Tuesday, November 10, 2009

Siasa za Kyela na kivuli cha Dk Mwakyembe


Date::10/27/2009

CCM kuamua kunyoa au kusuka

Daniel Mwaijega






Mbunge wa Kyela
Dk. Harrison Mwakyembe
"HAPA Kyela hakuna machafuko ya kisiasa. Hali ni shwari kabisa. Vurugu mnazosikia si za kisiasa, bali zinasababishwa na kundi la wahuni. Siyo siasa hata kidogo; ni uhalifu unaosababishwa na vijana wavuta bangiĆ¢€¦" Ndivyo anavyosema Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Luteni Abdallah Kihato akielezea kuhusu hali ya kisiasa wilayani humo na kuongeza:

"Hata kijana aliyedaiwa kuuawa na polisi kwa sababu za kisiasa si kweli na wala hakuuawa. Alikuwa miongoni mwa wavuta bangi wa mjini hapa. Alikamatwa katika msako wa polisi, alipofikishwa kituoni alianza kutapika na kuishiwa nguvu.

Ndugu zake waliitwa na kupelekwa hospitali ambako aligundulika kuwa ana malaria kali na kwa sababu alikuwa amedhoofu kwa kutokula, hakuwa na nguvu za kutosha kukabiliana na ugonjwa huo akafariki baada ya siku nne. Baada ya hapo vijana wenzake wakaanza fujo kwa madai kuwa polisi wamemuua".

Maelezo hayo ni sehemu ya majibu ya maswali yanayoulizwa na watu wengi kuhusu mazingira ya kisiasa wilayani Kyela, kufuatia msuguano mkali, uliodumu kwa karibu miaka minne sasa; kati ya wapambe na mashabiki wa mbunge wa eneo hilo, Dk Harrison Mwakyembe na wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile.

Mvutano huu ulianza wakati Dk Mwakyembe alipojitokeza kuwania ubunge wa Kyela, jimbo ambalo awali lilikuwa chini ya Mwakipesile ambaye alikuwa anawania tena. Hali ilizidi kuwa tete baada ya Mwakipesile kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM. Licha ya CCM kutangaza kuvunja makundi, chuki binafsi zimeendelea kujionyesha dhahiri mpaka sasa.

Mwakipesile alipochaguliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya, hali iliendelea kuwa mbaya na kutengeneza hoja nyingine ambazo zilidhihirisha kuwa mambo bado si shwari.

Ukifika Kyela hali ni shwari kwa sababu huwezi kuona vurugu.

Lakini ukikaa na wananchi unaweza kuona hali halisi ya mvutano uliopo kati ya makundi ya mafahali hao wa kisiasa wilayani humo.

Siasa za Kyela zina msisimko wake kutokana na msimamo wa wananchi wa huko, ambao kwa asilimia kubwa siyo wanafiki; wako wazi na huru kueleza wanachoamini kinafaa na wanachokipenda.

Ni rahisi kuwashawishi wapokee zawadi au takrima; lakini si rahisi kubadili misimamo yao katika jambo lolote wanaloona lina manufaa na ambalo wamekubaliana. Hawafichi kueleza ukweli wa nini au nani wanamtaka.

Maelezo ya mkuu wa wilaya hiyo alipohojiwa na mwandishi wa makala haya hivi karibuni, hayapingani na ukweli wa hali halisi inavyoonekana katika wilaya hiyo. Hakuna vurugu ila kuna msuguano wa kisiasa. Hakuna kupigana na kupigwa ila kuna mvutano wa kimapenzi kwa wanasiasa hao.

Kitu kimoja ambacho huwezi kukiweka bayana ni ugomvi kati ya Dk Mwakyembe na Mwakipesile; hauko wazi, hivyo unaweza kusema haupo.

Lakini upo kwa mtazamo wa kifikra, uwezo kiutendaji na kukubalika na wananchi. Hata hivyo, hakuna anayeweza kusema wazi kuwa mafahali hao hawapikiki chungu kimoja, ingawa mazingira yanaonyesha hivyo. Zaidi ya hapo hakuna anayeweza kusema sababu za kuwapo kwa mvutano huo ni nini.

Akizungumzia kuhusu hali ya kisiasa wilayani Kyela na hasa ndani ya CCM, Mwenyekiti wa chama wa wilaya hiyo, Japhet Mwakasuma anasema: "Hali ndani ya CCM ni shwari kabisa na chama hakijatikisika.

Yanayosikika mitaani ni siasa zinazochochewa na wapambe. Dk Mwakyembe na Mwakipesile wana wapambe wao ambao ndiwo wanaochuana"

Anasema, kimsingi wanachofanya wapambe ni kupigania maslahi yao, ambayo kwa namna fulani kama mgombea wao akishindwa yanakwisha, hivyo wanatumia mbinu za kuhakikisha wanaonekana wanafanya kazi ya kumsaidia.

"Kuna watu wananufaika moja kwa moja kutoka kwa wanasiasa, hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanafanikisha mipango yao na ndiyo wanaokoleza mvutano na uhasama," anasema Mwakasuma.

Mwakasuma anasema kuwa yeye aliwania nafasi hiyo pamoja na Mwakipesile mwaka 2000 lakini akashindwa kwenye kura za maoni na pia aliingia katika kinyanganyiro cha 2005 ambapo Dk Mwakyembe alishinda uteuzi wa chama. Safari zote nilikubali matokeo na sina kinyongo na yeyote na ninafanya kazi nao vizuri.

Ila kitu kimoja, siasa za uchaguzi zina mambo yake ambayo hutegemea sana wapambe."

Kuhusu ugomvi wa Mwakyembe na Mwakipesile anasema: "Sisi kama chama hatuoni tatizo liko wapi na hawagombani kama mnavyosikia.

Ni kweli kulikuwapo makundi wakati wa mchakato wa kupata mgombea na hali ya hewa mbaya ambayo iliibuka hata baada Uchaguzi Mkuu.

Ila chama kilishazungumza na kila mmoja; hata katika vikao vya CCM mkoa tulikaa na kukubaliana kuvunja makundi. Pia Kamati maalumu ya CCM taifa iliyoongozwa na Abdulrahman Kinana ilifika mkoani hapa kusuluhisha na kumaliza mambo."

Pamoja na maelezo ya Mwakasuma, bado kuna vuguvugu la mvutano miongoni mwa wanachama na wananchi kwa ujumla kiasi cha kuwapo kwa vita za chini chini.
Kwa mfano, baadhi ya wananchi wanasema kunapotokea mikutano au shughuli za maendeleo, kunakuwa na mvutano wa wazi unaoonyesha kuwa makundi ya Mwakipesile na Dk Mwakyembe hayaivi.

Habari za ndani zinasema hata wanapokuwa kwenye vikao vya chama mkoani au wilayani akiwapo Mkuu wa Mkoa, kunakuwa na msuguano baina yake na baadhi ya watu. Kejeli na mafumbo kutoka pande zote hutawala na wakati mwingine kunyoosheana vidole bila kujali utofauti wa nafasi na nyadhifa zao.

Hata hivyo, kisiasa bado Dk Mwakyembe anashika mioyo ya watu wilayani Kyela kutokana na ukweli kwamba, anaungwa mkono hata na vijana wadogo wanaoona amesukuma maendeleo ya Kyela na yuko karibu nao.

Wengi wanaona kuwa mbunge wao ni jasiri anayeweza kuwatetea na kuwapigania kutokana na kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ufisadi.

"Mbali na kusimamia na kuhamasisha maendeleo katika wilaya yetu, ametuletea sifa sana kutokana na ujasiri aliouonyesha katika mapambano ya ufisadi, hasa aliposimama bila hofu kuweka wazi kashfa ya Richmond ambayo iliwahusisha vigogo wa serikali.

Huyu ndiye mtu anayetakiwa kuongoza, siyo wale wanaojipendekeza tu kwa wakubwa, wakati mambo hayaendi sawa.

"Nadhani tungekuwa na wabunge 100 kama Mwakyembe nchi hii ingebadilika na viongozi wangenyookaĆ¢€¦," anasema Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwaikambo.
Hivi karibuni kumekuwapo fununu za baadhi ya watu kujitokeza kuchuana na Dk Mwakyembe katika kuwania nafasi ya kuwa wagombea wa kiti hicho kupitia CCM
.

Tayari kuna fununu kuwa mtu mmoja ambaye yuko Uingereza amejitokeza na anadaiwa kuungwa mkono na kundi la wapambe wa Mwakipesile ili kumwondoa Dk. Mwakyembe ambaye anaonekana kuwa kisiki kilichojimbia chini kutokana na jinsi wananchi wanavyomuunga mkono.
Hata tukio lililoripotiwa hivi karibuni kuwa kuna watu walitaka kumchoma kisu mbunge huyo liliunganishwa na kampeni hizo; ingawa taarifa sahihi ni kwamba, mmoja wa wapambe wa mgombea mtarajiwa alikamatwa na wapambe wa Dk Mwakyembe akirekodi hotuba yake kwa kificho kwa kutumia simu ya mkononi.

Walimnyang'anya simu hiyo, walipoipekua walikuta hotuba za mikutano kadhaa ya Mwakyembe ambazo alikuwa anazipeleka kwa mtu wao, pamoja na meseji (ujumbe wa maandishi) za mawasiliano kati yao na ndugu yao wa Uingereza zinazoelezea mikakati ya kumbwaga Mwakyembe.

Wakati hayo yakiendelea , Dk Mwakyembe hakujua lolote mpaka alipomaliza mkutano wake jioni. Mbunge huyo amekuwa akieleza kuwa hakuona tukio hilo; lakini sasa kambi ya upande wa pili wanamshutumu kwamba anadanganya kwa ajili ya kujipatia umaarufu.

Siasa ni kama upepo unaobadili mwelekeo wakati wowote nani atakuwa mbunge wa Kyela katika uchaguzi mkuu ujao bado ni fumbo ambalo wakati wake wa kufumbuka haujafika. Ila CCM iko katika mtego ambao ikikosea kuchanganya karata itakiona kilichomkosesha kanga manyoya!

1 comment:

  1. Naomba ifahamike kwamba siasa za Kyela mara zote si za kinafiki na ni za ''black and white'' na wananchi wa Kyela wanampenda mtu asiyeumauma maneno kupindisha uongo ukawa ukweli na ukweli ukawa uongo.

    Kwa kipindi hiki hakuna mtu anayeweza kumg'oa Dk. Mwakyembe kwenye jimbo la Kyela kwasababu ni mbunge ambaye wanakyela wangependa awe na yuko vile. Kwa kila mwanakyela anayeishi Kyela au nje ya Kyela lazima atamuunga mkono mbunge wao huyo kwa kazi nzuri ya maendeleo jimboni na Taifa kwa ujumla.

    ''ebu jiulize kama mtoto wako anapendwa na majirani zako na watu wengine wa nje kwanini wewe usimpende?''

    Nitamuunga mkono Dk. Mwakyembe kwa sasa kwani ni mtu anayenifaa kwa maendeleo ya jimbo langu.

    ReplyDelete