Monday, November 23, 2009

Mwakyembe akataa kuzungumzia hoja za Rostam Aziz

Fidelis Butahe na Mussa Mkama


MBUNGE wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe jana aliamua kutozungumzia sakata la Richmond, na hasa hoja za hivi karibuni za mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ya kutaka uchunguzi mpya wa kashfa hiyo kwa kuwa ripoti ya kamati teule ya Bunge ni ya uongo na haikuwa na baadhi ya nyaraka muhimu.


Katika siku za karibuni, Rostam amenukuliwa akitaka uchunguzi mpya wa kashfa hiyo ufanyike, akipendekeza kazi hiyo ifanywe na jopo la majaji na kwamba endapo jopo hilo litamkuta na hatia, atakuwa tayari kujiuzulu nyadhifa zake zote, hoja ambayo imepingwa kwa maelezo kuwa maamuzi ya Bunge hayawezi kuchunguzwa upya na muhimili mwingine wa dola.


Dk Mwakyembe, mmoja wa wabunge wanaojilikana kama makamanda wa vita ya ufisadi, ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo teule ya Bunge ambayo ripoti yake ilisababisha Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu na mawaziri wengine wawili.


Lakini jana, mbunge huyo wa Kyela alikataa kata kata kuzungumzia suala hilo pamoja na hoja za Rostam.


Dk Mwakyembe aliombwa kuzungumzia suala hilo wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa Mfuko wa Maendeleo wa Watu wa Kyela (KDF), uliofanyika Chuo Cha Ufundi (Veta) jijini Dar es Salaam.


"Hapana siwezi kuzungumza lolote leo hapa ni masuala ya KDF tu... nisingependa kuzungumza mambo ambayo sikupanga kuyasema na wala hayahusiani na mkutano huu,"alifafanua na Dk Mwakyembe.


"Nimetoka Mbeya leo na kule kuna ugeni wa Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa, lakini watu wa Kyela wameniambia nije kwa sababu ya umuhimu wa mkutano huu. Kwa hiyo siwezi kuzungumza mada iliyo nje ya mkutano huu, samahani sana."


Mwenyekiti wa KDF, Gray Mwakalukwa alisema katika ufunguzi wa mkutano huo kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuchangia juhudi za serikali katika maendeleo hasa katika elimu.


"Tangu kuanza kwa mfuko huu mwaka 2006 hivi sasa Kyela kuna maendeleo makubwa, hasa katika sekta ya elimu... sasa kuna shule nyingi za sekondari tofauti na kipindi cha nyuma," alisema Mwakalukwa ambaye pia ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na ambaye alikuwa kamishna wa madini.


"KDF imefanya mengi Kyela, ilinunua vitanda 60 kwa ajili wa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Kiwira Coal Mines, lakini pamoja na hayo tumefanya mengi sana ambayo kuyasema yote inahitaji muda wa kutosha."

No comments:

Post a Comment