• Yarejesha mitaa mingi iliyoshikiliwa na CUF D'Salaam-Tanzania Daima
na Waandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi mkubwa katika matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliofanyika nchini juzi.
Mkoani Dar es Salaam, chama hicho tawala kimeibuka na ushindi mnono kwa kupata viti 402 kati ya 448, sawa na asilimia 91, huku wapinzani wakiambulia viti 40, sawa na asilimia tisa tu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema ushindi huo ni mkubwa ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi huo mwaka 2004 ambapo CCM ilipata viti 307 kati ya 387, sawa na asilimia 79, huku kambi ya upinzani ikiambulia viti 80, sawa na asilimia 20.
Alisema matokeo ya vitongiji sita, yamefutwa na kupangiwa tarehe nyingine za uchaguzi kutokana na wagombea kufariki dunia ghafla na maeneo mengine uchaguzi huo kufutwa kutokana na kuvurugika kwa taratibu za uchaguzi.
Hata hivyo, Guninita alisema matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa leo.
Kutoka mkoani Iringa, inaripotiwa kuwa CHADEMA, imefanikiwa kushinda mtaa mmoja wa Kihesa Kilolo "B", kwenye Kata ya Mtwivila Manispaa ya Iringa baada ya kuzoa kura zote kuanzia wajumbe wa mtaa hadi nafasi ya mwenyekiti.
Wakati CHADEMA ikiambulia mtaa huo mmoja, CCM imeshinda katika mitaa 13 kati ya 14 ya manispaa hiyo.
Hata hivyo, wafuasi wengi wa vyama vya upinzani, walipinga matokeo hayo kwa kuzomea, kwa madai kuwa CCM ilifanya hujuma kuhakikisha inashinda uchaguzi huo.
Kutoka mkoani Morogoro, CCM imeshinda mitaa 259 kati ya 274, iliyopo katika Manispaa ya Morogoro Mjini.
Vyama vingine na idadi ya mitaa waliyoshinda kwenye mabano ni CUF (10), TLP (4) na CHADEMA mtaa mmoja.
Hata hivyo katika matokeo ya jumla, vyama vya upinzani vimefanikiwa kuongeza viti witatu zaidi kutoka 12 ilivyopata mwaka 2004 hadi 15 vya mwaka huu.
Kutoka Kahama, mkoani Shinyanga, inaripotiwa kuwa Mtaa wa Korogwe, Kata ya Kahama anapoishi Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo, Hamis Mgeja, umechukuliwa na CHADEMA.
Habari kutoka Shinyanga, zilisema kuwa licha ya kampeni kubwa zilizofanywa na mwenyekiti huyo akiambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Zainabu Kawawa, mgombea Leonard Mayala wa CHADEMA, aliibuka kidedea kwa kupata kura 214, dhidi ya Amos Maganga wa CCM aliyeambulia kura 156.
Kushindwa kwa CCM katika mtaa huo, kumetokana na mizengwe iliyofanywa na chama hicho wakati wa kura za maoni, jambo ambalo liliwakasirisha wapiga kura, hivyo kuamua kuiadhibu CCM kwa kuichagua CHADEMA.
Mkoani Mbeya, taarifa zinasema CHADEMA, imeonyesha taswira ya kulitwaa Jimbo la Mbeya Vijijini katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kupata ushindi mnono katika vijiji vya Mbalizi na Ilembo ambavyo ni ngome ya CCM.
Katibu wa chama hicho Wilaya ya Mbeya Vijijini, Ipyana Seme, alisema mbali na ushindi katika vijiji hivyo, CHADEMA imeshinda vitongoji vya Ndola, Maguzi, Mlimareli na Tunduma Road vilivyopo katika Kijiji cha Mbalizi.Hata hivyo, matokeo ya jumla katika Wilaya ya Mbeya Vijijini, yanaonyesha CCM imepata viti 169, CHADEMA 6 na NCCR –Mageuzi kiti kimoja kati ya 180.
Mbali ya taarifa za matokeo, uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu ambapo watu 30 kutoka mkoani Dar es Salaam, Pwani na Mwanza, wanashikiliwa na polisi kwa madai ya kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa watu 18 walikamatwa katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Mrisho Nyembo ambaye anadaiwa kusababisha vurugu zilizowajeruhi askari polisi mwenye namba E.6401 S/SGT Salaika Zomboko Kiborongwa, D.9490 D/CPL Lucas, F.80884 PC Sultani Bugoro, WP 3706 PC Asha na E.2122 D/C Hashimu.
Wengine ni Msafiri Gasper (31), Seif Ally Masoud (44), Khadija Salum (18), Bakari Hamisi (27), Rashid Hamad (25), Riziki Hamad (23), Hamis Amir (38) na Cleophace Barongo (45).
Kwa mujibu wa Kova, wengine ni Philipo Mikorogoro, Said Rashid (51), Hamisi Lupamba (45), Suleiman Kitamba (35), Funua Ally Funua (33), Gilbert Mushi na Azimio Milinga (39).
Hata hivyo, Kova hakuwataja watuhumiwa wengine wawili akisema bado uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya vurugu katika vituo vya kupigia kura na kujihusisha na vitendo vya uharibifu wa mali.
Aidha, Kova alisema baadhi walikamatwa na vitabu vya orodha ya kupiga kura na kutumia majina mawili tofauti wakati wa kupiga kura.
Kutoka mkoani Pwani, watu watano wanashikiliwa na polisi kutokana na kufanya vurugu zilizoibuka katika maeneo mbalimbali ya uchaguzi.
Mmoja kati ya watuhumiwa hao, anadaiwa kulipiga teke sanduku la kupigia kura na kupasuka hatimaye kura kutawanyika na kusababisha uchaguzi huo kusitishwa hadi hapo utakapotangazwa tena.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma, aliwaambia waandishi wa habari mjini Kibaha kuwa, tukio hilo la kupiga teke limetokea katika Kijiji cha Mgomba, wilayani Rufiji.
Alimtaja anayetuhumiwa kupiga teke sanduku hilo kuwa ni David Malecela (41).
Wengine ni Hassan Hafif (53), Ramadhani Hojaj (45), Mwajabu Mnete na Marvelous Sylvester (30).
Kutoka mkoani Mwanza, inaripotiwa kuwa polisi lililazimika kutumia nguvu ya ziada kwa kufyatua risasi za moto katika vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi katika eneo la Machinjoni, Wilaya ya Nyamagana.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi nchini, Jamal Rwambow (RPC), alimtaja aliyepigwa risasi na kujeruhiwa kuwa ni Emmanuel Tungaraza (17).
“Polisi tulilazimika kutumia risasi kutuliza ghasia hizo, na katika matumizi hayo ya risasi, kijana mmoja alijeruhiwa maeneo ya tumboni, lakini hali yake inaendelea vizuri na kuna watu saba tumewakamata kutokana na vurugu hizo,” alisema Kamanda Rwambow.
Alisema, katika vurugu hizo, gari binafsi la Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Mwatex (OCS), lilipigwa mawe na wafuasi wa vyama vya siasa na kuharibika vibaya. “Mambo yalikuwa mabaya sana katika maeneo haya ya Machinjioni na Mahina shuleni... OCS wa Mwatex gari lake lilipondwa mawe na kuvunjwa vioo, lakini tunashukuru hakukutokea madhara zaidi,” alisema.
Alitaja maeneo mengine yaliyogubikwa na vurugu mkoani humo kuwa ni Wilaya ya Geita, Katoro na Rwamgasa na Kisiwa cha Nyakanyasi Chifunfu ambapo zilitokea vurugu baada ya mfuasi mmoja kutaka kubeba masanduku yote ya kura ili yasihesabiwe.
Taarifa hii imeripotiwa na Ghisa Abby na Anitha Challi, Morogoro, Francis Godwin, Iringa, Herman Meza, Shinyanga, Julieth Mkireri, Pwani na Andrew Chale, Dar.
Monday, October 26, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment