Thursday, November 26, 2009

Dk Salim: Ukiona nchi ina matatizo, wa kulaumiwa ni viongozi

Hawra Shamte


Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) Dk Salim Ahmed Salim ambaye ameeleza kuwa nchi inapokuwa na migogoro mingi wanaostahili kulaumiwa ni viongozi.


JITIHADA mbalimbali zinafanyika kuhakikisha kuwa nchi za Kiafrika zinafuata utawala wa sheria na pia kuzingatia haki za binadamu.

Mbali na nhi wahisani, nchi zilizoendelea na hata mashirika ya umoja wa mataifa kusisitiza umuhimu wa utawala wa sheria na haki za binadamu, zipo taasisi huru zilizo ndani ya nchi za Kiafrika ambazo nazo zinashajiisha uwepo wa utawala bora katika nchi za Afrika.

Mojawapo ya asasi za namna hiyo ni taasisi ya Mo Ibrahim ambayo mwanzilishi wake ni Dk Mohamed Ibrahim mzaliwa wa Sudan na tajiri aliyejikita katika masuala ya mawasiliano.

Mjumbe wa bodi ya taasisi ya Mo Ibrahim, Dk Salim Ahmed Salim anasema tatizo la nchi nyingi za Afrika ni ukosefu wa Utawala Bora, katika Makala hii, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) Dk Salim aliyezungumza na mwandishi wetu HAWRA SHAMTE anaeleza jinsi ukosefu wa utawala bora unavyokinza demokrasia barani Afrika...

Swali: Bara la Afrika linakabiliwa na matatizo mengi ya kivita, ya kiuchumi, ya kisiasa na ya kijamii.

Mwasisi wa taasisi ya Mo Ibrahim, Dk Mohamed Ibrahim, raia wa Sudan hivi karibuni alizungumza katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam na kusema kwamba tatizo kubwa la nchi za Kiafrika ni ukosefu wa utawala bora, lakini dhana ya utawala bora ni pana sana, je, wewe unazungumza nini kuhusu dhana hii?

Jibu:Hakuna asiyetambua kuwa Bara hili lina nyenzo nyingi sana, lina kila aina ya mali, rasilimali yetu kubwa kuliko zote ni watu wetu ambao wanafanyakazi usiku na mchana tena katika mazingira magumu.

Kuna kila aina ya madini katika bara letu, dhahabu almasi na kadhalika, pamoja na hayo tuna mafuta pia katika bara letu. Kuna ardhi kubwa sana katika Afrika, kuna mito na maziwa ya kila aina lakini bado nchi zetu, watu wetu ndio wenye umasikini kuliko watu wote duniani.

Kwanini inakuwa hivyo? Kwa kweli hii inatokana na uongozi, kwa hiyo suala la uongozi bora ni suala la msingi, pale ambapo uongozi wa nchi umekuwa na uwezo wa kuhakikisha kwamba wanashughulikia maslahi ya watu wao, kunakuwa na tofauti kubwa.

Katika utoaji zawadi kwa viongozi bora, mchakato unaofanywa na taasisi ya Mo Ibrahim tunaangalia kiongozi alifanya nini kuboresha hali ya watu wake wakati akiwa madarakani.

Bara letu lina matatizo ya kiuchumi, lina matatizo ya rushwa kubwa sana, lina matatizo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, lina matatizo ya uvunjaji wa haki za binadamu.

Taasisi ya Mo Ibrahim inachofanya ni kusaidia mchakato wa kidemokrasia na utawala bora, kwani si kweli kama bara la Afrika ni matatizo tu, si kweli kwamba kila nchi ya Afrika inanuka rushwa.

Kwa kweli kuna juhudi kubwa zinafanyika katika bara letu na mchakato wa kidemokrasia umepiga hatua nzuri pamoja na kwamba mwaka jana na mwaka huu tumepata misukosuko kidogo; matukio ya Guinea kwa mfano ambako wananchi wanauliwa na utawala wa kijeshi, matukio ya Mauritania, matukio ya Guinea Bissau na halafu zaidi matukio ya Somali na matukio ya Sudan.

Kwa mfano Sudan siyo suala la Darfur tu lakini ni nini mustakabali wa Sudan na nini itakuwa taathira ya mambo yanayotokea Sudan kwa bara letu la Afrika.

Kote unapoona kunakuwa na matatizo, kwa kweli wa kulaumiwa kwanza ni uongozi. Pale panapokuwa na uongozi safi, unaojitolea, uongozi usioshiriki ufisadi, uongozi unaojali zaidi maslahi ya watu wake, gurudumu la maendeleo linasonga mbele, lakini pale ambapo viongozi wanajilimbikizia mapesa, wanafanya mambo ya kidikteta na kadhalika, nchi hiyo hata ikiwa na nyenzo vipi haiwezi kwenda mbele.

Swali: Umeeleza kuwa katika maeneo yenye matatizo kama vile ya kivita ni ukosefu wa uongozi, lakini je, nchi kama Somalia ambayo wanapigana wenyewe kwa wenyewe na mpaka sasa inaitwa nchi isiyokuwa na dola je, tatizo ni hilo tu la kukosa uongozi bora?

Jibu:Ukitazama sana matatizo ya Somalia utaona kuwa ni ukosefu wa uongozi. Wanaopigana Somalia hivi sasa ni watu na wanaopata matatizo makubwa ni wananchi wa kawaida. Majemedari wa kivita ni viongozi mbalimbali wa Somalia na hawa walichofanya ni kuweka maslahi yao mbele kuliko maslahi ya watu wao.

Kama kuna nchi ya Kiafrika ambayo haikutegemewa kuwa na matatizo kama haya ilikuwa ni Somalia kwa sababu ni nchi ambayo watu wake wana dini, moja, wana utamaduni mmoja na wanazungumza lugha moja, isingetegemewa kuwa watu kama hao itatokea siku watapigana wenyewe kwa wenyewe, familia moja inaua familia nyingine.

Tatizo la Somalia ni ukosefu wa uongozi bora unaofikiria maslahi ya watu wake, lakini tatizo hilo si la Somalia tu, tazama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ni nchi moja ambayo pakiwa na utulivu, pakiendeshwa utawala bora itakuwa ni chachu ya maendeleo siyo ya Kongo tu bali ya sehemu kubwa sana ya bara la Afrika.

Lakini Kongo haikupata amani kwa muda mrefu sana, ingawa hivi sasa Rais Kabila anajitahidi kujaribu kuleta amani kwa kiwango kikubwa lakini bado kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe, bado kuna watu wanafikiria maslahi yao, namna gani ya kupata fedha kwa njia za haramu kuwa ni jambo kubwa zaidi kuliko jambo jengine.

Swali: Unafikiri ni nini suluhisho la matatizo haya?

Jibu: Sidhani kama unaweza kuwa na suluhisho la namna moja kwa sababu kila pahala na mazingira yake.

Chukulia Somalia kwa mfano, Somalia kuna Al Shabab, hawa wanasema wao ndio Waislam safi na wanataka kuleta Uislam, lakini ni upuuzi mtupu, kwa sababu haiwezekani kuwa brandi yako tu ya Uislam ndiyo iwe bora kuliko nyingine hufiki mbali.

Lakini pia Somalia ilipuuzwa, baada ya matatizo yaliyotokea Mogadishu wakati wa Jenerali Aideed na Marekani kupata msukosuko; wanajeshi wa Kimarekani waliingia kwa dhamira ya kutoa misaada ya kibinadamu 'humanitarian' halafu humanitarian ikabadilika wakaanza kuingia katika mapambano, askari wa Kimarekani wakauliwa katika helikopta yao na wakaburutwa; toka wakati ule Marekani iliitenga kabisa Somalia.

Nakumbuka nilipokuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika, nikienda Marekani naweza kuzungumza tatizo lolote lakini si Somalia, ilikuwa ukitaja Somalia wanakwambia achana nao hao.

Kwa hivyo ni nchi ambayo ilitengwa, Marekani waliitenga lakini na jamii kubwa pia waliitenga, tukaiachia inaendelea tuĆ¢€¦

Jingine ni kuwa viongozi wa nchi ile wakaanza kugawana; Somalia iliyokuwa jamii moja, wakaanza kugawana sasa kuna makabila, ukoo, familia na kadhalika. Ingawa hivi sasa Somalia kuna juhudi zinafanyika lakini juhudi zozote zinazofanyika lazima waishirikishe Al Shabab. Huwezi kupata ufumbuzi wa kivita pale lazima pawe na mazungumzo ya dhati kabisaĆ¢€¦

Kwa DRC juhudi kubwa imefanyika, hali iliyoko DRC sasa hivi tofauti sana na miaka mitatu, minne, mitano iliyopita lakini bado kuna matatizo Mashariki ya Kongo, kwanini? Moja ya matatizo yetu katika bara letu, imekuwa hizi rasilimali tulizonazo, nyenzo tulizonazo, madini tuliyonayo baada ya kuwa faida kwa watu wetu imekuwa kama ni dhambi, kama ni laana, sasa inakuwa pale palipo na mafuta matatizo, palipo almasi matatizo, palipo dhahabu matatizo, mimi nadhani changamoto kubwa ya bara letu ni namna gani ya kugeuza hizi rasilimali, hizi nyenzo tulizonazo, baada ya kuwa ni sehemu ya matatizo iwe ni sehemu ya kuleta maendeleo kwa bara zima na kwa manufaa ya watu wetu.

Kwa upande wa Sudan kwanza tatizo lilikuwa baina ya Kaskazini na Kusini, vita viliendelea kwa muda mrefu sana na watu wengi walifariki, takwimu zinasema watu kama milioni nne walifariki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya Kaskazini mwa Sudan na Kusini mwa Sudan.

Mwaka pale. Mwaka 2005 yakapatikana makubaliano ya kijumla (Comprehensive agreement).

Halafu kuna suala la Darfur, huko nako kuna matatizo makubwa, mpaka hivi sasa juhudi zilizofanyika kujaribu kutanzua hazijafanikiwa.

Lakini hivi sasa hali ya Sudan imekuwa ngumu zaidi na mimi binafsi inanitisha kidogo, inanitisha kwa sababu siyo tu suala la Darfur lakini kuna uwezekano wa kuwa na fujo zaidi kama ndugu zetu wa serikali ya Sudan ya Kaskazini na ndugu zetu wa SPLM hawakuwa na makubaliano ili kura ya maoni ya mwaka 2011 ikafanyika katika mazingira mazuri na halafu wakaheshimu matokeo ya kura ile.

Tatizo lililopo hivi sasa inaonyesha kuwa badala ya kuwa na umoja wa Sudan kuna uwezekano kuwa watu wengine wakataka kujitenga.

Najua kama kuna watu wengine wanafurahia kujitenga, wanasema kujitenga ni nzuri, lakini ukianza suala la kujitenga katika bara letu na hasa katika nchi kubwa kama Sudan kuna taathira zinazoweza kutokea siyo tu ndani ya Sudan lakini pia katika majirani wa Sudan.

Kwa hiyo mimi nafikiri hili jambo la Sudan kwa sasa Jumuiya ya Kimataifa na hasa nchi za Kiafrika zinapaswa kulipa uzito wake na kujaribu kuhakikisha kwamba katika huu muda uliobakia kila jitihada zinafanywa ili kuwafanya wananchi wa Sudan wajione kuwa ni wamoja na hasa ambao wanahisi kwamba wameonewa.

Tatizo kubwa la Sudan ni kwamba wananchi walio katika pembezoni wanahisi kwamba wametengwa (siyo kama hawana sababu) na maslahi yote na maendeleo yote yanatokea katika sehemu moja tu ya Sudan.

Jambo moja ambalo linaweza kuwa zuri ni kujaribu kuibana serikali ya Sudan kuzungumza na ndugu zetu wa SPLM waandae mazingira ili wananchi wa Kusini mwa Sudan watakaopiga kura waseme kwamba jamani tuhakikishe hili suala la umoja linapatikana.

Lakini kama hilo halipatikani basi angalau waandae mazingira ya kuwa huo mchakato wa kura za maoni uwe wa amani na wakubaliane na mapema kama kuna kura ya maoni likitokea hili tutafanya nini, lisiachwe tu kama bomu likapasuka kwa sababu kama hakuna hivyo kuna hatari kabisa kwamba ufikapo mwaka 2011 bila mawasiliano,

bila mapatano bila ushirikiano hali ya Sudan ikaendelea kuwa tete na inapoendelea kuwa tete haitokuwa tu Kusini mwa Sudan lakini itaathiri pia sehemu mbalimbali za Sudan ambazo pia zina matatizo yake, Darfur, Kordufan, Blue Nile na kadhalika.

Swali: Kumezuka mtindo mwengine wa demokrasia barani Afrika, sasa hivi demokrasia mbali ya kuwa ni mchakato wa uchaguzi lakini mwisho wa siku inabidi lazima watu wakae katika meza za majadiliano. Na zimezuka hizi serikali za mseto kama Kenya na Zimbabwe, je, nini maoni yako kuhusu hilo?

Jibu: Kila sehemu ina mazingira yake maalum. Demokrasia maana yake ni kwamba wananchi wenyewe wawezeshwe kuchagua viongozi wao na namna serikali wanayoihitaji na serikali hiyo iwaongoze kwa muda gani na wawe na uwezo wa kubadilisha viongozi wao muda ule unapofika.

Lakini mazingira yatofautiana, kwa mfano; katika Kenya baada ya mauaji yaliyotokea mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na kuleta taathira kubwa kwa maendeleo ya Kenya kulikuwa na umuhimu wa kutafuta usuluhishi na mawasiliano na maafikiano ya namna fulani, kwa hivyo serikali ya mseto iliyoundwa Kenya, ilikuwa na madhumuni hayo.

Ukitazama mazingira yalivyokuwa, ukawa mkaidi tu ukasema hakuna haja ya kuwa na serikali ya pamoja kwa kweli unakosea, unawatakia ndugu zetu wa Kenya waendelee katika maafa tu.

Zimbabwe kidogo tofauti na Kenya, lakini kama wenyewe wamekubaliana, tunapaswa kuheshimu makubaliano. Ukitazama uchaguzi wa Zimbabwe ulivyokwenda, Chama cha MDC katika uchaguzi wa wabunge kilishinda, suala lilikuwa je, uchaguzi wa Rais ulikuwaje? Bahati mbaya mazingira hayakuwa yanaruhusu kufanya uchaguzi ambao ungekuwa huru na wa haki.

Kwa hivyo katika mazingira kama hayo, mimi nadhani ilikuwa ni busara kujaribu kuwakutanisha viongozi ili waweze kuona jinsi ya kuwa na muundo wa serikali ambao utazingatia maslahi ya watu wote wa Zimbabwe.

Na pamoja na kuwa bado kuna matatizo nchini Zimbabwe, lakini nadhani hilo lilikuwa ni jambo la busara. Mimi nadhani pale ambapo kuna ushindani mkubwa sana wa kisiasa na ambapo bado watu hawajaweza kustahmiliana na kuweza kujua kuwa wewe unaweza ukawa chama fulani, mimi nikawa katika chama kingine, hata katika familia moja; baba akawa chama fulani, mama akawa chama kingine na watoto wakawa chama kingine na mkaendelea katika familia bila matatizo; pale ambapo ustahmilivu kama huo haupo.

Ni muhimu sana kufanya utaratibu wa kushirikisha watu wote katika utawala, vinginevyo utaendelea katika mapambano tu na panapo mapambano ni muhali kupata maendeleo ya kudumu ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment