Monday, November 9, 2009

KASHIFA YA RICHMOND HAITAKWISHA BILA KUTAJWA JINA LA MR X

Nimejaribu kufuatilia ripoti ya Richmond na vilevile kutoka katika vyombo vingi vya habari, nimegundua kuwa kashifa hii haitafika mwisho bila kutajwa kwa jina la Mr. X . Mr. X ni jina lililofichika katika kashifa hii lakini limekuwa likitajwa kwa mafumbo tu bila kuwaelewesha Watanzania kuwa huyu ni nani haswa.

Katika kashifa hii ya Richmond na ile ya Kagoda utagundua kuwa wahusika ni walewale. Ukifuatilia kwa karibu sana katika kashifa hizi utakutana na majina matatu ambayo ni ‘’the big three’’. Katika majina haya matatu habari nyingi ukizisoma utafahamu kuwa majina mawili tayari yameshatajwa ambayo ni Rostan Aziz na Edward Lowassa, lakini jina hili moja linaogopwa sana kutajwa kwa madai ya maslahi ya nchi.

Kauli mbalimbali na utetezi mbalimbali ambao unatolewa katika nyakati tofauti pindi jina la Mr. X linapotajwa kwa mafumbo na watu na taasisi nyingi hapa nchini zinanipa mwanya wa kutambua kuwa kuna jina moja tu ambalo likitajwa basi suala hili la Richmond litafika mwisho, lakini bila hivyo kamwe halitakwisha na kama likiisha litaendelea kutajwa mpaka Mr. X atajwe.

Hebu msomaji mwenzangu tafakari uchunguzi wa TAKUKURU ya Dr. Edward Hosea dhidi ya wabunge tena wale wanaopambana na ufisadi. Jiulize kwanini unafanyika wakati huu, jiulize nani asiyepokea posho mbili Tanzania ukianzia na Rais , Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Hosea Mwenyewe? Jiulize kwanini hawakuanzwa hawa kwanza ambao ndiyo vinara. Jiulize kati ya hao hapo juu nani anapotembelea Mikoani, Wilayani na hata vijijini hakirimiwi na Halmashauri ya Wilaya na taasisi husika, na je pesa zao wanazotoka nazo Ikulu na kwenye taasisi nyingine wanazotoka wanazifanyia nini? Jiulize hizo sio posho mbili? Sasa kwanini kwa wabunge pekee na kwanini waanzwe wao? Kwa kujiuliza maswali mengi ukiwahusisha pia Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na hata watendeji wengine serikalini utangundua kuwa uchunguzi huu kwa wabunge unalengo la kuwanyamazisha ili wasiongelee tena suala la Richmond diri ya ‘’the big three’’ kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Hii inaonyesha kuwa sasa wabunge hawa hasa wa kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dr. Harrison Mwakyembe na Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Shelukindo ndiyo inamshika pabaya Mr. X na ndiye anayeamuru sasa wafwatwefwatwe na TAKUKURU.

Hapa ndipo panajitokeza kuwa kwenye kashifa hii kuna jina lingine la mhusika limejificha na halitajwi kwa maslahi ya nchi. Hili jina litasumbua sana nchi hii kama hapatatokea jasiri mmoja kulitaja jina hii bila kutumia mafumbo. Watanzania sasa wangependa kusikia jina hili likitajwa kwa vielelezo ambavyo vimesainiwa au vimemhusisha yeye moja kwa moja na hata kupitia kwa washirika wake yaani Edward Lowassa na Rostam Aziz. Huu si wakati wa kumung’unyamung’unya maneno ni wakati wa kusema tena kwa uwazi. Katika hili najikumbushia enzi zile za Waziri Mkuu Edward Morringe Sokoine, kiongozi aliyekuwa jasiri na ambaye alikata kama msumeno bila kujali aliyemkata alikuwa mkubwa wake wa kazi au la, alipopambana na uhujumu uchumi (Ufisadi) na rushwa na kuwa tayari kufa kwa ajiri ya nchi yake na akafa kweli. Lakini pamoja na kufa bado Sokoine tunaishi naye mitaani katika shughuli zetu za kila siku na hata unapozungumzia maslahi ya nchi. Kila unapozungumzia maslahi ya nchi hii na watu waliojitoa mhanga kwa ajili ya nchi hii huwezi ukatamka maneno yako bila kutaja jina la Edward Morringe Sokoine. Hivyo ni bora kufa kwa kuishi kuliko kufa kwa kupotea.

Kama wazalendo wa kweli wapo na wanajua kuwa siku moja watakufa, kwanini wanaogopa kusema ukweli kuhusu Richmond na Kagoda? Wanaogopa nini? Napenda kuwakumbusha tu kwamba kifo cha Morringe Sokoine wakati ule (1984) kilikuwa cha mizengwe na wala haikuwa ajali kama tulivyotangaziwa. Kwa hiyo watu wote mnaopambana na ufisadi mnapaswa kutegemea kitu kama kilichompata mpambanaji mwenzenu aliyetangulizwa katika haki, lakini kumbukeni kuwa majina yenu,kazi zenu na umuhimu wenu katika nchi hii utadumu milele na utaendelea kuishi pamoja nasi na vizazi vijavyo.

Nachelea kusema kamwe kazi hiyo mnayoifanya haitokani na upeo wenu, bali nyuma yenu kuna nguvu ya Mungu ambaye anawalida kila kukicha. Pasingelikuwepo na nguvu ya Mungu nyuma yenu msingelikuwepo kamwe hapa duniani ndiyo maana ajali za akina Mwakyembe zinapita tu kama pepo za kusi zisizozulu. Kwa imani yangu na mungu wangu ninyi hamtakufa kwa sasa mpaka kazi ya aliyewatuma na anayewalinda ikamilike na wadhalimu waweze kupata fundisho.

Nchi hii imezurumiwa vya kutosha, imeporwa vya kutosha, imehujumiwa vya kutosha, imetapeliwa vya kutosha, imefilisiwa vya kutosha, imeibiwa vya kutosha tena na watu wanaojiita wazawa na wazalendo kumbe mbwa mwitu wanaokula nyama za watanzania huku wakipokezana. Umefika wakati sasa tuseme kuwa Richmond, Meremeta, Kagoda, Tangold ni za akina nani bila kuumauma maneno kama vibogoyo. Hatutaki majina ya Mr. X yatawale uzalendo wetu bali majina halisi ya wahusika wa uovu huu. Watanzania watakuwa tayari kuwalinda kwa njia yoyote dhidi ya wadhalimu hawa wanaofilisi utajiri wetu na kuhamishia mali zetu kwenye nchi zao na za marafiki zao kwa maslahi yao, watoto na jamaa zao.

Nimefuatilia kwa makini sana kuhusu sakata hili, nimeona jinsi gani wabunge waliounda kamati teule ya bunge iliyoongozwa na Dr. Harrison Mwakyembe walivyofuatiliwa, walivyotishwa na wanavyoendelea kuhujumiwa na serikali hii. Nilishituliwa na kauli ya Mheshimiwa Rais akijibu swali la mwananchi kwenye Television na Radio Miezi mitatu iliyopita kwa kusema katika rushwa hana rafiki wala ndugu, kauli nyingine huko nyuma alishasema kuwa uraisi wake hauna ubia na mtu yeyoye. Hii kauli inakinzana na ile iliyotolewa na mbia wake Edward Lowassa aliyeongea na vyombo vya habari na kusema urafiki wake na JK haukuanzia barabarani hivyo hautaishia barabarani kwa sababu ya watu wachache.

Kauli hizi zinanitatiza na kufikiria kuwa kumbe rafiki na mbia wa Urais wa Kikwete ambaye amekuwa akimsema mara kwa mara ni Edward Lowassa. Kuanzia sasa kila nikimsikia Rais JK akijinadi kuwa katika rushwa hana rafiki wala ndugu basi nitajua moja kwa moja anamsema Edward Lowassa. Ingawaje nasita kutambua kama kauli hizi haziwajumlishi marafiki na wabia wengine kama akina Rostam Aziz. Ingawaje Rostam Aziz hana haja ya kutetea urafiki wake na Kikwete kwa kuwa yeye ameunganishwa tu na Edward Lowassa kama mtafuta pesa za dili kama za Richmond na Kagoda na akishazifuma anawaacha maswahiba hawa wawili wamwage wino na yeye kukaa pembeni akiwaangalia jinsi wanavyosulubiwa na wananchi.

Kama ulifuatilia sana kikao cha NEC utagundua kuwa wakati akina Guninita na Kusila na wajumbe wengine wengi wanamsulubu Spika Sita na wabunge wengine na kuwaita wahaini marais wote wa awamu ya pili, tatu na nne walikuwamo na inasemekana walikuwa wakiangua kicheko cha kebehi kuwakejeli wabunge wanaopambana na ufisadi na kulifananisha bunge kama mchezo wa ZE KOMEDY. Sasa jiulize je rais anapambana na rushwa na ufisadi upi wakati anawakebehi wapambanaji wenzake? Hapo hutachelewa kupata jibu kuwa rais hapambani na ufisadi unaofanywa na marafiki na wabia wenzake katika urais bali anapambana na ufisadi unaofanywa na watu wasio kwenye mtandao ambao yeye ni mwenyekiti.

Tazama sasa maazimio ya bunge yaliyofukuzwa na bunge katika kikao cha kumi na sita na kutakiwa kutekelezwa katika kikao cha kumi na saba hayajatekelezwa. Angalia utekelezaji wa mazimio ya Bunge kuwawajibisha mwanasheria mkuu Johnson Mwanyika na katibu wa Wizara ya Nishati na Madini Arthur Mwakapugi ulivyofanyika, unatia simanzi kwa bunge letu tukufu. Achilia mbali kutotekelezwa, bali serikali inazidi kulidhalilisha bunge kwani Spika wa bunge alipohojiwa na vyombo vya habari alivihakikishia vyombo hivyo kuwa lazima maazimio hayo hajadiliwe tarehe 6.11.2009 siku ya Jumatano ambapo hayakujadiliwa mpaka kikao cha kumi na saba kinaahirishwa. Tambua kuwa hali ya serikali kulidharau bunge ilianza kujionyesha pale Wizara ya Nishati na Madini iliposhindwa kuwasilisha maazimio hayo kwenye kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Shellukindo ili yaweze kupitiwa kabla ya kuwasilishwa bungeni ilivyo kawaida kwa kisingizio kwamba Waziri anayebeba dhamana hiyo alikuwa nje ya nchi kikazi.

Kwa mazingaombwe haya ya Richmond ndipo nahisi kuna haja ya kumtaja Mr.X katika kashifa hii ambaye anaonekana ndiye kinara wa kufanya mazingaombwe yote haya ya kuliyumbisha bunge. Nasema ifike wakati huyu mtu atajwa kwa majina yake halisia tunayoyafahamu ili aunganishwe na wenzake katika kashifa hii. Kauli za akina Mwakyembe na Watanzania wengine zilizofichika zitolewe sasa. Bila kulitaja jina hili Watanzania watakuwa hawajatendewa haki na masilahi ya nchi yatakuwa hayajalindwa kikamilifu. Tumtaje Mr. X katika kashifa ya Richmond kwa ubini wake sasa tuinusuru nchi.

Ninapatikana kwa;
atkagema@live.com

No comments:

Post a Comment