Friday, November 20, 2009

WANUFAIKA, WAATHIRIKA NA WANUSURIKA WA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Na. M. M. Mwanakijiji

Katika sehemu ya kwanza tuliangalia kwa ujumla kuwa utawala wa kifisadi unaonekana katika maeneo makubwa matatu yaani kisheria, kiuchumi na kisiasa. Tukatambua kwamba ili utawala wa aina hiyo ufanikiwa ni lazima upenye katika maeneo hayo matatu na mabadiliko yoyote ya kuumomonyoa utawala huo ni lazima yalenge kugusa maeneo hayo matatu. Tumeuangalia kwa nje utawala huo na pole pole katika sehemu hii ya pili tujaribu kuangalia utawala huo kwa karibu na kuangalia ni vitu gani hasa vinaustawisha utawala huo kiasi cha kuweza kutengeneza mfumo unaofanya kazi na watu wakaishi ndani yake na kukubali kama namna ya maisha yao (lifestyle).

Mfumo wa utawala wa kifisadi hausimami hewani na hautokei kama ukungu asubuhi au umande wa alfajiri. Ufisadi hujengwa na kutengenezwa pole pole katika jamii kwa kuanzia katika sehemu au maeneo madogomadogo na pole pole kuanza kupenya kwenye maeneo mbalimbali ya maisha na kuwa ni sehemu ya utamaduni na hatimaye kuwa mfumo uliorasmishwa de facto.

Ufisadi (mfumo) hujengwa na WATU.

Kama nilivyosema hapo juu ufisadi hautokei hivi hivi tu na hatuwezi kumsingizia shetani; ufisadi hujengwa, hupaliliwa, na kulelewa na watu. Lakini siyo watu hivi hivi tu bali kuna mazingira yanayowatengenezea watu hao sababu ya kuanza kujihusisha na vitendo vya kifisadi na matokeo yake kuanza kujenga utamaduni wa kifisadi ambao huanza kuchimbwa na kusimikwa taratibu katika sheria, siasa na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kimaisha kijumla.

Katika mfumo huu wa kifisadi watu hugawanyika katika matabaka kama ilivyo katika mifumo mingine ya kimaisha iliyopo duniani. Kwenye utumwa wapo mabwana na watumwa; kwenye ubepari wapo manyonyaji na wanyonywaji, n.k Kwenye ufisadi kuna matabaka makubwa matatu ambayo yanaingiliana na kuhusiana kila siku na hivyo kuendelea kufanikisha kwa namna ya kila mmoja wao kudumisha na kukoleza mfumo huu dhalimu wa utawala wa kifisadi.

Makundi hayo ni Wanufaika, Waathirika na Wanusurika wa ufisadi. Na ndani ya kila kundi kuna makundi madogo madogo ambayo ndiyo yanaunda kundi hilo kubwa.

WANUFAIKA WA UFISADI

Kundi hili linajumuisha watu wote ambao moja kwa moja (directly) wananufaika na uwepo wa mfumo wa kifisadi. Kama tukitumia mfano wa shamba, basi wanufaika ni wale wakulima waliolima shamba la ufisadi ambamo ndani yake wakapanda mazao mbalimbali. Ni wao ndio huvuna na kunufaika moja kwa moja na mavuno ya matunda ya shamba lao. Siyo tu wao ni wamiliki wa shamba hilo, bali ndio wakulima, wavunaji na walaji wa kwanza wa matunda ya ufisadi. Kundi hili linajumuisha makundi madogo mawili.

WANAONUFAIKA MOJA KWA MOJA

a. watawala serikalini

Hawa ni wale wanaosimama kama wenye madaraka serikalini; ni viongozi wa ngazi za juu katika nafasi mbalimbali kuanzia Ikulu, Mahakama, Majeshi, vyombo vingine vya usalama, n.k Tunapozungumzia watawala hatuzungumzii wafanyakazi wa serikali au maafisa wa ngazi za chini; la hasha! Tunazungumzia kundi lile la watu wenye uamuzi juu ya maisha yetu, sera gani tufuate, tutozwe kodi kiasi gani na tusipolipa tuadhibiweje; hela zetu ziende wapi na kwanini, ni wale wenye uamuzi kwa kweli juu ya hatima ya maisha ya mtu mmoja mmoja kama vile wana uamuzi wa mwisho juu ya maisha ya jamii nzima.

Nilipoliingiza hili neno “watawala wetu” sikuwa namaanisha ni watawala wetu “kisiasa” kama ambavyo tumekuwa tukiwaita zamani tukimaanisha “viongozi” bali ni watawala wetu wa jumla ya maisha yetu. Ni wao ndio wanatuamulia barabara gani zijengwe, shule zetu ziweje, mwekezaji gani apewe nini na kwa muda gani. Hili ndilo kundi la kwanza la wanufaika wa ufisadi. Ukifikiria sana utaona kuwa hawa ndio watu wana nguvu zaidi katika maisha yako kuliko hata familia yako au wale unaowapenda; na yawezekana tunawaona au kuwadhania kuwa wana nguvu kuliko Mungu.

Hawa Watawala wametujaza fikra za kujiona duni na tusiojua kiasi kwamba wametengeneza utegemezi mbaya wa kifikra juu yao. Ndani yetu tumejawa fikra ya “serikali” kama dudu fulani lenye kumiliki maisha yetu na lenye kuamua matokeo ya maisha yetu; dudu hili serikali basi “likisema” au likifanya jambo basi watawaliwa hawana budi kukubali kwani kupinga kokote kule kutaambatana na matokeo mabaya.

Ni roho hii ya kujiamini iliyosababisha kwa muda mrefu watu kukubali maelezo na visingizio vya “serikali” pale ambapo mambo hayaendi sawasawa. Ikafikia mpaka mahali watu walishindwa kuhoji zaidi. Watawala wakapewa ufunguo wa maisha yetu kiasi kwamba katika upotovu wa fikra zao walikuwa ni kama wakoloni tuliowakataa; wakitukebehi hadharani, wakitutukana kama watoto wadogo na wengine hata kutuzaba vibao utadhani vile vya “kelbu” vya mbwa.

Watawala ndio wanufaikaji wa kwanza wa mfumo huu wa kifisadi na kutokana na hilo haiwezekani kwa wao kuubomoa au kuuvunja vunja mfumo unaowahakikishia uwepo wao usiokoma na chakula chao na cha watoto wao. Tukielewa ukweli huu tutambue ni kwanini kundi la wanufaika wa ufisadi walioko serikalini siyo wa kuwategemea kuutokomeza mfumo wa ufisadi. Hawawezi kukata tawi wanalokalia.

b. Chama tawala

Katika mfumo wa ufisadi mahali popote duniani ni chama tawala kilichounda serikali ndiye pia mnufaika wa kwanza na wa moja kwa moja wa mfumo wa utawala wa kifisadi. Ukweli huu ulionekana Mexico chini ya Utawala wa Chama cha Mapinduzi cha Mexico kwa karibu miaka 70, na ni ukweli unaonekana huko Syria chini ya utawala wa Baath, na ndio ulionekana kwa muda mrefu katika utawala wa Kikomunisti wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi. Ni ukweli pia ulionekana kwa miongo karibu minne ya utawala wa chama cha Baath cha Iraq chini ya Sadam Hussein.

Katika mfumo huo wa utawala wa kifisadi mafanikio ya mtu au kikundi cha watu yanahusishwa moja kwa moja na uwepo wao au ushiriki wao katika chama tawala. Kwa wao hao chama tawala ndio mlango rahisi, wa haraka na wa uhakika wa kuwahakikishia mafanikio yao na usalama wa maisha na mali yao. Hivyo, chama tawala katika utawala wa kifisadi hutukuzwa kuliko Bunge, Mahakama, au Urais; chama tawala kiko juu ya vyombo vingine vinavyofanya kazi katika nchi ya utawala wa sheria na demokrasia.

Hivyo, katika mfumo huo wa kifisadia wanachama waandamizi wa chama tawala ndio wanaonesha mafanikio ya mfumo huo. Hawa ndio wabebaji wa kwanza na watetezi wa sera mbalimbali za chama chao na hivyo zawadi ya utii na kujitoa kwao kukitetea chama chao huzaa zawadi ya mafanikio katika mambo mbalimbali. Utawakuta ndio wao wabia wakuu katika makampuni mbalimbali, wananunua viwanja vya ujenzi kwa njia rahisi kuliko mtu mwingine, wanapata taarifa za ndani za mambo mbalimbali yenye manufaa katika biashara zao na hupewa kipaumbele wao na watoto wao (wakati mwingine hata wajukuu) katika nafasi mbalimbali za mafanikio.

Ukitaka kujua kama kweli mfumo wa kifisadi unanufaisha chama tawala, angalia wanachama wake wakuu wana mafanikio gani na jinsi gani wamepata mafanikio hayo, halafu sogea pande zote nne za huyo mwanasiasa na uone jinsi gani watu wa karibu yake nao walivyofanikiwa.

Katika Tanzania basi mfumo huu unanufaisha chama tawala; CCM. Mtu yoyote akitaka kunufaika na kufanikiwa pasipo shaka au kuvutia udadisi usio wa lazima ni lazima ahusiane kwa namna moja au nyingine na Chama cha Mapinduzi. Ukitaka mambo yako “yakunyokee” jiunge nacho; ukitaka usisumbuliwe sana naserikali yake toa michango ya hapa na pale; ukitaka ukumbukwe katika “ufalme” wao hakikisha hukosi unapoitwa na wakubwa wake.

Ukitaka wakutambue uwepo wako jioneshe kuwa ni “mkereketwa”. Nunua nguo kadhaa (na kofia) za kijani na manjano; wakishangilia “CCM, CCM” hakikisha sauti yako ni ya juu zaidi; hata kama unajua kuna madudu ndani ya chama hakikisha “hukichafui” chama bali laumu watu wengine na vitu vingine nje ya chama na ukitetea chama kwa mujibu wa Ibara ya 15:1 ya Katiba ya CCM.

Ukifanya hivyo na kujionesha mapenzi yako yasiyo na shaka kwa CCM basi jiandae kwa neema; jiandae kwa “wema na fadhili” kutoka CCM. Utafanya mambo yako kwa uhakika, utaendesha biashara zako bila kubughudhiwa sana, utawaona na kukutana na vigogo ambao watakufungulia milango ya ajabu ilimradi tu uendelee kutukuza chama tawala.

Na katika hilo utaona kuwa CCM itaendelea kutimiza lengo lake la kushinda uchaguzi na kushika serikali. Wataendelea kutunga na kusimamia sheria ambazo zinawahakikishia kuwa wao ndio watawala milele; hawatabadilisha muundo wa tume ya Uchaguzi ili iwe huru zaidi; hawatabadilisha sheria ya uchaguzi ili kuhakikisha nafasi sawa kwa vyama vyote, hawataruhusu wagombea binafsi, na kwa hakika kabisa watahakikisha kuwa Bunge halipati nguvu ya kuweza kutishia uwepo wa serikali yao madarakani. Itatengeneza mbinu na mikakati ya kushinda chaguzi mbalimbali, haijalishi wanafanya vipi au kwa namna gani. Watashirikiana na watumishi walioko serikalini katika kuhakikisha kuwa mambo yanakuwa vizuri. Mtumishi yoyote atakayejaribu kuonekana yuko huru au anataka kutoipendelea CCM atapewa onyo lisilo na utata naye atanywea kama jani la mgomba lililokatwa na kutupwa nje katika jua la kiangazi.

WANAONUFAIKA KWA NJIA NYINGINE

Katika mfumo huu wapo wanufaika wengine wa ufisadi ambao kwao mfumo huu unawahakikishia maisha yao na hivyo hawana maslahi ya kuubomoa au kuuvunja vunja. Ni wanufaikaji wa pili wa mfumo wa utawala wa kifisadi na maslahi yao yamefungamana moja kwa moja na uwepo wa mfumo wa utawala wa kifisadi (MUK). Wanufaika hawa wa MUK ndio kwa namna moja wanachochea sana uwepo wa mfumo huu na ni kama mbolea ya kuurutubisha mfumo huo.

a. Wawekezaji wa Kimataifa

Hawa hujionesha kwa kuingiza makampuni ya kibepari ya kimataifa ambayo lengo lake kubwa ni kuchota raslimali kwa ajili ya makampuni yao mama huko kwao. Hawa hawaji kwenye nchi yoyote kirahisi rahisi; wanakuja baada ya kuhakikishiwa mambo kadhaa ambayo hutumika kama chambo cha kuyavutia makampuni haya. Mambo hayo katika Tanzania yamepewa jina la “mazingira ya kuvutia wawekezaji wa kimataifa”.

Sasa mazingira tunayowatengenezea hawa wawekezaji ambao miongoni mwao ni makuwadi wa ufisadi wa kimataifa ni yale ya kuwakaribisha kwenye raslimali zetu muhimu zaidi hasa madini, mafuta, maliasili na fedha. Ili waweze kuingia katika nchi kama ya kwetu tunatakiwa kufungua milango yetu, kuwahakikishia mambo kadha kadha wa kadha kama kusafirisha kwa asilimia mia moja faida wanayopata nchini, kutatua migogoro ya kibiashara katika nchi zao, uwezo wao wa kuajiri watu wa kwao hata katika nafasi kama za kwetu, na kuwahakikishia kuwa ije mvua au jua hatutataifisha au kuingilia kazi za makampuni yao nchini. Na wakati mwingine (kama walivyofanya Bulyanhulu, Buzwagi, Tarime, na sasa Loliondo-kama ilivyokuwa miaka ya tisini) wanataka tuwahakikishie kuwa tuko tayari kuwatimua wananchi wetu (kama nitakavyoonesha hapa chini) kutoka katika ardhi yao ili “kuwapisha wawekezaji”.

Hawa wanapoanza kuzalisha watatumia kila mwanya kutorosha mabilioni ya utajiri wa urithi wa watoto wetu kwenda kwenye nchi zao kujenga maisha ya watu wao kama walivyofanya wakati wa Ukoloni na wakati wa Utumwa. Kama vile makampuni ya watawala wa Kikoloni leo hii makampuni ya kimataifa kutoka kwa nchi zilizoendelea yanaendelea kufanya kitu kile kile nacho ni kupenya katika nchi maskini, kuwaahidi mbingu lakini kuwaacha wakiwa jehanamu.

Nchi yenye kutegemea MUK imejiambia katika fikra zake na kuamini kwa dhati kabisa kuwa bila ya kulegeza masharti na kufungua mlango kwa hawa wawekezaji basi nchi haiendi. Hivyo, kwa jina la “ubinafsishaji” Tanzania ikafungua mlango wake kwenye TTCL, Tanesco, Buhemba, NBC, Dawasco, ATCL, TRL, n.k na kuwakaribisha wageni kuendesha nchi kwa namna ya kushangaza. Na watawala wakithibitisha kuwa wao ni watumishi wazuri wa ufisadi hawafikirii njia nyingine ya kutatua matatizo haya isipokuwa kuendelea kupiga magoti mbele ya mafisadi wa kimataifa kama machangudoa mbele ya wateja wao.

b. Wafanyabiashara wakubwa

Wanufaika wengine wa MUK ni wafanyabiashara wakubwa ambao katika mazingira ya mfumo huu faida yao inahakikishwa. Wafanyabiashara hawa ndio ambao kwa kiasi kikubwa hujijengea utajiri mkubwa na wa haraka haraka wakiwa na uhakika wa usalama wao na wa mali zao. Wafanyabiashara wa aina hii kama wangekuwa na uwezo wangetaka nchi isiwe na sheria yoyote na vitu kama kodi, sheria za mazingira, haki za wafanyakazi n.k zisingekuwepo na wao wangeruhusiwa kufanya wanalotaka.

Lakini kutokana na kuelewa kuwa ufisadi ndio utawala wenyewe basi wafanyabiashara wa aina hii wanatumia mapengo mbalimbali ya kiutawala na kiungozi ambayo yamejitokeza kwa wao kupanua biashara zao mbalimbali na hata kujenga himaya za biashara.

Wanaponogewa na hili utaona kuwa wafanyabiashara hawa wanataka kunufaika mara mbili na hapo hujiingiza kwenye siasa na kuanza pia kushiriki katika kutunga sheria na kusimamia sheria ambazo zinagusa biashara zao. Matokeo yake utakuta wafanyabiashara wamegeuka wanasiasa na katika kofia zao mbili hizo wanauwezo wa kujua na kufanya lolote.

Ni kwa sababu hiyo basi utaona kuwa mahali penye MUK wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa wamefungamana sana kama chanda na pete na wanategemeana sana kama vile mti na matawi yake. Mtu yeyote ambaye atajaribu kupendekeza mabadiliko yoyote yale atapata mapingamizi makubwa toka kwa wanasiasa na wafanyabiashara wa aina hii.

Ili kutuliza munkari wa watu wafanyabiashara hawa hujikuta wakimwaga misaada ya hapa na pale ili kupunguza maumivu kwa watu (hasa waathirika). Katika biashara zao watatumia mazingaombwe ya hapa na pale kuendelea kuvutia wateja huku wakichuma faida ambayo ikiangaliwa kwa karibu utaona ni kama kufuru. Lengo lao ni kutengeneza jina jema mbele ya jamii. Lakini hawa hawatapigia kelele mabadiliko ya kiutendaji au kisiasa kwani yaliyopo yanawafaa sana.

Katika MUK wafanyabiashara wakubwa hutengeneza utajiri wa kutisha kwa njia za mchoromchoro, ukwepaji kodi, uvunjaji mbalimbali wa sheria na wanayafanya yote haya wakati mwingine kwa kushirikiana na makuwadi wa ufisadi wa kimataifa (wawekezaji uchwara). Hawa wanasukumwa (kama mabepari wengine) na lengo la kupata faida kwa njia yoyote ile (by any means necessary).

Hata hivyo kundi la wanufaika wa mfumo wa utawala wa kifisadi mahali pote duniani ni dogo sana ukilinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo. Mara zote ni kikundi cha watu wachache lakini chenye nguvu kubwa ya kiuchumi, kisiasa na madaraka.

Vile vile lipo kundi la wanufaika wa mfumo wa ufisadi ambao naweza kuwaita ni machangudoa wa ufisadi. Hawa nimeandika makala inayojitegemea juu yao.

WAATHIRIKA WA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Pamoja na wanufaika wa ufisadi, katika mfumo huu dhalimu wapo waathirika wa mfumo wa ufisadi. Hawa ni wale ambao kutokana na uwepo wa mfumo wa ufisadi wanajikuta wakinyanyaswa katika nchi yao, wakipata kibarua cha ziada kupata nafasi ya kufanikiwa na mara zote huishi kama wahamiaji au wapangaji ambao hutegemea mara zote kupiga magoti na kuomba omba mbele ya wanufaika wa mfumo huu.

Kundi hili mara zote huombea wale wanufaika wa ufisadi watawakumbuka na kuwasaidia au kuwarahisishia kwa namna fulani kupata nafasi ya wao nao kufanikiwa. Kundi hili katika nchi zote duniani ni kubwa zaidi na huundwa na watawaliwa. Hawa ni ndio watu wengi zaidi katika nchi. Tuangalie baadhi ya makundi yanayojikuta yakiathirika katika mfumo huu wa kifisadi.

1. WAKULIMA

Hakuna waathirika wakubwa zaidi wa mfumo wa kifisadi kama wakulima. Hawa ambao ni wengi wanajikuta wanakabiliwa na athari kubwa za ufisadi kwa sababu kubwa tatu. Kwanza, bado wanatumia pembejeo na nguvu kazi ya kijima. Hutumia nguvu nyingi kuzalisha kitu kidogo na wengi wao bado hulima kilimo cha kujikimu (subsistence farming) na ni kile kidogo cha ziada ndio hutegemea kwa mauzo. Pili, wengi wao wako vijijini ambako miundo mbinu ya uhakika bado ni ya kijima. Bado wakulima wetu husafiri umbali mrefu, hutumia muda mwingi, na huhenyeka katika kuhakikisha kuwa mazao yao yana ubora na hatimaye kumfikia mlaji au mnunuzi. Tatu, wakulima wetu wengi bado hawana ufahamu na uelewa wa mahusiano mbalimbali ya siasa, uchumi, maisha, na kilimo chao. Bado wanawategemea wanasiasa kuwaambia nini cha kufanya na jinsi gani ya kukifanya. Matokeo yake wamekuwa wakijikuta wakirubuniwa, kuzugwa na mara kadha wa kadha kuvutiwa na maneno matamu na ahadi hewa.

Mahali pote duniani ambapo mfumo wa kifisadi umekomaa, wakulima hulisha mafisadi na huhimizwa kuzalisha zaidi lakini wakati huo huo kuwekwa nje ya mduara wa madaraka. Huombwa kura zao kila chaguzi zikifika, na husauliwa hadi uchaguzi mwingine. Hawana nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa siasa zao kwani hufanywa duni na watawala na kuoneshwa kuwa wao ni “washamba”. Tumefika mahali ukulima umekuwa ni kama kazi ya fedheha na aibu kiasi kwamba vijana wetu wengi sasa na hata watu wazima hujaribu kutafuta sababu ya kuachana na kilimo na kukimbilia mijini kutafuta shughuli nyingine mbadala ya kilimo.

2. WANAWAKE NA WATOTO

Waathirika wa kwanza wa mfumo huu wa kifisadi ni kundi la kina mama na watoto. Kundi hili linabeba athari za moja kwa moja za ufisadi kwanza kutokana na kutokuwa katika nafasi za juu ya madaraka, biashara, na mahali pa kufanya maamuzi ya kubadili mwelekeo wa taifa na pili kutokana na mfumo dume ambao umejenga utamaduni wa manyanyaso dhidi ya wanawake.

Hatuzungumzii wanawake “wote” kwamba wanapata athari za moja kwa moja kwani wapo wanawake ambao ni sehemu ya wale wanaonufaika na mfumo uliopo sasa; wanawake tunawaozungumzia kwanza ni wale kina mama wa kijijini ambao ndio nguvu kazi kubwa zaidi iliyopo nchini ambayo bado inatumia mbinu na zana za kizamani huku ikiwa imebebeshwa majukumu makubwa ya malezi ya familia.

Kundi hili halina wasomi wengi, na wale wachache waliopo wanajikuta wanaangukia kwenye kundi la tatu la matabaka yaliyopo kwenye MUK. Hili ni kundi la kina mama na kina dada ambao kutokana na matatizo mbalimbali hawakuweza kupata nafasi ya kuendelea na masomo, walijikuta wakianza maisha ya malezi ya watoto mapema, na wale ambao kutokana na tamaduni na mila za mahali walipo wanajikuta hawana sauti ya maamuzi ya mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao.

Japo kuna juhudi katika Tanzania ya kuwaongezea wanawake nguvu zaidi kama vile uanzishwaji wa vyama vya kukopa (SACCOS), benki ya wanawake, asasi mbalimbali n.k bado tunaweza kuona kuwa nguvu ya maamuzi (power to decide) inabakia mikononi mwa watu wachache ambao wengi wao bado wanaangukia katika kundi la wanufaika wa ufisadi. Kina mama hawa kama ilivyo sehemu nyingine zenye MUK huwa wanatulizwa na vitu mbalimbali vinavyowafanya watulie na wasiwe na muda kupiga kelele ya mabadiliko.

Athari zinazowakuta kina mama hawa ni ukosefu wa huduma bora na za kina za kijamii na kimaisha, kuendelea kuishi maisha duni ya kutumia muda mrefu wa siku kutafuta kuni, maji, na chakula, na vile vile kufuatilia maisha ya maendeleo ya familia. Kina mama kama hawa hata wale walioko mjini hujikuta hulazimika hata kujidhalilisha na kujifanya duni ili waweze kuokoa maisha ya familia zao na kutoa msaada wa kifamilia.

Watoto wao wanajikuta wanapata athari za ufisadi kwa sababu vitu vingi ambavyo vingeweza kufanywa na watoto katika kuwaandaa kwa maisha bora vimeachwa kufanywa au kufanywa kiuvivu na kwa uzembe. Nitolee mfano hali ya lishe (nutrition) kwa watoto wetu katika Tanzania katika nchi ambayo ina ubwelele wa nyama, maziwa, samaki, mboga, matunda, na nafaka nyingi tu.

Takwimu mbalimbali za hivi karibuni (angalia ripoti ya REPOA kuhusu lishe kwenye mwanakijiji.com sehemu ya vielelezo) zinaonesha kuwa asilimia 40 ya watoto wetu chini ya miaka mitano wamedumaa – urefu wao hauendeni na umri wao (stunted) na hiyo ni mojawapo ya ishara ya lishe ya kiwango cha chini; asilimia tatu wana uzito wa chini ukilinganisha na urefu wao – dalili ya utapiamlo wa hali ya juu, na karibu asilimia 22 ya watoto wetu wana uzito wa chini ukilinganisha na umri wao – ambayo ni dalili ya ukosefu wa lishe ya kutosha kwa muda mrefu. Takwimu hizo zinaonyesha pia kuwa kuna tofauti kubwa kati ya lishe ya watoto wa mjini na wa kijijini ambapo asilimia 26 ya watoto wa mjini wanaupungufu wa lishe na wamedumaa wakati kule vijijini ni asilimia 41.

Wakati haya tunayaangalia utashangaa kuona nchi yetu ina chakula cha kutosha cha kila aina. Miaka ya zamani tulikuwa na kampeni za “mtu ni afya”, “kuleni chakula bora”, n.k na tulifika mahali tukaweza hata kutoa maziwa kwenye shule zetu za chekechekea hata shule za msingi. Leo hii tukiuliza juu ya mlo kwa watoto wetu jibu la haraka litakuwa ni “hatuna fedha” au “tunatafuta wafadhili”.

Ipo na mifano mingine ya takwimu za afya na masuala mengine ya jamii ambazo zinaonesha jinsi gani watoto wetu wanalipa gharama kubwa ya vitendo vya kifisadi. Matokeo yake huwa tunashangazwa inakuwaje watoto wetu hawafaulu vizuri darasani, na wanafanya vibaya kwenye mitihani tumeshindwa kuoanisha hali ya lishe na ukuaji wa kiakili (cognitive development). Tunafikiri yote haya yanatokea katika ombwe!

3. VIJANA

Mojawapo ya waathirika wakubwa wa mfumo huu ni vijana. Kundi hili lina vijana wa kati ya miaka 18 na 35 na ambao kutokana na sababu mbalimbali wamekosa nafasi ya kujiendeleza kielimu au kuwa katika mazingira ya kupata mafunzo rasmi na hivyo kulazimika kuishi kwa “kujishughulisha” katika kile ambacho kimebatizwa jina la “ajira zisizo rasmi” a.k.a kubangaiza na kuhangaika. Kundi hili la vijana wanatumia nguvu nyingi ya mwili kufanya vitu ambavyo vingetumia mbinu rahisi au utaalamu rahisi, na wakati mwingine wanajikuta wanatumia nguvu zaidi za misulu kuliko za ubongo katika maisha yao.

Hawa (ambao wengine utotoni hawakupata milo mizuri) wanajikuta wamekua kimwili lakini kiakili na kifahamu bado ni watu wa kusukumwa na hisia au nawatu wanaojiita “wataalamu”. Kundi hili ni kundi ambalo ni hatari kwenye taifa lolote lenye mfumo wa utawala wa kifisadi. Kundi hili halihitaji kushawishiwa kuona ubovu wa maisha yao; wanaoishi maisha hayo. Kundi hili haliitaji kuhubiriwa juu ya kile kilicho bora; wanakiona kwa wengine.

Matokeo yake utaona kuwa kundi hili halitoi mchango unaostahili katika kujenga taifa kwani hakuna mtu ambaye anaamini kwa dhati kuwa linamchango; matokeo yake limebakia kuwa ni kundi kubwa lililo nje ya madaraka na nje ya mfumo wa maisha ya kawaida. Mamilioni ya vijana wetu wanajikuta wakizunguka kila kukicha wakitafuta nafasi katika maisha yao. Na mambo yanakuwa mabaya zaidi pale kundi hili linapoanza kuona watawala wanaendelea kujenga mbingu zao hapa hapa duniani huku wao wakiendelea kuwa kituko katika mitaa yao na maeneo yao.

Baadhi yao hulazimika kuanza kuishi maisha ya kujidhalilisha na uhalifu; wanageukia wizi, ubakaji, na uporaji na wengine hasa kina dada hujiingiza katika biashara ya ngono kama hatua za mwisho za kusalimisha utu wao na hadhi yao kama binadamu.

Vijana ndio wanabeba uzito mkubwa wa athari ya utawala wa kifisadi kwani ni hawa ambao wanajikuta wamesukumwa nje ya malango ya mafanikio, na kama ombaomba wanalazimika kukinga mikono yao ili kuweza kupata nafasi ya kula matunda ya urithi wa taifa lao.

4. WENYE KIPATO NA ELIMU YA CHINI

Wananchi wenye kipato cha chini ambao wana elimu duni hujikuta wakiathirika zaidi na ufisadi kwani hawa njozi yao ya maisha ya manufaa na yenye unafuu inabakia katika vichwa vyao lakini isiyotimilika. Hawa hujikuta wakiwa kama abiria wanaoenda uwanja wa ndege kuangalia ndege za walionufaika zikipaa huko wao wameachwa wameduwaa. Hubakia kuambizana tu kuwa “siku moja nikipata nauli na mimi nitaruka”.

Mfumo wa ufisadi huwatengenezea mazingira ya kuwatuliza kwa kuwapa ajira ndogo ndogo, misaada ya hapa na pale na kuwaahidi mema huko mbeleni. Hawa hujikuta wakiambiwa kila siku na watawala kuwa wafanye kazi “kwa bidii na maarifa” bila ya kujiuliza kuwa ulimwengu wa leo kazi hufanywa kwa akili, utaalamu, na weledi wa hali ya juu na maarifa ambayo hubadilika kila kukicha. Matokeo yake kundi hili hujaribu kujiendeleza kwa fani mbalimbali na ujuzi wa aina tofauti lakini wakiamka asubuhi hujikuta wako katika hali ile ile.

WANUSURIKA WA MFUMO WA UFISADI

Vile vile lipo kundi la wanusurika wa MUK. Kundi hili linawajumuisha wale wote ambao kutokana na nafasi zao wanajua madhara ya ufisadi, uovu wa mfumo wa kifisadi na wanajua kabisa kuwa nini kinapaswa kufanyika. Kundi hili linawajumuisha watu ambao wanauwezo wa kubadilisha mambo lakini kutokana na kujikuta wakiwa wananufaika vile vile na mfumo huo hujikuta wakifanya kazi ndani yake kwa manung’uniko na kukerwa nao lakini hawawezi kuuacha kwani kwa kufanya hivyo watajikuta kuwa ni waathirika.

Hawa hawataki kuonekana ni mafisadi na huwabeza mafisadi sirini (siyo hadharani); lakini hawawezi kutoka kwenye mfumo huo wa kifisadi kwani na wao ni wanufaika aidha kutokana na ajira zao, nafasi zao za kisiasa, biashara au mahusiano yao ya karibu na watawala. Wanusurika wa ufisadi ni majeruhi wa mfumo huo lakini wasiopona. Baadhi ya wanusurika wa ufisadi wako katika makundi yafuatayo.

1. WATUMISHI WA UMMA

Hawa ni watumishi ambao wanauona kila kukicha mfumo wa ufisadi ukifanya kazi; ni wao ndio kwa namna ya pekee wanatumika pasipo matakwa yao kuundeleza mfumo huu. Ni hawa ambao kutokana na nafasi zao hutekeleza maagizo na maelekezo mbalimbali hata wakijua kuwa yana matokeo maovu kwa “waathirika”; badala ya kupinga au kuyafichua mambo hayo hujikuta wakikubali (hata kama kwa shingo upande) kupitisha sera, kutekeleza maamuzi ambayo kwa kweli wanajua mioyoni mwao kuwa si yenye maslahi kwa taifa au kwa wananchi moja kwa moja.

Ndio hawa ambao tumeona mambo yao kwenye kashfa za BoT, ni hawa tumewaona kwenye kashfa za ATCL, TRL, Tanesco na kwingine. Hawawezi kuachia nafasi zao kwani ukiwauliza watasema “sasa mimi nile wapi?”

Kwa vile wanajua madudu yanayofanywa na vikaragosi vya ufisadi (mabosi wao) basi hujikuta na wenyewe kutumia nafasi hizo hizo na wao kula. Huandaa visemina uchwara, mikutano ya “tathmini” na kozi za “kujiendeleza” ambazo wakati mwingine hurudiwa kwa jina jingine na kwenye hoteli nyingine. Hujikatia posho za kila namna ilimradi waweza kufuja fedha za umma bila kumuogopa yoyote.

Lakini ni hawa hawa upande mwingine wanachukizwa na vitendo vya ufisadi mkubwa na ndio wamekuwa wa kwanza vile vile kufichua ufisadi mkubwa katika taasisi zao kwani wanajua kabisa na kwa undani mambo yanayofanywa na makuwadi wa ufisadi wenyewe. Katika mikutano mbalimbali na pembeni hulalamika sana juu ya vitendo vya rushwa na milungula ya aina mbalimbali, lakini wakati huo huo na wenyewe hujikuta kupokea au kukubali vitu hivyo ili “maisha” yaende mbele. Hawa kama ingepatikana jinsi ya kuondoa rushwa na kunufaisha maisha yao kihalali wangeachana na vitendo vya kifisadi kwani baadhi yao wanaporudi nyumbani ni watu wa imani, na maadili lakini wanapokuwa kazini au maofisini hujihusisha na vitendo hivyo kwa kisingizio kuwa “kila mtu anafanya hivyo”.

2. VYOMBO VYA HABARI

Kama kuna kitu ambacho ninakielewa vizuri sasa hivi zaidi kuliko miaka karibu minne iliyopita ni kuwa vyombo vya habari vinanufaika na ufisadi lakini kwa namna ya kunusurika. Vyombo hivi hujionesha kuwa vinapigana na ufisadi na vinaandika sana habari ya ufisadi; tatizo ni kuwa ili viendelee kuwepo vinategemea mafisadi hao hao!

Hivyo, utaona baadhi ya magazeti hata ambayo husifiwa kwa kupiga vita ufisadi hutegemea matangazo ya biashara kutoka kwa watawala na wakati mwingine huenda kubembeleza kwa watawala hao hao ili “walete” matangazo kwenye magazeti au vyombo hivyo vya habari. Na watawala wanajua udhaifu huu. Kuna wakati watawala huamua kuvisusia vyombo kadhaa vya habari kwa sababu vinaziandika wizara, idara au vyombo Fulani vibaya na hivyo hawapeleki matangazo yao mbalimbali huko.

Na cha kusikitisha zaidi ni kuwa watawala wale wale ambao ndio wanufaika wa ufisadi wamekamata vile vile vyombo vya habari huku wengine wakiwa na maslahi ya wazi kabisa katika vyombo hivyo. Hawa huajiri waandishi wa habari kufanya kazi ya habari lakini wakati huo huo hupeleka matangazo ya idara, wizara au serikali kwenye vyombo vyao bila ya kutangaza maslahi (without declaring interest).

Sasa, utaona kuwa vyombo vya habari vinanufaika pia kwa namna nyingine; kwa kuandika habari kwa hisia na wakati mwingine kwa kama kuchonganisha. Magazeti haya hupata wasomaji wengi wenye hamu na kiu ya kujua mambo mengi. Mfano mzuri wa jinsi gani magazeti yanacheza mchezo huu ni katika sakata la Mengi na Rostam, na suala la Mwakyembe na Mwakipesile, n.k Ni jambo moja kutoa habari na kuburudisha watu lakini ni jambo jingine kabisa kuchochea ugomvi na wakati huo huo kutengeneza fedha.

Inakuwa kama watu wanaochonganisha watu huku wao wakikaa pembeni kusubiri nani ashinde ili wawe upande wake na waendelee kumchuna.

Vyombo vimenusurika kwa sababu, baadhi yake vingeweza kuendeshwa kwa biashara ya kuuza magazeti na mambo mengine vingekuwa kweli huru na vingependa kuwa hivyo lakini kutokana na ukweli kuwa bado serikali ndiyo yenye biashara kubwa kwenye vyombo hivyo basi vyombo hivyo vya habari hujikuta vinapiga magozi na kucheza ngoma ya mafisadi.

3. TAASISI ZA KIDINI

Kwa muda mrefu taasisi za kidini zimeweza kukua na kunufaishwa sana na mfumo wa kifisadi. Nilipoandika barua yangu ya kwanza kwa wachungaji na makala zilizofuatia baadaye zilikuwa na lengo la kuamsha kundi hili ili watoke katika kile nilichokiita wakati ule “kitanda cha ufisadi” ambao viongozi wetu wa dini na wanasiasa wamelala huku wakijifunika blanketi moja. Kwa muda mrefu viongozi wetu wa dini hawakuwa tayari kuunyoshea mkono utawala wa kifisadi zaidi ya kukiri uwepo wa vitendo vya rushwa na uvunjaji wa sheria wa hapa na pale. Lakini wakati huo huo viongozi hao wa dini na taasisi zao walijua kabisa wakitaka baadhi ya mipango na miradi yao ifanikiwe hawana budi kuimba nyimbo za watawala.

Katika siku za karibuni tumeanza kuona mwamko wa aina yake ambapo viongozi wa dini wakiwa kama watu waliochelewa stesheni ya garimoshi wameanza kudandia mjadala dhidi ya ufisadi kwa namna ya pekee zaidi; kuuita uovu huo kwa jina lake mbele ya watawala.

Jawabu la watawala tuliliona kwenye jaribio la kujaribu kutishia mapato na shughuli za taasisi hizo za kidini katika mapendekezo ya kufuta misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini isipokuwa kwa mambo ya ibada. Ile ilikuwa ni kama onyo na sitoshangaa huko mbeleni watawala wakaamua kufanya kweli na hivyo kutishia taasisi hizo za dini kukaa pembeni ya mambo ya siasa.

Pamoja na hilo bado taasisi na viongozi wa kidini hawajaacha kunufaika kwa namna moja au nyingine na mfumo huu wa ufisadi. Ili miradi yao, makanisa, misikiti, mashule na mahospitali yao yafanikiwe na misaada yao isipate shida bandarini ni lazima wawe tayari kula “sahani moja” na watawala.

Lakini viongozi hawa hawa hujikuta wanalazimishwa na ukweli wa mambo kukemea ufisadi hadharani na kuukataa. Lakini jambo moja ambalo hawawezi kulifanya ni kupambana na ufisadi hadharani; hawatoandamana kupinga mafisadi, hawatokataa kuwapigia magoti watawala, na kamwe katika MUK usitarajie viongozi wa dini kuchukua msimamo mkali unaoambatana na vitendo vya kiupingaji ambavyo vina lengo la kuamsha dhamira ya wananchi.

Taasisi hizi za kidini nazo zimenusurika na ufisadi lakini pia zinanufaika na uwepo wake.

4. ASASI MBALIMBALI

Mojawapo ya wanusurika wa ufisadi ni asasi mbalimbali za kijamii. Hizi leo hii zimegeuzwa kuwa mitaji ya kujitengenezea utajiri wa haraka haraka kwa kutumia visingizio vya kutoa misaada au kusaidia jamii. Hivyo, haishangazi kuona kuwa wanufaika wa ufisadi na wao wenyewe wameanzisha asasi zao mbalimbali ambazo zinapokea misaada mbalimbali kama makanisa lakini hizi haziongozwi na imani (japo nyingine ni za kidini); zinaongozwa na kile kinachodhaniwa kuwa ni huruma kwa watu.

Sizijumuishi asasi zote za makanisa au viongozi wote wa dini na kuwaweka kwenye kundi la wasio wa kweli na wenye malengo zaidi ya yale yaliyomo kwenye asasi zao; nazungumzia wale ambao kama wanasiasa waliopotoka au polisi waliopotoka wamejikuta wakitumia nafasi ya uwepo na ukomavu wa mfumo wa kifisadi kujenga na kujijenga wao wenyewe wakitumia shida na mahangaiko ya watu wengine.

Hawa huwa na urafiki wa karibu na wanufaika wa ufisadi na utakuta wakijitangaza aidha kupitia makampuni yao au asasi zao wakigawa misaada ya kila aina na kutoa misaada wakati wa sherehe za kidini na matukio mbalimbali. Lengo lao ni kujenga jina “jema” la asasi, mashirika au makampuni yao mbele ya wananchi na mbele ya watawala. Lakini, wakati huo huo wanatumia kila aina ya ujanja kutumia misaada vibaya na kwa maslahi yao wenyewe nje ya yale ya watu wanaosema wako tayari kuwasaidia.

NI MFUMO WA HATARI

Mfumo huu kwa kila kipimo ni mfumo ambao hatuwezi kuuvumilia, kuuendeleza, wala kuutafutia udhuru wa uwepo wake. Ni mfumo ambao hauna budi kubomolewa na kuvunjwa vunjwa na kutupwa katika shimo la usahaulifu la historia. Ni mfumo ambao hudumaza jamii kubwa huku ukinufaisha kikundi cha watu wachache ambao kutokana na nguvu zao za kisiasa na kiuchumi huharibu hata nafasi ya utawala wa sheria.

Kimsingi kabisa mfumo huu haupatani (incompatible), hauwezi kupatana sasa na hata milele na utawala wa kidemokrasia hauwezi kushikana na utawala wa sheria na kamwe hauwezi kuwa sehemu moja na jamii ya watu walio huru na sawa. Ni mfumo ambao huinua katika jamii tishio kubwa zaidi la mafanikio ya taifa na wananchi, ukiahidi uongo huku ukibeza ukweli, ukigeuza udhalimu kuwa haki na uonevu kuwa maelewano.
Ukweli huo unanifanya niamini kuwa mfumo huu hauwezi kuvunjwa majukwaani, kwa kusoma magazetini au kwa kulumbana mitaani. Mfumo huu hauwezi kuvunjwa na kuharibiwa kwa kuandika na kujadiliana kwenye mitandao ya intaneti au kwa kutumiana barua pepe kusimuliana kilichojiri.

Mfumo wa aina hii huangushwa kisayansi na kitaalamu kwa kutumia nguvu za kisiasa na mikakati yenye matokeo mema. Hauwezi kuangushwa kwa kusubiri bahati itokee. Tutaendelea kuangalia mbele katika masomo mengine zaidi ya huu mfumo.

No comments:

Post a Comment