Wednesday, November 25, 2009

Tabia za Watoto zinatokana na Makuzi.

Na Africar T Kagema




Makuzi ya mtoto yanaweza kugawanywa katika nyanja kadhaa mfano makuzi ya kimiwili, kiakili, kimaono,kimaadili n.k. Katika makala hii tutajaribu kuona jinzi marafiki wanavyoweza kuathri ukuaji wa mtoto kimaadili. Upo msemo kuwa tabia ya mtu inaweza kueleweka vyema kwa kuzingatia tabia ya rafiki yake au marafiki zake. Msemo huu unatilia mkazo dhana nzima ya kuchagua marafiki wema ili kujenga tabia njema.

Malezi ya mtoto huanzia nyumbani kwa wazazi wake. Kipindi cha awali cha maisha ya mtoto (miaka 0-2) mtoto huishi zaidi katika mazingira ya nyumbani na tabia zake zote hutegemea tabia za watu wa nyumba husika. Baada ya hapo mtoto huanza kutoka na kuchanganyika na watoto wa nyumba jirani pamoja na watu wa vimo tofauti na yake.

Pia kwa hali ilivyo sasa watoto huanza kwenda shule za awali au madrasa (miaka 3-6). Baadaye hujiunga na shule za msingi kuanzia miaka 7 - 14 na hatimaye kuingia sekondari akiwa na umri wa miaka 15-19. Tutaona kuwa umahiri wa stadi mbalimbali kama lugha, michezo,hobi na mengineyo hupatikana katika kipindi ambacho mtoto ameshaanza kuwa na maingiliano na watu wa nje ya familia yake.

Tutakubaliana kuwa wazazi kama waalimu wa mwanzo kabisa wa motto (Nursery Teachers) watahusika sana na mustakabali mzima wa tabia za mtoto wako. Hawa ndiyo wenye jukumu ya kumjengea msingi mzuri wa maadili ya jamii ambapo chimbuko la tabia njema hupimwa kutokana na jinsi mtu anavyoweza kutenda mambo yake kwa kuzingatia maadili ya jamii husika.

Katika nyumba ambayo maadili huchungwa watoto hujifunza pia kuchunga maadili. Marafiki katika familia hizi hulingana kabisa na familia husika katika suala zima la kuzingatia maadili.

Utakapofika wakati wa mtoto kutoka nyumbani na kuingia mitaani tayari kuwa amejengewa msingi ambao utamsaidia kupata marafiki wema. Awali wazazi humsaidia mtoto kuchagua marafiki ambao huwa ni wale wanaotoka katika familia zenye maadili mema.

Msingi huu pia humsaidia mtoto kuchagua hobi nzuri ambazo haziendi kinyume na maadili ya jamii. Izingatiwe kuwa tabia za wizi, uvutaji wa bangi, madawa ya kulevya, utoro shuleni n.k. huigwa na watoto wakiwa katika vikundi. Kama wazazi watawaacha watoto wao bila kuwapa muongozo bora wa namna ya kupata marafiki wema basi wasishangae watoto wao kukosa kabisa makuzi mema katika hii nyanja ya maadili na hivyo kuishia kuwa watu mizigo "liability" katika jamii.

Hivyo natoa wito kwa wazazi kukaa na watoto wao bila kuchoka kung’amua mabadiliko ya tabia zao ili waweze kuzibadilisha mapema kabla hazijazoeleka na kuonekana ni kitu cha kawaida kwao. Ni vema pia kufuatilia mafundisho wanayopewa watoto wawapo shule za awali ili kutambua maadili yanayoizunguka shule hiyo na kuchukua hatua mapema.

Kanisa au Misikiti ni sehemu muhimu sana kwa watoto kuhamasishwa kuhudhuria ili waweze kujifunza maadili ya Mungu. Watoto wanaoshindwa kuhudhuria makanisani au Misikitini huwa wanakosa mengi kwani zile ni sehemu zinazofundisha watoto maadili mema katika jamii. Vipindi kama vya Sunday School kwa wakristo na madrassa kwa waislam ni vipindi vizuri sana katika maadili ya watoto katika umri wao mdogo.

Watoto wakalishwe chini na waelezwe kipi cha kufanya na wakati gani, na kipi cha kutofanya na katika mazingira gabi. Wazazi wasipuuzie na kuacha tabia mbaya za watoto zikiendelea kukomaa, kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha kushindwa kuwarekebisha mara wakiachwa na tabia zao. Kama wazee wasemavyo ‘’mkunje samaki angali mbichi’’, kwani akikauka (akikomaa awezi kufunzika tena).

Watoto wadogo wanahitaji watu wazima ili waweze kuwaongoza na kuwasaidia ili wajifunze tabia na maadili yanayokubalika na yale yasiyokubalika. Wanahitaji pia watu wa kuwasaidia ili wajifunze namna ya kushirikiana na wengine. Jinsi tunavyotoa muongozo wa namna hii inategemea malengo yetu kwa watoto tunaowafundisha, tunataka watoto hawa wawe watu wa aina gani? Je wawe na nidhamu ya woga na kutojiamini au wafundishwe tabia ya kutegemeana na yale yanayokubalika na yasiyokubalika.

Kumuongoza mtoto kunahitaji muda na uvumilivu, ni jambo muhimu sana iwapo mzazi anatumia muda fulani katika kuchunguza tabia na mwenendo na kujitahidi kurekebisha kwa upole. Hasira na ukali havisaidii; kama maji yazimavyo moto, upole hurekebisha tabia ya mtoto haraka sana. Tukumbuke pia watoto ni wanafunzi siku zote, wanahitaji uzoefu kutoka kwetu. Ni juu yetu basi kuwapa kilicho bora na muhimu katika uanafunzi wao.

No comments:

Post a Comment