Wednesday, November 18, 2009

KUUELEWA MFUMO WA UTAWALA WA KIFISADI

Na. M. M. Mwanakijiji

Maadui wa Tanzania siyo Rostam, Lowassa, Chenge, Mramba, Yona au mtu yeyote ambaye ameonakana na kutajwa kuwa ni fisadi au kuhusishwa na kashfa za kifisadi. Hawa wote na wengine wengi ambao nimewabatiza majina ya “makuwadi wa ufisadi” na “vikaragosi vya ufisadi” ni matokeo tu ya yule adui yetu namba moja ambaye bila ya kumshughulikia basi juhudi zote za kupigana na “ufisadi” zitakuwa ni kama juhudi za anayezama majini huku kwa hasira akiyapiga ngumi maji hayo ili “kuyakomoa”. Ni zoezi lisilo na tija.

Anayepigana vita dhidi ya ufisadi (awe ndani ya CCM au nje yake) akifikiria kuwa anapigana dhidi ya watu “fulani” basi hajajua uzito wa vita hii iliyo mbele yetu; vita ambayo hatukuitafuta bali tumejikuta tunalazimika kuipigana kwani imeletwa kwetu bila kumchokoza mtu na haitaondoka isipokuwa kwa kuishinda tu.

Tukijifunza katika vita ya Kagera tunaweza kuona kuwa lingekuwa kosa kubwa sana kwa wapiganaji wetu kuwaadhibu wanajeshi wa UPDF (Jeshi la Wananchi wa Uganda) tukifikiria kuwa wao ndio walikuwa adui zetu. Tunaelewa kwamba wanajeshi wale walikuwa wanatekeleza amri ya vita toka kwa amiri Jeshi Mkuu wao wa wakati ule Idi Amin Dada. Sasa kama tungepigana ili kushinda wapiganaji wa Uganda kwenye jukwaa la vita halafu basi tungechekwa na jumuiya ya kimataifa kwa kutokuelewa tulipigana dhidi ya nani hasa.

Adui yetu wakati ule ulikuwa ni utawala wa Nduli Idi Amin na mfumo mzima wa utawala wake uliosababisha sisi twende vitani licha ya juhudi zote za kuepuka vita kuchukuliwa na kushindikana. Ndio sababu wakati wa tangazo la vita kwa Taifa letu Baba wa Taifa aliweka lengo lililokuwa wazi kabisa, kuyarudisha majeshi ya Amin toka ardhi yetu (kama kuwarudisha nyuma makuwadi wa ufisadi), kumkata makali Amin kabisa asiweze kuthubutu kutuvamia na kuwa tishio kwetu tena.(kama kuwakata makali mafisadi wasipate nafasi za kuchukua pesa zetu).

Katika hilo lengo la pili vikosi vyetu vilipewa jukumu la kuhakikisha vinammaliza kabisa adui na kuhakikisha kuwa habakii tena madarakani. Hivyo, tunajifunza kutoka vita vya Uganda kuwa haikutosha kumrudisha adui nyuma au kuyatoa majeshi yake toka ardhi yetu; ilitupasa kuhakikisha kuwa adui hapati tena nafasi ya kuthubutu kutishia mpaka wetu na hivyo licha ya kuingia Uganda hadi Kampala, vikosi vyetu vilisonga mbele hadi Jinja na Entebbe na kusababisha Idi Amin kuachia ngazi na kukimbia taifa lake kwa aibu.

Vikosi vyetu havikuondoka Uganda mara tu baada ya Amin kutoroka bali baadhi ya wapiganaji wetu walibakia Uganda kusaidia katika ujenzi wa taifa hilo na hasa ujenzi wa jeshi jipya lisilokuwa tishio kwa majirani zake kwa kutoa mafunzo na kulinda amani wakati jeshi la Uganda linapangwa upya.

Vita ya ufisadi nayo ni vivyo hivyo. Wale tunaowaita mafisadi, makuwadi wa ufisadi, vikaragosi vya ufisadi ni watumishi wanaofaidika na mfumo wa utawala wa kifisadi. Ndugu zangu, adui nambari moja wa maendeleo na mafanikio ya Watanzania ni mfumo haramu uliotengenezwa na utawala wa kifisadi. Ni lazima kwa mpiganaji yeyote kuelewa mfumo huu unavyofanya kazi kwani wale wote tunaowaita mafisadi leo hii ni matokeo ya mfumo huu wa kiutawala; mfumo ambao ni mchanganyiko wa mifumo midogo midogo ya kisiasa, kiuchumi, na kisheria ambayo msingi wake ni ubinafsi, kutokuwajibika, kulindana, utawala wa hofu, kubebana na kuvumiliana kwa kadiri ya kwamba wanufaikaji ni kikundi cha watu wachache walio katika utawala na wale wanaohusiana nao kwa karibu.


Mfumo wa utawala wa kifisadi ni nini basi?
Ni muungano wa utendaji kazi wa mifumo ya kisiasa, uchumi, na kisheria ambao msingi wake ni kujitajirisha kwa haraka haraka pasipo kuogopa matokeo yake. Mfumo wa kifisadi unahusiana moja kwa moja na utajiri wa “haraka haraka” ambao unafanywa kwa kulainisha utendaji kazi wa vyombo mbalimbali vya dola vyote vikitengeneza kama mwamvuli mkubwa kwa watawala. Lengo kubwa la mfumo huo ni kuwalinda watawala.

“Mfumo” ni nini hasa?
Mfumo yaani “system” kwa kiingereza unaweza kuelezewa kama muunganiko wa michakato, kanuni, shughuli mbalimbali vikifanya kazi kwa pamoja kufikia lengo moja. Neno “system” linatokana na neon la Kigiriki “systema” yaani “kuleta pamoja”. Ndani ya mfumo mmoja mkubwa unaoweza kuzaa mifumo mingine midogo midogo ikifanya kazi mahsusi lakini yote ikitekeleza lengo moja kubwa.

Mfano mzuri hapa ni wa kutumia motokari (gari). Lengo kubwa la gari ni uwezo wake wa kuendeshwa. Hivyo, ukiona gari linakwenda basi unajua kuwa lengo lake limefanikiwa na wakati wowote ukiona gari linazimika zimika au kukwama kwama basi unajua kuna tatizo fulani. Mafundi wa magari wanapoletewa gari bovu wanauliza tatizo nini au dalili gani dereva aliziona. Katika kufanya hivyo fundi-gari anaanza kufikilia ni mfumo gani mdogo (sub-system) wenye tatizo.

Ataangalia mafuta ya breki, mafuta ya injini, maji ya kupoozea, oili n.k na kama gari haliwaki kabisa likiwaswa basi ataangalia kama stata bado inafanya kazi, betri kama bado ina nguvu n.k Ni katika kuiangalia hii mifumo midogo midogo ndivyo anaweza kugundua tatizo na kulishughulikia na hatimaye kulirudisha gari barabarani.

Mfano mwingine mzuri ni wa kuelewa mfumo wa mwanadamu. Mwanadamu ameumbwa akiwa na mifumo mikubwa mikubwa na mingine midogo midogo lakini yote ikifanya kazi kuhakikisha mtu huyo ni hai na anaishi kwa afya. Wengi tunaifahamu mifumo ile mikubwa ya mwili kama Mfumo wa Fahamu (nervous system), mfumo wa chakula (digestive system), mfumo wa Uzazi (Reproductive System), mfumo wa utoaji uchafu mwilini, mfumo wa pumzi, na mfumo wa damu. Ndani ya mifumo hii mikubwa ipo mifumo mingine midogo midogo na yote hii ikifanya kazi “kwa pamoja” inafikia lengo la kutufanya tuwe na afya na kuendelea kuishi.

Kunapotokea tatizo kwenye mfumo wowote kati ya hiyo mtu atajikuta ni mgonjwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia leo hii kunawezesha baadhi ya mifumo kusaidiwa kufanya kazi na mashine mbalimbali.

Madaktari wote na wauguzi na wataalamu mbalimbali wa tiba wanajifunza juu ya mifumo hii na ile mingine na kwa kadiri ya taaluma zao wengine wanajikuta wanasomea zaidi utendaji kazi wa mfumo mmoja maalum na kuwa mabingwa wa eneo hilo. Vivyo hivyo wataalamu wa magari wapo ambao wamekubuhu katika mambo ya umeme wa magari na wengine katika injini n.k

Katika haya yote, mifumo hii inaangaliwa kwa ukaribu wake na ni msingi wa kuelewa utendaji kazi wa gari, kiumbe au kitu chochote kinachohusisha mfumo zaidi ya mmoja. Ni kwa sababu hiyo basi ni muhimu kuelewa kuwa mfumo wa utawala wa kifisadi huundwa na utendaji kazi wa mifumo mikubwa mitatu ambayo ndiyo huwezesha mfumo huo kufanya kazi yake ya kukitengenezea kikundi cha watu wachache utajiri wa haraka haraka bila kuogopa matokeo yake. Kimsingi kabisa, mfumo wa utawala wa kifisadi umejengwa ili kunyonya na kukandamiza.

Ni mifumo ipi inayounda mfumo huu?
Kama nilivyodokeza hapo juu mfumo wa utawala wa kifisadi huundwa na utendaji kazi wa mifumo ya kisiasa, kisheria, na kiuchumi. Mifumo hii mitatu ikifanya kazi kwa pamoja huuisha utawala wa kifisadi, uupa nguvu na kuufanya udumu. Tuangalie mifumo hii mitatu jinsi ilivyo katika Tanzania.

Mfumo wa Kisiasa:
Mfumo wetu wa kisiasa umetengenezwa ili kulinda maslahi ya kikundi cha watu walio madarakani. Haujatengenezwa ili kuruhusu ushindani wa haki wa kisiasa, na hauruhusu changamoto ya kweli ya siasa za kidemokrasia. Utaona kuwa katika mfumo wetu wa kisiasa, katiba ya nchi inaelezea juu ya ujenzi wa taifa la kijamaa na ile ya chama tawala nayo ikisema hivyo hivyo. Hata hivyo hakuna mtu yeyote ndani ya serikali ya sasa au kwenye chama anayeweza kutetea ujamaa leo hii au kutuelezea ni “ujamaa” wa aina gani wanauunda.

Maana yake ni kuwa, watawala waliopo sasa hawajali hasa katiba inasema nini kwani kwao katiba ni kama mapendekezo ya aina fulani tu na siyo mkataba unaowafunga watawala kwa watawaliwa. Leo hii siyo Kikwete, Makamba wala Kingunge wanaoweza kutuambia ni aina gani ya ujamaa wanaoutekeleza kwa mujibu wa Katiba.

Ni mfumo ambao umewekeza nguvu kwenye chama cha kisiasa kiasi kwamba watu wachache kwenye chama hicho wanaweza kutuamulia ni nani anakuwa Rais wetu au Spika wetu wakiamua tu kumvua uanachama. Ni mfumo ambao unafanya geresha ya demokrasia kwa kufanya uchaguzi wa vyama vingi huku mfumo wa sheria walioutengeneza ukizuia kabisa uchaguzi huru na wa haki.

Hivyo, mfumo wa kisiasa wa kwetu ni kiinimacho cha siasa za kidemokrasia kwani ndani yake kuna vizuizi vingi vya utendaji kazi wa demokrasia; kutokuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, matokeo ya uchaguzi wa rais hayawi rasmi hadi tume isiyo huru itangaze, kukataza wagombea huru, ukosefu wa chombo cha kusimamia Bunge, n.k

Mfumo wa Kisheria
Mfumo wetu wa kisheria katika utawala wa kifisadi umeundwa ili kuondoa hasira na siyo kushughulikia tatizo lenyewe hasa linalosumbua jamii. Kwa kiasi kikubwa utaona kuwa sheria mbalimbali zimeundwa zikiwa na majina mazuri na ya kupendeza lakini zikiangaliwa kwa karibu utaona kuwa zimeundwa ili kuwafanya watu wasikasirike sana.

Sheria mbalimbali zilizotungwa kwenye utawala wa kifisadi zimetengenezwa ili kuzuia watu wasijichukulie sheria mikononi lakini wakati huo huo kutoa ulinzi wa aina yake kwa wahalifu wanasiasa.

Mojawapo ya vitu ambavyo vimeondolewa kwenye sheria nyingi ambazo zingeweza kuwakamata wanasiasa na watendaji wazembe ni kile ambacho tunakiita kama “trigger clauses”. Kwamba endapo kitu x kitatokea basi mtu y atachukuliwa hatua zifuatazo. Kwa mfano, endapo mtendaji anatakiwa kutoa maelezo na Mkaguzi Mkuu ya matumizi ya shilingi milioni 300 na akashindwa nini kimtokee? Utaona sheria zetu haziko wazi zaidi ya kumpa CAG uwezo wa kuonesha au kutoa maelekezo kuwa huyo “y” achunguzwe au kuchukuliwa hatua “zinazopasa”.

Utaona kuwa sheria zetu zina matundu ya makusudi kabisa yenye kuzuia utekelezaji wake wa mara moja na hivyo matundu hayo yamekuwa ni kinga kubwa ya makuwadi wa ufisadi kwani wanajua kabisa kuwa mtu akitaka kuzifuata sheria hizo atajikuta anashindwa kabla hajafika mbali.

Hivyo, mfumo wetu wa kisheria umeundwa ili kuzuia hasira lakini kushindwa kuzuia vitendo vya ufisadi uliokubuhu. Mtu yeyote anayesoma sheria ya kupambana na kuzuia rushwa, sheria ya madini, sheria ya usalama wa taifa na sheria ya makosa ya kuhujumu uchumi utaona kuwa watawala wamezitengeneza ili zisifanikiwe. Na hivi karibuni watawala hao hao wamepunguza nguvu ya baadhi ya sheria hizo kwa sababu wanajua akiingia mtu kichaa kwenye ofisi ya DPP kuna watu wengi watatiwa pingu.

Mara zote kwenye utawala wa kifisadi, watawala hutumia mianya mbalimbali kuvuruga utawala wa sheria ili kujikinga na mashtaka huko mbeleni. Ndio maana leo hii tuna mtu ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu kwa miaka 10 na ambaye yeye mwenyewe anashtumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa sheria lakini hakuna mtu mwenye ubavu wa kunyosha kidole na badala yake anakingiwa kifua; ndio maana leo hii baadhi ya “watunga sheria” wetu ndio wale wale wanaotajwa kwenye baadhi ya uvunjaji mkubwa kabisa wa sheria katika jamhuri yetu.

Mfumo wa kiuchumi
Katika utawala wa kifisadi, mfumo wa kiuchumi hufanana na mfumo wa kiuchumi katika utawala wa kidemokrasia. Ukiangalia kwa juu juu mfumo wa kiuchumi unaundwa na taasisi kama zile zilizopo kwenye nchi za kidemokrasia na ukisoma maandishi mbalimbali unaweza kabisa kuamini kuwa mfumo huo wa uchumi katika utawala wa kifisadi unalingana kiutendaji na mfumo wa kiuchumi katika utawala wa kidemokrasia. Hili si kweli.

Unapokuwa na mfumo mbovu wa kisiasa na kisheria, mfumo wa kiuchumi nao hauwezi kuwa salama. Kwa maneno mengine, mfumo wa kiuchumi hauwezi kusalimika pale ambapo mfumo wa kisiasa na ule wa kisheria inapokuwa matatani. Mara zote ubovu wa mfumo wa kisheria na kisiasa huonekana katika ubovu wa mfumo wa kiuchumi.

Katika Tanzania ya leo hii tunaweza kujiuliza ni mfumo wa aina gani wa kiuchumi tunaoufuata? Je ni ubepari au ujamaa? Je ni mchanganyiko wa aina hizo mbili na kwa namna gani? Mara nyingi utamsikia Kikwete na wanasiasa wengine wa CCM wakielezea juu ya “mfumo wa Soko” au mfumo wa “ushindani” je hii kiitikadi ina maana gani? Je, ni mashindano kati ya tajiri na maskini, aliyenacho na asiyenacho, mwanaCCM na asiye mwanaCCM?

Na hata wakati mwingine unaposikia takwimu mbalimbali za kiuchumi toka Benki Kuu hatuna budi kujiuliza hivi ni kweli takwimu hizo ziko sahihi kwa kiasi gani? Kwenye nchi ambayo uzalishaji unafanyika kwa zaidi ya asilimia 90 kwa njia zisizorasmishwa tunaweza vipi kuelezea kwa uhakika hali ya kiuchumi? Kwenye nchi ambapo asilimia zaidi ya 20 (Kikwete hivi karibuni alidai asilimia 30) ya bajeti inaishia kwenye vitendo vya rushwa na ufisadi, unaweza vipi kuelezea kuwa mfumuko wa bei uko chini ya tarakimu mbili?

Unawezaje kuelezea “kukua kwa uchumi” na ukawa sahihi kwenye taifa ambalo madini yake haijulikani kwa hakika ni kiasi gani kinatolewa nje na mahali ambapo makampuni yanaweza kusafirisha nje faida yao kwa asilimia 100 huku yakitangaza kupata hasara kila mwaka kwa mujibu wa sheria nyingine tuliyowatengenezea?

Tunaweza vipi kupima kwa haki pato la mwananchi wakati sehemu ya pato hilo ni lile linalotokana na rushwa kidogo? Unaposema bei ya kitu (bidhaa au huduma) ni kiasi fulani lakini wakati huo huo mtu anatakiwa kubajeti ndani yake “kitu kidogo” juu ya bei hiyo, mchumi anapopiga hesabu zake anachukulia na hicho “kitu kidogo” ndani au hapana?

Kimsingi utaona kuwa katika mfumo wa utawala wa kifisadi, mfumo wa uchumi ni wa kudanganya. Yaani, taarifa rasmi za kiuchumi haziakisi ukweli hasa wa shughuli za kiuchumi na uwezo wa uchumi huo (kwa uzuri au kwa ubaya). Matokeo yake wakati mwingine watu wanaamini kuwa uchumi wao unafanya kazi vizuri zaidi wakati hiyo “vizuri zaidi” ni kwa sababu ya vitendo vya kifisadi.

Ndio maana kuna baadhi ya watu wanaamini kabisa kuwa endapo ufisadi utapigwa marufuku kabisa na kila mtu kulazimishwa kuishi kwa haki kunaweza kutokea maandamano makubwa sana. Kwani kwa mara ya kwanza, watu watatakiwa kuishi kwa uhalisi wa vipato na matumizi yao.

Sasa basi, tunaweza kuona kuwa mafisadi waliopo sasa ni mazao ya mfumo uliopo sasa hivi. Hata tukiweza kuwaangusha na kuwatia pingu mafisadi wote bado tutakuwa na kizazi kipya cha mafisadi kwani mfumo uliowatengeneza bado upo.

Itakuwa ni sawasawa na kiwanda cha kutengeneza magari; kama kuna mahali ambapo mashine moja haiingizi breki kwa usawa kwenye gari, basi magari yatakayotoka yatakuwa na matatizo na breki zake. Watu watapata ajali na mengine itabidi yaondolewe barabarani. Lakini kama suluhisho ni kuondoa magari mabovu ambayo tunajua yanatoka kwenye kiwanda fulani lakini wakati huo huo kiwanda bado kinatengeneza magari mabovu kwa sababu sehemu ya mashine yake (mfumo wake mmoja au zaidi) imeharibika basi tutakuwa tunacheza “pata potea”.

Suluhisho siyo tu kuondoa magari mabovu barabarani bali vile vile kurekebisha mashine kiwandani ili zisitengeneze gari lenye matatizo ya breki.

Leo hii ninachosikia ni watu kulalamikia “mafisadi” (magari mabovu), watu wanapiga kelele ni kwa kadiri gani mafisadi wameifisadi nchi n.k lakini sijamsikia hata mtu mmoja mwenye ujasiri wa kusema kuwa tatizo letu ni “kiwanda”.

Ndio maana nimesema awali kuwa tatizo letu siyo Rostam, Lowassa, Chenge au Yona; hawa ni dalili tu ambazo tunaweza kuziondoa barabarani. Tutakuwa hatuna hekima kama tunaamini kuwa tukiwaondoa hawa toka madarakani basi ufisadi utakwisha. Tusipobadilisha mfumo wa kiutawala ufisadi tutaendelea kuzalisha mafisadi tu. Haijalishi ni chama gani kiko madarakani.

Ndio sababu, tunapowasikiliza wanaotaka kugombea mwakani hatuna budi kujiuliza na kuwauliza wao, wanampango gani wa kuubadilisha mfumo wa kiutawala wa ufisadi badala ya kuwashughulikia mafisadi wa sasa tu? Watafanya nini kuurekebisha mfumo wetu wa kiutawala ili usitoe mafisadi na vifaranga vyao?

Ni katika kuelewa hili ndipo tunaweza kuelewa kuwa adui yetu wa kwanza kabisa katika vita hii ni mfumo wa utawala wa kifisadi. Lakini ni nani huyu aliyejemedari aliyeuunda, kuupanga, na kuusimamia mfumo huu wa kifisadi kiasi kwamba tunavuna matunda yake machungu leo hii? Ni nani huyo ambaye anapaswa kuzuiliwa asiendelee kutufyatulia matofali ya mchanga mtupu kujengea taifa letu? Wengine, wanafikiria ni mtu mmoja au kikundi cha mafisasdi.

Mimi napendekeza; ni mfumo wa utawala wa Chama cha Mapinduzi. Unabisha?

Niandikie:

mwanakijiji@mwanakijiji.com

1 comment:

  1. Nimesoma makala hii ya rafiki yangu Mwanakijiji na nikapendezewa nayo na ninatamani na wewe pia uisome kwa umakini na utulivu ili kuiokoa nchi yetu katika hili janga.

    Lazima tujipange kupambana na hawa watu kwa kila namna ili wasije wakazaliana na kuongezeka na kuwa tatizo kwa vizazi vyetu vijavyo.

    ReplyDelete