Friday, October 16, 2009

MISINGI 25 YA USHIRIKI WA WANANCHI KATIKA KULETA MAENDELEO

Mada hii imeandaliwa kwa ufupi kuchochea fikra na mjadala kuhusu “Ushiriki wa Wananchi Katika Kuleta Maendeleo”; na haki / wajibu wa mwananchi wa Wilaya ya Kyela.


Yapo masuala na mahitaji mengi ambayo kiongozi ama mwananchi anapaswa kuyafanya katika kuleta maendeleo katika eneo lake. Eneo inaweza kuwa ni asasi/taasisi, kijiji/mtaa, jimbo/wilaya nk. Ieleweke kwamba maendeleo yanayozungumzwa hapa si maendeleo ya mtu binafsi bali ni maendeleo ya jumuia/jamii.


Masuala na mahitaji hayo yako katika sehemu kadhaa mathalani haki, wajibu, zana, mikakati, maangalizo, dondoo, stadi, mazingatio, shughuli na kadhalika. Mada hii imeyaweka pamoja masuala na mahitaji hayo kwa pamoja katika mtiririko rahisi na kuyaita jina la pamoja “Misingi 25”. Hivyo misingi iliyoainishwa hapa ni sehemu ya mambo muhimu ambayo mwananchi anapaswa kuyafanya yaweze kumsadia ili kuleta maendeleo katika eneo lake.


Ifuatayo ni misingi ambayo kila mtu katika sehemu yake na nafasi yake anapaswa kuifanya ili kuleta maendeleo;


I. UPATAJI WA RASLIMALI: Upataji wa raslimali ni suala la msingi ambalo mtu anapaswa kulifahamu na kulitilia maanani ili kuweza kuleta maendeleo kutokana na raslimali zilizopo. Hivyo ni wajibu wa kila mtu kufahamu aina, vyanzo na namna ya kupata raslimali. Raslimali ni pamoja na watu, fedha, vitu na hata mawazo. Vyanzo vya raslimali vyaweza kuwa wananchi, serikali, wadau wa kimaendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali nk. Hivyo ni vyema ukawa na stadi au ukatumia wenye stadi za uandishi wa miradi na ukusanyaji wa raslimali. Baadhi ya vyanzo muhimu vya kiserikali ni pamoja na: Pesa za Maendeleo (capital development fund) ambazo zinatolewa kwa idadi ya watu kwa wastani wa dola moja na nusu kwa kila kichwa katika kata; Pesa za PADEP-Participatory Agricultural Development Programme(hizi zinatolewa kwa ajili ya miradi ya kijamii na miradi ya vikundi); Pesa za VVU/UKIMWI kupitia TACAIDS; pesa za mradi wa elimu ya msingi-MMEM; pesa za mpango wa elimu ya sekondari-MMES, pesa za TASAF-miradi ya vijiji/mitaa na mikopo kwa vikundi na vyanzo vingine vingi. Hivi vinashindwa kutumika baadhi ya maeneo kutokana na kutokufahamika ama kutokufuatiliwa ipasavyo. Baadhi ya vyanzo vya washirika wengine wa kimaendeleo ni PACT, SATF, Foundation for Civil Society, GTZ, USAID, FHI, DFID, CARE nk. Kuna haja ya kufuatilia kujua taratibu za kupata ruzuku au kujenga ushirika na taasisi hizi.



II. USHAWISHI NA UTETEZI: Kila mtu anapaswa kuwa na stadi za ushawishi na utetezi kwani hizi ni zana muhimu sana ili kuweza kutekeleza wajibu wa kuleta maendeleo. Uzoefu unaonyesha kuwa kuna watu ambao wameweza kuleta maendeleo katika maeneo yao kutokana na kutumia vizuri stadi hizi. Kwahiyo ni wajibu wa kila mtu kuelewa kuwa ‘ukitaka kuwamba ngoma lazima uvutie upande wako’. Hivyo mwananchi anapaswa kutumia kila fursa ya vikao na nafasi nyinginezo kushawishi miradi ya kimaendeleo kuelekezwa katika eneo lake. Utetezi unahusisha pia kuweza kujenga hoja katika medani mbalimbali kwa niaba ya wananchi wenye matatizo mbalimbali. Stadi za ushawishi na utetezi zinawezesha kujua wajibu huu unatekelezwa namna gani.

III. UHAMASISHAJI NA KAMPENI: Kila mtu anatakiwa kufahamu jinsi ya kufanya uhamasishaji na kampeni. Huu ni msingi muhimu katika kuunganisha nguvu za pamoja kwa ujumla. Pia hii ni zana muhimu katika kutatua masuala yanayokabili halaiki ya wananchi yanayohusika na kubadili fikra na mitazamo. Mathalani kila mtu lazima awe mstari wa mbele katika kupiga vita UKIMWI. Ifahamike tu kwamba UKIMWI ni janga kubwa katika Wilaya ya Kyela hivyo kila mtu kwa nafasi yake lazima ajikinge dhidi ya kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI, pia awe mstari wa mbele kuhamasisha wananchi wengine kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza. Kufanya mikutano ya jumuia ni wajibu wa msingi katika kufanikisha malengo haya.


IV. UFAHAMU WA SHERIA ZA MSINGI: Ufahamu wa sheria za msingi ni jambo la muhimu sana kwa kila mtu. Ni wajibu wa kila mtu kutambua kuwa yeye binafsi ni tegemea la mwingine katika msaada wa sheria. Hivyo kila mtu anapaswa kuzifahamu sheria za msingi ingawaje si lazima kuzifahamu kwa kina sheria zote maana anaweza kutumia misaada mbalimbali ya kisheria katika masuala tata. Chukulia mfano haki yako unapokamatwa na Polisi kama ifuatavyo;
Ø Raia una haki ya kumwomba askari ajitambulishe kwako
o Muulize jina lake
o Muulize namba yake ya uaskari
o Muulize kituo chake cha kazi
Ø Raia una haki ya kujulishwa kwanini unatiliwa mashaka ama unakamatwa.
Ø Raia una haki ya kuwajulisha ndugu, jamaa ama sehemu unakofanyia kazi kwamba ama umekamatwa na polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa.
Ø Raia una haki ya kuomba na kupewa dhamana wakati ukiwa kituo cha Polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa.
o Hutakiwi kutoa fedha kama dhamana uwapo kituo cha Polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa, isipokuwa maelezo utakayoandika.
Ø Raia una haki ya kuwaeleza Polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa kwamba lolote atakalosema linaweza kutumiwa kama ushahidi mahakamani, na asiburuzwe kuandika tu.
Ø Raia una haki ya kuomba Wakili wako awepo kituo cha Polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa wakati unatoa maelezo yako.
Ø Raia una haki ya kuyasoma maelezo yako kabla ya kutia sahihi yako.
Ø Raia una haki ya kudai risiti ya orodha ya vitu vyako / fedha zako ulizozitoa ama kukabidhi kituo cha polisi ama Taasisi ya Kuzuia Rushwa.
Ø Raia kama ni Mwanamke una haki ya kupekuliwa na Polisi wa kike, na iwapo hakuna polisi mwanamke, basi mwananke yeyote na vile vile kwa mwanamume.
Ø Raia una haki ya kufikishwa mahakamani katika muda usiozidi saa 24 tangu ulipokamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi.
Ø Pia , askari polisi hawana haki ya kuingia kwenye gari, nyumba au ofisi ya mtu wanayemtuhumu, kwa madhumuni ya kufanya upekuzi, bila kuwapo kwa;
a) Hati ya upekuzi ambayo hutolewa mahakamani
b) Mashahidi wanaotambuliwa rasmi kisheria, kama vile mwenyekiti / mjumbe wa serikali ya mtaa au mwenyekiti wa nyumba kumi (iwapo mfumo huu unatumika) au
c) Jirani wa mtu anayetuhumiwa au kupekuliwa.
Ø Aidha, mtuhumiwa hatakamatwa au kupekuliwa na askari polisi baada ya saa 12:30 jioni au kabla ya saa 12:30 alfajiri, kwa mujibu wa mwenendo wa makosa ya jinai (Penal Code Act), isipokuwa tu, kama kutakuwa na ushahidi wa kutosha kwamba, kumpekuwa mtuhumiwa kabla ya saa 12:30 alfajiri au baada ya saa 12:30 jioni kunaweza kuleta madhara kwa askari polisi.

V. UFAHAMU WA SERA ZA MSINGI: Kila mtu anapaswa kufahamu masuala ya msingi ya kisera, hasa sera za serikali zinazogusa moja kwa moja makundi maalumu ama wananchi kwa ujumla katika eneo husika kwa kuwa ni msingi muhimu katika kuandaa miradi ya kimaendeleo na kujenga hoja za kupata raslimali katika maeneo hayo.


VI. UPANGAJI WA MIPANGO: Ni wajibu wetu sote kujua stadi za msingi za kupanga mipango au kuwatumia vizuri wataalam. Baadhi ya stadi za msingi ni pamoja na maandalizi ya mapendekezo ya miradi, kuandaa mipango kazi na kutayarisha mipango kazi. Katika mazingira ya sasa, raslimali ziko nyingi na zinapatikana kwa ushindani. Uwezo wa kupanga mipango inayotimiza vigezo ni msingi muhimu kuweza kutekeleza wajibu wa kuleta maendeleo. Pia ni wajibu wa kila mtu kuielewa mipango iliyopo ikiwemo ya serikali ambayo inaigusa eneo lako kwa namna moja au nyingine.


VII. UPANGAJI WA BAJETI: Ukiwa kama mwananchi unapaswa kuelewa michakato ya upangaji wa bajeti hususani bajeti katika eneo lako. Hii ni kwa sababu bajeti ni zana inayoongoza mgawanyo wa matumizi ya raslimali. Hivyo maendeleo ya eneo la kila sehemu yanategemea kiasi ambacho eneo husika limepangiwa katika bajeti za ujumla. Uwezo wa kila mtu kushawishi bajeti kuelekezwa katika eneo lake inategemea ujuzi na ushiriki katika hatua za muhimu za kupanga bajeti.


VIII. UUNDAJI WA ASASI NA VIKUNDI VYA MAENDELEO: Katika muelekeo wa sasa wa kimaendeleo vikundi vinachukuliwa na serikali na wadau mbalimbali kama njia ya msingi ya kuleta maendeleo hususani katika ngazi za chini. Hivyo katika kuzitumia fursa hizi ni muhimu kwa kila mtu kuwa na uwezo wa kuhamasisha vikundi vidogo vidogo kuundwa katika eneo lake hususan wanawake na vijana. Vikundi vinaweza kuundwa kulingana na mahitaji lakini ni muhimu kukawa na vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) pamoja na vikundi vya uzalishaji mali. Ni muhimu pia kwa kila mtu kujiunga na asasi ya kijamii (CBO) katika eneo lake ambayo atashiriki na kuitumia kama mwanya wa kuvuta raslimali ambazo ni mahususi kwa ajili ya mashirika yasiyo ya kiserikali.


IX. KUTUMIA UZOEFU WA MAENEO MENGINE: Ni muhimu kuamua kwa dhati kutumia uzoefu wa maendeleo ya maeneo mengine katika kuleta maendeleo kwenye eneo yako. Kuna msemo usemwao ‘’hakuna haja ya kugundua gurudumu kama gurudumu lipo tayari’’. Msemo huu unamtaka kila mtu kuchota uzoefu katika maeneo mengine na kutumia uzoefu huo ili kuleta maendeleo katika maeneo yake. Yapo maeneo ambayo watu wake wametekeleza wajibu wa kuleta maendeleo kwa namna ya kuigwa, hivyo ni wajibu wetu kubadilishana uzoefu na wenzetu kutoka sehemu mbalimbali kwa kutembelea au kwa mawasiliano au kwa kusoma ripoti mbalimbali za msingi kutoka sehemu hizo.


X. KUTUMIA WANACHAMA: Pamoja na kutumia jamii / chama / kikundi / asasi kama taasisi mwananchi lazima aweke kipaumbele kuwatumia wanachama katika jamii / chama / kikundi / asasi ili kushiriki katika kuhakikisha wanafanikiwa ili chama/kikundi/asasi kiweze kujijengea heshima na kukubalika. Hivyo kushiriki katika shughuli za chama/kikundi/asasi/ jamii ni hatua ya msingi kuweza kuwa karibu na wanachama na hatimaye wanachama kwa upande wao kuweza kujitolea katika kuunga mkono juhudi zinazofanyika kwa ajili ya kuleta maendeleo.


XI. KUTUMIA WATAALAMU: Si misingi yote iliyotajwa humu ambayo mtu atakuwa na utaalamu nayo, hivyo ni muhimu kuamua kwa dhati kuwatumia wataalam mathalani katika kuandaa mipango, kuandika miradi nk. Mtu hapaswi kuona aibu kuhusisha wataalamu katika mambo yanayohusu utaalamu.Kushirikisha wataalamu kamwe si ishara ya udhaifu bali ni suala la mgawanyo wa majukumu kati ya yale ya kitaalamu na majukumu ya kawaida ya mwananchi.


XII. KUTUMIA MAWASILIANO: Uwezo wa mtu kutumia mawasiliano ni msingi muhimu katika kufanikisha wajibu wa mwananchi katika kuleta maendeleo. Inapaswa kufahamu njia mbalimbali za mawasiliano na jinsi ya kuzitumia kwa ufanisi kwa mfano kuandika barua kwa mamlaka zinazohusika na wadau mbalimbali katika kuhamasisha maendeleo katika eneo lako inaweza kufanya maajabu. Hata hivyo kwa masuala makubwa ni vyema mwananchi akatumia njia za mawasialiano ya umma kwa mfano kubandika matangazo na kufanya mikutano ya jumuia. Lakini pale yanapotokea matatizo makubwa ni vyema kutumia hata vyombo vya habari pale vinapoweza kufika. Mathalani tatizo la njaa katika kijiji / mtaa / kata likitokea katika vyombo vya habari mamlaka zinazohusika zinaweza kuingilia kati kwa haraka zaidi kuliko mawasiliano ya chini kwa chini.


XIII. STADI ZA MAHUSIANO: Stadi za mahusiano (interpersonal skills) ni msingi muhimu kuleta maendeleo, hivyo ukaribu miongoni mwetu ni hatua muhimu sana katika kuvutia mipango ya kimaendeleo. Pia baadhi ya miradi hutegemea mahusiano ya ukaribu kati ya wadau wa maendeleo pamoja na watendaji katika asasi hizo, kwahiyo kila mtu achukulie ukaribu wake na mtu mwingine kama daraja la kupata fursa za kimaendeleo katika eneo lake. Vilevile kwa watu ambao wako mbali na maeneo yao yaani nje ya Kyela wajitahidi kuwa karibu na watu walio kwenye maeneo ili kuweza kusaidia katika kuleta maendeleo wanapohitajika.


XIV. KUJENGA MTANDAO NA USHIRIKA: Kuna umuhimu kujenga mtandao na ushirika (network and coalition) hususan kwa watu wote wa wilaya ya Kyela wanaoishi ndani na nje ya Wilaya katika kuleta maendeleo katika maeneo yetu. Mwananchi achambue masuala yanayogusa kijiji / mtaa / kata kwenye maeneo ya jirani ili kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha yanafanikiwa. Hii ni muhimu katika kujenga nguvu ya pamoja katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kimaendeleo hivyo ni budi mwananchi wa Wilaya ya Kyela waishio ndani na nje ya Wilaya kujenga mtandao wa ushirikiano ili kuongeza nguvu ya pamoja katika kushughulikia masuala ya kimaendeleo.


XV. KUTUMIA WADAU WENGINE: Ikumbukwe kuwa kuwatumia wadau wengine katika maendeleo ni jambo la msingi sana kwani wanaweza kusaidia kifedha, mawazo au utaalamu. Ni wajibu wetu sote kwa pamoja kuanza kutambua wadau muhimu waliopo katika maeneo yetu , maeneo jirani na nje ya maeneo yetu katika kuleta maendeleo. Hii ni muhimu kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kuna miradi mingi ya kimaendeleo ambayo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali na wadau kama asasi zisizo za kiserikali, mashirika ya dini na kadhalika.


XVI. KUELEWA MIPANGO YA KISERIKALI: Ni wajibu wa kila mtu kuelewa mipango mbalimbali ya serikali na kuhakikisha mipango hii inatekelezwa katika eneo lake. Baadhi ya mipango ya kiserikali ambayo kila mtu anapaswa kufahamu michakato yake ni pamoja na: Mpango wa uwezeshaji kuanzia vijijini.


XVII. UMUHIMU WA VIKAO: Ni wajibu wetu sote kufahamu kuwa nguvu ya vikao katika kuleta maendeleo ni jambo la muhimu sana. Masuala mengi ya kimaendeleo yanahitaji maamuzi ambayo hufanyika katika vikao, hivyo utaratibu wa kuitisha vikao au mikutano na wanachama / wananchi kwa ajili ya kupata maoni, kutoa taarifa ama kujenga ukaribu itasaidia sana kuleta maendeleo. Kwahiyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anahudhuria vikao vyote muhimu anavyopaswa kuhudhuria ili kuhakikisha maslahi ya eneo lake yanazingatiwa. Kwa upande mwingine kila mwanchi ahakikishe vikao vya kimaendeleo katika eneo lake vinakuwepo ili kufanya maamuzi ya msingi kwa ajili ya maendeleo ya wilaya yetu.


XVIII. KUEPUKA VIKWAZO VYA KITAASISI: Kila mmoja wetu anapaswa kuwa na uwezo wa kuvuka vikwazo vya kitaasisi vikiwemo vya kiserikali katika kuleta maendeleo, vikwazo hivyo ni kama urasimu, kutopewa kipaumbele, tofauti zinazotokana na misimamo na kadhalika. Vilevile mwanachi awe tayari kubuni mbinu za kukabiliana na vikwazo hivi, mbinu za msingi ni kwa mwananchi kufahamu vizuri haki na wajibu wake pamoja na kujua jinsi sheria na sera zinazomlinda. Pia ni wajibu wa mwananchi kujenga ukaribu na baadhi ya watendaji / wataalamu katika taasisi / serikali ili waweze kujikwamua katika vikwazo vilivyopo mbele yao. Kwa upande mwingine wale watendaji wanaoweka vikwazo lazima wachunguzwe udhaifu wao na kuwabana katika udhaifu wao na kuwafanya watimize wajibu wao. Mwananchi atambue kuwa kuunganisha nguvu na wadau wengine ni njia ya ziada ya kuruka vikwazo. Pia mwananchi anaweza kutumia viongozi wa juu zaidi, ili kupata ufumbuzi wa vikwazo na ili kufanikisha hili ni lazima kwa mwanachi kuweka mambo bayana kupitia vyombo vya habari ama njia nyinginezo ili taasisi au serikali kwa ujumla wake iweze kutambua na kurekebisha hali hiyo.

XIX. USHIRIKI, USHIRIKISHAJI NA USHIRIKISHWAJI: Hizi ni dhana zinazorandana ambazo zinapaswa kutumika ili kushiriki katika michakato ya maendeleo katika eneo husika. Kila mwananchi anapaswa kuelewa kuwa ushiriki wake katika kuleta maendeleo ni hatua muhimu kwa michakato hiyo kufanikiwa. Inapaswa pia kutilia mkazo kuwashirikisha wanachama / wananchi na wadau wengine kama msingi muhimu wa kuunganisha nguvu za pamoja. Kwa upande mwingine kila mmoja wetu ahakikishe kwamba anashirikishwa katika mahali ambapo ni muhimu kwake lakini kwa namna moja au nyingine amesahaulika.

XX. KUJENGA IMANI KUPITIA UKWELI, UWAZI NA UWAJIBIKAJI: Kwa ujumla viongozi na wadau wengine wa kimaendeleo katika maeneo mbalimbali wasiwe wepesi wa kupoteza imani na baadhi ya wananchi wao kwani kwa kufanya hivyo kutawafanya wananchi kutoshiriki kwa kikamilifu katika maendeleo. Ni dhahili kuwa ikifikia hali hii itawafanya wananchi wasiunge mkono kikamilifu masuala ya kimaendeleo yanayoratibiwa na viongozi hao ikiwemo katika baadhi ya maeneo kutotoa michango ya kutosha katika shughuli za kimaendeleo hali ambayo itakuwa mbaya sana. Hii ni changamoto kwa kila mmoja wetu kutambua kuwa njia pekee ya msingi ya kukabiliana na hali hii ni kujenga imani kupitia ukweli, uwazi na uwajibikaji. Kuhakikisha kuwa pesa zilizopangwa zinatumika kwa uaminifu ili kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana katika eneo lake.

XXI. NGUVU YA UBUNIFU NA KUCHUKUA HATUA: Hatuna budi kufahamu kuwa katika mazingira ya sasa ya ushindani ubunifu ni msingi muhimu katika kufanikisha kuleta maendeleo katika maeneo yetu, mathalani pesa nyingi za miradi ya maendeleo zinatolewa kwa ushindani. Pia wakati mwingine wananchi wa sehemu nyingine wanategemea fikra za viongozi katika kutoa muelekeo wa kimaendeleo katika maeneo yao, wanasau kuwa kila mmoja anawajibu wa kutekeleza msingi huu na kutoa mchango wa kuleta maendeleo. Si lazima ubunifu wote utoke kwa mtu mmoja bali anaweza kuchota mawazo toka kwa watu wengine na kuyatoa katika sura yenye kuchochea mwamko na kuungwa mkono. Lakini mawazo ya ubunifu pekee hayawezi kuleta maendeleo kama hayakutekelezwa, hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhamasisha na kuchochea mawazo ya ubunifu yaweze kuwekwa katika mipango na hatimaye kutekelezwa. Pia ifahamike kuwa kuchukua hatua na kufuatilia ni nyenzo za muhimu kwa mwananchi kuweza kutekeleza azima iliyokusudiwa. Ukitaka kuanzisha miradi lenga katika ile inayoonekana, na wakati wote jitahidi kuanza kwa raslimali watu. Miradi mingi inatumia mfumo wa “changa, uchangiwe”, hivyo ni vyema mwananchi kuwa mbunifu wa kuanza.


XXII. KUWA MSTARI WA MBELE: Kila mmoja anapaswa kutambua kwamba, kuwa mstari wa mbele ni faida na kwa hivyo kutekeleza wajibu kwa moyo wote na hatimaye kuleta maendeleo katika maeneo yetu. Kwa upande mmoja uongozi na uanaharakati ni faida kwa jamii kwani kwa kupitia mtu mmoja mmoja maendeleo/mabadiliko yanaweza kupatikana ambayo ni manufaa kwa jamii ya sasa na jamii ya baadaye.Hivyo mwananchi anapokuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo inamwezesha kutambulika katika jamii, kukutana na watu/asasi mbalimbali, kupata ufahamu na kupata fursa mbalimbali za ziada.

XXIII. TUMIA MIFUMO/MIUNDO ILIYOPO: Kila mtu anapaswa kuweka mkazo katika kuitumia mifumo/miundo iliyopo kwa kuchambua ni mifumo/miundo gani iliyoko katika eneo lake ambayo anaweza kuitumia. Ukweli ni kwamba katika maeneo mengi ya nchi yetu iko miundo/mifumo mingi ambayo haitumiki ipasavyo ikiwa ni pamoja na wilaya ya Kyela. Kutumia mifumo/miundo iliyopo kutamwezesha mtu kupata matokeo ya kimaendeleo kwa haraka na nafuu zaidi bila kupoteza muda na raslimali za kuanzisha ama kushawishi mifumo mingine.


XXIV. NGUVU YA HOJA: Ni wajibu wetu sote kutambua kwamba nguvu ya hoja ni mhimili muhimu katika kufanikisha misingi yote muhimu ya kuleta maendeleo.Nguvu ya hoja inawezesha mawazo ya kimaendeleo kueleweka na kutekelezwa, hivyo mtu ajenge utamaduni wa kuhakikisha hoja zake zinakuwa na uzito. Ili kuwa na nguvu ya hoja ni lazima kwa mtoa hoja kuwa na taarifa za msingi kuhusu suala analolitolea hoja na kuweza kuthibitisha kwa mifano halisi na kuepusha migongano isiyokuwa ya lazima katika jamii ya Kyela. Kila mmoja wetu anapaswa kuwa mchunguzi ama mfuatiliaji na asiogope uchache mathalani wakati ambapo suala analolisimamia halijatokana na hoja iliyoletwa na wengi. Kila mmoja wetu afahamu kuwa cha muhimu ni ‘’nguvu ya hoja’’ na wala si ‘’hoja ya nguvu ‘’ambayo inaweza kutengeneza nguvu ya kuungwa mkono na kuhakikisha anazungumza kitu chenye uhakika ili kuepuka kudharauliwa au pengine hata kuchukuliwa hatua. Suala la msingi kwa mtoa hoja ni kusoma-sheria, kanuni, taratibu na nyaraka mbalimbali.

XXV. ENEZA TAARIFA NA ELIMU YA URAIA: Ukichambua kwa makini utagundua kuwa chanzo kikuu cha matatizo mengi miongoni mwetu ni kukosa taarifa ama elimu ya uraia. Wapo watu wanaonyanyashwa kwa kushindwa tu kujua haki zao, wapo wanaokosa fursa za kielimu kwa kushindwa kujua wapitie hatua zipi, wapo wajane wanaonyang’anywa mirathi kwa kushindwa tu kujua jinsi ya kusimamia stahili zao, wapo waopoteza maisha kwa magonjwa kutokana na kukosa tu taarifa za msingi, wapo wanaoshindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa kukosa taarifa ya taratibu za kujiunga na kadhalika. Hivyo yapo maendeleo ambayo mtu anaweza kuyaleta kwa kuwezesha tu taarifa za msingi na elimu ya uraia kuenea kwa watu wengine. Hivyo Kila mtu aweke mkazo kwa namna ya pekee sana kuhakikisha taarifa zinaenea na elimu ya uraia inatolewa kwa kila mtu aliye karibu naye. Wote kwa pamoja tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha msingi huu kupitia mikutano ya jumuia, tovuti kama hii ya http://kyelacommunity.blogspot.com, vipeperushi na njia nyinginezo. Kwa upande mwingine mwananchi ahakikishe wadau wengine ikiwemo serikali wanatoa taarifa muhimu na kueneza elimu ya uraia kuhusu fursa na michakato mbalimbali ya kimaendeleo.

''Tukifuatilia misingi hii na Kuitekeleza tutafika mbali''

No comments:

Post a Comment