Thursday, October 22, 2009

Urithi aina gani huu tunawaachia watoto?

SIKU moja nikiwa likizo kijijini kwangu, nilikuwa nimepanda gari aina ya Toyota Coaster kutoka mji mdogo wa Ipinda kwenda Kyela. Gari lilijaa abiria.

Tulipofika Kituo Kikuu cha Tenende mwendo wa nusu saa hivi, alipanda kikongwe akisaidiwa na dada mmoja. Inaelekea alikuwa anakwenda hospitalini Kyela.

Kwa kuwa gari ilikuwa imejaa aliamua kukaa sakafuni kwenye gari. Nilipoona vijana wengi ‘wamejikausha’ niliamua kumwachia kiti na kumlipia nauli. Tulipofika Kyela yule mama aliniita na kuniuliza; “wewe ni mtoto wa kiongozi wa dini? Libarikiwe tumbo lililokuzaa.”

Na ni kweli mimi baba yangu (sasa marehemu) alikuwa kiongozi wa Kanisa la Kilutheri kijijini kwetu. Lakini jambo kubwa hapa ni kwamba mimi nilikuwa kijana wa darasa la sita tulipokuwa tunapata uhuru 1961. Malezi ya wakati huo ni kwamba tulikuwa tunamheshimu kila mtu mkubwa kwako kama baba, mama au dada yako. Wote walikuwa walezi wetu.

Tulikuwa tunampokea mzigo au jembe mzee yeyote tunayemwona mbele yetu na kumpelekea nyumbani kwake. Maduka enzi hizo yalikuwa mbali na vijiji, lakini ukitumwa na mkubwa yeyote unakimbia bila kusita. Tuliwaheshimu walimu wetu sambamba na wazazi wetu. Watu wazima, hasa wazazi, wakitoa hewa chafu tulikuwa tayari ‘kununua kesi’ kwa kusema; “ni mimi nilitoa kile ‘kijambo’,” ili kutunza heshima ya mkubwa. Maadili yalitangulia mbele ya vyote.

Maendeleo yaliposhika hatamu nidhamu kwa mtu mzima na mtoto ikazidi kuyeyuka. Mtoto akawa si wa jumuiya tena bali ni mali ya wazazi, na asiguswe na mtu baki kwa kumtuma shughuli yoyote yenye suluba, labda iwe kuendesha ‘balloon’.

Wazazi wetu walikuwa ni wachapa kazi kikweli kweli ingawaje katika mazingira magumu sana. Shule nyingi, barabara na zahanati zilijengwa kwa nguvu ya wananchi (kujitolea) bila kushurutishwa.

Nakataa kabisa kuwa wakoloni walikuwa wanatumia viboko, maana hata baada ya uhuru machifu wengi walihamasisha maendeleo, na kupitia kwa hamasa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kila mwananchi aliona sifa kuchapa kazi kwa bidii.

Mwaka 1965 Serikali ilifuta ada ya sekondari. Na huo huo ndio mwaka niliobahatika kujiunga na elimu ya sekondari. Nilisoma shule ya sekondari iliyojengwa kwenye nyayo za Mlima Rungwe.

Kuna baridi kipindi karibu chote cha mwaka. Pamoja na hali hiyo wanafunzi tulikuwa tunaamka usiku wa manane na kujimwagia maji kichwani na kujisomea, iwe bafuni au darasani – maana walimu wetu walikuwa wanapiga vita kusoma usiku.

Shule hiyo ilikuwa inafundisha vizuri sana. Ikawa tishio. Kwenye miaka ya ’70 Serikali ilibidi itoe zawadi ya gari aina ya lori jipya baada ya shule hiyo kuongoza matokeo kwa muongo mzima.

Kuona hivyo wakubwa serikalini waliwahamishia watoto wao pale. Maadili ya shule yakatoweka. Mashangingi yakaanza kuleta vyakula vya nje ya shule kwa watoto wa wakubwa na pengine kuwachukua kwenda kula wikiendi Mbeya.

Walimu ikawa hawaheshimiki tena. Hapo ndio ikawa mwanzo wa kufifia kwa maendeleo ya Sekondari ya Rungwe, na mpaka leo hii sidhani kama hata kwenye ‘hamsini bora’ kitaifa inakuwamo tena.

Hiyo ndiyo hali halisi ya sasa, eti kwenda na wakati. Utandawazi umetukumba vibaya Watanzania. ‘Uzungu’ umevuka mipaka. Watoto wa kike wanavaa nguo za aibu hata kwenye ibada, hasa makanisani; migongo nje, maziwa nje nusu, wakikaa mapaja yote nje, ni kama wanakuwa robo tatu uchi. Wenzetu Waislamu kwa hilo wameshinda.

Watoto wa kiume kusuka nywele, kuvaa hereni kutoboa masikio na pua na mpaka suruali za sare za shule zinavaliwa chini ya makalio! Walimu nao sasa wamenawa mikono, wanajua wazazi wanatoa baraka hizo.

Nyimbo za ‘Bongo fleva’ matusi matupu yenye kutaja tungi na mikasi (pombe na ngono) ndio kipaumbele. Vyombo husika vipo kimya. Vituo vya redio za kisasa (FM) vipindi vyao ni kuhamasisha ngono tu. Maneno kama mihemuko, kufika kileleni, msononeko ndiyo mafundisho makubwa kila kunapokucha. Hakuna anayekemea.

Wazazi wanafanikisha kununua matokeo ya mitihani kuanzia darasa la saba mpaka vyuoni. Watoto wa ‘wakubwa’ hawataki kufanya kazi za suluba ila kuendesha magari ya kifahari na kuzunguka mitaani, wanashindana katika hayo.

Ni hatari tupu kwa vizazi vijavyo. Wawekezaji wengi wameliona hilo na wanakwepa kuajiri wasomi wa Kitanzania kwani wanasema hawana tija.

Na hakika ni kweli, maana hatuko makini katika elimu ambayo ndiyo urithi sahihi kwa watoto wetu. Kwa kuongea tu na msomi wa kileo utaona upungufu mwngi ukiwalinganisha na wenzetu wa nchi jirani.

Haya sasa, sisi ndio tunaondoka hivyo, watoto wetu hawataki kazi. Aidha ni wavivu au legelege. Starehe kwao na vijiwe ndio muhimu.

Binafsi nachelea sana kuwa tukiwaacha katika silka na hulka hii ya ulegelege, hakika urithi wa namna hii utakuja kuwafanya watumwa kwenye nchi yao wenyewe.


''Mungu Ibariki Tanzania''
Na Lugano Mwamakula Mwansasu
0787198462

No comments:

Post a Comment