema;"Sikiliza, shule hii ina muda wa miaka sita mpaka sasa lakini ina darasa hili moja tu na ambalo linatumika kwa ajili ya watoto wa darasa la sita na hawa wa madarasa mengine wanasoma kwenye mti wa mbuyu ambao pale kuna madarasa matano yaani la kwanza, pili, tatu, nne na tano kama mnavyoona wenyewe."

Hayo ndiyo maisha ya wanafunzi wa shule hiyo na uamuzi wa kutumia mti huo kama darasa ulipitishwa na kamati ya shule.

Madhara

Mazingira hayo yamewasaidia zaidi watoto wasiopenda elimu maana huona heri kwenda kujishughulisha na uvuvi wa samaki kwenye Ziwa Rukwa lililojirani na shule hiyo badala ya kushinda kwenye juakali chini ya mti.

"Mazingira ya shule hii ni magumu kutokana na kuwa na darasa moja ambalo linatumiwa na wanafunzi wa darasa la sita. Shule yenyewe kama unavyoiona iko kandokando ya Ziwa Rukwa hivyo inapelekea watoto kuamua kujishughulisha na ajira ya uvuvi wa samaki kutokana na mazingira magumu ya shule na ugumu wa maisha wa familia zao na hivyo kukosa haki ya kupata elimu bora," anaongeza Juakali.

Aliyeamua kubadili matumizi ya mbuyu kutoka kwenye imani za asili kwamba ni makazi ya mashetani hadi kuwa darasa la wanafunzi 134 ni kamati ya shule. Kamati hiyo ya shule imeshindwa kuhamasisha wananchi yajengwe madarasa mengine.

Kinachofanyika chini ya mti wa mbuyu, Mdamu anasema wanafunzi huchukua mabanzi na kuweka juu ya matofali na sehemu ya kuandikia wakitumia matofali kama meza na wengine wakishindwa kupata mabanzi hutumia matofali kama viti.

"Hali hii ni mbaya kielimu kwani hata sisi walimu hatujui tumwachie nani hawa wanafunzi, basi tumeona tuungane na usemi usemao 'Ualimu ni Wito', lakini kwa ujumla hali ni mbaya sana. Hata mahudhurio ya wanafunzi ni finyu kutokana na kukatishwa tamaa na mazingira na kupelekea kujiingiza katika shughuli za uvuvi wa samaki,” anasema

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Leopard Ngairo mbali ya kuelezea historia anakiri kwamba mazingira ya ufundishaji ni magumu na yanachangia wanafunzi kukosa elimu bora na hivyo wengine kuamua kuacha shule na kujiingiza katika ajira ya shughuli za uvuvi wa samaki.

"Shule ina darasa moja pekee, ina uhaba wa madawati, ofisi za walimu, vifaa vya kufundishia hakuna ambapo kwa sasa shule ina vitabu viwili kwa kila darasa, kwa kweli walimu wanashindwa kutoa elimu ipasavyo kwa wanafunzi," anasema Ngairo.

“Hii shule ina matatizo makubwa huwezi kufananaisha na shule zingine kwani wazazi wengi wanakatishwa tamaa na mazingira yake na inasababisha wazazi kuwaruhusu watoto wao kutafuta ajira katika shughuli za uvuvi badala ya kwenda shule,” anasema

Darasa la saba

Septemba mwaka huu walimu na kamati ya shule walisugua vichwa kuona namna nzuri ya kuwasaidia wanafunzi wa darasa la saba waliotarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi. Hapo tena, walimu na kamati ya shule walikubaliana kulihamishia darasa hilo Udinde kwa ajili ya kumalizia elimu yao ya msingi.

"Hapa kwa kweli hakuna elimu bora inayopatikana kwani mazingira yote kwa ujumla ni magumu siyo kwa wanafunzi wala sisi walimu kwani hakuna hata vitendea kazi na tunaishi mbali na shule na inatulazimu kutembea umbali wa kilometa tisa ili kuweza kufika hapa shuleni," anasema Mdamu.

Mahitaji ya shule hiyo ni kuwa na walimu watano lakini waliopo wanaofanya kazi ni wawili pekee, hakuna vitabu vya kufundishia kwani vilivyopo ni vitabu viwili kila darasa na kwamba madawati ni tatizo kubwa hali inayopelekea watoto hao kukaa kwenye matofali.

Walimu hao wamekuwa wakifundisha kwa moyo wote na wamekuwa wakipeleka ripoti kila mwezi kwa afisa elimu wa halmashauri kuwajulisha hali halisi ya shule, lakini hakuna kinachofanyika na kuifanya shule hiyo kutokuwa na maendeleo yoyote.

Mdamu analalamika pia kwamba hali hiyo kwa kiasi fulani inachangiwa na baadhi ya wazazi katika kitongoji hicho kukosa mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule na badala yake wamekuwa wakijikita zaidi kwenye shughuli za uvuvi kuliko suala la elimu kutokana na mazingira ya shule hiyo.

Mwalimu mkuu anadhani kwamba ufumbuzi wa haraka juu ya matatizo ya shule umo kwenye mikono ya viongozi wa wilaya na mkoa.

"Kama viongozi wa serikali ya wilaya na mkoa wangetembelea na kushuhudia mazingira ya shule na kuwahamasisha wananchi wajitolee nguvu zao kujenga shule ni jambo ambalo lingesaidia watoto hao kupata elimu bora badala ya bora elimu ambayo wanaipata kwa sasa," anasema.

Wanafunzi nao wamefikia hatua ya kuuona ukweli kwamba hakuna wanachopata katika mazingira kama haya. Adela Alex, mwanafunzi wa darasa la sita anasema mazingira ya shule hiyo ni magumu na hivyo kupelekea kushindwa kupata elimu bora na kusabibasha baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo kukatamaa na kuendelea na shule na kujiingiza katika shughuli za uvuvi wa samaki kwa kufanya vibarua na kujipatia fedha kidogo.

"Kwa kweli sisi wanafunzi tunaona hali hii ni mbaya kwetu tunaona kama tumetengwa labda sisi siyo raia wa Tanzania au labda serikali inatuona kama wanyama, haiwezekani tukawa tunasoma shule katika mazingira haya ya chini ya mti wa mbuyu halafu tukasema kuna kitu tunakipata; hakuna tunachokipata hapa chini ya mti,"anasema kiongozi wa wanafunzi Emanuel Mkombe.

Anasema kuwa mazingira hayo hayawawezeshi kusoma vizuri yanawakatisha tama ndiyo maana kuna baadhi ya wanafunzi wamekimbia na kuamua kufanyakazi ya vibarua ziwani. Lakini kuna wanafunzi wengine ambao wana nia ya kusoma ndiyo maana wameendelea kuwa wavumilivu na kukubali kusoma chini ya mti wa mbuyu.

Mkombe anasema kuwa kuna hatari ya wanafunzi wote wasichana kwa wanaume kukimbilia ziwani kwa ajili ya kupata ajira katika shughuli za uvuvi ambako wanalipwa fedha kidogo kuanzia kati ya Sh 500 hadi Sh 200 kwa kazi wanazopewa ikiwa ni pamoja na kupasua samaki, kutafuta kuni, kuosha nyavu na kukausha samaki.

Anasema kuwa ajira hiyo ni mbaya kwa watoto na ni hatari kutokana na wengi wao kupata ajali mbalimbali ziwani ikiwa ni pamoja na kukamatwa na mamba na kupoteza maisha bado wakiwa na umri mdogo.

"Tunaiomba Serikali iliangalie suala hili la mazingira ya shule yetu ili na sisi tuweze kupata haki ya kupata elimu kama wanavyopata wenzetu ili tuweze kuokoa maisha yetu na kujinusuru na ajira hii mbaya ya watoto katika Ziwa Rukwa kwani sidhani kama kuna watoto wenzetu wengine wanasoma katika mazingira kama haya," anasema.

Mtazamo huo ndio alionao Ngairo kwamba: "Kama unavyoona tunaendelea kuomba wananchi na wadau wa Elimu kutuchangia ujenzi wa shule yetu na na sasa tumeanza kujenga darasa lingine na nyumba za Walimu kwa mchango wa nguvu za wananchi lakini bado tunahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wananchi,wadau wa elimu na Serikalini."

Katibu wa Elimu, Uchumi, Malezi na mazingira wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Chunya, Philipo Mulugo anasema mazingira ya Iboma yanatia uchungu.

"Mazingira ya shule ya Iboma yanatia uchungu sana kwani serikali kupitia ilani ya CCM inapaswa kuliangalia hili na sisi kama viongozi wa chama na wadau wa elimu tunatakiwa kulipokea kwa masikitiko ikiwa ni pamoja na kushiriki kwa kuisaidia serikali katika ujenzi wa shule hii ya Iboma," anasema

"Sidhani kama kuna mtu ambaye atasikia taarifa ya mazingira ya shule ya Iboma ataamua kukaa kimya, basi huyo atakuwa siyo mpenda maendeleo ya elimu na mimi nitakwenda huko kama katibu wa elimu na nitapeleka mifuko ya saruji 10 ili iweze kuwasaidia,"anasema

Mulugo ametoa wito kwa wanachi wa Iboma na wale wa kata ya Kapalala wanaoishi nje kujitoa kwa hali na mali ili kuisaidia shule hiyo kuwanusuru wanafunzi kusoma chini ya mbuyu ili waweze kupata elimu bora.

Lakini Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chunya Maurus Sapanjo amesema kuwa haifahamu hiyo shule na hajawahi kufika katika shule hiyo.

"Kwa kweli lazima niwe mkweli na muwazi siifahamu hiyo shule na wala afisa elimu wangu hajawahi kunipa taarifa ya shule hiyo kwamba kuna shule ina darasa moja na wanafunzi wanasoma chini ya mti wa mbuyu. Ndiyo kwanza nimeisikia kupitia gazeti la Mwananchi na imenisikitisha sana kuona katika wilaya yangu kuna shule yenye matatizo kama haya,"anasema.

Sapanjo anasema kuwa siyo nia yake na hajafurahishwa na taarifa hizo kwani malengo yake ni kuhakikisha baada ya miaka 10 watoto wa wilaya ya Chunya wanafika vyuo vikuu.

Anasema angekuwa anaijua shule hiyo asingekimbilia kujenga shule za sekondari za kata 18 wakati kuna shule ya msingi ina darasa moja na wanafunzi wanasomea chini ya mti wa mbuyu.

"Nimemwagiza afisa elimu wangu pamoja idara nzima ya elimu kuhamia shuleni hapo na kuhakikisha madarasa yanajengwa kwa haraka ili kuondokana na adha hiyo," anasema juu ya hatua alizochukua.

Kuhusu wanafunzi kujishughulisha na uvuvi wa samaki badala ya masomo, amesema msako mkali unafanyika kuhakikisha watoto wote wanarudi shuleni haraka na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wote watakaobainika wanashiriki katika kuwaruhusu watoto wao kufanya kazi ya vibarua ya uvuvi wa samaki na shughuli nyingine ziwani.

No comments:

Post a Comment